Mafundisho na Maagano 2021
Novemba 29–Desemba 5. Mafundisho na Maagano 137–138: “Ono la Ukombozi wa Wafu”


“Novemba 29–Desemba 5. Mafundisho na Maagano 137–138: ‘Ono la Ukombozi wa Wafu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Novemba 29–Desemba 5. Mafundisho na Maagano 137–138,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

watu katika ulimwengu wa roho

Joseph anamwona baba yake, mama, na kaka katika ufalme wa selestia (Ono la Joseph Smith la Ufalme wa Selestia, Robert Barrett).

Novemba 29–Desemba 5.

Mafundisho na Maagano 137–138

“Ono la Ukombozi wa Wafu”

Rais M. Russell Ballard alifundisha: “Ninawaalika ninyi kikamilifu na kwa kufikiri msome [Mafundisho na Maagano 138]. Mnapofanya hivyo, Mungu na awabariki muweze kuelewa vyema zaidi na kuwa na shukrani kwa ajili ya upendo wa Mungu na mpango Wake wa wokovu na furaha kwa ajili ya watoto Wake” (“Ono la Ukombozi wa Wafu,” Ensign au Liahona, Nov. 2018, 73).

Andika Misukumo Yako

Funuo zilizoandikwa katika Mafundisho na Maagano 137 na 138 zimetenganishwa kwa zaidi ya miaka 80 na maili 1,500. Sehemu ya 137 ilipokelewa na Nabii Joseph Smith mnamo mwaka 1836 katika hekalu lililokuwa halijamalizika la Kirtland, na sehemu ya 138 ilipokelewa na Joseph F. Smith, Rais wa sita wa Kanisa, mnamo mwaka 1918 katika Jiji la Salt Lake. Lakini kimafundisho, maono haya mawili yanastahili kuwa pamoja. Yote mawili yanajibu maswali kuhusu majaliwa ya watoto wa Mungu katika maisha yajayo. Na yote yana maana ya kina iliyoongezwa wakati tunapofikiria matukio ya maisha ya manabii walioyapokea.

Ono la Joseph Smith lilimsaidia kuelewa majaliwa ya milele ya kaka yake mpendwa Alvin, ambaye alikufa miaka sita kabla ya mamlaka ya kubatiza kurejeshwa. Maswali kuhusu ukombozi wa milele wa Alvin yalikuwa yapo kwa Joseph tangu wakati huo. Ufunuo wa Joseph F.Smith ulifunua kweli tukufu kuhusu ulimwengu wa roho—hakika ufunuo wa faraja kwa yule aliyehuzunika kwa vifo vya wanafamilia wengi wa karibu. Joseph F. Smith alimpoteza baba yake, Hyrum Smith, akiwa na miaka 5 na mama yake, Mary Fielding Smith, akiwa na umri wa miaka 13. Wakati wa ono lake mnamo mwaka 1918, alikuwa ameomboleza kufariki kwa watoto 13.

Maswali mengi ambayo watu wanayo kuhusu maisha baada ya kifo yanajibiwa katika funuo hizi. Sehemu ya 137 inatoa mwanga kiasi wa mwanzo kwenye maswali kama hayo, na sehemu ya 138 inafungua mapazia kwa uwazi kabisa. Kwa pamoja, zinashuhudia juu ya “upendo mkuu na wa ajabu uliowekwa dhahiri na Baba na Mwana” (Mafundisho na Maagano 138:3).

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mafundisho na Maagano 137

Kila roho itakuwa na fursa ya kuchagua utukufu wa selestia.

Uelewa wa kawaida miongoni mwa Wakristo mnamo mwaka 1836 ulikuwa kwamba kama mtu alikufa bila kubatizwa—kama ilivyokuwa kwa Alvin kaka wa Joseph Smith—mtu yule asingeweza kwenda mbinguni. Lakini bado Joseph alimwona Alvin katika ono la ufalme wa selestia. Unaposoma sehemu ya 137, tafakari kile unachojifunza kuhusu Baba wa Mbinguni, mpango Wake wa wokovu, na ufalme wa selestia.

Ona pia Saints, 1:232–35.

Mafundisho na Maagano 138:1–11, 25–30

Kusoma na kutafakari maandiko kunaniandaa mimi kupokea ufunuo.

Wakati mwingine ufunuo unakuja hata kama hatuutafuti. Lakini mara nyingi, unakuja kwa sababu tunautafuta kwa bidii na kujiandaa kwa ajili yake. Unaposoma Mafundisho na Maagano 138:1–11, 25–30, fahamu kile Rais Joseph F. Smith alichokuwa anakifanya wakati “macho [yake] ya uelewa yalipofunguliwa” ili kuelewa vizuri zaidi misheni ya ukombozi ya Mwokozi. Kisha fikiria jinsi unavyoweza kufuata mfano wa Rais Smith. Kwa mfano, ni mabadiliko gani unayoweza kuyafanya kwenye mafunzo yako ya maandiko kuruhusu wingi wa “kutafakari juu ya maandiko” na zaidi “kutazama juu ya dhabihu [ya Mwokozi] iliyo kuu ya upatanisho”? (mistari 1–2).

