Njoo, Unifuate
Septemba 9–15: “Habari Njema ya Shangwe Kuu.” Helamani 13–16


“Septemba 9–15:‘Habari Njema ya Shangwe Kuu.’ Helamani 13–16,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Septemba 9–15. Helamani 13–16,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Samweli Mlamani akifundisha juu ya ukuta

Samweli Mlamani Juu ya Ukuta, na Arnold Friberg

Septemba 9–15: “Habari Njema ya Shangwe Kuu”

Helamani 13–16

Mara ya kwanza Samweli Mlamani alipojaribu kushiriki “habari njema” kule Zarahemla (Helamani 13:7), alikataliwa na kufukuzwa na Wanefi wenye mioyo migumu. Unaweza kusema ilikuwa kana kwamba walikuwa wamejenga ukuta usioweza kuvunjwa kuzingira mioyo yao ambao uliwazuia kupokea ujumbe wa Samweli. Samweli alielewa umuhimu wa ujumbe aliokuwa nao na alionesha imani kwa kufuata amri ya Mungu “kwamba anapaswa kurejea tena, na kutoa unabii ” (Helamani 13:3). Kama vile Samweli, sisi sote tunakabiliana na kuta wakati “tunapoiandaa njia ya Bwana” (Helamani 14:9) na kujitahidi kuwafuata manabii Wake. Na kama Samweli, sisi pia tunamshuhudia Yesu Kristo, “ambaye hakika atakuja,” na tunawaalika wote “kuamini katika jina Lake” (Helamani 13:6; 14:13). Si kila mmoja atasikiliza, na wengine watatupinga kwa nguvu. Lakini wale ambao wanaamini katika ujumbe huu wakiwa na imani katika Kristo wanajua kwamba kwa kweli ni ujumbe wa “habari njema ya shangwe kuu” (Helamani 16:14).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Helamani 13

Bwana hutoa maonyo kupitia manabii Wake.

Katika maandiko, manabii wakati mwingine wanalinganishwa na walinzi juu ya ukuta au mnara wanaoonya dhidi ya hatari (ona Isaya 62:6; Ezekieli 33:1–7). unapojifunza maneno ya Samweli katika Helamani 13, fikiria jinsi ambavyo yeye ni kama mlinzi kwa ajili yako. Alisema kitu gani ambacho kinaonekana kinahusiana na siku yetu? (ona hasa mistari 8, 21–22, 26– 29, 31, na 38). Kwa mfano, ni kipi Samweli alifundisha kuhusu toba? kuhusu unyenyekevu na utajiri? kuhusu kutafuta furaha “katika kufanya uovu”?

Ungeweza pia kupekua jumbe za mkutano mkuu wa hivi karibuni kwa ajili ya maonyo yanayofanana ambayo Bwana ameyatoa kupitia manabii wa sasa. Je, unahisi kutiwa msukumo wa kufanya nini kuhusu maonyo haya?

Tafuta mpangilio. Mpangilio ni mpango au mfano unaoweza kutumika kama mwongozo wa kutimiza kazi. Katika maandiko, tunapata mipangilio ambayo hutuonesha jinsi ambavyo Bwana hutimiza kazi Yake, kama vile kuwatuma watumishi Wake wawaonye watu.

familia ikiangalia mkutano mkuu

Tunapowasikiliza manabii, watatuongoza kwa Yesu Kristo.

Helamani 13–15

seminary icon
Mungu ananialika nitubu.

Maonyo ya Samweli juu ya hukumu za Mungu kila mara yalijumuisha mwaliko wa kutubu. Tafuta mialiko hii kote katika Helamani 13–15 (ona hasa Helamani 13:6– 11; 14:15–19; 15:7–8). Je, unajifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu toba? Baadhi ya watu wanaona toba kama adhabu kali—kitu cha kuepukwa. Kwa maoni yako, ni kwa jinsi gani Samweli alitaka Wanefi waione toba?

Ili kuongeza kina kwenye kujifunza kwako, ungeweza kusoma ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Tunaweza Kufanya Vizuri na Kuwa Bora” (Liahona, Mei 2019, 67). Je, Yeye anaielezeaje toba? Ni baraka zipi za toba ya dhati unazipata katika ujumbe wake? Ungeweza pia kutafuta vitu mahususi ambavyo nabii alitualika tuvibadilishe. Ni kipi Roho Mtakatifu anakuambia ambacho unahitaji kukibadilisha? Fikiria kuandika ufunuo binafsi unaoupokea.

Ni kwa jinsi gani toba ni tofauti kuliko kubadili tu tabia? Kwa nini ni muhimu kupokea mwaliko wa Mungu wa kutubu? Unapotafakari hili, fikiria kuimba au kusikiliza wimbo ambao unaonesha mwaliko huu, kama vile “Amri Zake Mungu” (Nyimbo za Dini, na. 71).

Ona pia “Yesu Kristo Atakusaidia,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi, 6–9; “Repentance: A Joyful Choice,” “Principles of Peace: Repentance” (video), Maktaba ya Injili; Mada za Injili “Toba,” Maktaba ya Injili.

Helamani 14; 16:13–23

Mungu alituma ishara na maajabu kama ushuhuda wa kuzaliwa na kifo cha Mwokozi.

