Maandiko Matakatifu
3 Nefi 1


Nefi wa Tatu

Kitabu cha Nefi
Mwana wa Nefi, Ambaye Alikuwa Mwana wa Helamani

Na Helamani alikuwa mwana wa Helamani, ambaye alikuwa mwana wa Alma, ambaye alikuwa mwana wa Alma, ambaye alikuwa wa uzao wa Nefi ambaye alikuwa mwana wa Lehi, ambaye alitoka Yerusalemu katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Zedekia, mfalme wa Yuda.

Mlango wa 1

Nefi, mwana wa Helamani, anaondoka nje ya nchi, na mwana wake Nefi anaandika maandishi—Ingawa ishara na maajabu ni mengi, walio waovu wanapanga kuwaua wenye haki—Usiku wa kuzaliwa kwa Kristo unafika—Ishara inatolewa, na nyota mpya inaonekana—Uwongo na udanganyifu unaongezeka, na wezi wa Gadiantoni wanawaua wengi. Karibia mwaka 1–4 B.K.

1 Sasa ikawa kwamba mwaka wa tisini na moja ulikuwa umepita na ilikuwa miaka mia sita tangu wakati ambao Lehi aliondoka Yerusalemu; na ilikuwa katika mwaka ambao Lakoneyo alikuwa mwamuzi mkuu na msimamizi juu ya nchi.

2 Na Nefi, mwana wa Helamani, alikuwa ameondoka kutoka nchi ya Zarahemla, na kutoa amri kwa mwana wake Nefi, ambaye alikuwa mwana wake mkubwa, kuhusu mabamba ya shaba nyeupe, na kumbukumbu zote ambazo zilikuwa zimewekwa, na vitu vyote ambavyo vilichukuliwa kama vitakatifu kuanzia kuondoka kwa Lehi kutoka Yerusalemu.

3 Kisha aliondoka nje ya nchi, na alikoenda, hakuna mtu yeyote ajuaye; na mwana wake Nefi alihifadhi maandishi badala yake, ndiyo, maandishi ya hawa watu.

4 Na ikawa kwamba katika mwanzo wa mwaka wa tisini na mbili, tazama, utabiri wa manabii ulianza kutimizwa zaidi kabisa; kwani kulianza kuwa na ishara kubwa na miujiza mikubwa kutokea miongoni mwa watu.

5 Lakini kulikuwa na wengine walioanza kusema kwamba wakati umepita kwa yale maneno kutimizwa, ambayo yalizungumzwa na Samweli, Mlamani.

6 Na walianza kufurahia ndugu zao, wakisema: Tazama wakati umepita, na maneno ya Samweli hayajatimizwa; kwa hivyo, shangwe yenu na imani yenu katika hiki kitu imekuwa bure.

7 Na ikawa kwamba walifanya makelele mengi kote nchini; na watu walioamini walianza kuwa na huzuni sana, wakiogopa kwamba hivyo vitu ambavyo vilizungumzwa havingetimizwa.

8 Lakini tazama, walichunguza wakati wote ule mchana na ule usiku na ule mchana siku ile ambayo itakuwa ni kama siku moja kama vile hakuna usiku, kwamba wangejua kuwa imani yao haikuwa bure.

9 Sasa ikawa kwamba kulikuwa na siku ambayo iliwekwa kando na wasioamini, kwamba wale wote ambao waliamini kwenye desturi hizo wangeuawa isipokuwa ishara zipate kutimizwa, ambazo zilitolewa na nabii Samweli.

10 Sasa ikawa kwamba wakati Nefi, mwana wa Nefi, aliona huu uovu wa watu hawa, moyo wake ulikuwa na huzuni sana.

11 Na ikawa kwamba alienda nje na kujiinamisha ardhini, na kuomba kwa Mungu wake kwa niaba ya watu wake, ndiyo, wale ambao walikuwa karibu kuangamizwa kwa sababu ya imani yao kwenye desturi za babu zao.

12 Na ikawa kwamba aliomba kwa nguvu kwa Bwana ile siku yote; na tazama, sauti ya Bwana ilikuja kwake, ikisema:

13 Inua kichwa chako na uchangamke; kwani tazama, wakati umefika, na kwa usiku wa leo ishara itatolewa, na kesho nitakuja ulimwenguni, kuonyesha dunia kwamba nitatimiza yote ambayo nimesababisha kuzungumzwa kwa midomo ya manabii wangu watakatifu.

14 Tazama, naja kwa watu wangu, kutimiza vitu vyote ambavyo nimefanya kujulikana kwa watoto wa watu tangu msingi wa dunia, na kufanya mapenzi, yote ya Baba na Mwana—ya Baba kwa sababu yangu, na ya Mwana kwa sababu ya mwili wangu. Na tazama, wakati umefika, na usiku huu ishara itadhihirishwa.

