Mafundisho na Maagano 2021
Februari 15–21. Mafundisho na Maagano 14–17: “Simama kama Shahidi”


“Februari 15–21. Mafundisho na Maagano 14–17: ‘Simama kama Shahidi,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Februari 15–21. Mafundisho na Maagano 14–17,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
Joseph Smith na Mashahidi Watatu wamepiga magoti kusali

Februari 15–21

Mafundisho na Maagano 14–17

“Simama kama Shahidi”

Familia ya Joseph Smith na marafiki wakati mwingine walimuomba atafute ufunuo kuhusu nini Mungu aliwataka wafanye. Unaposoma ufunuo huu, fikiria ni mwongozo gani Mungu anao kwa ajili yako.

Andika Misukumo Yako

Japokuwa kazi ya kutafsiri ilikuwa ikiendelea vizuri, mnamo Mei 1829 hali katika Harmony ilikuwa ngumu mno kwa Joseph, Emma, na Oliver. Uhasama kutoka kwa majirani ulikuwa unaongezeka wakati msaada kutoka kwa familia ya Emma ulikuwa unafifia. Akihisi kwamba Harmony haikuwa tena salama, Oliver alimwendea rafiki aliyeonesha mapenzi katika kazi ya Joseph: David Whitmer. David aliishi na wazazi na ndugu zake huko Fayette, New York, umbali wa takribani maili 100. Alikutana na Oliver mwaka mmoja kabla, na Oliver alikuwa amemwandikia barua kadhaa tangu hapo, akishiriki uzoefu wake wa kufanya kazi na Nabii. Si David wala yeyote katika familia yake aliyewahi kukutana na Joseph. Lakini wakati Oliver alipouliza kama yeye na Joseph wangeweza kuhamia kwenye nyumba ya Whitmer kumalizia kutafsiri Kitabu cha Mormoni, akina Whitmer bila wasiwasi walifungua milango yao. Na Bwana alikuwa na mengi zaidi kwa ajili ya akina Whitmer kuliko swala la kumpa tu makazi Nabii. Alikuwa na maelekezo maalumu kwa ajili yao, yanayopatikana katika Mafundisho na Maagano 14–17, na kwa muda walikuwa wawe mojawapo ya familia za msingi za Kanisa na mashahidi kwa Urejesho uliojifunua.

Kwa mengi zaidi kuhusu familia ya Whitmer, ona Saints, 1:68–71.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mafundisho na Maagano 14

Ninaweza kushiriki katika “kazi kuu na ya ajabu” ya Mungu.

Wakati alipokutana na Joseph Smith, David Whitmer alikuwa kijana aliyejitolea kwa dhati kwenye kazi yake katika shamba la familia. Lakini Bwana alikuwa na kazi tofauti akilini kwa ajili ya David—ingawa kwa njia fulani ilikuwa ikifanana na kulima. Unaposoma Mafundisho na Maagano 14:1–4, gundua jinsi Bwana anavyofananisha Kazi Yake na aina ya kazi David aliyoizoea. Unajifunza nini kuhusu kazi ya Mwokozi kutokana na mfanano huu?

Ni kwa jinsi gani unaweza “kuingiza mundu [yako]”? (mstari wa 4). Gundua ahadi zilizotolewa kote katika sehemu hii kwa wale ambao “wanatafuta kuanzisha na kustawisha … Sayuni” (mstari wa 6).

Mafundisho na Maagano 14:2

Neno la Mungu ni “hai na lenye nguvu.”

Bwana anafananisha neno Lake na “upanga wenye makali pande mbili” (Mafundisho na Maagano 14:2). Ni nini mfanano huu unapendekeza kwako kuhusu neno la Mungu? Kwa mfano, ni kwa jinsi gani neno lake ni hai, lenye nguvu, na kali? Ni kwa jinsi gani umepata uzoefu wa nguvu ya neno la Mungu?

Fikiria njia nyingine Mungu anavyoelezea neno Lake. Kwa mfano, unajifunza nini kuhusu neno la Mungu kutokana na mifanano katika vifungu vifuatavyo?

Zaburi 119:105 

Isaya 55:10–11 

Mathayo 4:4 

1 Nefi 15:23–24 

Alma 32:28 

Picha
upanga ukiwa juu ya maandiko

Bwana anafananisha neno Lake na upanga.

Mafundisho na Maagano 14:7

Uzima wa milele ni “kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu.”

