“Aprili 8–14: ‘Bwana Hufanya Kazi Nasi.’ Yakobo 5–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)
“Aprili 8–14: Yakobo 5–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)
Aprili 8–14: Bwana Hufanya Kazi pamoja Nasi
Yakobo 5–7
Kuna watu wengi, wengi mno ambao bado wangali hawajaisikia injili ya Yesu Kristo. Kama umewahi kuhisi kushindwa na uzito wa kazi ya kuwakusanya katika Kanisa la Bwana, kile ambacho Yakobo alikisema kuhusu miti ya mizeituni katika Yakobo 5 kina ukumbusho wa uhakika: shamba la mizeituni ni mali ya Bwana. Ametupatia kila mmoja wetu sehemu ndogo tusaidie katika kazi Yake—familia yetu, kundi letu la marafiki, eneo ambalo tuna ushawishi. Na wakati mwingine mtu wa kwanza ambaye tunasaidia kumkusanya ni sisi wenyewe. Lakini kamwe hatuko peke yetu katika kazi hii, kwa maana Bwana mwenye shamba anafanya kazi pamoja na watumishi Wake (ona Yakobo 5:72). Mungu anawajua na anawapenda watoto Wake, atatengeneza njia kwa ajili ya kila mmoja wao kuisikia injili Yake, hata wale ambao walimkataa kipindi cha nyuma (ona Yakobo 4:15–18). Na kisha, wakati kazi itakapokuwa imekamilika, wale wote ambao wamekuwa “na bidii katika kutumikia pamoja [Naye] … watapokea shangwe pamoja [Naye] kwa sababu ya matunda ya shamba [Lake] la mizeituni” (Yakobo 5:75).
Ona pia “Jacob Teaches about the Gathering of Israel” (video), Gospel Library.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Yesu Kristo ndiye Bwana wa shamba.
Yakobo 5 ni hadithi yenye maana ya alama. Inaelezea miti na tunda na wafanyakazi, lakini kiualisia ni kuhusu mchangamano baina ya Mungu na watu Wake katika historia yote. Hivyo wakati ukisoma hadithi hii muhimu, fikiria kuhusu baadhi ya vitu kwenye hadithi vinaweza kuwa na maana ipi.
Kwa mfano, kama shamba la mzeituni huwakilisha ulimwengu, na mti wa kupandikizwa wa mzeituni huwakilisha Israeli (au watu waliofanya maagano na Mungu; ona Yakobo 5:3) mizeituni pori inaweza kuwakilisha nini? Je, matunda mazuri na mabaya yangewakilisha nini? Ni alama zipi zingine ambazo unaziona?
Ingawa Yakobo 5 hufundisha kuhusu mataifa na karne za historia ya ulimwengu, pia ni kuhusu wewe na maisha yako. Ni jumbe zipi unazipata kwa ajili yako mwenyewe katika Yakobo 5?
Pengine la muhimu zaidi, Yakobo 5 ni kuhusu Yesu Kristo. Mtafute Yeye wakati ukisoma. Je, unajifunza kipi kuhusu Yeye, kwa mfano, katika mistari 40–41, 46–47?
Kwa umaizi wa ziada kuhusu Yakobo 5, ona mchoro mwisho wa muhtasari huu.
Bwana ananialika nifanye kazi pamoja Naye katika shamba Lake la mizeituni.
Wale “watumishi wengine” (Yakobo 5:70) ambao waliitwa katika shamba la Bwana la mizeituni ni pamoja na watu kama wewe. Ni kweli zipi unazipata katika Yakobo 5, hasa mistari 61–62 na 70–75, kuhusu kufanya kazi katika shamba la Bwana la mizeituni? Je, umejifunza kipi kuhusu Yeye kwa kusaidia katika kazi Yake?
Unaposoma kuhusu “mara hii ya mwisho” ambayo Bwana anafanya kazi katika shamba Lake, ni kipi kinakupa msukumo kumtumikia Bwana “kwa nguvu zako”? (Yakobo 5:71). Pengine ungeweza kufikiria uzoefu wako binafsi ambapo ulihisi shangwe wakati ukimtumikia Bwana wa shamba la mizeituni—kwa mfano, kupitia kushiriki injili, kutumikia hekaluni au kuwaimarisha wengine. Unaweza pia kutafiti mifano ambayo Mzee Gary E. Stevenson aliishiriki katika ujumbe wake “Yenye Kupendeza kwa urahisi—Yenye Urahisi wa Kupendeza” (Liahona, Nov. 2021, 47–50).
Rais M.Nelson alifundisha: “Wakati wowote unapofanya kitu chochote kinachomsaidia mtu yeyote—upande wowote wa pazia—unachukua hatua kuelekea kufanya maagano na Mungu na kupokea ibada zao muhimu za ubatizo na za hekaluni, unasaidia katika kukusanya Israeli. Ni rahisi kiasi hicho” (“Hope of Israel” [worldwide youth devotional, June 3, 2018], ChurchofJesusChrist.org). Fikiria kuanzisha orodha ya mawazo ya jinsi unavyoweza kufanya hili ili usaidie kuwakusanya Israeli. Kutoka kwenye orodha yako, je, unahisi Bwana angekutaka ufanye kipi kwenye shamba lake la mizeituni hivi leo? Kulingana na mstari wa 75, ni kwa namna gani Bwana hutuzawadia sisi kwa kutoa huduma kwenye shamba Lake la mizeituni?
