Mafundisho na Maagano 2021
Aprili 26–Mei 2. Mafundisho na Maagano 45: “Ahadi … Zitatimizwa”


“Aprili 26–Mei 2. Mafundisho na Maagano 45: ‘Ahadi … Zitatimizwa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Aprili 26–Mei 2. Mafundisho na Maagano 45,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021

vijana nje ya hekalu

Aprili 26–Mei 2

Mafundisho na Maagano 45

“Ahadi … Zitatimizwa”

Kama mwalimu, maandalizi yako ya muhimu sana ni ya kiroho. Anza kwa kujifunza Mafundisho na Maagano 45 na kusali kwa ajili ya mwongozo wa Roho Mtakatifu. Muhtasari huu unatoa mawazo ambayo yanaweza kuwa ya msaada kwako. Unaweza pia kupata mawazo katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia au kwenye Liahona au Friend.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Waulize watoto kama wangependa kushiriki kitu fulani walichojifunza kutoka kwenye maandiko wiki hii. Chagua mtu wa kushiriki, na waombe watoto wengine kuinua mikono yao kama walijifunza kuhusu kitu kinachofanana na hicho.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Mafundisho na Maagano 45:32

Ninaweza “Kusimama katika mahali patakatifu.”

Katika Mafundisho na Maagano 45:32, Bwana alifundisha kwamba wafuasi Wake watapata usalama katika siku za mwisho kwa kusimama katika mahali patakatifu—mahali palipo maalumu kwa Bwana. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kutambua mahali palipo patakatifu katika maisha yao?

Shughuli Yamkini

  • Weka picha za nyumba, jengo la kanisa, na hekalu, katika sehemu tofauti chumba kizima. Wape vidokezo vinavyoelezea sehemu hizi, na waalike watoto kusimama karibu na picha unayoielezea. Soma mstari wa kwanza kutoka Mafundisho na Maagano 45:32. Shuhudia kwamba tunabarikiwa tunapotumia muda katika mahali patakatifu kama nyumbani mwetu, kwenye majengo ya makanisa yetu, na hekaluni. Waombe watoto wazungumzie kuhusu jinsi wanavyohisi wanapokuwa katika mahali patakatifu kama maeneo haya.

  • Waalike watoto kukamilisha ukurasa wa shughuli ya wiki hii. Wasaidie kuandika “Ninaweza kusaidia nyumbani kwangu kuwa mahali patakatifu” na “Mafundisho na Maagano 45:32” kwenye mchoro wao. Wanaweza kufanya nini kusaidia nyumba zao kuwa mahali patakatifu?

  • Kuwasaidia watoto kufikiria kuhusu nini inamaanisha “kutoondoshwa,” watake kusimama kimya bila kusogea kwa dakika moja. Soma mstari wa kwanza kutoka Mafundisho na Maagano 45:32. Wasaidie watoto kuelewa kwamba “kusimama katika mahali patakatifu, na … kutoondoshwa” inamaanisha kuchagua mema wakati wote, bila kujali nini kinatokea. Watake “kutoondoshwa” mbali kutoka kwenye mawazo na vitendo vyenye uadilifu.

Mafundisho na Maagano 45:44–45

Yesu Kristo atakuja tena.

Wakati Watakatifu huko Kirtland, Ohio, waliposikia ufunuo unaopatikana katika Mafundisho na Maagano 45, unaozungumzia juu ya siku za mwisho na Ujio wa Pili wa Mwokozi, waliupokea kwa shangwe. Fikiria jinsi utakavyowasaidia watoto kujiandaa kwa furaha kwa ajili ya Ujio wa Pili.

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto kufikiria kuhusu jinsi wanavyohisi wakati wanapojua kwamba mtu fulani maalum anakuja kuwatembelea, kama vile babu au rafiki. Ni kwa jinsi gani wanajiandaa kwa ajili ya ziara? Onesha picha ya Mwokozi, na soma sehemu moja au yote ya Mafundisho na Maagano 45:44–45. Waambie watoto jinsi unavyohisi kuhusu Mwokozi kuja tena, na waruhusu washiriki hisia zao.

  • Onesha picha ya Ujio wa Pili wa Mwokozi (ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia), na waombe watoto kushiriki kile wanachohisi wanapoiona picha. Shiriki ushuhuda wako kwamba Yesu Kristo atakuja tena.

  • Imbeni wimbo kuhusu Ujio wa Pili wa Mwokozi, kama vile “When He Comes Again” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 82–83). Tumia wimbo kujadili njia tunazoweza kujiandaa kwa ujio mwingine wa Yesu, kama vile kwa kufanya mapenzi ya Mungu na kuacha nuru yetu iangaze kwa ajili ya wengine.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Mafundisho na Maagano 45:3–5

Yesu Kristo ndiye Mtetezi Wetu kwa Baba.