Unaposoma Mafundisho na Maagano 14:7, tafakari kwa nini uzima wa milele ni “kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu.” Umaizi huu kutoka kwa Rais Russell M. Nelson unaweza kusaidia: “Chini ya mpango mkuu wa furaha wa Mungu, familia zinaweza kuunganishwa katika mahekalu na kujiandaa kurudi kuishi katika uwepo Wake mtakatifu milele na milele. Huo ndio uzima wa milele!” (“Thanks Be to God,” Ensign au Liahona, Mei 2012, 77).

Fikiria kuongeza marejeleo yanayofanana kwenye mstari wa 7 ambayo yanakusaidia kuelewa zaidi kuhusu uzima wa milele (ona “Uzima wa milele” katika Mwongozo wa Mada au Mwongozo kwenye Maandiko, scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Unajifunza nini ambacho kinakutia msukumo kujitahidi kwa ajili ya uzima wa milele?

Mafundisho na Maagano 15–16

Kuleta nafsi kwa Kristo ni thamani kubwa.

John na Peter Whitmer wote walitaka kujua nini “kingekuwa cha thamani kubwa” katika maisha yao (Mafundisho na Maagano 15:4; 16:4). Je, umewahi kujiuliza kuhusu hili wewe mwenyewe? Unaposoma Mafundisho na Maagano 15–16, tafakari kwa nini kuleta nafsi kwa Kristo ni thamani kubwa. Ni kwa jinsi gani unaweza kualika nafsi kwa Kristo?

Ona pia Mafundisho na Maagano 18:10–16.

Mafundisho na Maagano 17

Bwana anawatumia mashahidi kuanzisha neno Lake.

Shahidi ni nani? Kwa nini Bwana anawatumia mashahidi katika kazi Yake? (Ona 2 Wakorintho 13:1). Tafakari maswali haya unaposoma maneno ya Mungu kwa Mashahidi Watatu katika Mafundisho na Maagano 17. Inaweza pia kuwa yenye msaada kurejea “Ushuhuda wa Mashahidi Watatu” katika Kitabu cha Mormoni. Ni kwa jinsi gani mashahidi wanasaidia kutimiza “madhumuni ya haki” ya Mungu? (mstari wa 4).

Je, ulijua kwamba Mary Whitmer pia alipokea ushuhuda wa mabamba ya dhahabu? Malaika Moroni alimwonyesha kama shukrani kwa dhabihu alizofanya wakati Joseph, Emma, na Oliver walipokuwa wanaishi nyumbani kwake (ona Saints, 1:70–71). Je, unajifunza nini kutokana na uzoefu wake kuhusu kupokea ushahidi?

Ona pia Saints, 1:73–75; Ulisses Soares, “Kujitokeza kwa Kitabu cha Mormon,” Ensign au Liahona, Mei 2020, 32–35.

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kwa Familia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 14:1–4.Fikiria kuwaalika wanafamilia yako kutafuta virai vyenye uhusiano na kulima katika mistari hii. Kwa nini Bwana anafananisha neno Lake na mavuno? Tunaweza kufanya nini kusaidia katika kazi yake?

Mafundisho na Maagano 14:2.Shughuli kwa ajili ya mstari huu katika “Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Binafsi” inaorodhesha baadhi ya vifungu vya maandiko kuhusu neno la Mungu. Pengine wanafamilia wangeweza kuvisoma na kushiriki kile wanachojifunza. Ni kwa jinsi gani vifungu hivi vya maandiko vinatutia msukumo “kutii” neno la Mungu?

Mafundisho na Maagano 15:6; 16:6.Mistari hii ingeweza kutia moyo mazungumzo kuhusu mambo ambayo ni ya thamani kubwa kwa familia yako (ona pia Mafundisho na Maagano 18:10).

Mafundisho na Maagano 17.Familia yako inaweza kufurahia kuchora picha ya kila kitu ambacho Mashahidi Watatu walikiona (ona mstari wa 1). Unaposoma sehemu ya 17, tafuta virai ambavyo vinafundisha kuhusu umuhimu wa Kitabu cha Mormoni. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa mashahidi wa Kitabu cha Mormoni? Familia yako ingeweza pia kuangalia video “A Day for the Eternities” (ChurchofJesusChrist.org).

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “I’ll Go Where You Want Me to Go,” Nyimbo za Kanisa, na. 270.