Ona pia “Israeli Mnaitwa,” Nyimbo za Dini, na 7; “Old Testament Olive Vineyard” (video), Gospel Library; Mada za Injili, “Kukusanya Israeli,” “Kuwaalika Wote Wapokee Injili ya Yesu Kristo,” “Kushiriki kwenye Kazi ya Hekalu na Historia ya Familia,” Gospel Library.
Bwana anawakumbuka watu Wake kwa upendo na huruma.
Maana moja ya neno ambatana ni kutii au kung’ang’ania kitu fulani kwa uthabiti, kwa karibu na bila kuyumbayumba. Ni kwa namna gani maana hiyo inaathiri jinsi unavyoelewa Yakobo 6:4–5? Kwenye hadithi ya mti wa mzeituni, ni kwa namna ipi Bwana wa shamba ananyosha “mkono wake wa rehema”? (ona, kwa mfano, Yakobo 5:47, 51, 60–61, 71–72). Je, ni jinsi gani amefanya hivi kwako?
Ninaweza kusimama imara wakati wengine wanapopinga imani yangu katika Yesu Kristo.
Uzoefu wa Wanefi na Sheremu mara kwa mara unarudiwa siku ya leo: watu wanajaribu kuangamiza imani katika Kristo. Je, Yakobo alijibu vipi wakati imani yake iliposhambuliwa? Unajifunza kipi kutokana na majibu yake? Je, ni kipi unaweza kufanya sasa ili kujiandaa kwa ajili ya nyakati ambapo imani yako katika Mwokozi itapingwa?
Ona pia Jeffrey R. Holland, “Gharama—na Baraka—ya Ufuasi,” Ensign au Liahona, Mei 2014, 6–9; “Sherem Denies Christ” (video), Gospel Library.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Bwana anawajali watu Wake.
-
Je, unawezaje kushiriki hadithi ya miti ya mizeituni katika njia ambayo watoto wako wanaweza kuelewa? Njia mojawapo ni kwa kutembea nje kuangalia miti na kwa haraka kupitia dondoo muhimu za hadithi hii. Je, Bwana wa shamba alifanya nini kwa ajili ya miti Yake? Je, tunawezaje kuwa kama wafanyakazi kwenye hadithi na kuwasaidia wengine wahisi upendo wa Mwokozi?
-
Yakobo alishiriki hadithi ya miti ya mizeituni ili kuwaalika watu Wake waje kwa Kristo. Hadithi hii inaweza kufanya vivyo hivyo kwa watoto wako. Pengine ungeweza kufanya ufupisho wa hadithi kwa mistari kama vile Yakobo 5:3–4, 28–29, 47, na 70–72 (ona pia “Old Testament Olive Vineyard” [video], Gospel Library). Wewe au watoto kisha mngeweza kusoma Yakobo 5:11, 41, 47, na 72, mkitafuta vitu ambavyo vinaonesha ni kwa kiasi gani Bwana wa shamba (Yesu Kristo) aliijali miti. Je, Mwokozi anafanya kipi ili kuonesha Anatujali sisi?
Baba wa Mbinguni ananipenda na atanisamehe pale ninapotubu.
-
Yakobo 6:4–5 ina ujumbe muhimu kwa ajili yetu wakati tunapofanya chaguzi zisizo sahihi. Pengine ungeweza kuwasaidia watoto wako watafute hilo. Ni maneno yapi kwenye mistari hii yanatupatia tumaini kweye upendo wa Mungu wenye kukomboa? Hadithi ya Mzee Allen D. Haynie kuhusu kuchafuka kwenye shimo la tope katika ujumbe wake “Kumkumbuka Yule Tuliyemtumainia” (Liahona, Nov. 2015, 121–22), ingeweza kusadia. Je, hadithi hii na Yakobo 6:4–5 hutufundisha nini kuhusu kile tunachopaswa kufanya ili tuokolewe katika ufalme wa Mungu?
Ninaweza kusimamia kile ninachojua kuwa ni cha kweli.
-
Ni kwa jinsi gani unaweza kuwashawishi watoto wako wasimame imara katika ukweli kama Yakobo alivyofanya? Watoto wako wangeweza kuangalia video ya “Mlango wa 10: Jacob and Sherem” (Gospel Library) na kuigiza mazungumzo kati ya Yakobo na Sheremu, wakitumia Yakobo 7:1–23 kama mwongozo. Ni kwa jinsi gani Yakobo alisimama imara kwenye kile alichojua kuwa kilikuwa cha kweli? Waalike watoto wako washiriki uzoefu wao wakati waliposimamia ukweli, au shiriki uzoefu wako mwenyewe. Pengine wangeweza pia kuimba wimbo ambao unaonesha ujasiri kama wa Yakobo, kama vile “Stand for the Right,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 159.