Njoo, Unifuate
Septemba 2–8. 1 Wakorintho 14–16: ‘Mungu Si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani’


Septemba 2–8. 1 Wakorintho 14–16: ‘Mungu Si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya (2019)

“Septemba 2–8. 1 Wakorintho 14–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Kisima cha ubatizo cha hekaluni

Septemba 2–8

1 Wakorintho 14–16

“Mungu Si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani”

Andika misukumo yako wakati unaposoma 1 Wakorintho 14–16. Omba kuhusu kile ambacho Roho amekufundisha, na mwombe Baba wa Mbinguni akujulishe kama kuna cha zaidi ambacho Yeye angetaka ujifunze.

Andika Misukumo Yako

Kwa sababu Kanisa na mafundisho yake vilikuwa kwa kiasi fulani vipya katika Korintho, ni ya kueleweka kwamba Watakatifu wa Korintho walikumbana na machafuko. Hapo mwanzo Paulo alikuwa amewafundisha ukweli muhimu wa injili: “Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu … na kwamba alizikwa, na kwamba alifufuka tena siku ya tatu” (1 Wakorintho 15:3–4). Lakini punde baadhi ya waumini walianza kufundisha kwamba “hakuna ufufuko wa wafu” (1 Wakorintho 15:12). Paulo aliwasihi “kuzishika” kweli walizokuwa wamefundishwa (1 Wakorintho 15:2). Tunapokumbana na mawazo yanayopingana kuhusu kweli za injili, ni vizuri kukumbuka kwamba “Mungu Si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani” (1 Wakorintho 14:33). Kuwasikiliza watumishi wa Bwana walioteuliwa na kushikilia kweli hizi rahisi walizofundisha kwa kurudia rudia kunaweza kutusaidia kupata amani na “kusimama imara katika imani” (1 Wakorintho 16:13).

ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Binafsi

1 Wakorintho 14

Ninaweza kutafuta kipawa cha unabii.

Je, umewahi kujiuliza kipawa cha unabii ni nini? Je, ni uwezo wa kutabiri yajayo? Je, mtu yeyote anaweza kupokea kipawa hiki? Au ni kwa ajili ya manabii pekee yao?

Rais wa Kanisa ndiye mtu pekee anayeweza kutoa unabii kwa ajili ya na kupokea ufunuo kwa niaba ya Kanisa zima; hata hivyo, Mwongozo wa Maandiko unaelezea maana ya unabii kama “maneno au maandishi matakatifu yenye mwongozo wa kiungu, ambayo mtu hupokea kupitia ufunuo kutoka kwa Roho Mtakatifu. … Wakati mtu anatoa unabii, yeye husema au huandika yale ambayo Mungu anataka yeye ajue, kwa faida yake mwenyewe au kwa faida ya wengine” (Mwongozo wa Maandiko, “Unabii,” scriptures.lds.org; ona pia M&M 100:5–8). Ufunuo 19:10 pia hutoa maana ya roho ya unabii kama “ushuhuda juu ya Yesu.”

Je, unajifunza nini kuhusu kipawa hiki cha kiroho kutoka 1 Wakorintho 14:3, 31, 39–40? Je, Paulo yawezekana alimaanisha nini wakati alipowaalika Wakorintho “kutaka kuhutubu”? (1 Wakorintho 14:39). Je, ni kwa jinsi gani wewe unaweza kukubali mwaliko huu?

Ona pia Hesabu 11:24–29; Yakobo 4:6–7; Alma 17:3; Mafundisho na Maagano 11:23–28.

1 Wakorintho 14:34–35

Kwa nini Paulo alisema wanawake wanyamaze katika kanisa?

Mafundisho ya Paulo katika 1 Wakorintho 14:34–35 yanaweza kuonekana ya kukanganya, kwani mapema katika waraka huu aliandika kwamba wanawake walisali na kuhutubu (ona 1 Wakorintho 11:5). Tafsiri ya Joseph Smith huchukua nafasi ya neno zungumza katika mistari 34 na 35 kwa neno ongoza. Ufafanuzi huu hupendekeza kwamba Paulo huenda alikuwa akiwaongelea wanawake waliokuwa wakijaribu kujitwalia mamlaka katika mikutano ya Kanisa. (Ona pia 1 Timotheo 2:11–12.)

Ona pia “Wanawake katika Kanisa” Mada za Injili, topics.lds.org.

1 Wakorintho 15:1–34, 53–58

Yesu Kristo alishinda mauti.

