Njoo, Unifuate
Aprili 22–28: “Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote.” Mosia 1–3


“Aprili 22–28: ‘Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote.’ Mosia1–3,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Aprili 22–28. Mosia 1–3,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

Mfalme Benjamini akiwafundisha watu wake

Kupokea Mafundisho ya Mfalme Banjamini, na Maria Alejandra Gil

Mosia 22–28: “Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote”

Mosia 1–3

Unaposikia neno mfalme, unaweza kufikiria mataji, watumishi na viti vya enzi. Katika Mosia 1–3, utasoma kuhusu mfalme wa aina tofauti. Badala ya kujikimu kutokana na jasho la watu wake, Mfalme Benjamini “alifanya kazi kwa mikono [yake] mwenyewe” (Mosia 2:14). Badala ya kuwahitaji wengine wamtumikie, yeye aliwatumikia watu wake “kwa uwezo wote, akili na nguvu ambazo Bwana [alimpatia]” (Mosia 2:11). Mfalme huyu hakutaka watu wake wamuabudu; badala yake, aliwafundisha wamuabudu Mfalme wa Mbinguni, Yesu Kristo. Mfalme Benjamini alielewa kwamba ni “Bwana Mwenyezi ambaye anatawala” (Mosia 3:5), ambaye “alikuja chini kutoka mbinguni” na akaenda “miongoni mwa watu, … ili wokovu upate kuwafikia watoto wa watu hata kupitia imani kwa jina lake” (Mosia 3:5, 9).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Mosia 1:1–7

“Yachunguze [Maandiko] kwa bidii.”

Katika mistari hii, zingatia jinsi kumbukumbu takatifu zilivyowabariki watu wa mfalme Benjamini. Je, maisha yako ni bora kwa kiasi gani kwa sababu unayo maandiko haya?

ikoni ya seminari

Mosia 2:10–26

Ninapowatumikia wengine, ninamtumikia Mungu pia.

Unafikiri Mfalme Benjamini angesema nini kama ungemuuliza ni kwa nini alihudumu kwa “uwezo, akili na nguvu zake zote”? (Mosia 2:11). Tafakari hili unaposoma Mosia 2:10–26. Je, Mfalme Benjamini alifundisha kipi ambacho kinakutia wewe msukumo wa kuwatumikia wengine katika njia yenye tija zaidi? Kwa mfano, ina maana gani kwako kujua kwamba wakati unapowatumikia watu wengine, unamtumikia pia Mungu? (ona Mosia 2:17). Tafuta mwongozo wa kiungu kuhusu jinsi gani unaweza kumhudumia mtu wiki hii.

Hata kama tunajua kwamba lazima tuwatumikie wengine, sisi wakati mwingine tunakumbana na changamoto. Njia nyingine ya kujifunza Mosia 2:10–26 ni kwa kutengeneza orodha ya kweli zilizofundishwa na mfalme Benjamini ambazo zinaweza kukusaidia ushinde changamoto ambazo zinaweza kukuzuia kutumikia. Je, ni uzoefu upi umekuonesha kwamba alichokifundisha Mfalme Benjamini ni cha kweli?

Rais Joy D. Jones alishiriki uzoefu wenye nguvu ambao ulibadilisha jinsi alivyochukulia kuwatumikia wengine. Soma kuhusu hili katika “Kwa Ajili Yake” (Ensign au Liahona, Nov. 2018, 50–52), na fikiria kuhusu fursa ambazo unazo za kuwatumikia wengine. Ungeweza hata kuorodhesha chache na utafakari jinsi ujumbe wa Rais Jones, pamoja na Mosia 2:17, vinavyoweza kuathiri jinsi unavyozifanyia kazi fursa hizi. Wimbo wa Dini kama “Msafiri kwa Miguu” (Nyimbo za Dini, na 19) au video kama “The Old Shoemaker” (Gospel Library) vingeweza kukusaidia ufikirie umaizi wa ziada.

Ona pia Mathayo 25:40; “Faith Murray’s Story: Overcoming Adversity through Service,” “King Benjamin Teaches about Serving God” (videos), Gospel Library; JustServe.org; Mada za Injili, “Huduma,” Gospel Library.

wanawake wawili wakikumbatiana

Ninapowatumikia wengine, ninamtumikia Mungu pia.

Mosia 2:38–41

Furaha inakuja kutokana na kushika amri za Mungu.

Utaielezeaje furaha ambayo huja kutokana na utiifu kwa Mungu? Je, kuna vifungu vyovyote vya maneno katika Mosia 2:38–41 ambavyo vingeweza kusaidia kufafanua kwa nini tunashika amri Zake?

Mosia 3:1–20

Ninaweza kuwa mtakatifu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Mfalme Benjamini, kama vile manabii wote, alitoa ushuhuda juu ya Yesu Kristo ili watu wake “wapate kupokea msamaha wa dhambi zao na kushangilia kwa shangwe kuu zaidi” (Mosia 3:13). Haya ni baadhi ya maswali ya kutafakari wakati unaposoma ushuhuda wa Mfalme Benjamini kuhusu Mwokozi katika Mosia 3:1–20:

  • Je, ninajifunza kipi kutoka kwenye mistari hii kuhusu Mwokozi na misheni Yake?

  • Je ninajifunza kipi kutoka Mosia 3:18–9 kuhusu kile ambacho kuwa mtakatifu humaanisha?

  • Je, Yesu Kristo amenisaidia kwa namna gani nishinde dhambi, nibadili asili yangu na niwe zaidi kama mtakatifu?

Mosia 3:5–21

“Bwana Mwenyezi … atashuka chini kutoka mbinguni.”

