Miito ya Misheni
Sura ya 5: Tumia Nguvu ya Kitabu cha Mormoni


“Sura ya 5: Tumia Nguvu ya Kitabu cha Mormoni,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 5,” Hubiri Injili Yangu

Yesu Akifundisha katika Nusutufe ya Kusini (Yesu Kristo Anazuru Amerika), na John Scott

Sura ya 5

Tumia Nguvu ya Kitabu cha Mormoni

Zingatia Hili

  • Ni kwa jinsi gani Kitabu cha Mormoni ni jiwe la katikati la tao la dini yetu?

  • Je, ni kwa nini Kitabu cha Mormoni kina nguvu zaidi katika mchakato wa uongofu?

  • Je, Kitabu cha Mormoni kinafundisha nini kuhusu Yesu Kristo?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kutumia Kitabu cha Mormoni ili kujisaidia mwenyewe na kuwasaidia wengine wasonge karibu na Mungu?

  • Ni kwa jinsi gani Kitabu cha Mormoni hutatua maswali ya nafsi?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwasaidia watu wasome na wapate ushuhuda juu ya Kitabu cha Mormoni?

Kitabu cha Mormoni, kikiunganishwa na Roho, ni nyenzo yako yenye nguvu zaidi katika uongofu. Kitabu hiki ni kumbukumbu takatifu ya kale iliyoandikwa ili kuwathibitishia watu wote kwamba Yesu ndiye Kristo (ona ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni). Kama kichwa kidogo cha jina kisemavyo, Kitabu cha Mormoni ni “ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo.” Pia ni ushahidi wa kuvutia kwamba Mungu alimwita Joseph Smith kama nabii na alirejesha injili ya Yesu Kristo kupitia yeye.

lango la tao na jiwe la katikati la tao

Kitabu cha Mormoni ni Jiwe la Katikati la Tao la Dini Yetu

Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba Kitabu cha Mormoni ni “jiwe la katika la tao la dini yetu” (dibaji ya Kitabu cha Mormoni). Nabii Joseph pia alitangaza: “Toa Kitabu cha Mormoni na ufunuo, je dini yetu iko wapi? Hatuna chochote” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 196).

Tao ni umbo imara la usanifu wa majengo lililotengenezwa kwa vipande vyenye umbo la kabari vinavyoegemeana. Kipande cha katikati, au jiwe la katikati la tao, kwa kawaida ni kubwa kuliko kabari zingine na huzishikilia pamoja.

Rais Ezra Taft Benson alisema Kitabu cha Mormoni ni jiwe la katika la tao la dini yetu kwenye angalau njia tatu:

Ushahidi wa Kristo. “Kitabu cha Mormoni ni jiwe la katikati la tao katika ushahidi wetu juu ya Yesu Kristo, ambaye Yeye mwenyewe ndiye jiwe la pembeni la kila kitu tunachofanya. Kinatoa ushahidi wa uhalisia Wake kwa nguvu na uwazi.”

Utimilifu wa mafundisho. “Bwana Mwenyewe amenena kwamba Kitabu cha Mormoni kina ‘utimilifu wa injili ya Yesu Kristo’ [Mafundisho na Maagano 20:9; 27:5]. … Katika Kitabu cha Mormoni tutapata utimilifu wa [mafundisho] yanayohitajika kwa ajili ya wokovu wetu. Na yamefundishwa kwa uwazi na urahisi ili kwamba hata watoto waweze kujifunza njia za wokovu na kuinuliwa.

Msingi wa ushuhuda. “Kama vile tao linavyodondoka ikiwa jiwe la katikati la tao litaondolewa, vivyo hivyo Kanisa lote litasimama au kuanguka kwa ukweli wa Kitabu cha Mormoni. … Kama Kitabu cha Mormoni ni cha kweli … basi mtu sharti akubali madai ya Urejesho.” (Teachings of Presidents of the Church: Ezra Taft Benson [2014], 129, 131128.)

