Miito ya Misheni
Sura ya 7: Jifunze Lugha ya Misheni Yako


“Sura ya 7: Jifunze Lugha ya Misheni Yako,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 7,” Hubiri Injili Yangu

Picha
tufe na bendera

Sura ya 7

Jifunze Lugha ya Misheni Yako

Zingatia Hili

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuimarisha imani yangu katika Bwana ili inisaidie nijifunze lugha mpya?

  • Kwa nini ninapaswa kuendelea kuboresha uwezo wangu wa lugha?

  • Jinsi gani ninapaswa kuboresha uwezo wangu wa kuzungumza na kufundisha katika lugha ya misheni yangu?

  • Jinsi gani ninaweza kupokea kipawa cha ndimi?

Jiandae Kiroho

Bwana alitangaza, “Kila mtu atasikia utimilifu wa injili katika ulimi wake mwenyewe, na katika lugha yake mwenyewe, kupitia wale waliotawazwa kwa uwezo huu” (Mafundisho na Maagano 90:11).

Zilizoorodheshwa hapa chini ni njia unazoweza kufuata ili kuimarisha imani yako kwamba Bwana atakusaidia ufundishe na ushuhudie katika lugha yako ya misheni.

  • Amini kwamba wewe umeitwa na Mungu kupitia nabii.

  • Omba msaada wa Mungu kupitia sala ya dhati.

  • Fanya kazi kwa bidii kwa kujifunza, kufanya mazoezi, na kutumia lugha ya misheni yako kila siku.

  • Kuwa mstahiki wa wenza wa Roho Mtakatifu kwa kushika amri na kuishi viwango vya umisionari.

  • Takasa nia zako kwa kumpenda Mungu na kwa kuwapenda watoto Wake na kutamani kuwabariki.

Jitolee na Uwe na Bidii

Kujifunza kufundisha ipasavyo katika lugha ya misheni yako kunahitaji jitihada ya bidii na vipawa vya Roho. Usishangae kama kazi inaonekana kuwa ngumu. Inachukua muda. Kuwa na subira kwako mwenyewe. Unapojitolea kujifunza lugha, utapata ujuzi unaohitajika ili kutimiza dhumuni lako kama mmisionari.

Hauko peke yako katika kujifunza lugha ya misheni yako. Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo watakusaidia unapotafuta msaada Wao. Tafuta na uwe muwazi kwa ajili ya msaada wa mwenza wako, waumini, wale unaowafundisha, wamisionari wengine, na watu wengine.

Sikiliza kwa makini na zungumza lugha hiyo katika kila fursa. Usiogope kufanya makosa. Kila mtu ambaye anajifunza lugha mpya hufanya makosa. Watu wataelewa, na watathamini juhudi zako za kujifunza lugha yao.

Endelea kuboresha ujuzi wa lugha yako mpaka mwisho wa misheni yako. Uwezo wako wa kuzungumza lugha unapokua, watu watasikiliza zaidi kile usemacho kuliko jinsi unavyokisema. Utakuwa na wasiwasi kidogo tu kuhusu jinsi ya kuwasiliana na kuweza kujibu vyema mahitaji ya wengine.

Picha
Mzee Jeffrey R. Holland

“Tungetumaini … kwamba kila mmisionari anayejifunza lugha … mpya angeweza kuwa stadi katika kila njia inayowezekana. … Na unapofanya hivyo, [ufundishaji] wako na ujuzi wa kushuhudia utaongezeka. Utapokelewa vyema na utakuwa wa kuvutia zaidi kiroho kwa [watu unaowafundisha]. …

“Usitosheke na kile tunachokiita msamiati wa umisionari pekee. Jisukume mwenyewe katika lugha, na utapata ufanisi mkuu wa kuifikia mioyo ya watu” (Jeffrey R. Holland, missionary satellite broadcast, Aug. 1998).

Endelea kutumia lugha ya misheni yako baada ya kurudi nyumbani. Bwana amewekeza sana ndani yako, na Yeye anaweza kuwa na matumizi ya uwezo wako wa lugha hapo baadaye katika maisha yako.

Jifunze Kingereza

Ikiwa hauwezi kuzungumza Kingereza, unapaswa kujifunza kama mmisionari. Hii itakubariki wakati wa misheni yako na kote katika maisha yako. Kujifunza Kingereza pia kutabariki familia yako.

