Sehemu ya 130
Orodha ya mafundisho yaliyotolewa na Joseph Smith Nabii, huko Ramus, Illinois, 2Â Aprili 1843.
1–3, Baba na Mwana wao wenyewe wanaweza kujionyesha kwa mwanadamu; 4–7, Malaika huishi katika mazingira ya selestia; 8–9, Dunia ya kiselestia itakuwa Urimu na Thumimu iliyo kuu; 10–11, Jiwe jeupe linatolewa kwa wote waingiao kwenye ulimwengu wa selestia; 12–17, Wakati wa Ujio wa Pili Nabii amefichwa; 18–19, Akili ipatikanayo katika maisha haya itafufuka pamoja nasi katika Ufufuko; 20–21, Baraka zote huja kwa kutii sheria; 22–23, Baba na Mwana wana miili ya nyama na mifupa.
1 Wakati Mwokozi atakapojidhihirisha tutamwona kama alivyo. Tutamwona kuwa yeye ni mtu kama sisi wenyewe.
2 Na kwamba uhusiano huu huu uliopo miongoni mwetu hapa utakuwepo miongoni mwetu kule, isipokuwa utazidishiwa utukufu wa milele, utukufu ambao sasa hatuufaidi.
3 Yohana 14:23—Kuonekana kwa Baba na Mwana, katika mstari ule, ni kujidhihirisha binafsi; na wazo la kwamba Baba na Mwana watakaa katika moyo wa mwanadamu ni wazo la zamani la kimadhehebu, na ni uongo.
4 Kama jibu kwa swali—Je, si kweli kwamba jinsi wakati unavyopimwa kwa Mungu, kwa malaika, kwa manabii, na kwa wanadamu, hutegemea na sayari ambayo wao huishi?
5 Najibu, Ndiyo. Lakini hakuna malaika ambao huhudumia dunia hii ila wale ambao ni wa dunia hii, au walikuwa wa dunia hii.
6 Malaika hawaishi katika sayari kama hii dunia;
7 Bali huishi mbele za Mungu, kwenye tufe mfano wa bahari ya kioo na moto, mahali ambapo mambo yote kwa ajili ya utukufu wao huonekana, yaliyopita, yaliyopo, na yajayo, na daima yapo mbele za Bwana.
8 Mahali ambapo Mungu hukaa ni Urimu na Thumimu iliyo kuu.
9 Dunia hii, katika hali yake ya kutakaswa na isiyokufa, itafanywa kuwa mfano wa jiwe angavu kama kioo nayo itakuwa Urimu na Thumimu kwa wakazi wakaao juu yake, humo mambo yote yahusuyo ufalme mdogo, au falme zote za daraja la chini, zitaonekana kwa wale wakaao juu yake; na dunia hii itakuwa ya Kristo.
10 Ndipo jiwe jeupe lililotajwa katika Ufunuo 2:17, litakapokuwa Urimu na Thumimu kwa kila mmoja aliyepokea moja, ambalo kwalo hilo mambo yote yahusuyo falme za daraja la juu zitajulikana;
11 Na jiwe jeupe limetolewa kwa kila mmoja wa wale wanaokuja katika ufalme wa selestia, ambapo juu yake jina jipya limeandikwa, ambalo hakuna mtu ajuaye isipokuwa yeye yule mwenye kulipokea. Jina hilo jipya ni neno la ufunguo.
12 Ninatoa unabii, katika jina la Bwana Mungu, kwamba kuanza kwa matatizo ambayo yatasababisha umwagaji mkubwa wa damu kabla ya kuja kwa Mwana wa Mtu yataanzia Carolina ya Kusini.
13 Huenda ikaanza kutokana na swali la utumwa. Hii sauti iliniambia, wakati nilipokuwa nikiomba kwa dhati juu ya jambo hili, Desemba, 25, 1832.
14 Nilikuwa wakati mmoja nikiomba kwa dhati kujua wakati wa kuja kwa Mwana wa Mtu, wakati niliposikia sauti ikirudia yafuatayo:
15 Joseph, mwanangu, kama wewe utaishi mpaka kufikia umri wa miaka themanini na tano, utauona uso wa Mwana wa Mtu; kwa hiyo, acha hiyo yatosha, acha usinisumbue zaidi juu ya jambo hili.
16 Hivyo niliachwa, bila kuweza kuamua kama ujio huu unaozungumziwa ni kuanzia kwa milenia au ni baadhi ya kuonekana kwake kabla, au kama lazima nife na hivyo ndipo niuone uso wake.
17 Ninaamini ujio wa Mwana wa Mtu hautakuwa mapema kabla ya wakati huo.
18 Kanuni yoyote ya akili tuipatayo katika maisha haya, itafufuka pamoja nasi katika ufufuko.
19 Na kama mtu anapata maarifa na akili katika maisha haya kwa njia ya juhudi yake na utii kuliko mwingine, yeye atakuwa na heri ya juu zaidi katika ulimwengu ujao.
20 Kuna sheria, isiyotenguliwa iliyowekwa mbinguni kabla ya misingi ya ulimwengu huu, ambapo juu yake baraka zote hutoka—
21 Na kama tunapata baraka yoyote kutoka kwa Mungu, ni kutokana na utii kwa sheria ile ambayo juu yake hutoka.
22 Baba ana mwili wa nyama na mifupa wenye kushikika kama wa mwanadamu; na Mwana vile vile; lakini Roho Mtakatifu hana mwili wa nyama na mifupa, bali ni mtu wa Kiroho. Kama isingekuwa hivyo, Roho Mtakatifu asingeweza kukaa ndani yetu.
23 Mwanadamu aweza kumpokea Roho Mtakatifu, na anaweza kushukia juu yake na asikae pamoja naye.