Historia ya Kanisa
Kupeleka Ukuhani Kikondja


“Kupeleka Ukuhani Kikondja,” Historia za Ulimwengu: Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (2020)

“Kupeleka Ukuhani Kikondja,” Historia za Ulimwengu: Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo

Kupeleka Ukuhani Kikondja

Asubuhi ya Jumamosi moja yenye mvua mwaka 2014, Rais Elie K. Monga, mshauri katika urais wa misheni ya Lubumbashi, na Mzee Jeffrey Wright, mmisionari mkubwa, walikuja kwenye nyumba ya mkutano huko Kolwezi mapema kutayarisha kwa ajili ya mkutano wa wilaya ambao ungefanyika ndani ya siku mbili zijazo. Walipowasili, wanaume wawili walioonekana kuchoka walikuwa wakiwasubiri. Walijitambulisha kama Yumba Muzimba Paul na Muba Wa Umbalo Delphin. Walikuwa tu na baiskeli iliyochakaa na tairi ya mbele isiyo na upepo na kifurushi kilichozungushiwa mfuko mchafu, wa plastiki uliochanika.

Siku nane kabla, Paul na Delphin walikuwa wameondoka kutoka nyumbani kwao Kikondja pamoja na kundi kubwa la watu ili kuhudhuria mkutano wa wilaya huko Kolwezi, zaidi ya kilomita 400 (maili 250) kusini magharibi. Ingawa hapakuwa na tawi rasmi huko Kikondja, waliripoti kwamba zaidi ya watu 60 walikuwa wakihudhuria mikutano ya kila wiki ya kundi. Wakati wa safari, wengi wa waumini walikuwa wameugua na waliamua kurudi majumbani mwao. Paul na Delphin pekee ndio walioendelea, wakiwa wamedhamiria kuhudhuria mkutano wa wilaya. Walisafiri usiku na mchana kwa siku tatu zilizopita, wakitembeza baisikeli yao kupita mvua iliyokuwa inanyesha kwa sababu baisikeli ilikuwa na tairi isiyo na upepo. Sasa pale, waliwasilisha kifurushi chao kwa Wright: zaka za mwaka mzima za waumini 33 wa kundi lao. Ingawa Wright alikuwa ameshughulikia matoleo makubwa hapo mwanzo, alikumbuka, “Kamwe sikuwahi kuhisi kama nimewahi kushika kiasi kama kile cha fedha takatifu hapo kabla.”

Picha
Paul, Delphin, Monga, na Wright

Yumba Muzimba Paul na Muba Wa Umbalo Delphin wakiwa wamesimama pamoja na Rais Elie Monga na Mzee Jeffrey Wright wakiwa na baiskeli yao iliyoharibika.

Zaka iliyolipwa, Paul alimwambia Monga na Wright sababu ya kweli ya yeye kudhamiria kuhudhuria mkutano wa wilaya. Mnamo mwaka 1975 yeye na wanaume wengine wawili kutoka Kikondja, pamoja na baba wa Delphin, walikuwa wameandika barua kwenda makao makuu ya Kanisa wakiomba wamisionari kuja kwenye kijiji chao. Ingawa washirika wa Paul katika jitihada hii wote wawili walikuwa wamekufa, yeye alikuwa amedumisha tamanio lake kwamba Kanisa siku moja litaanzishwa katika kijiji chake. “Nimengojea tukio hili kwa miaka 38,” Paul aliwaeleza.

Zaidi ya siku mbili zilizofuatia, Monga na wright waliwafundisha na kuwaelekeza Paul na Delphin katika kazi za wanaoshikilia ukuhani, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kusimamia sakramenti na kutumia ukuhani wao kubariki maisha ya familia zao pamoja na majirani. Kabla hawajaondoka kwa ajili ya safari ya kurudi, Paul na Delphin walisimikwa kama wazee na wakaruhusiwa kubariki sakramenti na kufanya mikutano katika nyumba zao.

Chapisha