(Kwa msaada zaidi katika kujifunza Kingereza, ona EnglishConnect kwa ajili ya Wamisionari.

Picha
mwanamke akiandika katika shajara

Kanuni za Kujifunza Lugha

Wajibika

Weka malengo ya kuboresha uwezo wako wa lugha, na rekebisha malengo hayo kila mara. Tengeneza mpango wa kujifunza lugha. Tumia lugha katika kila fursa.

Fanya Kujifunza Kwako Kuwe na Maana Zaidi

Tumia kile unachojifunza kwa hali halisi za maisha na katika shughuli zako za kila siku. Fokasi kwenye lugha ambayo itakusaidia useme kile unachohitaji kusema.

Tafuta Kuwasiliana

Zungumza lugha na mwenza wako kadiri iwezekanavyo. Chukua nafasi ya kila fursa ya kujifunza na kufanya mazoezi. Kwa mfano, ungeweza kumuomba muumini aliyerejea au mtu unayemfundisha akusaidie ujue lugha. Hakuna mbadala wa kuzungumza na wazungumzaji wenyeji wa lugha.

Usilinganishe

Usilinganishe ujuzi wako wa lugha na ule wa mwenza wako au wamisionari wengine. Kulinganisha huongoza kwenye majivuno au kukata tamaa.

Jifunze Dhana Mpya Kwa usahihi

Pitia kila mara kile ulichojifunza, na kifanyie mazoezi katika mazingira mapya. Hii itakusaidia ukumbuke na utumie kile unachojifunza.

Picha
mwanamume akiangalia kitabu

Tengeneza Mpango wa Kujifunza Lugha

Mpango wa kujifunza lugha huwasaidia wote wamisionari wapya na wenye uzoefu kufokasi kwenye kile wanachoweza kufanya kila siku ili kuboresha uwezo wao wa kuzungumza lugha ya misheni yao. Mpango huu utajumuisha kile wewe utakachofanya wakati wa muda wako wa kujifunza lugha na kote katika siku.

Hatua zifuatazo zinaonesha jinsi unavyoweza kutengeneza mpango wa kujifunza lugha kwa kutumia mchakato wa uwekaji lengo kutoka sura ya 8. Rekebisha mchakato huu kadiri inavyohitajika.

  1. Kwa sala weka malengo na weka mipango. Weka malengo kila wiki na kila siku ili kuboresha uwezo wako wa kawaida wa kuwasiliana na kujifunza injili. Jumuisha vitu ambavyo unataka kuvikariri, kama vile maneno, vishazi, maandiko, na vifungu vya maneno.

  2. Andika na Weka Ratiba. Amua ni nyenzo zipi za lugha zitakusaidia utimize malengo yako. Nyenzo za lugha zingeweza kujumuisha maandiko, kamusi, vitabu vya sarufi, app ya TALL Embark, na zinginezo. Weka ratiba ya nyakati ambapo utajifunza rasmi na kutumia lugha. Kwa mfano, ungeweza kutengeneza ratiba ya kusoma kwa sauti kutoka katika Kitabu cha Mormoni kwa dakika 15 kila siku wakati wa chakula cha mchana.

  3. Fanyia kazi mipango yako. Bwana hupenda juhudi, kwa hiyo fanya kazi kwa bidii ili utimize malengo yako. Linda muda wako wa kujifunza lugha na tengeneza upya ratiba kwa ajili ya baadaye kama mgongano unatokea.

  4. Pitia tena na fuatilia. Pitia upya mpango wako wa kujifunza kila mara ili kutathimini jinsi unavyofanya kazi vizuri. Mwalike mwenza wako, viongozi wa misheni, waumini, na wengine katika eneo lako ili wapendekeze jinsi unavyoweza kuboresha. Shiriki katika ukadiriaji wa lugha ulioratibiwa wa kila mara ili kupanga maendeleo yako na utambue njia za kuboresha.

Weka uwiano wa kujifunza kwako lugha kati ya malengo ya muda mrefu kwa ajili ya kutengeneza msingi wa lugha na malengo ya muda mfupi kwa ajili ya shughuli mahususi na watu unaowafundisha.