Ni kwa jinsi gani utawasaidia watoto kuimarisha imani yao kwamba Yesu Kristo ni Mtetezi wao? Ni kwa jinsi gani umejifunza hili kwa ajili yako mwenyewe?

Shughuli Yamkini

  • Andika maneno kadhaa na virai vinavyopatikana katika Mafundisho na Maagano 45:3–5 kwenye vipande tofauti vya karatasi. Wape watoto dakika moja ya kusoma mistari hii katika maandiko yao, na kisha watake kufunga maandiko yao na kuandika maneno kwenye karatasi kwa mpangilio wa jinsi yanavyotokea katika mstari. Kulingana na mistari hii, Mwokozi anasema nini ili kutetea kusudi letu mbele ya Baba wa Mbinguni?

  • Wasaidie watoto kufafanua neno mtetezi, labda kwa kulitafuta katika kamusi. Mwokozi alifanya nini kilichofanya iwezekane Kwake kuwa Mtetezi wetu? Shiriki hisia zako kuhusu kile Yesu Kristo alichokifanya kwa ajili yetu, na waruhusu watoto kushiriki hisia zao.

Mafundisho na Maagano 45:9

Injili ya Yesu Kristo ni nuru ya ulimwengu.

Wasaidie watoto unaowafundisha wafikirie njia ambazo injili inaandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi.

Shughuli Yamkini

  • Onesha picha za nuru na bendera, au chora vitu hivi ubaoni. Waalike watoto wasome Mafundisho na Maagano 45:9 na kufikiria juu ya jinsi injili ilivyo kama nuru, ishara (au bendera), na ujumbe. Unaweza kuelezea kwamba hapo zamani, ishara ilikuwa ni bango au bendera iliyochukuliwa kwenye mapambano. Iliwasaidia askari kujua wapi pa kukusanyika na nini cha kufanya.

    Kapteni Moroni akishikilia Bendera ya Uhuru

    Bendera ya Uhuru, na Larry Conrad Winborg

  • Wasaidie watoto kukariri wote au sehemu ya mstari wa 9 kwa kuuandika ubaoni na kufuta maneno machache kwa wakati.

Mafundisho na Maagano 45:37–38

Yesu Kristo atakuja tena.

Inaweza kuwa ya kutisha kwa watoto kusoma kuhusu vita, uovu, na uharibifu vilivyotabiriwa kutokea kabla ya Ujio wa Pili wa Mwokozi. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia kungojea kwa shangwe siku hii iliyoahidiwa?

Shughuli Yamkini

  • Waulize watoto jinsi wanavyojua wakati majira mapya yanapokaribia. Ni ishara gani wanazitazamia? Elezea kwamba kama zilivyo ishara za majira mapya, kuna ishara za Ujio wa Pili. Someni pamoja Mafundisho na Maagano 45:37–38. Yesu alisema ishara za Ujio Wake wa Pili zingekuwaje? Ili kuwasaidia watoto kugundua ishara tunazopaswa kutafuta, mpangie kila mtoto (au kikundi cha watoto) kusoma mistari michache kutoka Mafundisho na Maagano 45 ambayo inaelezea ishara hizi. Mistari 26–27, 31–33, 40–42 ingeweza kutumika, kwa mfano. Waruhusu watoto washiriki kile wanachokipata. Zipi kati ya ishara hizi zinatimizwa leo?

  • Kwenye vipande tofauti vya karatasi , andika baadhi ya ahadi kuhusu matukio yajayo ambazo ulizipata katika kujifunza kwako sehemu ya 45. Baadhi ya mifano ya ahadi hizi inaweza kupatikana katika mistari ya 44–45, 51–52, 55, 58–59, 66–71. Orodhesha ubaoni mistari ambapo ahadi zinapatikana. Wape watoto karatasi, na waombe kutumia maandiko yao kufananisha mistari iliyo ubaoni pamoja na ahadi. Jadili maana ya ahadi hizi, na waalike watoto kushiriki ahadi zinazowasaidia kuhisi msisimko kuhusu Ujio wa Pili wa Mwokozi.

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Waalike watoto kufikiria juu ya kitu kimoja walichojifunza wakati wa darasa ambacho wanaweza kushiriki pamoja na familia zao. Waombe baadhi yao kushiriki pamoja na darasa kile wanachotaka kushiriki nyumbani.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Wasaidie watoto kumtambua Roho. Unapowafundisha watoto, waambie wakati unapomhisi Roho Mtakatifu. Zungumza kuhusu jinsi unavyotambua uwepo Wake. Kwa mfano, unaweza kuhisi kuwa na amani au mwenye furaha wakati unapoimba wimbo kuhusu Mwokozi. Kutambua hisia hizi kutawasaidia watoto kufahamu wakati wanapomhisi Roho.