Mlango wa 2
Mormoni anaongoza majeshi ya Wanefi—Damu na mauaji yanajaa katika nchi—Wanefi wanalia na kuomboleza kwa huzuni ya waliolaaniwa—Siku yao ya neema imeisha—Mormoni anapata mabamba ya Nefi—Vita vinaendelea. Karibia mwaka 327–350 B.K.
1 Na ikawa kwamba katika mwaka huo huo kulianza kuwa na vita tena miongoni mwa Wanefi na Walamani. Na ingawaje mimi nikiwa kijana mdogo, nilikuwa mkubwa kwa kimo; kwa hivyo watu wa Nefi walinichagua kwamba niwe kiongozi wao, au kingozi wa majeshi yao.
2 Kwa hivyo ikawa kwamba katika mwaka wangu wa kumi na sita nilienda mbele kuliongoza jeshi la Wanefi, dhidi ya Walamani; kwa hivyo miaka mia tatu na ishirini na sita ilikuwa imepita.
3 Na ikawa kwamba katika mwaka wa mia tatu na ishirini na saba Walamani walitushambulia kwa nguvu nyingi sana, mpaka kwamba wakayatisha majeshi yangu; kwa hivyo hawangepigana, na walianza kurudi nyuma kuelekea nchi za kaskazini.
4 Na ikawa kwamba tulifika mji wa Angola, na tukaumiliki mji huo, na kufanya matayarisho kujilinda dhidi ya Walamani. Na ikawa kwamba tuliimarisha mji kwa nguvu zetu; lakini injapokuwa kuimarika kwetu Walamani walitushambulia na wakatufukuza hadi nje ya nchi.
5 Na walitukimbiza pia kutoka nchi ya Daudi.
6 Na tulienda mbele na tukafika nchi ya Yoshua, ambayo ilikuwa kwenye mipaka ya magharibi kando ya bahari.
7 Na ikawa kwamba tulikusanya watu wetu kwa haraka iwezekanavyo, ili tungewakusanya pamoja katika kundi moja.
8 Lakini tazama, nchi ilikuwa imejaa wanyangʼanyi na Walamani; na ingawaje kulikuwa na uharibifu mwingi ambao uliningʼinia juu ya watu wangu, hawakutubu vitendo vyao viovu; kwa hivyo kulikuwa na usambazaji wa mauaji na maangamizo kote usoni mwa nchi, kote kwenye sehemu ya Wanefi na pia kwenye sehemu ya Walamani; na ulikuwa upinduzi mmoja mkuu kote usoni mwa nchi.
9 Na sasa, Walamani walikuwa na mfalme, na jina lake lilikuwa Haruni; na alitushambulia na jeshi la elfu arubaini na nne. Na tazama, nilimzuia na watu elfu arubaini na mbili. Na ikawa kwamba nilimpiga na jeshi langu kwamba alitoroka mbele yangu. Na tazama, haya yote yalifanyika, na miaka mia tatu na thelathini ikawa imekwisha.
10 Na ikawa kwamba Wanefi walianza kutubu dhambi zao, na wakaanza kulalamika hata kama ilivyotabiriwa na nabii Samweli; kwani tazama hakuna mtu ambaye aliweza kuweka ile ambayo ilikuwa yake, kwa sababu ya wezi, na wanyangʼanyi, na wauaji, na ustadi wa uganga, na uchawi ambao ulikuwa katika nchi.
11 Hivyo kulianza kuwa na maombolezo na kulia katika nchi kwa sababu ya vitu hivi, na hasa zaidi miongoni mwa watu wa Nefi.
12 Na ikawa kwamba baada ya mimi, Mormoni, kuona kilio chao na maombolezo yao na huzuni yao mbele ya Bwana, moyo wangu ulianza kufurahi ndani yangu, kwa sababu nilijua huruma na uvumilivu wa Bwana, kwa hivyo nikidhani kwamba atakuwa na huruma kwao kwamba wangekuwa watu wa haki tena.
13 Lakini tazama hii shangwe yangu ilikuwa bure, kwani hii huzuni yao haikuwa ya toba, kwa sababu ya uzuri wa Mungu; lakini ilikuwa sana huzuni ya waliolaaniwa, kwa sababu Bwana hakuwaruhusu kufurahi katika dhambi.
