Maandiko Matakatifu
Alma 35


Mlango wa 35

Kuhubiriwa kwa neno kunaangamiza hila za Wazoramu—Wanawafukuza waliobadilika, ambao baadaye wanaungana na watu wa Amoni katika Yershoni—Alma anahuzunika kwa sababu ya uovu wa watu. Karibia mwaka 74 K.K.

1 Sasa ikawa kwamba Amuleki alipomaliza kuzungumza mambo hayo, waliondoka kutoka lile kundi na wakaenda kwenye nchi ya Yershoni.

2 Ndiyo, na ndugu wengine, baada ya kuhubiri neno kwa Wazoramu, pia walikuja kwenye nchi ya Yershoni.

3 Na ikawa kwamba baada ya Wazoramu wengi waliokuwa mashuhuri kushauriana pamoja kuhusu maneno ambayo yalikuwa yamehubiriwa kwao, walikasirika juu ya neno, kwani liliharibu hila yao; kwa hivyo hawangesikiliza maneno.

4 Na wakawatuma na waliwakusanya pamoja kote nchini watu wote, na kuwashauri kuhusu maneno ambayo yalikuwa yamesemwa.

5 Sasa watawala wao na makuhani wao na walimu wao hawakuwaruhusu watu kujua kuhusu nia yao; kwa hivyo waligundua kwa siri mawazo ya watu wote.

6 Na ikawa kwamba baada ya kupata mawazo ya watu wote, wale ambao waliunga mkono yale maneno ambayo yalizungumzwa na Alma na ndugu zake walitupwa nje ya nchi; na walikuwa wengi; na walikuja pia katika nchi ya Yershoni.

7 Na ikawa kwamba Alma na ndugu zake waliwahudumia.

8 Sasa watu wa Wazoramu waliwakasirikia watu wa Amoni ambao walikuwa Yershoni, na mtawala mkuu wa Wazoramu, akiwa mtu mwovu sana, alituma mjumbe kwa watu wa Amoni akiwataka wawatupe nje ya nchi yao wale wote ambao walitoka katika nchi yao.

9 Na alitoa vitisho vingi dhidi yao. Na sasa watu wa Amoni hawakuogopa maneno yao; kwa hivyo hawakuwatupa nje, lakini waliwapokea Wazoramu wote waliokuwa masikini ambao walikuja kwao; na waliwalisha, na wakawavisha, na wakawapatia ardhi kwa urithi wao; na wakawahudumia kulingana na mahitaji yao.

10 Sasa hii iliwavuruga Wazoramu kuwakasirikia watu wa Amoni, na wakaanza kuchanganyika na Walamani na wakawavuruga pia kukasirika dhidi yao.

11 Na hivyo Wazoramu na Walamani walianza kujiandaa kwa vita dhidi ya watu wa Amoni, na pia dhidi ya Wanefi.

12 Na hivyo ukaisha mwaka wa kumi na saba wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi.

13 Na watu wa Amoni waliondoka kutoka nchi ya Yershoni, na wakaingia katika nchi ya Meleki, na wakawapatia majeshi ya Wanefi mahali katika nchi ya Yershoni, ili wakabiliane na majeshi ya Walamani na majeshi ya Wazoramu; na hivyo vita vikaanza kati ya Walamani na Wanefi, katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa waamuzi; na historia itatolewa kuhusu vita vyao baadaye.

14 Na Alma, na Amoni, na ndugu zao, na pia wana wawili wa Alma walirejea katika nchi ya Zarahemla, baada ya kuwa vyombo mikononi mwa Mungu kuleta wengi wa Wazoramu kutubu; na vile walipoletwa katika toba, walikimbizwa kutoka katika nchi yao; lakini wana mashamba kwa urithi wao katika nchi ya Yershoni, na wametayarisha silaha zao kwa kujikinga wenyewe, na wake zao, na watoto, na mashamba yao.

15 Sasa Alma, akiwa amehuzunishwa na uovu wa watu wake, ndiyo, kwa vita, na umwagaji wa damu, na mabishano ambayo yalikuwa miongoni mwao; na akiwa ameenda kutangaza neno, au kwa maneno mengine, kutangaza neno miongoni mwa watu wote katika kila mji; na akiona kwamba mioyo ya watu ilianza kuwa migumu, na kwamba walianza kuudhika kwa sababu ya uhalisi wa neno, moyo wake ulihuzunika sana.

16 Kwa hivyo, alisababisha kwamba wanawe wakusanywe pamoja, ili atoe maagizo tofauti, kwa kila mmoja, kuhusu vitu vinavyohusiana na haki. Na tuna historia ya amri zake, ambazo aliwapatia kulingana na maandishi yake.