Wakati wa muda rasmi wa kujifunza lugha, weka uwiano baina ya malengo yako na mipango kote katika maeneo ya msingi ya lugha yaliyooneshwa hapa chini. Amua kile utakachojifunza kwa siku nzima.

ujuzi wa kusikiliza

ujuzi wa kusoma

sarufi

ujuzi wa kuzungumza

ujuzi wa kuandika

msamiati

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Tenga muda kila wiki kutathimini kujifunza kwako lugha kwa kuuliza maswali yafuatayo:

  • Je, nimejifunza lugha ya misheni yangu kila siku wiki hii? Je, ninaweza kufanya nini kwa uthabiti ili kuboresha lugha ya misheni yangu?

  • Je, mpango wangu unanisaidia nipate, nifundishe, na nifanye kazi vyema na waumini? Ni marekebisho yapi ninayohitaji kufanya kwenye mpango wangu?

  • Ni kipi ninakifurahia sana kuhusu kujifunza kwangu lugha? Je, ninaweza kufanya nini ili kukifurahia zaidi?

  • Ni muda kiasi gani ninapaswa kutumia ili kufanya mazoezi ya kusikiliza, kusoma, kuandika, na kuzungumza? Ni kwa jinsi gani ninaweza kujifunza msamiati, sarufi, na matamshi?

  • Ni shughuli na nyenzo zipi ninazitumia kujifunza lugha? Ni zipi zinazonisaidia zaidi mimi? Ni nyenzo au shughuli zipi zingine ambazo zingeweza kuwa zenye msaada?

  • Ni kipi kinahitaji usikivu zaidi?

Baada ya kujibu maswali haya, rekebisha mipango yako ya kujifunza na uone kama inaboresha matokeo yako. Roho atakuongoza pale unapoendelea kutafuta kuboresha kujifunza kwako lugha.

Jifunze pamoja na Wenza Wako

Wasaidie wenza wako wapate mafanikio na wapate kujiamini katika kujifunza lugha ya misheni au kujifunza Kingereza. Kwa dhati na mara kwa mara wapongeze wenza wako na wamisionari wengine kwa maendeleo yao.

Toa mrejesho rahisi na wenye tija kwa ukarimu. Wape nafasi nyingi za kufundisha na kushuhudia kwa ufanisi. Zingatia jinsi mmisionari mwenye uzoefu zaidi alivyomsaidia mwenza wake katika tukio la kweli lifuatalo.

Nilikuwa punde tu nimewasili katika eneo langu la pili wakati mwenza wangu aliponiambia ilikuwa zamu yangu kutoa wazo la kiroho katika miadi ya chakula cha jioni. Mwenza wangu wa kwanza kila mara alifurahia kufundisha, na mimi nilikuwa ninatoa sehemu yangu ndogo ya somo na kisha kusikiliza.

Nilijaribu kumshawishi mwenza wangu kwamba yeye anapaswa kutoa wazo la kiroho, lakini yeye alinitia moyo nichukue jukumu hili. Nilifanya mazoezi kwa msaada wake.

Wakati ulipowadia, nilifungua maandiko yangu na kusoma kutoka katika 3 Nefi 5 na 7. Nilihangaika lakini niliweza kuelezea kwa nini nilihisi vifungu nilivyovichagua vilikuwa muhimu, na nilisikia ahueni nilipomaliza. Wakati swali lilipoulizwa, nilimtazama mwenza wangu ili ajibu, lakini hakufungua mdomo wake. Hapo ndipo nilipojishangaza mwenyewe kwa kutoa jibu kwa Kifaransa kilichoeleweka. Hata nilishangaa zaidi kwamba muumini hakuonekana kutambua kwamba nilikuwa na wasiwasi kuhusu ujuzi wangu wa kuwasiliana. Nilipata kujiamini na kutambua kwamba Kifaransa changu kilikuwa bora kuliko nilivyokuwa ninajifikiria.

Wiki zilipita, na mwenza wangu aliendelea kuniacha nifundishe—hata wakati ambapo sikufikiria kama ningeweza kufanya hivyo na pengine hata yeye alikuwa na mashaka ikiwa ningeweza kufanya hivyo. Nilihisi kwamba nilikuwa nimekuwa chombo cha Baba yetu aliye Mbinguni badala ya kuwa tu mwenza mkimya.