Picha
ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Lucy Mack Smith na Mashahidi Watatu na Wanane

Malaika Moroni alimwonyesha Joseph Smith, Oliver Cowdery, David Whitmer, na Martin Harris mabamba ya dhahabu katika msitu karibu na nyumba ya Whitmer huko Fayette, New York. Wazazi wa Joseph walikuwa wakiwatembelea akina Whitmer wakati ule. Lucy Mack Smith, mama wa Joseph, alielezea athari ambazo uzoefu huu wa kimiujiza ulileta kwa mashahidi:

Picha
Lucy Mack Smith

“Ilikuwa kati ya saa tisa na kumi kamili. Bi. Whitmer na Bw. Smith na mimi tulikuwa tumeketi katika chumba cha kulala. Nilikaa kando ya kitanda. Wakati Joseph alipoingia, alijitupa chini karibu nami. ‘Baba! Mama!’ alisema. ‘Hamjui jinsi nilivyo na furaha. Bwana amesababisha mabamba kuoneshwa kwa watatu wengine zaidi yangu, ambao pia wamemuona malaika na watashuhudia kwenye ukweli wa kile nilichosema. Kwani wanajua wao wenyewe kwamba sizunguki zunguki kudanganya watu. Na ninahisi kama vile nimepunguziwa mzigo wa kuogofya, ambao ulikuwa mzito mno kwa mimi kuuvumilia. Lakini sasa itawabidi wabebe sehemu, na inafurahisha nafsi yangu kwamba sitakuwa tena peke yangu kabisa ulimwenguni.’ Martin Harris kisha akaingia ndani. Alionekana karibu kuzidiwa na furaha tele. Kisha alishuhudia juu ya kile alichokiona na kusikia, kama walivyofanya pia wengine, Oliver na David. Ushuhuda wao ulikuwa sawasawa katika ukweli kama ule uliopo katika Kitabu cha Mormoni. …

“Martin Harris hasa alionekana kabisa kushindwa kuelezea hisia zake kwa maneno. Alisema, ‘Sasa nimemuona malaika kutoka Mbinguni ambaye kwa uhakika ameshuhudia juu ya ukweli wa yale yote niliyoyasikia kuhusu kumbukumbu, na macho yangu yamemuona. Pia nimeyaangalia mabamba na kuyashika kwa mikono yangu na naweza kushuhudia hayo kwa ulimwengu wote. Lakini nimepokea mimi mwenyewe ushahidi ambao maneno hayawezi kuelezea, kwamba hakuna ulimi unaoweza kuelezea, na ninambariki Mungu kwa dhati ndani ya nafsi yangu kwamba ametenda wema kwa kunifanya mimi, hata mimi, shahidi wa ukuu wa kazi yake na mipango kwa niaba [ya] watoto wa watu.’ Oliver na David pia waliungana naye katika sifa za dhati kwa Mungu kwa ajili ya wema wake na rehema. Tulirudi nyumbani [Palmyra, New York,] siku iliyofuata, kundi dogo lenye furaha na shangwe.”1

Picha
Mashahidi Watatu

Picha za Oliver Cowdery, David Whitmer, na Martin Harris na Lewis A. Ramsey

Lucy Mack Smith pia alikuwepo wakati Mashahidi Wanane waliporudi kutoka kwenye tukio lao:

“Baada ya mashahidi hawa kurudi kwenye nyumba, malaika tena alijitokeza kwa Joseph; ndipo wakati huo Joseph aliyatoa mabamba na kumpa mikononi mwake. Jioni ile tulifanya mkutano, ambapo mashahidi wote walitoa ushuhuda wa mambo kama yalivyoelezwa hapo juu; na familia yetu yote, hata mpaka Don Carlos [Smith], ambaye alikuwa na umri wa miaka 14 tu, alishuhudia ukweli wa kipindi cha maongozi ya Mungu cha siku za mwisho—kwamba kilikuwa kimeanzishwa kikamilifu.”2

Picha
Joseph Smith akionyesha mabamba kwa Mashahidi Wanane

Sanamu ya kuchongwa ya Joseph Smith na Mashahidi Wanane na Gary Ernest Smith

Picha
malaika Moroni akionyesha mabamba ya dhahabu kwa Joseph Smith, Oliver Cowdery, na David Whitmer

Malaika Moroni Akionyesha Mabamba ya Dhahabu kwa Joseph Smith, Oliver Cowdery, na David Whitmer na Gary B. Smith

Chapisha