Mafundisho na Maagano 2021
Agosti 2–8. Mafundisho na Maagano 85–87: “Simameni katika Mahali Patakatifu”


“Agosti 2–8. Mafundisho na Maagano 85–87: ‘Simameni katika Mahali Patakatifu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Agosti 2–8. Mafundisho na Maagano 85–87,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
familia ikitembea kwenda hekaluni

Agosti 2–8

Mafundisho na Maagano 85–87

“Simameni katika Mahali Patakatifu”

Roho anaweza kukuongoza kujifunza kanuni katika sehemu za 85–87 ambazo hazikuoneshwa katika muhtasari huu. Fuata misukumo Yake.

Andika Misukumo Yako

Siku ya Krismasi kwa kawaida ni wakati wa kutafakari ujumbe kama “amani duniani” na “mapenzi mema kwa watu” (ona Luka 2:14). Lakini mnamo Desemba 25, 1832, akili ya Joseph Smith ilikuwa imetawaliwa na tishio la vita. Carolina ya Kusini ilikuwa kinyume na serikali ya Marekani na ilikuwa ikijiandaa kwa vita. Na Bwana alifunua kwa Joseph kwamba hii ilikuwa mwanzo tu: “Vita,” Yeye alitangaza, “vitamwagika juu ya mataifa yote” (Mafundisho na Maagano 87:2). Ilionekana kana kwamba unabii huu ungetimia punde tu.

Lakini haikuwa hivyo. Ndani ya wiki chahce tu, Carolina ya Kusini na serikali ya Marekani walifikia makubaliano, vita ilikuwa imezuiwa. Lakini ufunuo si lazima wakati wote utimizwe katika wakati au katika njia tunayoitarajia. Takribani miaka 30 baadaye, muda mrefu baada ya Joseph Smith kuuwawa na Watakatifu kuhamia magharibi, Carolina ya Kusini iliasi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilifuatia. Tangu hapo, vita kote ulimwenguni imesababisha “dunia kuomboleza” (Mafundisho na Maagano 87:6). Wakati unabii hatimaye ulitimizwa, thamani ya ufunuo huu ni ndogo katika kutabiri lini majanga yatakuja na kubwa zaidi katika kufundisha nini cha kufanya wakati yanapokuja. Ushauri ni uleule mwaka 1831, 1861, na 2021: “Simameni katika Mahali Patakatifu, wala msiondoshwe” (mstari wa 8).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mafundisho na Maagano 85:1–2

Ni vizuri “kuhifadhi historia.”

“Historia” iliyoelezwa katika mstari wa 1 iliweka kumbukumbu ya majina ya wale ambao “wamepata nafasi” katika Sayuni (ona Mafundisho na Maagano 72:24–26). Hata hivyo, historia hii ilikuwa zaidi ya utawala tu—ilikuwa pia ni kumbukumbu yenye thamani ya “namna wanavyoishi, imani yao, na matendo yao” (mstari wa 2).

Je, unatunza historia au shajara binafsi? Ni nini ungeweza kuweka kumbukumbu kuhusu namna unavyoishi, imani yako, na matendo yako ambavyo vingeweza kuwa baraka kwa vizazi vijavyo? Ni jinsi gani historia hii ingeweza kuwa baraka kwako?

Ona pia “Shajara: ‘Yenye Thamani ya Juu kuliko Dhahabu,’” Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Wilford Woodruff (2011), 125–33; “Turning Hearts” (video, ChurchofJesusChrist.org).

Mafundisho na Maagano 85:6

Roho huzungumza kwa “sauti ndogo tulivu.”

Tafakari maneno ya Joseph Smith yaliyotumika kumwelezea Roho katika Mafundisho na Maagano 85:6. Ni kwa namna gani sauti ya Roho ni “ndogo” na “tulivu”? Ni baadhi ya vitu gani “vimepenya” katika maisha yako?

Unapofikiria kuhusu jinsi Roho anavyozungumza nawe, fikiria maelezo haya yaliyotolewa kupitia Joseph Smith: Mafundisho na Maagano 6:22–24; 8:2–3; 9:7–9; 11:12–13; 128:1. Kwa kuzingatia kile ulichosoma, nini unahisi unahitaji kufanya ili kutambua vizuri zaidi sauti ya Roho?

Ona pia 1 Wafalme 19:11–12; Helamani 5:30.

Picha
Mwanamke akisoma maandiko

Kujifunza maandiko hutusaidia kumsikia Roho Mtakatifu.

Mafundisho na Maagano 86

Wenye haki wanakusanywa katika siku za mwisho.

