2021
Ustahimilivu, Uvumilivu, na Imani
Januari 2021


HISTORIA YA KANISA

Ustahimilivu, Uvumilivu, na Imani

“Alipata na kurekebisha kompyuta ya zamani, akaiunganisha kwenye intaneti, na, kwa kutumia mitandao ya kijamii, aliwasiliana na wamisionari wa kike waliokuwa wanatumikia Misheni ya Utah Jiji la Salt Lake Temple Square.”

Kote katika maandiko tunajifunza juu ya manabii pamoja na watu wengine ambao walistahimili katika magumu mengi, ikiwa ni pamoja na Mtume Paulo, Abinadi, Kapteni Moroni na Samweli Mlamani. Katika Helamani 13:2–4 tunasoma kuhusu Samweli ambaye alikwenda kwenye mji wa Wanefi wa Zarahemla ili kuhubiri toba, lakini watu “wakamtupa nje, na alikuwa karibu kurudi kwenye nchi yake.

Lakini tazama, sauti ya Bwana ilimjia, kwamba arejee tena na kuwatabiria watu . . .

. . . kwa hivyo alienda na kupanda juu ya ukuta wa mji . . . na kunyosha mkono wake mbele na kupaza sauti.”

Hakuna mtu anayetaka kuchangamana na watu ambao wameweka wazi kwamba mtu fulani hakubaliki, lakini Samweli alimtii Bwana na kurejea Zarahemla. Alistahimili katika kufanya jambo ambalo alijua lingekuwa gumu sana, ambalo lingeweza hata kupelekea kifo chake.

Kustahimili ni kuendelea kufanya bidii. Ni kufanya kazi kwa uthabiti katika kufikia lengo au mafanikio. Ni kuendelea kujaribu daima kutimiza jukumu hata wakati mtu anapokumbwa na vikwazo au ucheleweshaji.

Mfano wa hivi karibuni wa ustahimilivu ulitokea huko Kasungu, Malawi. Akiwa amesikia kuhusu Kanisa wakati wa masomo yake ya thiolojia, Weston Kapasule alitamani kujifunza zaidi kuhusu injili ya Mwokozi, lakini mnamo 2013 wamisionari walikuwa bado hawajatumwa kwenye mji wake ulioko kijijini. Weston hakukata tamaa, licha ya hilo. Alipata na kurekebisha kompyuta ya zamani, akaiunganisha kwenye intaneti, na, kwa kutumia mitandao ya kijamii, aliwasiliana na wamisionari wa kike waliokuwa wanatumikia Misheni ya Utah Jiji la Salt Lake Temple Square. Kwa miaka saba iliyofuata, Weston alifundishwa kwa njia ya mtandao na wamisionari tofauti tofauti, ambao waliungwa mkono na Amram Musungu, mzaliwa wa Kenya na mmisionari muumini mwenye shauku ambaye kwa sasa anaishi katika Jiji la Salt Lake, Utah, Marekani. Wakati huo, pale marais wa Misheni ya Zambia Lusaka walipojua kuhusu hamu ya Weston ya kuwa na injili katika maisha yake, waliwatuma wamisionari wazee ili wamhudumie na kumpa nakala za Kitabu cha Mormoni, vitabu vya kiada vya masomo na nyenzo zingine.

Lakini muda haukuwa sahihi kwa yeye kubatizwa. Kasungu ipo mbali kutoka Blantaya au Lilongwe, maeneo mawili ambapo Kanisa lilianzishwa huko Malawi na kuanza kujenga msingi imara wa matawi. Vituo hivi vyenye idadi kubwa ya watu, vinavyojulikana kama vituo vya nguvu, ni muhimu vikakua kabla ya Kanisa kupelekwa kwenye maeneo ya mbali. Mpangilio huu wa kujenga Kanisa kuanzia kwenye vituo vya nguvu unahakikisha uongozi imara na msingi wa msaada wa kudumu kwa ajili ya waumini na waongofu wapya. Pale vituo vya nguvu vinapokuwa vimesimama vyema, katika wakati wa Bwana, matawi ya ziada ya Kanisa, kama vile lililoundwa sasa huko Kasungu, yanaweza kuanzishwa.

Wakati Weston alipopata ushuhuda imara wa ukweli wa injili, alistahimili katika kuendelea kujifunza zaidi, na kusubiri kwa uvumilivu kwa ajili ya ubatizo na kuanzishwa kwa kanisa kufike Kasungu, alishiriki kile alichojifunza na familia yake pamoja na wengine—ambao bado waliwaleta wengine kwenye kusanyiko la Kasungu. Wamisionari wa kwanza wakaazi hatimaye waliruhusiwa mnamo mwishoni mwa 2019 na, baada ya kustahimili katika kusubiri kwa miaka, washiriki wa kundi la Kasungu walianza kubatizwa mnamo siku ya kwanza ya Februari 2020. Weston alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuingia ndani ya maji ya ubatizo. Wengine zaidi ya mia moja waliungana naye.

Je, kustahimili kulikuwa vigumu kwa Weston na wale waliokuwa Kasungu wakitafuta baraka za Kanisa la Bwana? Hakika. Lakini changamoto hazikuwazuia kutafuta na kujifunza injili ya Mwokozi au kukuza shuhuda zao wenyewe.

“Nadhani rehema ya Mungu ilikuwepo kwa ajili yetu,” alisema Weston. “Hatupaswi kujiondoa kutoka kwenye ukweli huu na kurudi kule tulikotoka. Hiki ndicho kile hasa kilichotutengeneza leo kuwa jinsi tulivyo na kile tulicho. Hivyo, nilistahimili . . . Ninajua kwamba Mungu alitaka [sisi] tupitie mchakato huo ili tuweze kuwa vile tulivyo leo.”

Leo, kuna tawi la Kanisa huko Kasungu na shangwe inatawala.

Chapisha