Je, umeme unakupa uwezo wa kufanya kipi? Je, maisha yako yangekuwaje bila umeme? Maswali haya yangeweza kukusaidia utafakari kuhusu hata nguvu kubwa zaidi ambayo Mwokozi anaweza kuileta maishani mwako.

Malaika aliyemtokea Mfalme Benjamini alimtaja Yesu Kristo kama “Bwana Mwenyezi,” jina linalomaanisha kwamba Yeye anazo nguvu zote. Unajifunza kipi kutoka Mosia 3:5–21 kuhusu jinsi ambavyo Mwokozi anatumia uwezo huo? Ni kwa jinsi gani umeweza kuona uwezo wa Mwokozi katika maisha yako na katika maisha ya wale wanaokuzunguka? Je, nguvu zake zinakuwezesha wewe ufanye kipi na uwe nani baadaye? Je, maisha yako yangekuwaje bila nguvu hiyo?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mosia 2:11–18

Ninapowatumikia wengine, ninamtumikia Mungu.

  • Ukurasa wa shughuli ya wiki hii una taji rahisi ambayo watoto wako wangeweza kutengeneza. Pengine wangependa kupeana zamu ya kusimama juu ya kiti au stuli na wajifanye kuwa Mfalme Benjamini wakati ukishiriki baadhi ya vitu ambavyo Mfalme Benjamini alivifundisha kwa watu wake, vinavyopatikana kwenye Mosia 2–3. Ungeweza pia kushiriki nao “Mlango wa 12: Mfalme Benjamini” (Hadithi za Kitabu cha Momoni, 32–35) ili kuwapa muhtasari wa mafundisho ya Mfalme Benjamini.

  • Mosia 2:17 unaweza kuwa mstari mzuri kwa ajili ya watoto wako kujifunza. Ungeweza kuwasaidia warudie baadhi ya maneno. Au ungeandika mstari, pamoja na maneno kadhaa ya msingi yanayokosekana, na waombe watoto wako watafute maneno yanayokosekana. Kisha ungeweza kuzungumza na watoto wako kuhusu kwa nini Mungu anatutaka tutumikiane.

  • Ungeweza kuwasaidia watoto wako watafute kwenye Mosia 2:11–18 ili kupata kile Mfalme Benjamini alichofanya ili kuwatumikia wengine. Kisha watoto wako wangeweza kuandika kwenye vipande vyembamba vya karatasi baadhi ya njia ambazo wanaweza kuwatumikia wanafamilia. Weka karatasi kwenye chombo, kama vile mkoba au jagi, ili kwamba watoto waweze kuchagua kila siku na kufanya kitendo hicho cha huduma kwa mtu fulani.

Watoto wananufaika kutokana na marudio. Usiogope kurudia shughuli mara nyingi, hususani na watoto wadogo. Marudio yatawasaidia watoto wakumbuke kitu wanachojifunza.

watoto wakikunja kipande cha kitambaa

Mfalme Benjamini alifundisha kwamba tunaweza kumtumikia Mungu kwa kuwatumikia wengine.

Mosia 2:19–25

Baraka zangu zote hutoka kwa Baba wa Mbinguni.

  • Huduma ya Mfalme Benjamini kwa watu wake ilitiwa msukumo na shukrani zake za dhati kwa Mungu. Je, unawezaje kuleta msukumo wa hisia sawa na hizo kwa watoto wako? Mngeweza kusoma pamoja Mosia 2:21 na kuandaa orodha ya baraka ambazo Baba wa Mbinguni ametupatia. Kisha ungeweza kuongeza kwenye orodha baraka zingine ambazo watoto wanazifikiria.

  • Hapa kuna mchezo ambao mngeweza kucheza ili kuwasaidia watoto watambue baraka kutoka kwa Baba wa Mbinguni. Watoto wangeweza kupitisha kwa mzunguko picha ya Mwokozi wakati wanapoimba au kusikiliza wimbo kuhusu shukurani (ona “Gratitude” kwenye kielezo cha mada cha Kitabu cha Nyimbo za Watoto). Acheni kuimba au simamisha muziki kila baada ya muda fulani, na mwalike yeyote aliyeshikilia picha azungumze kuhusu baraka anayoitolea shukrani. Kulingana na Mosia 2:22–24, tunawezaje kuonesha kwamba tuna shukrani kwa ajili ya baraka zetu?

Mosia 3:5–10, 19

Yesu Kristo atanisaidia niwe zaidi kama Yeye.

  • Malaika alimwambia Mfalme Benjamini kweli za muhimu kuhusu maisha na huduma ya Yesu Kristo. Pengine wewe pamoja na watoto wako mngeweza kuangalia picha za baadhi ya matukio yaliyosemwa kwenye Mosia 3:5–10 (ona, kwa mfano Kitabu cha Sanaa za Injiili, na. 30, 41, 42, 5759). Wakati ukisoma Mosia 3:5–10, watoto wako wangeweza kunyanyua mikono yao wakati wanaposikia kitu ambacho kinaonekana kwenye moja ya picha.

  • Je, watoto wako wamewahi kusaidia kuandaa chakula kwa kutumia maelezo ya upishi? Pengine ungeweza kuzungumza kuhusu uzoefu huo na kutumia Mosia 3:19 kutengeneza “maelezo ya upishi” ya jinsi tunavyoweza kuwa kama Yesu Kristo. Ni kwa jinsi gani Yesu anatusaidia tuwe kama Yeye?

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Mfalme Benjamini akiwahubiria watu wake

Hotuba ya Mfalme Benjamini, na Jeremy Winborg