“Agosti 16–22. Mafundisho na Maagano 89–92: ‘Kanuni yenye Ahadi,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Agosti 16–22. Mafundisho na Maagano 89–92,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021
Agosti 16–22
Mafundisho na Maagano 89–92
“Kanuni yenye Ahadi”
Kwa sala jifunze Mafundisho na Maagano 89–92, na andika misukumo yoyote ya kiroho unayopokea. Kuwa makini na jinsi “Roho anavyofunua ukweli” kwako wakati unapojifunza (Mafundisho na Maagano 91:4).
Andika Misukumo Yako
Kwenye Shule ya Manabii, Nabii Joseph Smith aliwafunza wazee wa Israeli kuhusu kuujenga ufalme wa Mungu duniani. Walijadili kweli za kiroho, waliomba pamoja, walifunga, na walijiandaa kuhubiri injili. Lakini kulikuwa na kitu kuhusu mazingira ambayo yangeweza kuonekana si ya kawaida kwetu leo, na haikuonekana sawa kwa Emma Smith pia. Wakati wa vikao, wanaume walivuta na kutafuna tumbaku, kitu ambacho hakikuwa cha kushangaza kwa wakati huo, lakini iliweka madoa meusi kwenye sakafu za mbao na kuacha harufu mbaya kwenye hewa. Emma alishiriki wasiwasi wake kwa Joseph, na Joseph alimwomba Bwana. Matokeo yalikuwa ufunuo ambao ulikwenda mbali zaidi ya kuvuta tumbaku na uchafu wa tumbaku. Uliwapa Watakatifu, kwa vizazi vijavyo, “kanuni yenye ahadi”—ahadi ya afya ya kimwili, “hekima,” na “hazina kubwa ya maarifa” (Mafundisho na Maagano 89:3, 19).
Ona pia Watakatifu, 1:166–68.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Neno la Hekima ni “Kanuni yenye Ahadi.”
Wakati wazee katika Shule ya Manabii waliposikia kwa mara ya kwanza Joseph Smith akisoma Neno la Hekima, kwa haraka “walirusha mirija na misokoto ya tumbaku ya kutafuna kwenye moto” (Watakatifu, 1:168). Wakati huo, Neno la Hekima lilichukuliwa zaidi kama tahadhari kuliko amri, lakini walitaka kuonesha utayari wao wa kutii. Pengine tayari “umerusha” kutoka kwenye maisha yako vitu ambavyo Neno la Hekima linaonya kuvihusu, lakini nini kingine unajifunza kutoka kwenye ufunuo huu? Fikiria mawazo haya:
-
Tafuta vifungu vya maneno ambavyo hukuvigundua—au kuvipa uzito sana—kabla. Je, unajifunza nini kutoka kwavyo?
-
Mafundisho na Maagano 89 inajumuisha ahadi kadhaa (ona mistari 18–21). Je, unadhani ahadi hizi zina maana gani?
-
Ni nini ufunuo huu unakufundisha kuhusu Bwana?
-
Ni mifano gani umeona ya “uovu na njama … katika mioyo ya watu wenye kula njama”? (mstari wa 4).
-
Fikiria ufunuo kama “kanuni yenye ahadi” (mstari wa 3)—kweli za kudumu ambazo zinaongoza ufanyaji maamuzi—si tu orodha ya mambo ya kufanya na kutofanya. Je, ni kanuni gani unazipata ambazo zinaweza kuongoza maamuzi yako?
Manabii wa siku hizi pia wameonya juu ya vitu na tabia hatari zaidi ya zile zilizotajwa katika Neno la Hekima (ona “Afya ya Mwili na Hisia,” Kwa Nguvu ya Vijana, 25–27). Nini unavuviwa kufanya ili kutunza vizuri akili na mwili wako?
Ona pia Danieli 1; 1 Wakorintho 6:19–20; Gospel Topics, “Neno la Hekima,” topics.ChurchofJesusChrist.org; “Neno la Hekima,” Ufunuo katika Muktadha, 183–91; addictionrecovery.ChurchofJesusChrist.org.
Urais wa Kwanza unashikilia “funguo za ufalme.”