Kwa kupata ushuhuda kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu, tunaweza kujua kwamba Joseph Smith alikuwa nabii. Kupitia yeye, mamlaka ya ukuhani wa Mungu yalirejeshwa na wajumbe wa mbinguni. Mungu pia alimwidhinisha Joseph aanzishe Kanisa la Yesu Kristo. Ufunuo unaendelea leo kupitia manabii walio hai.

mvulana akisoma maandiko

Kitabu cha Mormoni ni Muhimu kwa Uongofu Binafsi

Sehemu muhimu ya uongofu ni kupokea ushahidi kwa njia ya Roho Mtakatifu kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Unapokisoma na kujifunza kwa uaminifu, utahisi maneno yake yakiikuza nafsi yako. Maneno yake yataangaza uelewa wako wa maisha, mpango wa Mungu, na wa Yesu Kristo (ona Mafundisho na Maagano 32:28.). Sali kuhusu kitabu hiki kwa kusudi halisi na imani katika Kristo. Unapofanya hivyo, utapokea ushahidi kupitia Roho Mtakatifu kwamba ni neno la Mungu (ona Moroni 10:4–5).

Ushuhuda wako mwenyewe juu ya Kitabu cha Mormoni unaongoza hadi kwenye imani ya kina na ya kudumu katika nguvu zake za kuwasaidia wengine wawe waongofu. Wasaidie watu unaowafundisha watambue mwangaza wanaouona pale wanapokisoma kwa uaminifu. Sisitiza ushahidi wake wenye nguvu juu ya Yesu Kristo. Wahimize wasali ili wapokee ushahidi wao wenyewe kwamba kitabu hiki ni cha kweli.

Kuwahimiza watu watafute ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu Kitabu cha Mormoni kunapaswa kuwa kiini cha fokasi ya kufundisha kwako. Kitabu cha Mormoni kinaweza kubadilisha maisha yao milele.

Tumia Kitabu cha Mormoni Kufundisha Injili ya Yesu Kristo

Nabii Joseph Smith alisema, “Kitabu cha Mormoni [ni] kitabu sahihi zaidi kuliko kitabu chochote ulimwenguni” (dibaji ya Kitabu cha Mormoni). Kinashuhudia juu ya Kristo na kwa uwazi kinafundisha mafundisho Yake (ona 2 Nefi 31; 32:1–6; 3 Nefi 11:31–39; 27:13–22). Kinafundisha utimilifu wa injili Yake. Kanuni na ibada za kwanza za injili kama zinavyofundishwa katika Kitabu cha Mormoni ndiyo njia iongozayo kwenye maisha ya baraka.

Tumia Kitabu cha Mormoni kama chanzo chako muhimu kwa ajili ya kufundisha injili ya urejesho. Chati ifuatayo imeorodhesha baadhi ya kweli zilizomo ndani ya Kitabu cha Mormoni ambazo utaweza kufundisha.

Somo la Mmisionari katika Sura ya 3

Mafundisho

Marejeleo

Somo la Mmisionari katika Sura ya 3

Ujumbe wa Urejesho wa Injili ya Yesu Kristo

Mafundisho

Asili ya Mungu, huduma ya Mwokozi na Upatanisho, ukengeufu, Urejesho, Joseph Smith, mamlaka ya ukuhani

Marejeleo

1 Nefi 12–14

2 Nefi 3; 26–29

Mosia 2–5

Somo la Mmisionari katika Sura ya 3

Mpango wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni

Mafundisho

“Mpango mkuu wa Mungu wa Milele,” ikiwa ni pamoja na Anguko la Adamu na Hawa, Upatanisho wa Yesu Kristo, Ufufuko, na Hukumu

Marejeleo

2 Nefi 29

Mosia 3; 15–16

Alma 12; 34:9; 40–42

Somo la Mmisionari katika Sura ya 3

Injili ya Yesu Kristo

Mafundisho

Imani katika Kristo, toba, ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho

Marejeleo

2 Nefi 31–32

3 Nefi 11; 27:13–22

Somo la Mmisionari katika Sura ya 3

Kuwa Wafuasi wa Yesu Kristo kwa Maisha Yote

Mafundisho

Ibada kama ubatizo, kutawazwa katika ukuhani, na sakramenti

Marejeleo

3 Nefi 11:22–28;18

Moroni 2–6

Kujifunza Maandiko

Je, Mwokozi anasema nini kuhusu Kitabu cha Mormoni?

