Mlango wa 6
Wanefi wanajikusanya kwenye nchi ya Kumora kwa vita vya mwisho—Mormoni anaficha maandishi matakatifu katika kilima cha Kumora—Walamani wanashinda, na taifa la Wanefi linaangamizwa—Mamia ya maelfu wanachinjwa kwa upanga. Karibia mwaka 385 B.K.
1 Na sasa ninamaliza maandishi yangu kuhusu kuangamizwa kwa watu wangu, Wanefi. Na ikawa kwamba tulienda kutoka mbele ya Walamani.
2 Na mimi, Mormoni, niliandika barua kwa mfalme wa Walamani, na kumwuliza kwamba angetukubalia kwamba tukusanye watu wetu pamoja kwenye nchi ya Kumora, kando na kilima kilichoitwa Kumora, na hapo tungepigana nao.
3 Na ikawa kwamba mfalme wa Walamani alinikubalia kitu ambacho nilitaka.
4 Na ikawa kwamba tulienda mbele hadi kwenye nchi ya Kumora, na tukapiga hema zetu kuzunguka karibu na kilima Kumora; na ilikuwa katika nchi ya maji mengi, mito, na visima; na hapa tulikuwa na tumaini la kufaidika juu ya Walamani.
5 Na baada ya miaka mia tatu na themanini na nne kupita, tulikuwa tumekusanya watu wote waliosalia kwenye nchi ya Kumora.
6 Na ikawa kwamba baada ya kuwakusanya watu wetu wote pamoja katika nchi ya Kumora, tazama mimi, Mormoni, nilianza kuzeeka; na nikijua kwamba ni juhudi ya mwisho ya watu wangu, na nikiwa nimeamriwa na Bwana kwamba nisiyaache maandishi ambayo yametolewa kutoka zamani na babu zetu, ambayo ni matakatifu, kuchukuliwa na Walamani, (kwani Walamani wangeyaharibu) kwa hivyo nilitengeneza maandishi haya kutoka kwenye mabamba ya Nefi, na nikayaficha katika kilima cha Kumora maandishi yote ambayo yalikuwa yamekabidhiwa kwangu na mkono wa Bwana, isipokuwa mabamba haya chache ambayo nilimpatia mwana wangu Moroni.
7 Na ikawa kwamba watu wangu, na wake zao na watoto wao, sasa waliona majeshi ya Walamani yakisonga kuwaelekea; na kwa ule woga wa kutisha wa kifo ambao unajaa vifua vya waovu wote, walingoja washambuliwe.
8 Na ikawa kwamba walikuja kupigana dhidi yetu, na kila nafsi ilijawa na hofu kwa sababu ya wingi wa idadi yao.
9 Na ikawa kwamba walishambulia watu wangu kwa panga, na kwa pinde, na kwa mshale, na kwa shoka, na kwa kila aina ya silaha za vita.
10 Na ikawa kwamba watu wangu waliangushwa chini, ndiyo, hata elfu wangu kumi ambao walikuwa na mimi, na nilijeruhiwa nikaanguka katikati; na walipita kando yangu kwamba hawakumaliza maisha yangu.
11 Na baada ya kupita na kuangusha chini watu wangu wote isipokuwa sisi ishirini na wanne, (miongoni ambamo kulikuwa na mwana wangu Moroni) na sisi tukiwa tumenusurika kifo cha watu wetu, tulitazamia kesho yake baada ya Walamani kurudi kwenye vituo vyao, kutoka juu ya kilima Kumora, wale watu wangu elfu kumi ambao waliangushwa chini, wakiwa wameongozwa mbele na mimi.
12 Na pia tuliona wale elfu kumi ambao waliongozwa na mwana wangu Moroni.
13 Na tazama, elfu kumi wa Gidgidona walikuwa wameanguka, na yeye pia akiwa katikati.
14 Na Lama alikuwa ameanguka na wale wake elfu kumi; na Gilgali alikuwa ameanguka na wale wake elfu kumi; na Limha alikuwa ameanguka na wale wake elfu kumi; na Yeneumu alikuwa ameanguka na wale wake elfu kumi; na Kumeniha, na Moroniha, na Antionumu, na Shiblomu, na Shemu, na Yoshi, walikuwa wameanguka kila mmoja na wale wao elfu kumi.
15 Na ikawa kwamba kulikuwa na kumi zaidi walioanguka kwa upanga, kila mmoja na elfu kumi wao; ndiyo, hata watu wangu wote, isipokuwa wale ishirini na wanne waliokuwa na mimi, na pia wachache waliotorokea nchi za kusini, na wachache ambao walikimbia hadi kwa Walamani, walikuwa wameanguka; na miili yao, na mifupa, na damu vilitapakaa juu ya uso wa nchi, wakiwa wameachwa na wale ambao waliwachinja kuozea juu ya udongo, na kugeuka mavumbi na kurudi kwenye udongo walikotoka.
16 Na nafsi yangu ilipasuka kwa uchungu, kwa sababu ya mauaji ya watu wangu, na nililia:
17 Ee ninyi wenye umbo nzuri, ilikuwaje mkatoka kwenye njia ya Bwana! Ee ninyi wenye umbo nzuri, ilikuwaje mkamkataa Yesu, ambaye aliwangojea na mikono wazi kuwapokea!
18 Tazama, kama hamngefanya hivi, hamngekufa. Lakini tazama, mmekufa, na ninaomboleza kupotea kwenu.
19 Ee ninyi wana wa umbo nzuri, ninyi baba na mama, ninyi mabwana na wake, ninyi walio wazuri, vipi kwamba mmekufa!
20 Lakini tazama, mmetokomea, na huzuni yangu haiwezi kuwarejesha.
21 Na wakati unakuja upesi kwamba miili yenu yenye kufa itajivika kutokufa, na miili hii ambayo sasa inaoza kimwili lazima upesi itakuwa isiyooza; na hapo lazima mtasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, kuhukumiwa kulingana na vitendo vyenu; na ikiwa kwamba ninyi ni wenye haki, hasi mmebarikiwa na babu zenu ambao wamekufa mbele yenu.
22 Ee ingekuwa kwamba mlitubu kabla ya hili angamizo kuja kwenu. Lakini tazama, mmekufa, na Baba, ndiyo, Baba wa Milele wa mbinguni, anajua hali zenu; na anawafanyia kulingana na haki na rehema yake.