Mlango wa 15
Bwana aliwarudi Wanefi kwa sababu Yeye aliwapenda—Walamani walioongoka wako imara na thabiti katika imani—Bwana atakuwa na huruma kwa Walamani katika siku za mwisho. Karibia mwaka 6 K.K.
1 Na sasa, ndugu zangu wapendwa, tazama, ninawatangazia kwamba msipotubu nyumba zenu zitaachwa ziwe na ukiwa.
2 Ndiyo, msipotubu, wanawake wenu watakuwa na sababu ya kuomboleza wakati watakapokuwa wakinyonyesha; kwani mtajaribu kukimbia lakini hakutakuwa na mahali pa kimbilio; ndiyo, na ole kwa wale ambao wana mimba, kwani watakuwa wazito na hawataweza kukimbia; kwa hivyo, watakanyagwa chini na kuachwa kuangamia.
3 Ndiyo, ole kwa watu hawa ambao wanaitwa watu wa Nefi isipokuwa watubu, wakati wataona ishara hizi zote na maajabu ambayo yataonyeshwa kwao; kwani tazama, wamekuwa watu waliochaguliwa na Bwana; ndiyo, aliwapenda watu wa Nefi, na pia amewakemea; ndiyo, katika siku zao za dhambi amewakemea kwa sababu anawapenda.
4 Lakini tazama ndugu zangu, amewachukia Walamani kwa sababu vitendo vyao vimekuwa viovu wakati wote, na wanafanya hivyo kwa sababu ya uovu wa desturi ya babu zao. Lakini tazama, wokovu umekuja kwao kupitia kwa mahubiri ya Wanefi; na kwa kusudi hili Bwana amewaongezea siku zao.
5 Na ningetaka kwamba mwone kwamba sehemu yao kubwa wako kwenye kazi yao, na wanatembea kwa uangalifu mbele ya Mungu, na wanatii amri zake na sheria zake na maamuzi yake kulingana na sheria ya Musa.
6 Ndiyo, ninawaambia, kwamba sehemu yao kubwa wanafanya hivi, na wanajaribu kwa bidii bila kuchoka ili walete ndugu zao waliosalia kwa elimu ya ukweli; kwa hivyo, kuna wengi ambao wanaongeza idadi yao kila siku.
7 Na tazama, mnajua wenyewe, kwani mmejionea, kwamba vile wengi wao wanaletwa kuelimishwa ukweli, na kujua uovu na desturi za machukizo za babu zao, na wameongozwa kuamini maandiko matakatifu, ndiyo, utabiri wa manabii watakatifu, ambao umeandikwa, ambao unawaongoza kuwa na imani kwa Bwana, na kwenye toba, imani na toba ambavyo huwaletea mabadiliko katika mioyo yao—
8 Kwa hivyo, vile wengi wamekuja kwa ukweli huu, mnajua wenyewe kwamba wako imara na thabiti katika imani, na pia kitu ambamo kwayo wamefanywa huru.
9 Na mnajua pia kwamba wamezika silaha zao za vita, na wanaogopa kuzichukua wasije kwa njia yoyote wafanye dhambi; ndiyo, mnaona kwamba wanaogopa kutenda dhambi—kwani tazama wanakubali wenyewe kwamba wakanyagwe chini na kuuawa na maadui wao, na hawatainua panga zao dhidi yao, na hivyo kwa sababu ya imani yao kwa Kristo.
10 Na sasa, kwa sababu ya uthabiti wao wakati wanaamini kwenye hicho kitu ambacho wanaamini, kwani kwa sababu ya uthabiti wao mara wakielimishwa, tazama, Bwana atawabariki na kuongeza siku zao, ijapokuwa ubaya wao—
11 Ndiyo, hata kama wanafifia kwa kutoamini Bwana ataongeza siku zao, mpaka wakati utatimia ambao umezungumzwa na babu zetu, na pia nabii Zeno, na manabii wengine wengi, kuhusu kurudishwa kwa ndugu zetu, Walamani, tena kwa ufahamu wa ukweli—
12 Ndiyo, nawaambia, kwamba katika siku za baadaye ahadi za Bwana zimeelekezwa kwa ndugu zetu, Walamani; na ijapokuwa mateso mengi ambayo watakuwa nayo, na ingawa watafukuzwa huku na kule duniani, na kuwindwa, na kushambuliwa na kutawanywa ugenini, wakiwa hawana mahali pa kimbilio, Bwana atawarehemu.
13 Na hii ni kulingana na unabii, kwamba watarejeshwa kwenye ufahamu wa ukweli, ambao ni ufahamu wa Mkombozi wao, na mchungaji wao mkuu na wa kweli, na kuhesabiwa miongoni mwa kondoo wake.
14 Kwa hivyo nawaambia, itakuwa bora kwao kuliko kwenu isipokuwa mtubu.
15 Kwani tazama, kama kazi kuu zingeonyeshwa kwao ambazo zimeonyeshwa kwenu, ndiyo, kwao ambao wamefifia kwa kutoamini kwa sababu ya desturi za babu zao, mnaweza kuona wenyewe kwamba hawangeweza tena kufifia kwa kutoamini.
16 Kwa hivyo, Bwana asema: Sitawaangamiza kabisa, lakini nitasababisha kwamba wakati nitaona ni hekima kwangu watanirudia, asema Bwana.
17 Na sasa tazama, asema Bwana, kuhusu watu wa Wanefi: Kama hawatatubu, na kujaribu kufanya yale ninayotaka, nitawaangamiza kabisa, asema Bwana, kwa sababu ya kutoamini kwao ijapokuwa kazi nyingi kubwa ambayo nimefanya miongoni mwao; na kwa ukweli vile Bwana anavyoishi vitu hivi vitafanyika, asema Bwana.