Kitabu cha Mormoni Kinamshuhudia Kristo

Dhumuni muhimu la Kitabu cha Mormoni ni kushuhudia juu ya Yesu Kristo. Kinathibitisha uhalisia wa maisha Yake, misheni, ufufuko, na nguvu Zake. Kinafundisha mafundisho ya kweli kuhusu Kristo na Upatanisho Wake.

Manabii kadhaa ambao maandishi yao yamehifadhiwa katika Kitabu cha Mormoni walimwona Kristo kwa macho yao. Kaka wa Yaredi, Nefi, na Yakobo walimwona Kristo kabla ya kuzaliwa kwake. Makutano ya watu walikuwepo wakati wa huduma ya Mwokozi miongoni mwa Wanefi (ona 3 Nefi 11–28). Baadaye, Mormoni na Moroni walimwona Kristo aliyefufuka (ona Mormoni 1:15; Etheri 12:39).

Watu wanaposoma na kusali kuhusu Kitabu cha Mormoni, watakuja kumjua Mwokozi vyema na kupata uzoefu wa upendo Wake. Watakua katika ushuhuda wao juu Yake. Watajua jinsi ya kuja Kwake na kuokolewa. (Ona 1 Nefi 15:14–15.)

Rais Russell M. Nelson

“Kitabu cha Mormoni kinatoa uelewa kamili na wenye mamlaka zaidi juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo kuliko unavyoweza kupatikana sehemu nyingine yoyote. Kinafundisha kile hasa inachomaanisha kuzaliwa upya. … Sisi tunajua ni kwa nini tupo hapa duniani. Kweli hizi na zingine zimefundishwa kwa nguvu zaidi na kwa ushawishi zaidi katika Kitabu cha Mormoni kuliko kwenye kitabu kingine chochote. Nguvu kamili ya injili ya Yesu Kristo iko ndani ya Kitabu cha Mormoni (Russell M. Nelson, “Kitabu cha Mormoni: Maisha Yako Yangekuwaje Bila Hicho?Liahona, Nov. 2017, 62).

Kujifunza Binafsi

Kote katika misheni yako, andika majibu kwa maswali yafuatayo katika shajara yako ya kujifunzia:

  • Je, umejifundisha nini kumhusu Yesu Kristo kutokana na kijifunza kwako Kitabu cha Mormoni?

  • Ni kwa jinsi gani kujifunza Kitabu cha Mormoni kumeshawishi ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo?

  • Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia Kitabu cha Mormoni ili kuwasaidia watu waimarishe shuhuda zao?

Kujifunza Maandiko

Ni sababu zipi manabii wa Kitabu cha Mormoni walitoa kwa ajili ya kuandika kumbukumbu zao?

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Kitabu cha Mormoni kimeandikwa “kuwathibitishia [watu wote] kwamba Yesu Ndiye Kristo” (ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni). Jedwali lifuatalo linaorodhesha baadhi ya sura za Kitabu cha Mormoni ambazo zinashuhudia juu ya maisha, mafundisho, na huduma ya Yesu Kristo. Chagua vifungu vya kujifunza kote katika misheni yako.

Kwa nyongeza, fikiria kuhusu mahitaji ya watu unaowafundisha. Fanya mipango ya kusoma vifungu hivi pamoja nao ili kuimarisha maarifa na ushuhuda wao juu ya Mwokozi.

Ukurasa wa jina na dibaji

Eleza wazi dhumuni la kitabu hiki.

1 Nefi 10–11

Lehi na Nefi wanashuhudia juu ya Kristo.

2 Nefi 29

Lehi na Yakobo wanashuhudia juu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

2 Nefi 31–33

Nefi anafundisha mafundisho ya Kristo.

Mosia 2–5

Mfalme Benjamini anashuhudia juu ya Kristo.

Alma 57

Alma anashuhudia juu ya Mwokozi.

Alma 36

Alma anapata uzoefu wa nguvu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi.

3 Nefi 9–10

Mwokozi anawaalika watu waje Kwake.

3 Nefi 11–18

Mwokozi anawafundisha Wanefi juu ya Baba na mafundisho Yake.

3 Nefi 27

Mwokozi anafundisha injili Yake.

