2021
Kiini cha pasaka: Yesu Kristo Aliye Hai
Machi 2021


“Kiini cha pasaka: Yesu Kristo Aliye Hai,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi. 2021, 2–5.

Kiini cha pasaka: Yesu Kristo Aliye Hai

Katika kusherehekea Pasaka, tunashangilia kwamba Yesu Kristo yu hai sasa na kwa ajili yetu sote.

Picha
Yesu Kristo akiingia Yerusalemu kwa kutumia punda

Katika msimu huu wa Pasaka, tunamsherehekea Yesu Kristo aliye hai. Kwa upendo mkamilifu, Mwokozi wetu anatuhakikishia: “Mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33).

Katika kusherehekea Pasaka, tunashangilia kwamba Yesu Kristo yu hai—siyo tu hapo kale, bali sasa; si tu kwa wachache, lakini kwa wote. Alikuja na anakuja kuwaponya waliovunjika mioyo, kuwakomboa mateka, kuwaponya vipofu, na kuwaweka huru wale walioumia (ona Luka 4:18). Hao ni kila mmoja wetu. Ahadi zake za ukombozi zinatumika, bila kujali mambo yetu ya zamani, ya sasa, au wasiwasi wetu kwa ajili ya baadaye.

Hosana na Haleluya

Kwenye Jumapili ya mitende, Yesu aliingia Yerusalemu akiwa juu ya mwanapunda na watu “wengi … wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki” (Yohana 12:12–13; ona pia Mathayo 21:8–9; Marko 11:8–10). Kwa utamaduni, mitende ni ishara takatifu ya kuelezea shangwe katika Bwana wetu. Waaminifu walitambua hili kama utimizwaji wa unabii na kwa ufahamu walipaza sauti, “Hosana juu mbinguni” (Mathayo 21:9). Hosana maana yake ni “okoa sasa” (ona Kamusi ya Biblia, “Hosanna”).

Wiki moja baada ya Jumapili ya Mitende ni Jumapili ya Pasaka. Rais Russell M. Nelson anafundisha kwamba Yesu Kristo “alikuja kulipa deni ambalo si Lake kwa sababu tulikuwa na deni ambalo tusingeweza kulipa.”1 Hakika, kupitia Upatanisho wa Kristo, watoto wote wa Mungu “wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili” (Makala ya Imani 1:3). Wakati wa Pasaka, tunaimba haleluya. Haleluya maana yake ni “usifiwe wewe Bwana Yehova” (ona Kamusi ya Biblia, “Hallelujah”).

Matukio matakatifu kati ya Jumapili ya Mitende na Jumapili ya Pasaka ni hadithi ya hosana na haleluya. Hosana ni ombi letu kwa Mungu kuokoa. Haleluya inaelezea sifa yetu kwa Bwana kwa tumaini la wokovu na kuinuliwa. Katika hosana na haleluya tunamtambua Yesu Kristo aliye hai kama kiini cha Pasaka.

Picha
Yesu Kristo

Urejesho na Ufufuo

Mnamo Jumapili ya Pasaka, Aprili 3, 1836, katika siku za mwanzo za Urejesho, Yesu Kristo aliye hai alionekana baada ya Hekalu la Kirtland kuwekwa wakfu. Wale waliomuona Yeye huko walimshuhudia katika tofauti zinazoambatana na moto na maji: “Macho yake yalikuwa kama mwale wa moto; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama theluji safi; uso wake ulinga’ra kupita mng’aro wa jua; na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yakimbiayo, hata sauti ya Yehova” (Mafundisho na Maagano 110:3; msisitizo umeongezwa).

Kwenye tukio hilo, Mwokozi wetu alitangaza, “Mimi ni mwanzo na mwisho; Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa; Mimi ni Mwombezi wenu kwa Baba” (Mafundisho na Maagano 110:4). Tena, tofauti zinazoambatana—mwanzo na mwisho, hai na kuuwawa. Yeye ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho (ona Ufunuo 1:8; 3 Nefi 9:18; Mafundisho na Maagano 19:1; 38:1; 45:7), mwanzilishi na mtimizaji wa imani yetu (ona Waebrania 12:2; Moroni 6:4).