15 Na ikawa kwamba maneno ambayo yalimjia Nefi yalivyotimizwa, kulingana na vile yalizungumzwa; kwani tazama, wakati jua lilipotua hapakuwa na giza; na watu walianza kustaajabu kwa sababu hapakuwa na giza wakati usiku ulipofika.

16 Na kulikuwa na wengi, ambao hawakuwa wameamini maneno ya manabii, ambao walijilaza kwenye ardhi na wakawa kama waliokufa, kwani walijua kwamba mpango mkubwa wa uangamizo ambao walikuwa wamewawekea wale ambao waliamini maneno ya manabii umezuiliwa; kwani ishara ambayo ilitolewa ilikuwa ipo.

17 Na wakaanza kujua kwamba Mwana wa Mungu lazima aonekane karibuni; ndiyo, kwa kifupi, watu wote usoni mwa ulimwengu kutoka magharibi hadi mashariki, kote katika nchi ya kaskazini na katika nchi ya kusini, walistaajabu sana kwamba walianguka ardhini.

18 Kwani walijua kwamba manabii walikuwa wameshuhudia vitu hivi kwa miaka mingi, na kwamba ishara ambayo ilitolewa ilikuwa ipo kitambo; na walianza kuogopa kwa sababu ya uovu wao na kutoamini kwao.

19 Na ikawa kwamba hapakuweko na giza usiku ule wote, lakini kulikuwa na mwangaza kama kwamba ilikuwa adhuhuri. Na ikawa kwamba jua lilitokea asubuhi tena, kulingana na utaratibu wake; na walijua kwamba ilikuwa ni siku ambayo Bwana angezaliwa, kwa sababu ya ishara ambayo ilitolewa.

20 Na ikawa imekuwa, ndiyo, vitu vyote, kila chembe, kulingana na maneno ya manabii.

21 Na ikawa pia kwamba nyota mpya ilitokea, kulingana na neno.

22 Na ikawa kwamba kutoka wakati huu kuendelea kulianza kuwa na udanganyifu ulioletwa na Shetani, miongoni mwa watu, kushupaza mioyo yao, kwa kusudi kwamba wasiamini kwenye hizo ishara na miujiza ambayo walikuwa wameona; lakini ingawaje kulikuwa na huu udanganyifu na uwongo sehemu kubwa ya watu iliamini, na wakamgeukia Bwana.

23 Na ikawa kwamba Nefi alienda mbele miongoni mwa watu, na pia wengine wengi, akiwabatiza ubatizo wa toba, ambamo kwake kulikuwa na kusamehewa kwingi kwa dhambi. Na hivyo watu wakaanza tena kuwa na amani nchini.

24 Na hapakuweko na mabishano, isipokuwa wachache ambao walianza kuhubiri, wakijaribu kuthibitisha kutumia maandiko kwamba haikuwa tena muhimu kutii sheria ya Musa. Sasa kwa kitu hiki walikosa, wakiwa hawajaelewa maandiko.

25 Lakini ikawa kwamba mara moja waligeuka, na walisadikishwa kwa makosa ambayo walikuwa nayo, kwani walifahamishwa kwamba sheria haijatimizwa, na kwamba lazima itimizwe kwa kila chembe; ndiyo, neno lilikuja kwao kwamba lazima itimizwe; ndiyo, kwamba nukta moja wala chembe moja haitapita mpaka yote yatimie; kwa hivyo kwenye huu mwaka walielemishwa kwa makosa yao na wakaungama makosa yao.

26 Na hivyo mwaka wa tisini na mbili ulipita, ukileta habari njema kwa watu kwa sababu ya ishara ambazo zilitimizwa, kulingana na maneno ya uaguzi wa manabii wote watakatifu.

27 Na ikawa kwamba mwaka wa tisini na tatu pia ulipita katika amani, isipokuwa wezi wa Gadiantoni, ambao waliishi juu ya milima, ambao waliingilia nchi; kwani ngome zao zilikuwa na nguvu sana na mahali pao pa siri kwamba watu hawangewashinda; kwa hivyo walitenda mauaji mengi sana, na kuua wengi miongoni mwa watu.

28 Na ikawa kwamba katika mwaka wa tisini na nne walianza kuongezeka kwa idadi kubwa, kwa sababu kulikuwa na wengi wasiokubaliana na Wanefi ambao walikimbilia kwao, ambao walisababisha huzuni nyingi kwa Wanefi ambao walibaki nchini.

29 Na pia kulikuwa na sababu ya huzuni nyingi miongoni mwa Walamani; kwani tazama, walikuwa na watoto wengi ambao walikuwa na kuanza kuwa wazee katika miaka, kwamba walijitegemea wenyewe, na waliongozwa vibaya na wengine ambao walikuwa Wazoramu, kwa udanganyifu wao na maneno yao ya kusifu ya uongo, kujiunga na wale wezi wa Gadiantoni.

30 Na hivyo Walamani walihuzunishwa pia, na walianza kupungukiwa na imani na haki yao, kwa sababu ya uovu wa vijana wa kizazi hiki.