Etheri 12

Etheri na Moroni wanafundisha kwamba imani katika Yesu Kristo ni kanuni ya matendo na nguvu.

Moroni 7–8

Mormoni anafundisha juu ya upendo halisi wa Kristo na Upatanisho Wake.

Moroni 10

Moroni anawaalika wote waje kwa Kristo na kukamilishwa katika Yeye.

Kitabu cha Mormoni Hutusaidia Sisi Tusonge Karibu Zaidi na Mungu

Kuhusu Kitabu cha Mormoni, Nabii Joseph Smith alisema kwamba “mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafundisho yake, kuliko kitabu kingine” (dibaji ya Kitabu cha Mormoni). Kwa kuwafundisha watu kila mara na kuwaalika waishi kanuni za Kitabu cha Mormoni, unawasaidia wakuze imani katika Yesu Kristo na wakaribie zaidi kwa Mungu.

Kitabu cha Mormoni hujenga ushuhuda na hualika ufunuo binafsi. Tumia Kitabu cha Mormoni ili kuwasaidia watu wapate uzoefu wa kiroho, hasa ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu kwamba kitabu chenyewe ni neno la Mungu.

Vipe kipaumbele vifungu vya Kitabu cha Mormoni wakati unapofundisha. Vina nguvu ya kuongoa kupitia Roho Mtakatifu. Unapofundisha injili ukitumia Kitabu cha Mormoni, kufundisha kwako kutavuma kwa nguvu na uwazi katika moyo na akili.

Rais Gordon B. Hinckley alifundisha kwamba “wale waliosoma [Kitabu cha Mormoni] kwa sala, wawe ni matajiri au masikini, wasomi au wasio wasomi, wamekua chini ya nguvu zake. Aliendelea kufundisha:

“Bila kusita ninawaahidi kwamba kama mtakisoma Kitabu cha Mormoni kwa sala, bila kujali ni mara ngapi mmekisoma hapo awali, kutakuja katika mioyo yenu ongezeko la Roho wa Bwana. Kutakuja mwamko ulioimarishwa wa kutembea katika utiifu kwa amri zake, na kutakuja ushuhuda wenye nguvu zaidi wa uhalisia wa uhai wa Mwana wa Mungu” (Nguvu ya Kitabu cha Mormoni; Ensign, Juni 1988, 6).

wamisionari wakisoma maandiko

Kitabu cha Mormoni Hujibu Maswali ya Nafsi

Kusoma Kitabu cha Mormoni kwa mwongozo wa Roho kunaweza kuwasaidia watu wapate majibu au umaizi kwa maswali yao binafsi—au maswali ya nafsi. Wasaidie watu waone jinsi ambavyo mafundisho katika Kitabu cha Mormoni hujibu maswali ya maisha.

Baadhi ya maswali haya yameorodheshwa hapo chini, pamoja na marejeleo ya Kitabu cha Mormoni ambayo yanayajibu.

Kitabu cha Mormoni pia hutoa mwongozo kuhusu maswali mengine yaliyo muhimu, kama vile:

Rais Dallin H. Oaks

“Wamisionari lazima wajue jinsi ya kutumia Kitabu cha Mormoni ili kujibu maswali yao wenyewe ili waweze kukitumia kwa ufanisi zaidi kuwasaidia wengine wajifunze kufanya vivyo hivyo. … Wao lazima waunganishe nguvu ya Kitabu cha Mormoni katika kufundisha injili ya iliyorejeshwa, kwanza kwa kukitumia katika maisha yao wenyewe na kisha kukishiriki pamoja na wale wanaowafundisha” (Dallin H. Oaks, “Counsel for Mission Leaders,” seminar for new mission leaders, June 25, 2022).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Orodhesha maswali ya nafsi ambayo unayo au umeyasikia kutoka kwa wengine. Tafuta mistari katika Kitabu cha Mormoni ambayo inasaidia kujibu maswali haya. Andika umaizi na marejeleo ya Kitabu cha Mormoni katika shajara yako ya kujifunzia. Yatumie unapofundisha.