Kufuatia kuonekana kwa Yesu Kristo, Musa, Elia, na Eliya pia walikuja. Kwa mwongozo mtakatifu, manabii hawa wakuu wa kale walirejesha funguo na mamlaka ya ukuhani. Kwa hivyo, “funguo za kipindi hiki cha nyakati zimekabidhiwa” (Mafundisho na Maagano 110:16) ndani ya Kanisa Lake lililorejeshwa ili kuwabariki watoto wote wa Mungu.

Kwa umuhimu, Kitabu cha Mormoni kinaelezea “nguvu na ufufuko wa Kristo” (Alma 41:2)—kiini cha Pasaka—katika urejesho wa aina mbili.

Kwanza, ufufuo unajumuisha urejesho wa kimwili wa “umbo sahihi na kamilifu”; “kila sehemu na kiungo,” “hata nywele ya kichwa haitapotea” (Alma 40:23). Ahadi hii inatoa tumaini kwa wale waliopoteza viungo; wale waliopeteza uwezo wa kuona, kusikia, au kutembea; au kumbukumbu zile zilizopotea kwenye ugonjwa wa kudhoofisha mwili, ugonjwa wa akili, au uwezo mwingine hafifu. Yeye anatutafuta sisi. Anatufanya tuwe wazima.

Ahadi ya pili ya Pasaka na Upatanisho wa Bwana wetu ni kwamba, kiroho, “vitu vyote vitarudishwa kwenye hali yake ya kawaida” (Alma 41:4). Urejesho huu wa kiroho unaangazia kazi zetu na matamanio yetu. Unarejesha “kile kilicho chema,” “adilifu,” “haki,” na “chenye rehema” (Alma 41:13). Haishangazi kwa nabii Alma kutumia neno rejesha mara 222 pale anapotutaka sisi “kutenda haki, kuhukumu kwa haki, na kutenda mema kila mara” (Alma 41:14).

Kwa sababu “Mungu mwenyewe alimwaga damu kwa dhambi za ulimwengu” (Alma 42:15), Upatanisho wa Bwana unaweza kurejesha si tu kilichokuwepo bali pia kile kinachoweza kuwa. Kwa sababu anajua maumivu yetu, mateso, magonjwa, “majaribu yetu ya kila aina” (Alma 7:11), Yeye anaweza, kwa rehema, kutusaidia kulingana na unyonge wetu (ona Alma 7:12). Kwa sababu Mungu ni “mkamilifu, Mungu wa haki, na pia Mungu wa rehema,” mpango wa rehema unaweza “kuwezesha mahitaji ya haki” (Alma 42:15). Tunatubu na kutenda yote tunayoweza. Anatuzingira milele “katika mikono ya upendo wake” (2 Nefi 1:15).

Kuimba Nyimbo za Shangwe ya Milele

Pamoja nanyi, msimu huu wa Pasaka, ninatoa ushuhuda wa Mungu, Baba yetu wa Milele, na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo aliye hai. Wanadamu walisulubiwa kikatili na baadaye wakafufuliwa. Lakini Yesu Kristo aliye hai pekee katika hali Yake kamilifu ya ufufuko bado ana alama za vidonda mikononi, miguuni, na ubavuni Mwake. Ni Yeye pekee Anayeweza kusema, “Nimewachora kwenye viganja vya mikono yangu” (Isaya 49:16; 1 Nefi 21:16). Ni yeye pekee Anayeweza kusema: “Mimi ndiye yule aliyeinuliwa. Mimi ni Yesu ambaye alisulubiwa. Mimi ni Mwana wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 45:52).

Katika nyakati hizi, tunaweza kujifunza mengi juu ya wema wa Mungu na uwezekano wetu mtakatifu kwa upendo wa Mungu kukua ndani yetu pale tunapomtafuta Yeye na kumfikia kila mmoja.“ Na itakuwa kwamba wenye haki watakusanywa kutoka miongoni mwa mataifa yote, nao watakuja Sayuni, wakiimba nyimbo za shangwe isiyo na mwisho” (Mafundisho na Maagano 45:71). Katika kipindi hiki cha hosana na haleluya, imba haleluya—kwani Atatawala milele na milele! Paza sauti ya hosana, kwa Mungu na Mwanakondoo!

Chapisha