Ufufuko wa Yesu Kristo ni muhimu sana kwenye Ukristo, mtu anaweza kusema kwamba bila ufufuko hakuna Ukristo—kwa kutumia maneno ya Paulo, “kuhubiri kwetu ni bure, na imani yenu ni bure” (1 Wakorintho 15:14). Bado baadhi ya Watakatifu wa Korintho walikuwa wakifundisha kwamba hakutakuwepo na “ufufuko wa wafu” (1 Wakorintho 15:12). Unaposoma jibu la Paulo katika 1 Wakorintho 15, chukua muda kidogo kutafakari ni jinsi gani maisha yako yangekuwa tofauti kama usingeamini katika Ufufuko. Je, ni kwa jinsi gani hili limekubariki? Ni baraka zipi zitakuja kwako kwa sababu Yesu Kristo alifufuka? (ona 2 Nefi 9:6–19; Alma 40:19–23; Mafundisho na Maagano 93:33–34). Je, kirai “kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure” kina maana gani kwako? (mstari 17).

1 Wakorintho 15:35–54

Miili iliyofufuka ni tofauti na miili yenye kufa.

Je, umewahi kujiuliza mwili uliofufuka unafananaje? Kulingana na 1 Wakorintho 15:35, baadhi ya Wakorintho walijiuliza jambo kama hilo. Soma jibu la Paulo katika mistari 36–54, na andika maneno na virai ambayo huelezea tofauti kati ya miili yenye kufa na miili iliyofufuka. Kwa mfano, mstari 40–42 hufundisha kwamba miili iliyofufuka itang’ara kwa utukufu katika viwango tofauti, kama vile jua, mwezi, na nyota zinavyotofautiana katika kung’ara (ona pia Tafsiri ya Joseph Smith, 1 Wakorintho 15:40; MM 76:50–112).

Ona pia Alma 11:43–45; Luka 24:39.

mawio

“Kuna fahari moja ya jua” (1 Wakorintho 15:41).

ikoni  ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo:

1 Wakorintho 15:29

Tunajifunza kutoka mstari wa 29 kwamba Watakatifu wa kale walishiriki katika ubatizo wa wafu, kama vile tunavyofanya katika Kanisa leo. Tunaendeleaje kama familia katika kuandaa majina ya mababu zetu kwa ajili ya ibada za hekaluni? Ona pia “Ubatizo kwa niaba ya Wafu” Mada za Injili, topics.lds.org.

1 Wakorintho 15:35–54

Ni vitu au picha gani unazoweza kuonyesha ili kusaidia familia yako kuelewa baadhi ya maneno ambayo Paulo aliyatumia kuelezea jinsi miili yenye kufa ilivyo tofauti na miili iliyofufuka? Kwa mfano, kuonyesha kwa mfano tofauti kati ya kuharibika na kutokuharibika (ona mstari 52–54) unaweza kuonyesha metali iliyopata kutu (kama vile chuma) na metali ambayo haipati kutu (kama vile chuma cha pua). Au unaweza kutofautisha kitu dhaifu na kitu chenye nguvu (ona mstari 43).

1 Wakorintho15:55–57

Majadiliano kuhusu mistari hii yanaweza kuwa ya maana hasa kama familia yako inamjua mtu ambaye amefariki. Wanafamilia wanaweza kutoa shuhuda juu ya jinsi Yesu Kristo anavyoondoa “uchungu wa mauti” (mstari wa 56). Ujumbe wa Mzee Paul V. Johnson “Na Hakutakuwepo Kifo Tena” (Ensign au Liahona, Mei 2016, 121–23) unaweza kuwa nyongeza nzuri kwenye majadiliano yenu.

1 Wakorintho 16:13

Kuwasaidia washiriki wa familia yako kujihusisha na mstari huu, unaweza kuchora duara ardhini na kumuelekeza mwanafamilia “kusimama imara” ndani yake akiwa amezibwa macho wakati wengine wakijaribu kumuondoa kutoka kwenye mduara huo. Je, kuna tofauti gani iliyopo wakati mwanafamila huyo ndani ya duara anapokuwa hajazibwa macho na anaweza “kuangalia”? Je, tunaweza kufanya nini ili “kusimama imara” katika maisha yetu wakati tunapojaribiwa ili tufanye chaguzi mbaya?

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Tafuta mpangilio. Katika maandiko tunapata mpangilio ambao hutuonyesha jinsi Bwana anavyofanya kazi Yake. Ni mpangilio upi unapata katika 1 Wakorintho 14 unaotusaidia kuelewa jinsi ya kufundishana na kurekebishana? Ona pia M&M 50:13–23.

Yesu akimtokea Mariamu kaburini

Mwanamke, Kwa nini Unalia? Na Simon Dewey