Kitabu cha Mormoni na Biblia Husaidiana

Bwana alisema “fundisha kanuni za injili yangu, ambazo ziko kwenye Biblia na Kitabu cha Mormoni, ambamo kuna utimilifu wa Injili” (Mafundisho na Maagano 42:12). Watakatifu wa Siku za Mwisho, “wanaamini Biblia kuwa ni neno la Mungu ilimradi imetafsiriwa kwa usahihi” (Makala ya Imani 1:8; ona pia 1 Nefi 13:29). Biblia ni maandiko matakatifu. Kitabu cha Mormoni ni maandiko mwenza matakatifu ambayo yana utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.

Kitabu cha Mormoni na Biblia vinakamilishana na kustawishana (ona Ezekieli 37:16–17; 1 Nefi 13:40; Mormoni 7:8–9). Juzuu zote za maandiko ni makusanyo ya mafundisho yaliyoandikwa na manabii wa kale. Biblia husimulia mwingiliano wa Mungu na watu katika nusutufe ya Mashariki kwa maelfu ya miaka. Kitabu cha Mormoni husimulia mwingiliano wa Mungu na watu katika mabara ya Amerika ya kale kwa zaidi ya miaka elfu moja.

mtu akiweka alama kwenye maandiko

Cha muhimu zaidi, Biblia na Kitabu cha Mormoni vinakamilishana katika kushuhuda juu ya Yesu Kristo. Biblia hutoa maelezo ya kuzaliwa kwa Mwokozi, huduma ya duniani, na Upatanisho—ikijumuisha kifo Chake na Ufufuko. Kitabu cha Mormoni hujumuisha unabii wa kuzaliwa na misheni ya Mwokozi, mafundisho kuhusu Upatanisho Wake, na maelezo ya huduma Yake katika mabara ya Amerika. Kitabu cha Mormoni kinathibitisha na kufafanua ushuhuda wa Biblia kwamba Yesu ndiye Mwana Mpendwa wa Pekee wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu.

Vyote Biblia na Kitabu cha Mormoni vinafundisha sheria ya mashahidi: “Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa” (2 Wakorintho 13:1; ona pia 2 Nefi 11:2–3). Sambamba na sheria hii, vitabu vyote vya maandiko vinashuhudia juu ya Yesu Kristo (ona 2 Nefi 29:8).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Tafuta marejeleo mtambuka juu ya mada zifuatazo katika Kitabu cha Mormoni na Biblia. Mifano imetolewa katika mabano baada ya kila mada. Ongeza mada zako na vifungu vyako mwenyewe.

Wasaidie Watu Wasome na Waelewe Kitabu cha Mormoni

Wale ambao hawasomi au hawaelewi Kitabu cha Mormoni watakuwa na ugumu wa kupokea ushahidi kwamba ni cha kweli. Unaweza kuwasaidia waelewe kitabu hiki kwa kukisoma pamoja nao. Soma wakati wa miadi ya kufundisha, wakati wa matembezi ya kufuatilia, au kupitia teknolojia. Unaweza pia kupanga waumini wasome pamoja nao. Kutazama video ya Kitabu cha Mormoni na kisha kusoma sura husika kunaweza kuwa msaada mkubwa sana.

Sali kwa ajili ya msaada unapochagua vifungu ambavyo vinajibu wasiwasi na mahitaji ya watu. Soma na jadili vifungu vifupi, kama vile 1 Nefi 3:7 au Mosia 2:17. Pia soma na jadili vifungu virefu au sura nzima, kama vile 2 Nefi 31, Alma 7, au 3 Nefi 18. Wahimize watu wasome Kitabu cha Mormoni kuanzia mwanzo, ikijumuisha shuhuda za mashahidi Watatu na Mashahidi Wanane na ushuhuda wa Nabii Joseph Smith.

darasa la shule ya jumapili

Zingatia mapendekezo yafuatayo unaposoma Kitabu cha Mormoni pamoja na watu:

  • Sali kabla ya kusoma. Omba msaada katika kuelewa. Sali kwamba Roho Mtakatifu awashuhudie wao kwamba ni cha kweli.

  • Someni kwa zamu. Nenda kwa kasi ambayo wanaona kuwa ni sawa. Elezea maneno na vishazi visivyofahamika.

  • Pumzika kidogo mara kwa mara ili kujadili kile mnachosoma.

