“Hekalu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo,” Historia za Ulimwengu: Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (2020)
“Hekalu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo,” Historia za Ulimwengu: Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo
Hekalu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo
Thierry Mutombo alikuwa na umri wa miaka minane wakati yeye na wazazi wake, Antoine K. Mutombo na Marie Therese M. Nzambu, walipobatizwa mwezi Juni mwaka 1986. Wiki mbili baadae, Antoine aliota ndoto kuhusu “nyumba kubwa nyeupe “ nzuri sana ambayo “ilionekana kama lulu nyeupe kutoka mbali sana.” Kwa kutokuelewa na kustaajabishwa, aliwauliza wamisionari wanandoa ndoto yake inamaanisha nini. Walimwambia jengo lilikuwa hakalu na kwamba siku moja ataweza kwenda huko. “Kwa baba yangu, kwenda hekaluni ikawa ndoto ya maisha yake yote,” alisema Thierry. “Alizungumza kuhusu mahekalu wakati wa mkutano wa jioni ya familia nyumbani maisha yetu yote.”
Baada ya kuhudumu misheni nchini Cote d’lvoire, Thierry alikutana na Nathalie Sinda, ambaye alikuwa na upendo kama wake kwa hekalu. Mnamo mwaka 1994 wazazi wa Nathalie na baadhi ya ndugu zake walikuwa wamekufa. Miaka mitatu baadae, alibatizwa na alianza kuota kuhusu wazazi na ndugu zake wakimwomba awasaidie. Ingawa alikuwa amehudumu misheni, Nathalie hakuwa amepata nafasi ya kuhudhuria hekaluni. “Siku moja, nitakwenda kuliona hekalu na kufanya kazi zote za hekaluni kwa ajili ya wazazi wangu,” Nathalie aliandika katika shajara yake akiwa mmisionari.
Mnamo mwaka 2002 Thierry na Nathalie Mutombo walifunga ndoa ya kiserikali. Mwaka mmoja baadae, mwana wao mzaliwa wa kwanza alikufa wiki mbili baada ya kuzaliwa. “Nilipolia kuhusu mtoto wetu,” alikumbuka Nathalie, “mume wangu alisema, usilie, siku moja tutaunganishwa na yeye kwa muda na milele yote.” Mnamo Novemba 18, 2004, Thierry, Natahlie, na mwana wao wa pili walisafiri kwenda Hekalu la Johannesburg, Afrika Kusini kuunganishwa kama familia. “Kwetu sisi, tumeusubiri wakati huo kuwa pamoja kama familia ya milele,” alisema Thierry. Wakati wa safari, Nathalie pia alitimiza ndoto yake ya kufanya ibada za hekaluni kwa ajili ya wazazi na ndugu zake, akiendeleza mnyororo wa muunganiko kwa kizazi kimoja nyuma.
Miaka saba baadae, jioni ya Jumamosi ya Oktoba 1, 2011, Thierry na Nathalie Mutombo walikuwa nyumbani kwao Kinshasa pamoja na watoto wao wakiangalia mkutano mkuu wakati Rais wa Kanisa Thomas S. Monson alipotangaza mipango ya kujenga hekalu Kinshasa. Kwa Thierry, hekalu huko lilimaanisha sio tu baraka za milele, bali matumaini ya baraka kwa ajili ya nchi yake. “Hekalu katika Demokrasia ya Kongo inamaanisha kwamba Bwana anaiangalia nchi yetu na hatimaye tutakuwa na amani,” alisema.
Thierry pia alifurahishwa kwamba baba yake aliishi kufikia kulisikia tangazo. “Baba yangu amekuwa akisubiri hekalu Kinshasa kwa maisha yake yote,” alisema. Mnamo Februari 2016 familia ya Mutombo, pamoja na Antoine Mutombo, walikuwepo kwa ajili ya sherehe ya kuwekwa msingi wa Hekalu la Kinshasa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. “Hili ni jibu kwa maombi yangu,” alisema Antoine. Miezi michache baadae, akiwa ameona ndoto yake ikianza kubadilika kuwa uhalisia, Antoine K. Mutombo alifariki dunia.