“Septemba 12–18. Isaya 13–14; 24–30; 35 “Kazi ya Ajabu na Mwujiza,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022 (2021)
“Septemba 12–18. Isaya 13–14; 24–30; 35,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2022
Septemba 12-18
Isaya 13–14; 24–30;35
“Kazi ya Ajabu na Mwujiza”
Rais Bonnie H. Cordon alifundisha, “Maandiko huangaza akili zetu, hurutubisha roho zetu, hujibu maswali yetu, huongeza imani yetu kwa Bwana, na kutusaidia kuweka maisha yetu Kwake” (“Mtegemee Bwana na Usiegemee,” Liahona, Mei 2017, 7).
Andika Misukumo Yako
Mojawapo ya mambo ambayo Bwana huwaomba manabii kufanya ni kuonya juu ya matokeo ya dhambi. Kwa upande wa manabii wa Agano la Kale, hii mara nyingi ilimaanisha kuwaambia watawala wenye nguvu wa falme kuu kuwa lazima watubu au waangamizwe. Ilikuwa ni kazi ya hatari, lakini Isaya hakuwa na woga, na maonyo yake kwa falme za siku zake—zikiwemo Israeli, Yuda, na mataifa jirani—yalikuwa ya ujasiri (ona Isaya 12–23).
Hata hivyo, Isaya pia alikuwa na ujumbe wa matumaini. Ijapokuwa uharibifu uliotabiriwa mwishowe ulikuja juu ya falme hizi, Isaya aliona nafasi ya urejesho na kufanywa upya. Bwana angewaalika watu Wake warudi Kwake. Angefanya “mchanga ung’aao … utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji” (Isaya 35:7). Angefanya “kazi ya ajabu na mwujiza” (Isaya 29:14), kurejesha kwa Israeli baraka ambazo Yeye aliwaahidi. Si Isaya wala mtu yeyote aliye hai kwa wakati huo aliishi kuona kazi hii ya ajabu. Lakini tunaona utimilifu wake wa mwisho leo. Hakika, sisi ni sehemu yake!
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Falme mbaya za ulimwengu na watawala wao wataanguka.
Isaya 13–14 inaitwa “mzigo wa” (ujumbe wa unabii kuhusu) Babeli (Isaya 13:1). Uliokuwa ufalme wenye nguvu ukiwa na mtawala mwenye nguvu, Babeli sasa inachukuliwa kama historia ya zamani. Kwa nini basi ujumbe kwa Babeli ni muhimu kwetu leo? Katika maandiko, Babeli inaashiria kiburi, ulimwengu, na dhambi, na leo tumezungukwa na haya yote. Fikiria kuhusu ishara hii unaposoma Isaya 13:1–11, 19–22; 14:1–20. Unaweza pia kufikiria maswali kama haya:
-
Je! Maonyo ya Isaya kwa Babeli yanafananaje na unabii kuhusu ulimwengu kabla ya Ujio wa Pili wa Mwokozi? (ona Alma 13:1–11; Mafundisho na Maagano 45:26–42).
-
Je! Ni kufanana gani unakokuona kati ya kiburi cha mfalme wa Babeli na kiburi cha Shetani? (ona Isaya 14:4–20; Musa 4:1–4). Ni maonyo gani unayapata kwa ajili yako katika mistari hii?
-
Je! Mwokozi hutoaje “raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako”? (Isaya 14:3).
Isaya 24:21–23; 25:6–8; 26:19; 28:16
Maandishi ya Isaya yananielekeza kwa Yesu Kristo.
Mafundisho ya Isaya mara nyingi yanarejea huduma ya Mwokozi, pamoja na dhabihu Yake ya upatanisho, Ufufuo, na Ujio wa Pili. Ni mambo gani ya huduma Yake yanayokuja akilini unaposoma mistari ifuatayo: Isaya 24:21–23; 25:6–8; 26:19; 28:16? Je! Ni vifungu vipi vingine ambavyo vinakukumbusha juu ya Mwokozi?
Ona pia Isaya 22:22–25.