Mafundisho na Maagano 86:1–7 ina maelezo ya Bwana ya mfano wa ngano na magugu, pamoja na msisitizo tofauti kidogo na ule Yeye alioutoa katika Mathayo 13:24–30, 37–43. Unapolinganisha mifano hiyo miwili, unagundua tofauti zipi? Fikiria kwa nini mfano huu—pamoja na tofauti hizi—vina thamani kurudiwa “katika siku za mwisho, hata sasa” (Mafundisho na Maagano 86:4). Unaweza kujifunza nini kutokana na mfano huu na tafsiri yake ya siku za mwisho?

Kama ilivyoandikwa katika mistari 8–11, Bwana wakati huo alizungumzia ukuhani, urejesho, na wokovu wa watu Wake. Ni muunganiko upi unauona kati ya mistari hii na mfano wa ngano na magugu? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwa kama “mwokozi kwa watu wa [Bwana]”? (mstari wa 11).

Ona pia Mada za Injili, “Ukengeufu,” “Urejesho wa Ukuhani,” topics.ChurchofJesusChrist.org.

Mafundisho na Maagano 87

Imani inapatikana katika “mahali patakatifu.”

Kwa kuongezea kwenye hatari za kimwili za “umwagaji damu … [na] njaa, na magonjwa, na matetemeko” (Mafundisho na Maagano 87:6), ushauri katika ufunuo huu unaweza pia kuhusika kwenye hatari za kiroho ambazo sote tunakabiliana nazo katika siku za mwisho. “Mahali pako patakatifu” (mstari wa 8) ambapo unapata amani na usalama ni wapi? Nini hufanya mahali kuwa patakatifu? Kwa kuongezea kwenye maeneo yanayofikika, pengine kuna nyakati takatifu, matendo matakatifu, au mawazo matakatifu ambayo yanaweza kuleta amani. Inamaanisha nini “kutoondoshwa” kutoka mahali hapo?

Ona pia Henry B. Eyring, “Nyumba ambayo Roho wa Bwana Anakaa,” Ensign au Liahona, Mei 2019, 22–25; Watakatifu, 1:163–64; “Amani na Vita,” Ufunuo katika Muktadha, 158–64.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 85:6.Ni kwa jinsi gani unaweza kuifundisha familia yako kutambua sauti ndogo, tulivu ya Roho? Pengine mngeweza kucheza mchezo ambapo mtu ananong’ona maelekezo muhimu katikati ya kelele za kuvuruga mawazo. Nini kinaweza kuwa cha kutuvuruga mawazo kutoka kwenye kumsikia Roho Mtakatifu? Pengine wanafamilia wangeweza kushiriki kile wanachofanya ili kusikia sauti ya Roho.

Mafundisho na Maagano 86.Kuchora au kutazama picha kungeweza kuwasaidia wanafamilia kuelewa mfano wa ngano na magugu. Ungependa kuanza na picha za vitu vilivyoelezewa katika Mathayo 13:24–30. Kisha familia yako ingeweza kujaza picha kwa maelezo kutoka Mafundisho na Maagano 86:1–7. Ni kwa jinsi gani sisi ni kama ngano? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa kama malaika wanaokusanya ngano?

Mafundisho na Maagano 87:8.Ili kutambulisha mjadala kuhusu jinsi ya kuiweka nyumba yako kuwa mahali patakatifu zaidi, ungeweza kuwaalika wanafamilia kupangilia nyumba kwa ajili ya mtu anayempenda Mwokozi. Hili linaweza kuongoza kwenye mawazo kuhusu jinsi ya “kupangilia upya nyumba yako ili kuifanya mahali pa amani katikati ya hatari ya kiroho ulimwenguni. Nyimbo kama “Love at Home,” “Home Can Be a Heaven on Earth” (Nyimbo za Kanisa, na. 294, 298), au “Where Love Is” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 138–39) zingeweza kukupa mawazo.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Where Love Is,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 138–39.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia ubunifu wako. Unapoifundisha familia yako kutoka kwenye maandiko, usijiwekee kikomo kwenye maswali na mawazo ya shughuli yaliyopendekezwa katika muhtasari huu. Acha mawazo haya yachochee ubunifu wako mwenyewe. Fikiria kuhusu kile familia yako itakachofurahia na kile kitakachowasaidia kupata muunganiko kati ya maandiko na maisha yao.

Picha
shamba la ngano

Bwana alitumia mfano wa ngano na magugu kuelezea jinsi watu Wake watakavyokusanywa katika siku za mwisho.

Chapisha