Maandiko Matakatifu
1 Nefi 21


Mlango wa 21

Masiya atakuwa nuru ya Wayunani na atawafungua wafungwa—Israeli itakusanywa kwa uwezo katika siku za mwisho—Wafalme watakuwa baba zao walezi—Linganisha Isaya 49. Karibia mwaka 588–570 K.K.

1 Na tena: Sikiliza, Ee ninyi nyumba ya Israeli, nyote ambao mmetenganishwa na kufukuzwa kwa sababu ya uovu wa wachungaji wa watu wangu; ndiyo, ninyi nyote ambao mmetenganishwa, na kutawanywa ugenini, wale ambao ni wa watu wangu, Ee nyumba ya Israeli. Sikilizeni, Ee visiwa, nisikilizeni mimi, na watu walio mbali pia sikilizeni; Bwana ameniita kabla sijazaliwa, kutoka tumboni mwa mama yangu, ametaja jina langu.

2 Na amefanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; amenificha katika kivuli cha mkono wake, na akanifanya mshale uliongʼaa; amenificha katika podo lake.

3 Na akaniambia: Wewe ndiye mtumishi wangu, Ee Israeli, ambaye nitatukuzwa ndani yake.

4 Kisha nikasema, nimefanya kazi bure, nimetumia nguvu zangu bure na bila faida; kwa hakika hukumu yangu iko na Bwana, na vitendo vyangu na Mungu wangu.

5 Na sasa, asema Bwana—ambaye aliniumba kutoka tumboni ili niwe mtumishi wake, kumrejesha Yakobo kwake tena—ingawa Israeli haijakusanyika, bado nitakuwa mwenye utukufu machoni mwa Bwana, na Mungu wangu atakuwa nguvu yangu.

6 Na alisema: Ni kitu rahisi kuwa wewe uwe mtumishi wangu ili uinue makabila ya Yakobo, na kurudisha waliohifadhiwa kutoka Israeli. Nitakufanya pia uwe nuru kwa Wayunani, kwamba uwe wokovu wangu hadi mwisho wa ulimwengu.

7 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana, Mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, kwa yule anayechukiwa na watu, kwa yule anaye dharauliwa na mataifa, kwa mtumishi wa watawala: Wafalme wataona na kuinuka, wana wa wafalme pia wataabudu, kwa sababu ya Bwana ambaye ni mwaminifu.

8 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Kwa wakati uliokubalika nimekusikia, Ee visiwa vya bahari, na kwa siku ya wokovu nilikusaidia; na nitakuhifadhi, na ninakupatia mtumishi wangu uwe agano la watu, kuimarisha nchi, kuwasababisha kurithi makao yaliokuwa yenye ukiwa.

9 Ili uwaambie wafungwa: Ondokeni; kwa wale ambao wanaketi gizani: Jidhihirisheni. Watakula njiani, na malisho yao yatakuwa juu ya majabali.

10 Hawataona njaa wala kiu, wala joto au jua kuwachoma; kwani yule anayewarehemu atawaongoza, hata kwenye chemchemi za maji atawaongoza.

11 Na nitafanya milima yangu yote iwe njia, na njia zangu zitainuliwa.

12 Na kisha, Ee nyumba ya Israeli, tazama, haya yatatoka mbali; na tazama, haya kutoka kaskazini na kutoka magharibi; na haya kutoka nchi ya Sinimu.

13 Imbeni, Ee mbingu; na ushangilie, Ee dunia; kwani miguu ya wale ambao wako mashariki itaimarishwa; na anzeni kuimba, Ee milima; kwani hawatapigwa tena; kwani Bwana amewafariji watu wake, na atawarehemu wanaosumbuka.

14 Lakini, tazama, Sayuni imesema: Bwana ameniacha, na Bwana wangu amenisahau—lakini ataonyesha kwamba hajafanya hivyo.

15 Kwani mwanamke anaweza kusahau mtoto wake ambaye anamnyonyesha, kwamba asiwe na huruma kwa mwana wa tumbo lake? Ndiyo, wanaweza kusahau, lakini sitakusahau, Ee nyumba ya Israeli.

16 Tazama, nimekuchora viganjani mwa mikono yangu; kuta zako daima ziko mbele yangu.

17 Watoto wako wataharakisha dhidi ya waharibifu wako; na wale waliokuharibu wataondoka kutoka kwako.

18 Inua macho yako pande zote na utazame; hawa wote wanakusanyika pamoja, na watakuja kwako. Na vile ninavyoishi, Bwana asema, wewe utajivika na wao wote, kama pambo, na kujifunga kwao kama bibi arusi.

19 Kwani utupu wako na kwenye ukiwa, na nchi yako ya maangamizo, itakuwa hata sasa nyembamba kwa sababu ya wakazi; na wale ambao walikumeza watakuwa mbali.

20 Watoto utakaopata, baada ya kupoteza wale wa kwanza, watasema tena masikioni mwako: Hapa mahali ni padogo sana kwangu; nipe mahali ili niishi.

21 Kisha utasema moyoni mwako: Nani alinizalia hawa, akiona nimepoteza watoto wangu, na nina ukiwa, mtumwa, na akizurura hapa na pale? Nani amelea hawa? Tazama, niliachwa pekee yangu; hawa, walikuwa wapi?

22 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu: Tazama, nitawanyooshea Wayunani mkono wangu, na nitapeperusha bendera yangu miongoni mwa watu; na wataleta wana wako kwa mikono yao, na mabinti zako watabebwa mabegani mwao.

23 Na wafalme watakuwa baba zako walezi, nao malkia wao watakuwa mama zako walezi; watainama mbele yako nyuso zao zikiielekea ardhi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; na utajua kwamba mimi ni Bwana; kwani hawataaibika wanaoningojea.

24 Kwani mateka watanyakuliwa kutoka kwa shupavu, au watumwa halali kukombolewa?

25 Lakini hivyo ndivyo asemavyo Bwana, hata watumwa wa shupavu watachukuliwa, na mateka wa wale walio wa kutisha watakombolewa; kwani nitashindana na yule anayeshindana nawe, na nitaokoa watoto wako.

26 Na nitawalisha wanaokudhulumu kwa nyama yao wenyewe; watalewa kwa damu yao wenyewe kama kwa mvinyo mtamu; na watu wote watajua kwamba mimi, Bwana, ni Mwokozi wenu na Mkombozi wenu, Mwenyezi Mkuu wa Yakobo.