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Fanya kazi na wamisionari wengine wakusaidie ujifunze lugha ya misheni yako.

  • Kama unafanya kazi na mmisionari mpya, ni kwa jinsi gani unaweza kumsaidia vizuri mwenza wako ajifunze lugha au ajifunze Kingereza?

  • Kama wewe ni mmisionari mpya, ni aina ipi ya msaada ungeweza kuomba kutoka kwa mwenza wako?

Picha
wamisionari wakimfundisha mwanamke

Kujifunza Utamaduni na Lugha

Utamaduni na lugha vinahusiana kwa karibu sana. Kuelewa utamaduni wa watu kutasaidia kufafanua jinsi lugha inavyotumika. Uelewa huu pia utakusaidia wewe uwasilishe vipengele vya kipekee vya ujumbe wa Urejesho katika njia ambayo itakuwa wazi kwa watu.

Mojawapo ya vitu vikuu unavyoweza kufanya ili kupata kuaminiwa na watu na kupata upendo wao ni kuheshimu na kukumbatia utamaduni wao katika njia zinazofaa. Wamisionari wengi maarufu wamefanya hivi katika 1 Wakorintho 9:20–23).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Tumia wazo lililo hapa chini kukusaidia ujiandae kumfundisha mtu ambaye ana utamaduni au historia tofauti.

  • Fikiria kuhusu asili ya utamaduni na ya kidini ya watu unaowafundisha. Tambua hali ya asili yao ambayo ingeweza kufanya iwe vigumu kwao kuelewa kanuni ya injili. Panga njia za kufundisha kanuni hii kwa uwazi.

Kipawa cha Ndimi

Vipawa vya Roho ni halisi. Kipawa cha ndimi na tafsiri za ndimi kina madhihirisho mengi. Baadhi yake hujumuisha kuzungumza, kuelewa, na kufasiri lugha. Leo kipawa cha ndimi mara nyingi hudhihirika katika kusoma na kujifunza kulikoimarishwa na Roho ili kuwasaidia wamisionari wajifunze lugha katika misheni yao.

Roho Mtakatifu anaweza kudhihirisha ukweli wa ushuhuda wako hata ingawa kizuizi cha lugha kinaweza kuwa kiko kati yako na wale unaowafundisha. Vivyo hivyo, Roho Mtakatifu anaweza kuleta maneno na vishazi katika ufahamu wako na kukusaidia uelewe kile ambacho watu wanasema kutoka katika mioyo yao.

Kwa sehemu kubwa, hautapata vipawa hivi bila juhudi. Utahitajika kuvitafuta kwa bidii sana ili kuvitumia kuwabariki wengine (ona Mafundisho na Maagano 46:8–9, 26). Sehemu ya kutafuta kipawa cha ndimi ni kufanya kazi na kufanya yale yote unayoweza ili kujifunza lugha. Kuwa na subira unapojifunza kwa sala na kufanyia mazoezi lugha. Amini kwamba Roho atakusaidia kadiri unavyoweka bidii ya dhati. Kuwa na imani kwamba unaweza kuwa na kipawa cha ndimi kukusaidia wewe na wale unaowafundisha.

Unapohangaika kujieleza mwenyewe kwa uwazi kama vile ambavyo ungependa, kumbuka kwamba Roho anaweza kuzungumza na mioyo ya watoto wa Mungu. Rais Thomas S. Monson alifundisha:

“Kuna lugha moja … ambayo ni kawaida kwa kila mmisionari—lugha ya Roho. Haujifunzi kutoka katika vitabu vya kiada vilivyoandikwa na wasomi, wala haipatikani kupitia kusoma na kukariri. Lugha ya Roho huja kwake yule ambaye hutafuta kwa moyo wake wote kumjua Mungu na kushika amri Zake takatifu. Ufasaha katika lugha hii humruhusu mtu avuke vizuizi, ashinde vikwazo, na aguse moyo wa mwanadamu” (“Roho Huleta Uzima; Ensign, Juni 1997, 2).

Kujifunza Binafsi au na Mwenza

Tumia kauli zifuatazo kutathimini juhudi zako za kutafuta kipawa cha ndimi. Andika misukumo na malengo ili vikusaidie uboreshe kujifunza kwako lugha.


Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kutumia

Kujifunza Binafsi

  • Pitia tena nyenzo za lugha kwenye Ukurasa wa Tovuti wa Mmisionari. Bainisha kitu ambacho haujawahi kukijaribu, na weka lengo la kukijaribu katika wiki chache zijazo.

  • Katika mkutano ujao wa wilaya, muulize mmisionari mzoefu mwenye uwezo mzuri wa lugha ni kitu gani yeye alifanya katika kujifunza lugha.

Kujifunza na Mwenza na Kubadilishana Mwenza

  • Fanyeni mazoezi ya kufundishana masomo ya mmisionari katika lugha ya misheni yenu. Mwanzoni, wamisionari wapya wangeweza kufundisha kwa urahisi, kushiriki ushuhuda rahisi, na kusoma maandiko yaliyokaririwa. Kadiri kujiamini na uwezo wao unavyoongezeka, wataweza kushiriki kikamilifu zaidi katika kufundisha.

  • Pitia tena mawazo katika sura hii na nyenzo za lugha kwenye Ukurasa wa Tovuti wa Mmisionari. Jadilini mapendekezo ambayo mngeweza kutumia katika kujifunza na mmisionari mwenza wakati wa wiki ijayo.

  • Muombe mwenza asikilize matamshi yako na akusaidie uyaboreshe. Muombe azingatie wakati unapokuwa haueleweki. Tengeneza orodha ya maneno, vishazi, au sarufi ambazo zingesaidia. Elezea na ufanye mazoezi ya jinsi ya kutumia kile kilicho kwenye orodha ya shughuli zijazo.

  • Fanya mazoezi ya kusikiliza kwa makini. Panga muda wakati wa mchana kusikiliza kwa makini ili kutambua misamiati na mpangilio uliojifunza. Unaposikia kishazi kinatumiwa tofauti na jinsi ambavyo wewe ungekisema, kiandike na ukifanyie mazoezi.

  • Tengeneza orodha ya vitu ambavyo watu wangesema siku hiyo. Panga na fanya mazoezi ya jinsi ambavyo ungeweza kujibu.

Baraza la Wilaya, Mikutano ya Kanda na Baraza la Uongozi la Misheni

  • Waalike wazungumzaji wenyeji kuhudhuria mojawapo ya mikutano hii. Panga kwa wamisionari kuwafundisha wao katika vikundi vidogo vidogo. Waombe wazungumzaji wenyeji wazingatie na watoe maoni juu ya uwezo wa lugha wa wamisionari.

  • Mpangie mapema mmisionari mmoja au wawili wasimulie kuhusu mafanikio ambayo wamekuwa nayo katika kujifunza lugha.

  • Mpangie mmisionari mwenye uzoefu kwa ufupi awasilishe sehemu fulani ya lugha ambayo kwa kawaida ni ngumu kwa wamisionari. Mruhusu awasilishe mifano ya matumizi mazuri ya lugha, na waruhusu wamisionari waifanyie mazoezi.

  • Waruhusu wamisionari ambao ni wenyeji wa utamaduni washiriki umaizi wao.

Viongozi wa Misheni na Washauri wa Misheni

  • Sisitiza juu ya umuhimu wa kujifunza lugha kwa uthabiti kila siku.

  • Wahimize wamisionari watumie lugha ya misheni mara nyingi iwezekanavyo.

  • Jumuisha vipengele vya mpango wa kujifunza lugha ya misheni katika ratiba ya kujifunza kwa utaratibu. Pitia tena hili katika mikutano ya baraza la wilaya.

  • Tafuta fursa za kuzungumza na wamisionari katika lugha wanayojifunza. Mara kwa mara wafanyie mahojiano katika lugha hii.

  • Waombe viongozi na waumini wenyeji mawazo juu ya jinsi wamisionari wanavyoweza kuboresha uwezo wao wa lugha.

  • Toa maelekezo katika mikutano ya kanda au baraza la uongozi la misheni juu ya makosa ya kawaida ambayo yamefanywa na wamisionari wanaojifunza lugha ya misheni yao.

  • Wafundishe wamisionari kuhusu vipawa vya kiroho.

  • Watizame wamisionari wakati wanapofundisha katika lugha ya misheni.

Chapisha