Sehemu ya 24
Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Oliver Cowdery, huko Harmony, Pennsylvania, Julai 1830. Ijapokuwa si zaidi ya miezi minne kupita toka Kanisa lianzishwe, mateso yamekuwa makali, na viongozi iliwabidi watafute usalama kwa kujitenga na wengine. Mafunuo matatu yanayofuata yalitolewa kwa wakati huo ili kuwaimarisha, kuwahamasisha, na kuwaelekeza.
1–9, Joseph Smith ameitwa ili kutafsiri, kuhubiri, na kuelekezea maandiko; 10–12, Oliver Cowdery ameitwa ili kuhubiri injili; 13–19, Sheria imefunuliwa kuhusiana na miujiza, laana, kukungʼuta mavumbi ya miguu, na kwenda pasipo mfuko wala mkoba.
1 Tazama, wewe uliitwa na kuteuliwa kuandika Kitabu cha Mormoni, na katika huduma yangu; nami nimekutoa katika dhiki zako, na nimekushauri, nikisema kwamba umeponywa kutoka kwa maadui zako, na wewe umeponywa kutoka katika nguvu za Shetani na za giza!
2 Hata hivyo, wewe huna udhuru katika uvunjaji wako wa sheria; kwa hivyo, enenda zako, wala usitende dhambi tena.
3 Itukuze ofisi iliyo yako; na baada ya kuwa umepanda mashamba yako na kuyalinda, nenda haraka katika kanisa lililoko Colesville, Fayette, na Manchester, na wao watakukimu; na Mimi nitawabariki vyote kiroho na kimwili;
4 Lakini kama hawatakupokea wewe, nitapeleka juu yao laana badala ya baraka.
5 Na wewe utaendelea katika kumlingana Mungu katika jina langu, na kuandika mambo ambayo yatatolewa kwako na Mfariji, na kuelezea maandiko yote kwa kanisa.
6 Na itatolewa kwako saa ile ile utakayosema na kuandika, na wao watayasikia, au nitapeleka juu yao laana badala ya baraka.
7 Kwani wewe utajitolea utumishi wako wote katika Sayuni; na katika hili, utakuwa na nguvu.
8 Kuwa mvumilivu katika mateso, kwani utapata mengi; lakini utayastahimili, kwani, lo, Mimi nipo pamoja nawe, hata mwisho wa siku zako.
9 Na kazi za kimwili wewe hutakuwa na nguvu, kwani, huo siyo wito wako. Tekeleza wito wako ambao unao kwa kuitukuza ofisi uliyo nayo, na kuyaelezea maandiko yote, na kuendelea katika kuwawekea mikono na kuyathibitisha makanisa.
10 Na ndugu yako Oliver ataendelea katika kulichukua jina langu mbele ya ulimwengu, na pia kwa kanisa. Na hapaswi kudhani kwamba ataweza kusema ya kutosha katika kazi yangu; na lo, Mimi nipo pamoja na yeye hata mwisho.
11 Ndani yangu atapata utukufu, na siyo kutoka kwake mwenyewe, iwe katika udhaifu au katika nguvu, iwe katika utumwa au huru;
12 Na kwa nyakati zote, na katika mahali pote, yeye atafumbua kinywa chake na kutangaza injili yangu kama vile kwa sauti ya baragumu, usiku na mchana. Na nitampa yeye nguvu ambazo hazijawahi kujulikana miongoni mwa wanadamu.
13 Usiombe miujiza, ila nitakapokuamuru, isipokuwa kwa kutoa mapepo, kuwaponya wagonjwa, na dhidi ya nyoka wenye sumu, na dhidi ya sumu zenye kufisha;
14 Na mambo haya usiyafanye, isipokuwa utakapohitajika kufanya na wale wenye kutaka, ili kwamba maandiko yapate kutimia; kwani itakupasa kufanya kulingana na yale yaliyoandikwa.
15 Na katika mahali popote mtakapoingia, na wasipo wakaribisha katika jina langu, mtaacha laana badala ya baraka, kwa kukungʼuta vumbi la miguu yenu dhidi yao kama ushuhuda, na kusafisha miguu yenu njiani.
16 Na itakuwa kwamba yeyote atakayeweka mikono yake juu yenu akiwakamata kwa fujo, mtaamuru apigwe katika jina langu, na, tazama nitawapiga kulingana na maneno yako, katika wakati wangu mwenyewe.
17 Na yeyote atakaye wapeleka mbele ya sheria atalaaniwa kwa sheria.
18 Na msichukue mfuko wala mkoba, wala fimbo, wala makoti mawili, kwani kanisa litawapatia katika saa ile ile mtakapohitaji chakula na mavazi, na kwa viatu na kwa fedha, na kwa mkoba.
19 Kwani wewe umeitwa kupogoa shamba langu la mizabibu kwa kupogoa kwenye nguvu, ndiyo, hata kwa mara ya mwisho; ndiyo, na pia kwa wale wote ambao wewe umewatawaza, na watafanya kulingana na utaratibu huu. Amina.