Mlango wa 51
Watu wa mfalme wanatazamia kugeuza sheria na kumchagua mfalme—Pahorani na watu wa uhuru wanaungwa mkono kwa sauti ya watu—Moroni analazimisha watu wa mfalme kulinda nchi yao au wauawe—Amalikia na Walamani wanatega miji mingi iliyoimarishwa—Teankumu anarudisha nyuma mwingilio wa Walamani na kumuua Amalikia katika hema lake. Karibia mwaka 67–66 K.K.
1 Na sasa ikawa katika mwanzo wa mwaka wa ishirini na tano wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi, hao wakiwa wameanzisha amani miongoni mwa watu wa Lehi na watu wa Moriantoni kuhusu nchi zao, na wakiwa wameanza mwaka wa ishirini na tano kwa amani;
2 Walakini, hawakudumisha amani kwa muda mrefu nchini, kwani kulianza kuwa na ubishi miongoni mwa watu kuhusu mwamuzi mkuu Pahorani; kwani tazama, kulikuwa na sehemu ya watu ambao walitaka kwamba sehemu fulani za sheria ibadilishwe.
3 Lakini tazama, Pahorani hakubadilisha wala kukubali sheria ibadilishwe; kwa hivyo, hakuwasikiliza wale ambao walikuwa wamepeleka mashauri na maombi kuhusu kubadilishwa kwa sheria.
4 Kwa hivyo, wale ambao walitamani kwamba sheria ibadilishwe walimkasirikia, na wakataka kwamba asiwe tena mwamuzi mkuu katika nchi; kwa hivyo kulitokea ugomvi mkali kuhusu jambo hili, lakini damu haikumwagwa.
5 Na ikawa kwamba wale ambao walitaka kwamba Pahorani aondolewe kutoka kiti cha hukumu walikuwa watu wa ufalme, kwani walihitaji kwamba sheria igeuzwe kwa njia ambayo ingeiondoa serikali huru na kuweka mfalme katika nchi.
6 Na wale ambao walitaka kwamba Pahorani abaki mwamuzi mkuu juu ya nchi walijiita watu huru; na hivyo ndivyo ulikuwa mgawanyiko miongoni mwao, kwani watu huru walikuwa wameapa au kutoa agano kulinda haki yao na heshima yao ya dini kwa serikali huru.
7 Na ikawa kwamba jambo hili lao la ubishi lilitulizwa kwa sauti ya watu. Na ikawa kwamba sauti ya watu ilipendelea watu huru, na Pahorani akabaki kwenye kiti cha hukumu, ambayo ilisababisha furaha nyingi miongoni mwa ndugu za Pahorani na pia watu wengi waliotaka uhuru, ambao pia waliwanyamazisha watu wa mfalme, kwamba hawakupinga lakini walihitajika kulinda mwendo wa uhuru.
8 Sasa wale ambao walipendelea wafalme walikuwa wale ambao ni wa cheo cha juu, na walitaka kuwa wafalme; na walisaidiwa na wale ambao walitaka nguvu na uwezo juu ya watu.
9 Lakini tazama, huu ulikuwa wakati wa hatari wa mabishano kuwa miongoni mwa watu wa Nefi; kwani tazama, Amalikia alikuwa amevuruga tena mioyo ya watu wa Walamani dhidi ya watu wa Wanefi, na alikuwa akikusanya pamoja askari kutoka kila sehemu ya nchi yake, na kuwahami kwa silaha, na kuwatayarisha kwa vita kwa bidii yake yote; kwani alikuwa ameapa kunywa damu ya Moroni.
10 Lakini tazama, tutaona kwamba ahadi yake aliyofanya ilikuwa ni ya upumbavu; walakini, alijitayarisha na majeshi yake kupigana dhidi ya Wanefi.
