UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO HUSIKA
Kujilinda na Kibali changu cha Hekaluni
Acha tuchukulie kwa uzito wajibu wa kuwa na kibali hai cha hekaluni—ni “silaha ya kiroho” dhidi ya adui.
Moja ya njia za kukuza imani yetu katika Mwokozi Yesu Kristo ni daima kuwa na, na kutunza kibali hai cha hekaluni. Ni ishara kuu au nyenzo ya imani ambayo kwayo tutajilinda, ili kuzuia mipango ya adui katika jaribio lake la kutuondosha kwenye ukweli.
Tunaambiwa katika Kitabu cha Mwongozo kwamba “kuingia hekaluni ni fursa takatifu”.1 Kwa hivyo, tunapaswa, kujitahidi kuwa wenye kustahili na kuwa na kibali hai cha hekaluni, “hata ikiwa hatuishi karibu na hekalu.”2 Tunapoenda kwa ajili ya usaili na askofu au rais wa tawi, yeye ataamua ikiwa tunahitaji kibali chenye ukomo wa matumizi, kibali kwa ajili ya ibada za walio hai au kibali cha hekaluni.
Mzee Ronald A. Rasband wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili anashiriki somo kuu alilojifunza wakati yeye pamoja na mke wake walipokwenda kumtembelea baba mkwe wake mgonjwa. Walipowasili, walimkuta askofu akiondoka nyumbani kwa baba mkwe wake. Mzee Rasband aligundua kwamba baba mkwe wake alikuwa amemwalika askofu kwa sababu alitaka usaili wa kibali cha hekaluni, kwa sababu, kwa maneno yake mwenyewe, “nataka kwenda nikiwa nimejikabidhi kwa Bwana”.3
Na, anasema Mzee Rasband, “ilikuwa hivyo baada ya muda mfupi”.
Sisi, pia, tunahitaji kujikabidhi kwa Bwana katika maisha yetu ya kila siku ili kwamba tuweze kufurahia baraka ambazo huja kama matokeo ya kuishi viwango vilivyowekwa vya kuishi kama muumini mwenye kustahili wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Baadhi ya viwango hivi hujumuisha kuwa mkweli, usafi wa kimwili, uaminifu, kutii neno la hekima, sheria ya zaka, na kutii siku ya Sabato.
Kama askofu, miaka michache iliyopita nilifanya usaili wa kibali cha hekaluni kwa mmoja wa akina kaka wema, muumini mzuri hasa wa kata. Yote yalikuwa sawa mpaka tulipofikia swali, “je unalipa zaka zako?” Hapo alianza kupata kigugumizi; maneno hayakutamkwa kwa ufasaha. Nilimtazama moja kwa moja machoni na kuuliza kwa mara ya pili, “je unalipa zaka zako?”
Jibu kisha lilitoka kwa upole, “mimi si mwaminifu katika kulipa zaka zangu, kwa sababu mara nyingi ninapopata malipo yangu, huwa ninakuwa na mahitaji mengi muhimu na pesa haionekani kutosheleza kukidhi gharama zote au malengo yote.” Nilijua kwamba hii ilikuwa fursa ya kumfunza kuhusu kanuni ya kulipa zaka kamili na kwa uaminifu, kama ilivyoamriwa na Bwana. Kisha aliomba apewe muda kwenda kutimiza ahadi yake ya kuwa mlipa zaka kamili. Ilichukua miezi sita kabla ya kuwa na usaili mwingine pamoja naye ili kutathmini ustahiki wake. Hakika, alikuwa ameanza kupiga hatua za mtoto katika uelekeo sahihi.
“Usaili wa kibali cha hekaluni huwaruhusu waumini kuonesha kwa mfano kwamba wana ushuhuda na wanajitahidi kutii amri za Mungu na wanawafuata manabii Wake,”4 Kitabu cha Mwongozo kinatuelekeza.
Waumini ambao wanakwenda kupokea endaomenti zao wenyewe lazima wakidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye kitabu hicho hicho cha Mwongozo:
-
Wanapaswa kuwa angalau na umri wa miaka 18;
-
Wanapaswa kuwa wamemaliza au hawahudhurii tena shule ya upili ya juu, shule ya upili, au sawa na hizo;
-
Mwaka mmoja unapaswa kuwa umepita baada ya uthibitisho wao; na
-
Mwanamume lazima awe na Ukuhani wa Melkizedeki kabla ya kupokea endaomenti yake5
Tunapaswa kukumbuka kuwa kibali cha hekaluni kinashikiliwa kwa kipindi cha miaka miwili, isipokuwa kibali cha ibada za walio hai, ambacho kinaweza kudumu kwa mwaka mmoja tu. Kinapokwisha muda wa matumizi, tafadhali daima kumbuka kurudi kwa askofu wako au rais wa tawi kwa ajili ya usaili na baadaye kupata kipya.
Ninawasihi kaka zangu na dada zangu tuchukulie kwa uzito wajibu wa kuwa na kibali hai cha hekaluni—ni “silaha ya kiroho” dhidi ya adui. Tumeonywa na Mwokozi katika Mafundisho na Maagano:
“Jiandaeni wenyewe; tayarisheni kila kitu kinachohitajika; na ijengeni nyumba, hata nyumba ya sala, nyumba ya kufunga, nyumba ya imani, nyumba ya kujifunza, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu.”6
Acha tukumbuke kwamba, tunaposhindwa katika jukumu letu la kusikiliza onyo hilo, na kwenda nje ya njia, askofu au rais wa tawi anaweza kuzuia fursa ya sisi kutunza kibali hicho cha hekaluni. Acha pia daima “tukumbuke kwamba kile ambacho huja kutoka juu ni kitakatifu”7 na kwamba tumeambiwa “Usifanye kipawa chako kijulikane kwa yeyote ila kwa wale tu wa imani yako. Usicheze na mambo matakatifu.”8
Tunapotunza kibali hai cha hekaluni, tutasimama kama askari shujaa katika jeshi la Bwana. “Na watakatifu wote ambao wanakumbuka kushika na kutenda maneno haya, wakitembea katika utii kwa amri hizi, watapata afya mwilini mwao na mafuta mifupani mwao; na watapata hekima na hazina kubwa ya maarifa, hata hazina zilizofichika. Na watakimbia na wasichoke, na watatembea wala hawatazimia. Na Mimi, Bwana, ninatoa ahadi kwao, kwamba malaika mwangamizaji atawapita, kama watoto wa Israeli, na hatawaua. Amina.”9
Frederick M. Kamya aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2021. Amemuoa Stella Kamya; wao ni wazazi wa watoto sita. Anaishi Kampala, Uganda.