14 Na hawakuja kwa Yesu na mioyo iliyovunjika na roho zilizopondeka, lakini walimlaani Mungu, na wakataka kufa. Hata hivyo wangepigana wakitumia upanga kwa maisha yao.
15 Na ikawa kwamba huzuni yangu ilinirudia tena, na niliona kwamba siku ya neema ilikuwa imepita na wao, kimwili pamoja na kiroho; kwani niliona maelfu wakiangushwa chini kwenye uasi wa wazi dhidi ya Mungu wao, na kurundikwa kama fungu la mbolea juu ya uso wa nchi. Na hivyo miaka mia tatu na arobaini na minne ilikuwa imepita.
16 Na ikawa kwamba katika mwaka wa mia tatu na hamsini na tano Wanefi walianza kutoroka mbele ya Walamani; na walifuatwa mpaka walipofika hata kwenye nchi ya Yashoni, kabla ya kuwezekana kuwazuia katika kukimbia kwao.
17 Na sasa, mji wa Yashoni ulikuwa karibu na nchi ambayo Amaroni alikuwa ameficha maandishi kwa Bwana, ili yasiharibiwe. Na tazama nilikuwa nimeenda kulingana na neno la Amaroni, na kuchukua mabamba ya Nefi, na niliandika kulingana na maneno ya Amaroni.
18 Na niliandika juu ya mabamba ya Nefi nakili kamili ya uovu na machukizo yote; lakini kwenye mabamba haya nilijizuia kuweka nakili kamili ya uovu wao na machukizo, kwani tazama, mfululizo wa kuonekana kwa uovu na machukizo umekuwa mbele ya macho yangu tangu nitoshee kuona mwenendo wa binadamu.
19 Na ole kwangu kwa sababu ya uovu wao; kwani moyo wangu umejawa na huzuni kwa sababu ya uovu wao, maisha yangu yote; walakini, ninajua kwamba nitainuliwa juu katika siku ya mwisho.
20 Na ikawa kwamba katika mwaka huu watu wa Nefi waliwindwa na kukimbizwa. Na ikawa kwamba tulikimbizwa mbele mpaka tulipofika kaskazini kwa nchi ambayo iliitwa Shemu.
21 Na ikawa kwamba tuliimarisha mji wa Shemu, na tuliwakusanya humo watu wetu kadri ilivyowezekana, ili labda tungewaokoa kutoka kwenye maangamizo.
22 Na ikawa katika mwaka wa mia tatu na arubaini na sita walianza kutushambulia tena.
23 Na ikawa kwamba niliwazungumzia watu wangu, nikiwasihi kwa juhudi kuu, kwamba wasimame kwa ujasiri mbele ya Walamani na kupigana kwa ajili ya wake zao, na watoto wao, na nyumba zao, na miji yao.
24 Na maneno yangu yaliwaamsha kidogo kuwa na nguvu, mpaka kwamba hawakukimbia kutoka mbele ya Walamani, lakini walisimama kwa ujasiri dhidi yao.
25 Na ikawa kwamba tulikabiliana na jeshi la elfu thelathini dhidi ya jeshi la elfu hamsini. Na ikawa kwamba tuliwazuia na uthabiti hivyo kwamba walikimbia kutoka mbele yetu.
26 Na ikawa kwamba baada ya kukimbia tuliwafuata na majeshi yetu, na tulipigana na wao tena, na tukawashinda; walakini nguvu za Bwana hazikuwa nasi; ndiyo, tuliachwa peke yetu, kwamba Roho wa Bwana haikuwa nasi; kwa hivyo tulikuwa tumekuwa wanyonge kama ndugu zetu.
27 Na moyo wangu ulihuzunika kwa sababu ya huu msiba mkubwa wa watu wangu, kwa sababu ya uovu wao na machukizo yao. Lakini tazama, tulienda mbele dhidi ya Walamani na wale wanyangʼanyi wa Gadiantoni, mpaka, tulipokuwa tena tumeimiliki nchi ya urithi wetu.
28 Na mwaka wa mia tatu na arubaini na tisa ukawa umepita. Na katika mwaka wa mia tatu na hamsini tuliweka mkataba na Walamani na wanyangʼanyi wa Gadiantoni, ambamo tulipata nchi zetu za urithi kugawanywa.
29 Na Walamani walitupatia nchi ya upande wa kaskazini, ndiyo, hata njia nyembamba iliyoelekea nchi ya kusini. Na tukawapatia Walamani nchi yote ya kusini.