11 Sasa majeshi yake hayakuwa mengi kama vile yalivyokuwa hapo awali, kwa sababu ya maelfu wengi ambao waliuawa kwa mikono ya Wanefi; lakini ijapokuwa kupotewa kwao kwingi, Amalikia alikuwa amekusanya jeshi kubwa la ajabu, hivyo kwamba hakuogopa kuja chini kwenye nchi ya Zarahemla.
12 Ndiyo, hata Amalikia alikuja chini mwenyewe, mbele ya Walamani. Na ilikuwa katika mwaka wa ishirini na tano wa utawala wa waamuzi; na ilikuwa wakati huo ambao walikuwa wameanza kutatua mambo ya mabishano yao kuhusu mwamuzi mkuu, Pahorani.
13 Na ikawa kwamba wakati watu ambao waliitwa watu wa mfalme walipokuwa wamesikia kwamba Walamani wanakuja kupigana dhidi yao, walifurahi ndani ya mioyo yao; na wakakataa kuchukua silaha, kwani walimkasirikia sana mwamuzi mkuu, na pia watu wa uhuru, kwamba hawangechukua silaha kulinda nchi yao.
14 Na ikawa kwamba Moroni alipoona hivi, na pia kwamba Walamani walikuwa wanakaribia mipaka ya nchi, alikasirika sana kwa sababu ya ukaidi wa watu wale ambao alikuwa amefanyia kazi kwa bidii nyingi kuwalinda; ndiyo, alikasirika sana; nafsi yake ilijaa hasira dhidi yao.
15 Na ikawa kwamba alituma ombi, na sauti ya watu, kwa msimamizi wa nchi, akitaka kwamba alisome, na kumpatia (Moroni) uwezo kulazimisha hao waasi kulinda nchi yao au wauawe.
16 Kwani lilikuwa jukumu lake la kwanza kumaliza mabishano kama haya na mafarakano miongoni mwa watu; kwani tazama, hii ilikuwa mpaka sasa sababu ya maangamizo yao. Na ikawa kwamba lilikubaliwa kulingana na sauti ya watu.
17 Na ikawa kwamba Moroni aliamuru kwamba majeshi yake yaende dhidi ya watu wa ufalme, kuweka chini kiburi chao na daraja zao kubwa na kuwalainisha na ardhi, au wachukue silaha na kusaidia njia ya uhuru.
18 Na ikawa kwamba majeshi yalienda mbele dhidi yao; na yaliweka chini kiburi chao na daraja zao kubwa, hata kwamba wakati walipoinua silaha zao za vita kupigana dhidi ya watu wa Moroni waliangushwa chini na kulainishwa na ardhi.
19 Na ikawa kwamba kulikuwa na elfu nne ya wale waasi ambao walitupwa chini kwa upanga; na wale baina ya viongozi wao ambao hawakuuawa vitani walichukuliwa na kutupwa gerezani, kwani hapakuweko na wakati wa majaribio yao wakati huo.
20 Na waasi waliosalia, badala ya kukatwa chini kwa upanga, walijitolea kwa bendera ya uhuru, na walilazimishwa kuinua jina la uhuru kwenye minara yao, na katika miji yao, na kuchukua silaha kwa kulinda nchi yao.
21 Na hivyo Moroni alikomesha wale watu wa ufalme, kwamba hapakuwa na yeyote aliyejulikana kwa jina la watu wa ufalme; na hivyo akakomesha ukaidi na kiburi cha wale watu ambao walidai damu ya wale walio bora; lakini waliletwa chini kujinyenyekea kama ndugu zao, na kupigana kwa ushujaa kwa uhuru wao kutoka kifungoni.
22 Tazama, ikawa kwamba wakati Moroni alipokuwa akiondoa vita na mabishano miongoni mwa watu wake, na kuwaweka kwa imani na utamaduni, na kutengeneza sheria kwa kujiandaa kwa vita dhidi ya Walamani, tazama, Walamani walikuwa wamekuja kwenye nchi ya Moroni, ambayo ilikuwa mipakani mwa ukingo wa bahari.
