2021
Misingi Imara
Machi 2021


“Misingi Imara,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2021, 14–15.

Misingi Imara

Ukuta wa Kupanda

Picha
wasichana kwenye mahali pa kupandia ukuta

Vielelezo na Alyssa Petersen

Wasichana ishirini walisimama kando yangu, wakikodolea macho ukuta wa mbao wa futi 16. Changamoto yetu ilikuwa kumsaidia kila msichana kufika juu. Kwa wengi wa wasichana hao, huu ulikuwa mwaka wao wa kwanza kuhudhuria kambi ya Wasichana. Wasichana wakubwa pamoja nami ndio tulikuwa viongozi wa vijana, lakini ilikuwa mara yetu ya kwanza kushiriki katika shughuli kama hii. Sote tulisikiliza sheria kwa umakini.

Kila msichana alihitajika kupanda ukuta. Baada ya mmoja kufika juu, angesimama kwenye jukwaa kisha awavute wengine juu. Hata hivyo, ikiwa angegusa chini, asingeruhusiwa tena kusaidia kuwainua wasichana waliosalia.

Tulihangaika mwanzoni, lakini baada ya muda mfupi tuliweza kushirikiana na kuanza kuwainua wasichana. Baadhi yao waliogopa kuinuliwa juu sana licha ya usalama kutiliwa maanani. Wengine walikuwa na wasiwasi kutumia nguvu zao wenyewe kufika juu. Tulihitajika sote kuaminiana na kusaidiana zaidi. Mwishowe, tulikamilisha shughuli kwa ufanisi.

Wakati msichana wa mwisho alipokuwa akishuka chini, tulikusanyika kujadiliana mambo mengi ya kujifunza kutokana na shughuli ya kupanda ukuta.

Sote tunakabiliana na mambo yanayoonekana kuwa hayawezekani. Hata hivyo, hatupo peke yetu. Watu wametuzunguka kote ili kusaidia kutuinua na kutoa usaidizi. Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wapo ili kutusaidia na kututia nguvu wakati tunapowaelekea.

Megan B., Ohio, Marekani

“Niliahidi Ningekuja”

Picha
wavulana

Siku zote nimekuwa na hamu ya kushiriki injili na watu wengine, lakini kwa miaka mingi sikufanikiwa. Hadi tulipokuwa marafiki na kijana aliyejulikana kama Tiago. Tuliishi karibu, hivyo tulikwenda nyumbani pamoja tukitoka shuleni kila siku.

Siku moja, tulitumia njia nyingine na tukapita nje ya kanisa nililokuwa nikishiriki. Nilimweleza kwamba nimekuwa muumini wa Kanisa kwa muda mrefu. Nilimweleza kile tunachoamini na jinsi familia yangu ilivyokuwa imebarikiwa kupitia hilo. Nilimwalika Tiago kanisani Jumapili hiyo, na akasema kuwa angekuja.

Jumapili ilifika, na nilimsubiri kwa hamu kanisani, lakini hakuja. Baadaye wiki hiyo, nilimwalika tena. Hili liliendelea kwa miezi miwili au mitatu, lakini kila wakati alikuwa na sababu ya kutokuja. Lakini niliendelea kumwalika.

Jumapili moja asubuhi, nilikuwa kwenye mkutano wa sakramenti na nilipoangalia nilimwona Tiago amesimama hapo. Nilishangaa kumwona, lakini alikuja nilipokuwa na akaketi kando yangu kisha akasema, “Niliahidi Nitakuja!”

Nilimtambulisha kwa wamisionari na wakaanza kumfundisha. Baadaye, alibatizwa. Kwa sasa sote tunajiandaa kwenda kwenye misheni. Ninafurahi sana kuwa sikuacha kumwalika!

Meiry R., Brazili

Tumaini katika Wakati wa Mungu

Shangazi yangu alitalikiwa baada tu ya mwanawe wa kwanza wa kiume kubatizwa. Ili kudumisha uhusiano wa amani kati yake na baba wa watoto wake, alimwomba ruhusa kabla ya kuwabatiza watoto wake wengine. Kwa bahati mbaya, alimnyima ruhusa kwa miaka mingi.

Hatimaye, shangazi yangu aliamua kuwa watoto wake watabatizwa licha ya baba yao kukataa. Lakini baada ya shangazi na binamu zangu kufunga na kuomba kuhusu uamuzi huu, kila mtu alipokea msukumo kuwa walipaswa kuendelea kusubiri.

Wiki hiyo hiyo, baba wa binamu zangu alimweleza shangazi yangu kuwa alitaka watoto wakutane na wamisionari ili wabatizwe. Bado nakumbuka furaha niliyohisi wakati mama yangu aliponieleza habari hizi. Nilijua kuwa Baba wa Mbinguni alikuwa amewabariki binamu zangu baada ya wao kusubiri kwa miaka mingi.

Huenda siku zote tusifahamu wakati ambapo Bwana atajibu maombi yetu, lakini najua kuwa hakika Atajibu. Sijui ni kwa nini Baba wa Mbinguni alitaka binamu zangu wasubiri kubatizwa, lakini ninafahamu kuwa Aliwabariki kwa sababu ya uaminifu wao.

Bre J., Florida, Marekani

Chapisha