Isaya 24:1–12; 28:7–8; 29:7–10; 30:8–14
Ukengeufu unamaanisha kugeuka kutoka kwa Bwana na injili Yake.
Kuonya juu ya matokeo ya kugeuka kutoka kwa Bwana na kuwakataa manabii Wake, Isaya alitumia mifano mbali mbali. Hii ni pamoja na dunia tupu (Isaya 24:1–12), ulevi (Isaya 28:7–8), njaa na kiu (Isaya 29:7–10), na ukuta au chombo kilichovunjika (Isaya 30:8–14). Kutokana na yale uliyoyasoma katika mistari hii, kwa nini ni muhimu kutii maagano yetu? Fikiria yale unayoyafanya ili kubaki mkweli kwa Bwana na watumishi Wake.
Ona pia M. Russell Ballard, “Kaa kwenye Mashua na Shikilia!” Liahona, Nov. 2014, 89–92; Mada za Injili, “Ukengeufu,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
Bwana anaweza kurejesha vitu ambavyo vilipotea au kuvunjika.
Wakati watu au jamii zinapogeuka kutoka kwa Bwana, Shetani anataka tufikirie kuwa matokeo hayawezi kurekebishwa. Walakini, Isaya alielezea mambo mazuri ambayo Bwana atayafanya wakati watu watakapotubu na kumrudia Yeye. Unajifunza nini kutoka katika Isaya 29:13–24; 30:18 –26;35 kumhusu Bwana, upendo Wake, na nguvu Zake?
Njia moja Bwana ameonyesha nguvu Zake katika siku zetu ni kupitia Urejesho wa injili Yake. Isaya 29 inajumuisha vifungu kadhaa ambavyo vina kwenda sambamba na matukio ya Urejesho huo. Kwa mfano:
-
Linganisha Isaya 29:11–12 na 2 Nefi 27:6–26 na Joseph Smith—Historia 1:63–65.
-
Linganisha Isaya 29:13–14 na Mafundisho na Maagano 4 na Joseph Smith—Historia 1:17–19.
-
Linganisha Isaya 29:18–24 na ukurasa wa Jina wa Kitabu cha Mormoni.
Je! Una mawazo gani au maoni gani juu ya Urejesho wa injili unaposoma vifungu hivi?
Ona pia “The Restoration of the Fulness of the Gospel of Jesus Christ: A Bicentennial Proclamation to the World” (ChurchofJesusChrist.org).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Isaya 25:4–9.Je! Familia yako imewahi kupata baraka ya mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, Kivuli wakati wa hari? (ona mstari wa 4). Ongea kuhusu ya hili unaposoma mistari hii na maelezo mengine ya Bwana yanayopatikana katika Isaya 25:4–9. Ni kwa jinsi gani Bwana ni kama vitu hivi?
-
Isaya 25:8–9; 26:19.Kuonyesha picha za Mwokozi huko Gethsemane, msalabani, na baada ya Ufufuo Wake inaweza kuisaidia familia yako kuona uhusiano kati ya aya hizi na Yesu Kristo (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 56, 57, 58,59). Alika familia yako kushiriki kwa nini “wanafurahia wokovu wake” (Isaya 25:9).
-
Isaya 29:11–18.Mistari hii inaweza kuisaidia familia yako kujadili “kazi ya ajabu na mwujiza” (mstari wa 14) ya Urejesho wa injili na kuja kwa Kitabu cha Mormoni. Kwa nini mambo haya ni ajabu na mwujiza kwetu? Waalike wanafamilia kutafuta kitu katika nyumba yenu kinachowakilisha baraka za ajabu za Urejesho.
-
Isaya 35.Familia yako inaweza kufurahia kuchora picha za michoro katika sura hii ambazo zinatusaidia kuelewa jinsi Yesu Kristo anavyoijenga Sayuni katika siku zetu. Tunajifunza nini kutoka katika michoro hii? Tunaweza kufanya nini ili kusaidia kujenga Sayuni?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “On a Golden Springtime,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 88.