  • Eleza historia na muktadha wa kifungu, kama vile nani anazungumza, mtu huyu yuko vipi, na hali ikoje. Kama kuna video ya Kitabu cha Mormoni, fikiria kuionesha.

  • Taja jumbe au mafundisho muhimu ya kutafuta.

  • Toa ushuhuda wako na utambuzi sahihi, hisia, na uzoefu binafsi.

  • Fundisha mafundisho moja kwa moja kutoka kwenye maneno ya manabii wa Kitabu cha Mormoni. Hii itawasaidia watu wahisi nguvu za kiroho za kitabu hiki.

  • Wasaidie watu “walinganishe” kile ambacho wamesoma na maisha yao wenyewe (1 Nefi 19:23). Wasaidie waone jinsi gani maandiko yanavyohusiana na wao binafsi.

Unapotumia kanuni hizi, utawasaidia watu wakuze uwezo na hamu ya kusoma Kitabu cha Mormoni wao wenyewe. Sisitiza kwamba kusoma kitabu hiki kila siku ni muhimu katika kupiga hatua kwenye ubatizo na uongofu wa maisha yote.

Tegemea ahadi iliyopo katika Moroni 10:3–5. Wahimize watu wasome Kitabu cha Mormoni kwa moyo wa dhati, na kusali kwa kusudi halisi ili wajue kama ni cha kweli. Eleza kwamba kusudi halisi humaanisha kuwa radhi kutenda juu ya jibu wanalopokea kupitia Roho Mtakatifu. Kila mtu ambaye anasoma na kusali kwa kusudi halisi kuhusu Kitabu cha Mormoni anaweza kujua ukweli wake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Unapaswa pia kutumia ahadi hii kila mara ili kuimarisha ushuhuda wako wewe mwenyewe juu ya Kitabu cha Mormoni. Ushuhuda wako utakupa kujiamini kwamba wale ambao wanatumia ahadi hii watapokea ushahidi kwamba kitabu hiki ni neno la Mungu.


Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kutumia

Kujifunza Binafsi

  • Soma 2 Nefi 2; 9; 30; 3132. Wekea alama kila rejeleo la Yesu Kristo. Tengeneza orodha ya majina na vyeo tofauti vya Kristo katika sura hizi. Wekea alama maneno Yake aliyoyazungumza. Wekea alama sifa na matendo Yake.

  • Unaposoma kila siku kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, andika katika shajara yako ya kujifunzia vifungu ambavyo vina maana maalum kwako. Andika jinsi utakavyo vitumia katika maisha yako.

  • Andika katika shajara yako jinsi ambavyo ulihisi mara ya kwanza ulipopata ushahidi wa kiroho kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli.

  • Andika maswali matatu yafuatayo katika shajara yako ya kujifunzia. Kote katika misheni yako, ongeza majibu ya maswali haya.

    • Maisha yangu yangekuwaje bila Kitabu cha Mormoni?

    • Je, ni kitu gani nisingekijua bila ya Kitabu cha Mormoni?

    • Je, ni kitu gani nisingekuwa nacho bila ya Kitabu cha Mormoni?

  • Soma Mahubiri ya Mlimani katika Mathayo 5–7 na mahubiri ya Kristo hekaluni katika 3 Nefi 12–14. Je, ni kwa jinsi gani kusoma haya pamoja kunakusaidia uelewe vizuri zaidi mafundisho ya Mwokozi?

  • Soma kila tukio katika Kitabu cha Mormoni ambapo kuna rejeleo la mtu akisali. Katika shajara yako ya kujifunzia, andika kile ulichojifunza kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni kuhusu sala.

  • Kutoka kwenye vichwa vya sura za Mosia 11–16, andika muhtasari wa kile ambacho Abinadi alifundisha. Kisha soma sura hizi na uongeze muhtasari wako.

  • Kutoka kwenye vichwa vya sura za Mosia 2–5, andika muhtasari wa kile ambacho Mfalme Benjamini alifundisha. Kisha soma sura hizi na uongeze muhtasari wako.

Kujifunza pamoja na Mwenza na Kubadilishana Mwenza

  • Someni vifungu vya Kitabu cha Mormoni pamoja. Elezeni kile ambacho mmejifunza na jinsi mlivyohisi. Jadilini jinsi mtakavyokitumia katika maisha yenu.