Katika ujumbe wake “Ono la Ukombozi wa Wafu” (Ensign au Liahona, Nov. 2018, 71–74), Rais M. Russell Ballard alipendekeza njia nyinginezo ambazo kwazo Rais Smith alikuwa amejiandaa kupokea ufunuo huu. Fikiria jinsi ambavyo umekuwa ukijiandaa kwa ajili ya uzoefu ulionao au utakaokuwa nao hapo baadaye.

Ona pia video ya “Ministry of Joseph F. Smith: A Vision of the Redemption of the Dead,” ChurchofJesusChrist.org.

picha ya kuchora ya Joseph F. Smith

Joseph F.Smith, na Albert E. Salzbrenner

Mafundisho na Maagano 138:25–60

Kazi ya wokovu inatendeka kwenye pande zote mbili za pazia.

Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Ujumbe wetu kwa ulimwengu ni rahisi na wa kweli: tunawaalika watoto wa Mungu wote kutoka pande zote mbili za pazia waje kwa Mwokozi wao, wapokee baraka za hekalu takatifu, wawe na furaha ya kudumu, na kustahili uzima wa milele” (“Sote Tusonge Mbele,” Ensign au Liahona, Mei 2018, 118–19). Tafakari kauli hili unaposoma Mafundisho na Maagano 138:25–60. Ungeweza pia kufikiria maswali haya:

  • Unajifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu jinsi kazi ya ukombozi inavyokamilishwa katika ulimwengu wa roho? Kwa nini ni muhimu kwako kujua kwamba kazi hii inafanyika? Je, ni kwa jinsi gani mistari hii inaimarisha imani yako katika Upatanisho wa Mwokozi?

  • Aya hizi zinafundisha nini kuhusu wale wanaoshiriki katika kazi ya wokovu katika ulimwengu wa roho? Kwa nini ni muhimu kuelewa kwamba kazi ya ukombozi inafanyika pande zote mbili za pazia?

Ona pia Dallin H. Oaks, “Amini katika Bwana,” Ensign au Liahona, Nov. 2019, 26–29; “Susa Young Gates and the Vision of the Redemption of the Dead,” Ufunuo katika Muktadha, 315–22.

ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 137:1–5.Alika familia yako kuchora kile wanachofikiria ufalme wa selestia unavyoweza kuonekana kutokana na mistari hii. Unapata nini katika mistari hii ambacho kinakusaidia kutegemea kuishi huko? Tunafanya nini sasa kujiandaa kuishi katika ufalme wa selestia pamoja na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo?

Mafundisho na Maagano 137:5–10.Kujifunza kuhusu nini kingeweza kumaanisha kwa Joseph Smith kuwaona baadhi ya wanafamilia yake pamoja katika ufalme wa selestia, familia yako ingeweza kuangalia video “Ministry of Joseph Smith: Temples” (ChurchofJesusChrist.org). Pengine mngeweza pia kuzungumza kuhusu mtu fulani mnayemjua ambaye alikufa bila nafasi ya kubatizwa. Ni nini Mafundisho na Maagano 137:5–10 inatufundisha kuhusu mtu huyo?

Mafundisho na Maagano 138:12–24.Ni nini Mafundisho na Maagano 138:12–24 inafundisha kuhusu watu waliotembelewa na Mwokozi katika ulimwengu wa roho? Je, ni baraka gani walizipokea? Tunajifunza nini kutoka kwenye mfano wao?

Mafundisho na Maagano 138:38–55.Mistari hii inaelezea wale ambao Rais Joseph F. Smith aliwaona katika ulimwengu wa roho na maelezo kwa kifupi kuwahusu. Pengine familia yako ingeweza kutengeneza orodha ya mababu zako ambao wako katika ulimwengu wa roho, pamoja na maelezo kamili kuhusu maisha yao.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Search, Ponder, and Pray” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tafakari juu ya maandiko. Rais David O. McKay aliita tafakuri “moja ya … milango mitakatifu mno ambayo kwayo tunapita kwenda kwenye uwepo wa Bwana” (Mafundisho ya Marais wa Kanisa: David O. McKay [2003], 32).

Yesu Kristo katika ulimwengu wa roho

Waliopewa mamlaka, na Harold I. Hopkinson. Yesu Kristo aliwapa mamlaka roho wenye haki kuhubiri injili katika ulimwengu wa roho.