2021
Kama Dirisha Kwenye Nafsi Yako
Machi 2021


“Kama Dirisha Kwenye Nafsi Yako,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Machi 2021, 6–8.

Kama Dirisha Kwenye Nafsi Yako

Walipoimba katika kwaya ya kata yao kwenye tamasha la madhehebu tofauti, vijana hawa walijifunza mengi kuhusu jinsi muziki unavyoweza kuwaleta waumini wote pamoja.

vijana watatu

Megan C., Ethan M., na Romy C. wanafanana kwa kitu kimoja: Wanapenda muziki wa unyenyekevu. Wanapenda jinsi unavyowainua na kuwapa mwongozo wa kiungu, jinsi unavyowafanya wahisi. Na wanapenda kuona jinsi unavyowainua na kuwapa mwongozo wa kiungu watu wengine.

Megan, 18; Ethan, 19; na Romy, 17, pia wanafanana kwa kitu kingine: Wote wanaimba katika kwaya ya kata yao ya Florida, Marekani. Na hivi karibuni kwaya yao iliwapa fursa kubwa zaidi ya kueneza upendo wao wa muziki kwa kushiriki kwenye Tamasha la Muziki la Madhehebu Tofauti.

“Jumuiya yetu ina muungano wa madhehebu tofauti ambao unafanya mambo mengi ya kuwaleta pamoja watu wa madhehebu tofauti,” Ethan anafafanua. Kwa mfano, kikundi hiki kiliandaa mazungumzo wakati wa futari (chakula cha jioni kinacholiwa na Waislamu wanapokamilisha mfungo wa kila siku katika mwezi mtukufu wa Ramadhani), kilipanga miradi ya kutoa huduma kwa jamii kama vile kutayarisha mikoba ya wanafunzi kwa watoto wenye uhitaji, na mara kadhaa kiliandaa matukio ambapo chakula cha jioni kililetwa, ambapo watu ambao hawakufahamiana waliketi kando ya kila mmoja kwenye meza moja na kuzungumza kuhusu chakula, mila na imani zilizopendwa katika tamaduni zao.

vijana wakila, wakiimba na wakihudumu

Wanakwaya hufurahia kula chakula cha jioni na kuhudumu pamoja na wale wa madhehebu tofauti.

Acha Tuwe Marafiki

Lengo la muungano, bila shaka, ni kuwasaidia watu wa jamii tofauti tofauti kuwa marafiki.

“Kuna familia ya Kituruki ambayo mimi huiona kila wakati kwenye matukio ya chakula cha jioni cha madhehebu tofauti, na wao huja nilipo na kuniambia, ‘Tumefurahi sana kukuona tena!’” Romy anasema. “Katika ulimwengu ambapo kuna mateso mengi kwa misingi ya imani na dini, ni vyema kuwa sote tunaweza kuja pamoja na kuzungumza.” Katika mojawapo ya miradi ya kutoa huduma kwa jamii, “wanawake wa kanisa lingine walikuwa wenye fadhila sana,” anasema. “Hawakujali kuhusu dini ya mtu yeyote. Walijumuika pale ili tu kutoa usaidizi wao. Ilikuwa ya kutia moyo.”

“Inawezekana tunaamini vitu tofauti,” Megan anasema, “lakini daima ninaheshimu imani za watu wengine na imekuwa ya kuvutia kujihusisha nao hapa kwani sote tuna hamu ya kufahamiana.”

“Kanisa letu ni mojawapo ya yaliyojiunga kwenye muungano hivi karibuni tu,” Ethan anasema. “Hivyo nilithamini sana ukarimu wao kwetu na jinsi walivyotukubali. Ninafahamu kuwa katika sehemu fulani fulani, watu wanalikosoa Kanisa. Hivyo mimi huthamini kila wakati watu wanaporidhiana licha ya tofauti zao na kuzingatia kile kinachowaunganisha.”

Wa Moyo Mmoja

Na kitu kimoja ambacho ni sawa kwa madhehebu yote ni muziki. Tamasha la Muziki la Madhehebu Tofauti ingekuwa fursa nzuri kwa waumini kujumuika katika kumsifu Mungu. Kwaya ya kata ingekuwa mojawapo ya takribani vikundi sita vilivyowakilisha mkusanyiko kote katika jiji.

“Kulikuwepo na kwaya ya kupiga kengele, kikundi cha waimbaji wawili, kwaya ya watu wengi, kwaya ya watu wachache, kikundi cha mcheza kinanda na mcheza zumari, na kadhalika,” Megan anaeleza. “Kila kikundi kiliombwa kufanya nyimbo mbili.”