Katika Helamani 14, Samweli alieleza kwamba Bwana alitoa ishara za kuzaliwa na kifo cha Mwokozi ili kwamba watu “wangejua … ujio wake” na “wangeamini katika jina lake” (Helamani 14:12). Unapojifunza Helamani 14, tambua ishara za kuzaliwa kwa Mwokozi mistari 1–8 na ishara za kifo Chake katika mistari 20–28. Kwa nini unadhani ishara hizi zingekuwa njia zenye ufanisi za kuashiria kuzaliwa na kifo cha Yesu Kristo?

Ishara zingine binafsi zaidi na zisizo kubwa sana zinaweza kukusaidia “uamini juu ya [jina la [Mwokozi].” Ni nini Yeye amefanya kuimarisha imani yako katika Yeye?

Ni tahadhari ipi imetolewa kuhusu ishara katika Helamani 16:13–23? Ni kwa jinsi gani unaweza kuepuka mitazamo ya watu walioelezwa katika mistari hii?

Ona pia Alma 30:43–52; Ronald A. Rasband, “Kwa Mpango Mtakatifu,” Liahona, Nov. 2017, 55–57.

Helamani 15:3

Kurudiwa na Bwana ni ishara ya upendo Wake.

Maneno ya Samweli yana maadabisho mengi makali, lakini Helamani 15:3 inatoa mtazamo juu ya kuadabishwa kutoka kwa Bwana. Ni kwa jinsi gani adabisho toka kwa Bwana linaweza kuwa ishara ya upendo Wake? Ni ushahidi upi unauona wa upendo na rehema za Bwana katika unabii na maonyo ya Samweli?

Fikiria kujifunza ujumbe wa Mzee D. Todd Christofferson “Wengi Kadiri Niwapendao, Ninawarudi na Kuwakemea” (Liahona, Mei 2011, 97– 100). Ni lini umeona Mungu akifanya kazi katika njia hizi katika maisha yako?

Helamani 16

Manabii wananielekeza mimi kwa Yesu Kristo.

Katika Helamani 16, unajifunza nini kutoka kwa wale walioyakubali mafundisho ya Samweli? Je, unajifunza nini kutoka kwa wale waliomkataa? Fikiria kuhusu jinsi ambavyo kuwafuata manabii walio hai kumekusaidia usogee karibu zaidi na Yesu Kristo.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Helamani 13:2–5

Mungu anaweza kuzungumza nami ndani ya moyo wangu.

  • Ni kwa jinsi gani unaweza kuwafundisha watoto wako kwamba Mungu anaweza kuzungumza na moyo wetu, kama vile Yeye alivyofanya kwa Samweli? Pengine ungeweza kuwaomba wakuoneshe njia tofauti za kuwasiliana bila maneno (kama vile ishara au mwonekano wa sura). Hii ingeweza kuongoza kwenye majadiliano kuhusu njia tofauti ambazo Baba wa Mbinguni awasiliana na sisi. Kama sehemu ya mjadala huu, wewe na watoto wako mngeweza kutazama picha ya Samweli Mlamani (muhtasari huu unazo mbili) na usome Helamani 13:2–5 huku watoto wako wakisikiliza jinsi Mungu alivyomwambia Samweli cha kusema.

  • Wengi wetu—hasa watoto—wanahitaji kujifunza kutambua jinsi gani na wakati gani Mungu anazungumza nasi. Ungeweza kuwaambia watoto wako kuhusu wakati ambapo Roho Mtakatifu alikusaidia ujue katika moyo wako kile ambacho Mungu alitaka ufanye au useme. Eleza jinsi ulivyojua kwamba Mungu alikuwa akiwasiliana nawe. Pengine watoto wako wangeweza pia kushiriki uzoefu wowote sawa na huo waliowahi kuupata.

Helamani 14:2–7, 20–25

Manabii hufundisha kuhusu Yesu Kristo.

  • Kuimba pamoja “Samuel Tells of the Baby Jesus” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 36) inaweza kuwa njia nzuri ya kuwafundisha watoto kile Samweli alichofunza kuhusu Yesu Kristo. Kushiriki “Mlango wa 40: Samweli Mlamani Anazungumza kuhusu Yesu Kristo” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 111–13), inaweza kuwa njia nyingine. Ni kipi Samweli alifundisha kuhusu Mwokozi? Pengine ungeweza pia kushiriki kile ambacho manabii wa sasa wanakifundisha kumhusu Yeye. Ni kwa jinsi gani maneno yao yamejenga imani yako Kwake?

Helamani 16:1–6

Ninabarikiwa pale ninapomfuata nabii.

  • Unaweza kujenga imani ya watoto wako katika nabii kwa kuwaonesha mifano ya watu ambao walikuwa waaminifu. Baadhi yao wanapatikana katika Helamani 16:1, 5. Unaposoma, watoto wako wangeweza kusimama wakati wanaposikia jambo ambalo watu walifanya wakati walipoamini maneno ya Samweli. Kisha, unaposoma mstari wa 2 na wa 6, watoto wako wangeweza kuketi chini wakati wanaposikia jambo ambalo watu walilifanya wakati ambapo hawakuamini. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonesha kwamba tunaamini maneno ya nabii aliye hai? Waambie watoto jinsi ulivyobarikiwa pale ulipofuata ushauri wa Bwana kupitia manabii Wake.

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Samweli Mlamani

Samweli Mlamani, na Lester Yocum