  • Someni Alma 26 na29 kwa pamoja. Elezeni vile mnavyohisi kuhusu misheni yenu. Andikeni hisia zenu katika shajara zenu za kujifunzia.

  • Someni Alma 37:9 na mjadili jinsi gani maandiko yalivyokuwa muhimu kwa Amoni na wamisionari wenzake. Tafuteni marejeleo ambayo yanaeleza jinsi walivyoyatumia maandiko.

  • Someni Alma 11–14, mmoja wenu akichukua jukumu la Alma au Amuleki na mwingine akichukua nafasi ya wapinzani. Jadilini jinsi ambavyo wamisionari hawa walijibu maswali magumu.

Baraza la Wilaya, Mikutano wa Kanda na Baraza la Uongozi wa Misheni

  • Fanyeni mazoezi ya kutumia Kitabu cha Mormoni katika kila moja ya njia zilizotajwa katika vichwa muhimu vya sura hii.

  • Orodhesheni maswali yaliyoulizwa na wale mnaowafundisha. Eleza kwa kila mmoja jinsi ambavyo mngejibu maswali haya mkitumia Kitabu cha Mormoni.

  • Someni vifungu vya Kitabu cha Mormoni pamoja. Shirikini ujuzi, hisia, na ushuhuda.

  • Fanyeni mazoezi kutumia Kitabu cha Mormoni ili kuthibitisha ujumbe wa Urejesho.

  • Waalike wamisionari washiriki uzoefu ambapo Kitabu cha Mormoni kiliwasaidia wao na wale waliowafundisha katika mchakato wa uongofu.

  • Waruhusu wamisionari washiriki maandiko pendwa ya Kitabu cha Mormoni ambayo huwasaidia kujibu swali la nafsi.

  • Mwalike muumini ambaye ni mwongofu ajukumu lashiriki Kitabu cha Mormoni katika uongofu wake.

Viongozi wa Misheni na Washauri wa Misheni

  • Wafundisheni wamisionari jinsi ya kutumia Kitabu cha Mormoni ili kuthibitisha ukweli wa ujumbe wa Urejesho.

  • Someni 1 Nefi 1 pamoja na wamisionari na muilinganishe na uzoefu wa Joseph Smith.

  • Wape wamisionari nakala safi ya Kitabu cha Mormoni. Waalike wasome na kuwekea alama kitabu hiki mara mbili katika vipindi viwili au vitatu ya uhamisho.

    • Katika usomaji wa kwanza, waombe wawekee alama kila kitu kinachoonesha au kushuhudia juu ya Yesu Kristo.

    • Katika usomaji wa pili, waombe wawekee alama mafundisho na kanuni za injili.

    Waruhusu wamisionari washiriki kile walichojifunza na kuhisi. Mzee Ronald A. Rasband alieleza jinsi ambavyo kusoma Kitabu cha Mormoni kwa njia hii kulimgusa yeye kama mmisionari.

Mzee Ronald A. Rasband

“Kulikuwa na cha ziada kwenye usomaji wangu kuliko kuweka tu alama kwenye maandiko. Kwa kila usomaji wa Kitabu cha Mormoni, mwanzo mpaka mwisho, nilijawa na upendo wa dhati kwa Bwana. Nilihisi ushahidi thabiti wa ukweli wa mafundisho Yake na jinsi yanavyotumika hadi ‘leo hii.’ Kitabu hiki kinaendana na jina lake “Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo.” Kwa kujifunza huko na ushahidi wa kiroho ambao ulipokelewa, nilikuwa mmisionari wa Kitabu cha Mormoni na mfuasi wa Yesu Kristo” (“Siku Hii,” Liahona, Nov. 2022, 25).

  • Waalike wamisionari washiriki pamoja nawe maandiko ya Kitabu cha Mormoni ambayo yamekuwa muhimu katika maisha yao.

  • Tambua maswali ya nafsi kwa ajili ya watu katika misheni yenu. Waalike wamisionari wapate mistari katika Kitabu cha Mormoni ambayo inasaidia kujibu maswali haya.