23 Na ikawa kwamba Wanefi hawakuwa na nguvu ya kutosha katika mji wa Moroni; kwa hivyo Amalikia aliwafukuza, akiua wengi. Na ikawa kwamba Amalikia alimiliki mji, ndiyo, alimiliki ngome zao zote.
24 Na wale ambao walikimbia kutoka mji wa Moroni walingia kwenye mji wa Nefiha; na pia watu wa mji wa Lehi walijikusanya pamoja, na wakafanya matayarisho na wakawa tayari kuwapokea Walamani kwa vita.
25 Lakini ikawa kwamba Amalikia hakuwaruhusu Walamani kwenda dhidi ya mji wa Nefiha kupigana, lakini akawaweka chini kando ya ukingo wa bahari, akiwaacha watu katika kila mji kuushika na kuulinda.
26 Na hivyo aliendelea, akimiliki miji mingi, mji wa Nefiha, na mji wa Lehi, na mji wa Moriantoni, na mji wa Omneri, na mji wa Gidi, na mji wa Muleki, yote ambayo ilikuwa mashariki mwa mipaka kando ya ukingo wa bahari.
27 Na hivyo Walamani walikuwa wamepata, kwa ujanja wa Amalikia, miji mingi sana, na wenyeji wasiohesabika, yote ambayo ilikuwa imelindwa kwa nguvu kwa njia ya ulinzi wa Moroni; yote ambayo iliwezesha ulinzi kwa Walamani.
28 Na ikawa kwamba walienda taratibu hadi kwenye mipaka ya nchi ya Neema, wakiwafukuza Wanefi mbele yao na kuua wengi.
29 Lakini ikawa kwamba walikutana na Teankumu, ambaye alikuwa amemuua Moriantoni na kuwaongoza watu wake kwa ukimbizi wake.
30 Na ikawa kwamba alimwongoza Amalikia pia, wakati alipokuwa akienda taratibu na jeshi lake la idadi kubwa kwamba angemiliki nchi ya Neema, na pia nchi upande wa kaskazini.
31 Lakini tazama alikabiliana na uchungu kwa kurudishwa nyuma na Teankumu na watu wake, kwani walikuwa mashujaa wakuu; kwani kila mtu wa Teankumu alikuwa anashinda Walamani kwa nguvu na kwa ustadi wao wa vita, hata kuwa walikuwa bora juu ya Walamani.
32 Na ikawa kwamba waliwaangamiza kwa wingi, hata kwamba waliwauwa hata mpaka kukawa na giza. Na ikawa kwamba Teankumu na watu wake walisimamisha hema zao kwenye mipaka ya nchi ya Neema; na Amalikia akasimamisha hema zake kwenye mipaka kwenye pwani kando ya ukingo wa bahari, na kwa njia hii walifukuzwa.
33 Na ikawa kwamba wakati usiku ulipowadia, Teankumu na mtumishi wake walienda nje usiku kwa kujificha, na wakaenda kwenye kambi ya Amalikia; na tazama, usingizi ulikuwa umewalemea kwa sababu ya uchovu wao mwingi, ambao ulisababishwa na kazi na joto la mchana.
34 Na ikawa kwamba Teankumu aliingia kwa siri hadi kwenye hema la mfalme, na kumchoma kwa sagai kwenye moyo wake; na akasababisha kifo cha mfalme mara moja kwamba hakuwaamusha watumishi wake.
35 Na akarudi tena kwa siri hadi kwenye kambi yake, na tazama watu wake walikuwa wanalala, na akawaamsha na kuwaambia vitu vyote ambavyo alikuwa amefanya.
36 Na akasababisha kwamba majeshi yake yasimame tayari, isiwe Walamani wawe wameamka na kuwajia.
37 Na hivyo ukaisha mwaka wa ishirini na tano wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi; na hivyo zikaisha siku za Amalikia.