Megan anaendelea, “Tulitaka kuhakikisha kuwa nyimbo tulizoimba zingewajulisha watu kuwa tunamwamini Yesu Kristo na pia kwamba tunamwamini Baba wa Mbinguni. Tulitaka kuchochea hali ya kuabudu.”

Kwaya iliamua kuimba nyimbo mbili ambazo ilikuwa imeziimba awali, “Mambo Makubwa na Mambo Madogo,” wa Steven Kapp Perry, na “Sakramenti na Ishara,” wa Janice Kapp Perry, Steven Kapp Perry na Lynne Perry Christofferson.

“Wimbo wa kwanza ulikuwa mchangamfu. Unatoa hakikisho kuwa kupitia Mungu, hakuna kisichowezekana, iwe ni jambo dogo au muhimu sana,” Ethan anasema. “Wimbo wa pili una unyenyekevu mkubwa. Ni kama zaburi na unachochea hali halisi ya kuabudu.”

Mazoezi, Mazoezi, Mazoezi

Walipokuwa wakijiandaa kuimba, Ethan alitumia kanuni ambayo alikuwa amewahi kuitumia awali. “Mimi hujaribu kuzingatia kuzama kwenye wimbo,” anasema. “Nimegundua kuwa ninapoweka umakini kwenye ujumbe ulio kwenye wimbo, mimi huufurahia zaidi. Bila shaka huwa ninajizatiti kuuimba wimbo huo vizuri, lakini ninaona kwamba ni rahisi zaidi kwangu kufanya hivyo wakati ninapokuwa kwenye tuni na ujumbe ambao unatolewa na wimbo. Napenda kuweka msisitizo kwenye maandalizi ya kiroho.”

“Bado tulitakiwa kuimba katika mkutano wa sakramenti na kufanya mazoezi kwa ajili ya vitu vingine pia,” Megan anasema. “Lakini tulifahamu umuhimu wa hafla ya madhehebu tofauti, hivyo tulihakikisha mawasilisho yalikuwa tayari. Tulijitahidi katika kufanya mazoezi.”

Kwa wimbo wa pili, idadi ya wanakwaya ilipungua kutoka 14 hadi nane. “Tulifanya mazoezi kila Jumanne, mbele ya Wavulana na Wasichana,” Megan anasema. “Hili lilinifanya niufikirie wimbo kwa wiki nzima, kwa mwezi mzima, hakika. Kawaida huwa sifanyi hivi, lakini niliupata wimbo kwenye YouTube na nikaishia kuupiga tena na tena. Nilitaka kuimarika. Nilitaka tuimbe vizuri zaidi kwamba tuguse mioyo ya watu wengine.”

Ethan, Megan na Romy wanakiri kuwa mazoezi yote yalikuwa na ongezeko la manufaa. “Unaporudia nyimbo tena na tena,” Romy anasema, “jumbe zilizo kwenye nyimbo husalia akilini na moyoni mwako.”

kwaya ya vijana

Kwaya ikiimba kwenye Tamasha la Muziki la Madhehebu Tofauti.

Akilini, Moyoni

Uwepo huo wa akilini na moyoni ulikuwa dhahiri wakati wanakwaya walipokuwa wakiimba. “Nyimbo zote mbili zilipendeza,” Romy anasema. “Hadhira ilikuwa kimya kabisa na kila mtu alihisi Roho pale nyimbo hizo zilipokuwa zikiimbwa. Sote tulihisi kuwa wamoja.”

“Wimbo wa kwanza daima umekuwa wimbo wa furaha kwangu,” Megan anasema. “Ninahisi kuwa ulikuwa na matokeo hayo kwa watu kwenye tamasha. Nilikuwa na furaha nilipokuwa nikiuimba na ninatumaini kuwa watu wote waliufurahia pia. Na wimbo wa pili, sauti zilikuwa nyororo. Ninafikiri kila aliyeusikiliza alihisi roho ya kumwabudu na kumheshimu Mungu.”

Baadaye jioni, Megan anaendelea, “Tuliweza kuzungumza na waliokuwa kwenye hadhira na walioshiriki. Ninajua watu walikuwa wakimuuliza kiongozi wa kwaya yetu kuhusu nyimbo tulizoimba—‘Huo ni muziki wa aina gani?’ au ‘Mlitoa wapi mpangilio huo?’ Tuliweza kuchangamana na kuzungumza kuhusu nyimbo zilizoimbwa. Nilihisi kwamba niliweza kuwafahamu zaidi kupitia nyimbo zao, nao wakatufahamu zaidi kutokana na nyimbo zetu. Muziki ni kama dirisha kwenye nafsi yako.”