Katika sehemu ya 90, Bwana alitoa maelekezo kuhusu “huduma na urais” (mstari wa 12) wa Joseph Smith, Sidney Rigdon, na Frederick G. Williams—washiriki wa kile sasa tunachokiita Urais wa Kwanza. Unajifunza nini kuhusu Urais wa Kwanza kutoka mistari 1–17? Rejea ujumbe wa karibuni kutoka kwa washiriki wa Urais wa Kwanza. Ni kwa jinsi gani maneno yao “yanafichua siri za ufalme” kwako? (mstari wa 14). Ni kwa jinsi gani “yanaweka vyema mambo yote ya kanisa hili na ufalme”? (mstari wa 16).
Ona pia Henry B. Eyring, “Nguvu ya Kuidhinisha Imani,” Ensign au Liahona, Mei 2019, 58–60.
“mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida [yangu].”
Tafakari uzoefu wowote uliowahi kuwa nao ambao unashuhudia juu ya ahadi ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 90:24. Zingatia kuandika uzoefu wako na kuushiriki pamoja na mwanafamilia au mpendwa wako—pengine mtu anayehitaji uhakika mpya au kutiwa moyo. Ikiwa kuna baraka ambazo bado unazisubiri, tafakari kile unachoweza kufanya ili kubaki mwaminifu wakati unaposubiri kuona “mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida yako.”
Mafundisho na Maagano 90:28–31
Vienna Jaques alikuwa nani?
Vienna Jaques alizaliwa mnamo Juni 10, 1787, huko Massachusetts. Mwanamke wa imani ambaye alikuwa na kipato kikubwa, Vienna mara ya kwanza alikutana na wamisionari mnamo 1831. Baada ya kupata ushahidi wa kiroho kwamba ujumbe wao ulikuwa wa kweli, alisafiri kwenda kukutana na Nabii huko Kirtland, Ohio, ambapo alibatizwa.
Vienna alitii ushauri wa Bwana kwake katika Mafundisho na Maagano 90:28–31. Uwekaji wakfu wake kwa Bwana, ikiwa ni pamoja na michango aliyofanya Kirtland, vilikuja kipindi muhimu sana kwa kanisa, wakati viongozi walipokuwa wakijaribu kununua ardhi ambapo Hekalu la Kirtland lingejengwa. Vienna alikuwa “mwaminifu, na hakuwa … mvivu” kote katika maisha yake na hatimaye aliweza “kutulia katika amani” (mstari wa 31) huko Salt Lake Valley, ambapo alifariki akiwa na umri wa miaka 96.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani
-
Mafundisho na Maagano 89.Wanafamilia wako wangeweza kufurahia kuchora au kutafuta picha za vyakula na vitu vingine vilivyotajwa katika Mafundisho na Maagano 89. Kisha mngeweza kucheza mchezo—wanafamilia wangeweza kufanya zamu kuchagua picha bila mpangilio sahihi, wakiweka vitu ambavyo hatupaswi kutumia kwenye uchafu na vitu tunavyopaswa kutumia kwenye sahani. Je, ni kwa namna gani ahadi katika mistari 18–21 zimetimizwa katika maisha yetu?
Kusoma “Afya ya Mwili na Hisia” katika Kwa Nguvu ya Vijana (25–27) kungeweza kuchochea mjadala kuhusu njia zingine za kutunza afya zetu na kuhusu baraka ambazo Mungu anaahidi.
-
Mafundisho na Maagano 90:5.Zungumzeni kuhusu jinsi “mlivyopokea maagano [ufunuo au manabii] wa Mungu.” Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonesha kwamba si “kitu rahisi” kwetu?
-
Mafundisho na Maagano 91.Mngeweza kujadili jinsi ushauri wa Bwana kuhusu Apokrifa (ona mistari 1–2) unavyohusika kwenye vyombo vya habari familia yako inavyokabiliana navyo leo (ona pia Mwongozo kwenye Maandiko, “Apokrifa,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Ungeweza pia kushiriki uzoefu binafsi wakati “kuangazwa na Roho” (mstari wa 5) kulipokusaidia kutambua kati ya ukweli na kosa.
-
Mafundisho na Maagano 92:2.Inamaanisha nini kuwa “mshiriki hai” wa Kanisa?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “The Lord Gave Me a Temple,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,153.