Mlango wa 25
Katika Ujio wa Pili, wenye kiburi na waovu watateketezwa kama makapi—Eliya atarejea kabla ya ile siku kubwa na ya kutisha—Linganisha Malaki 4. Karibia mwaka 34 B.K.
1 Kwani tazama, ile siku inakuja ambayo itawaka kama tanuru; na wote wenye kiburi, ndiyo, na wote wanaotenda maovu, watakuwa makapi; na ile siku inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa Majeshi, kwamba haitawaachia shina wala tawi.
2 Lakini kwenu mnaolicha jina langu, yule Mwana wa Haki atawashukia na uponyaji katika mabawa yake; na ninyi mtaenda mbele na kukua kama ndama zizini.
3 Na mtakanyaga waovu; kwani watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu katika siku nitakayofanya hivi, asema Bwana wa Majeshi.
4 Kumbukeni ninyi sheria ya Musa, mtumishi wangu, niliyemwamuru huko Horebu kwa ajili ya Waisraeli wote, na amri za hukumu.
5 Tazama, nitawatumia Eliya nabii kabla ya kuja kwa ile siku kubwa na ya kutisha ya Bwana.
6 Na atageuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, nisije na kupiga dunia na laana.