Mafundisho na Maagano 2021
Oktoba 18–24. Mafundisho na Maagano 121–123: “Ee Mungu, Uko Wapi?”


“Oktoba18-24. Mafundisho na Maagano 121–123: ‘Ee Mungu, Uko Wapi?’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Oktoba18-24. Mafundisho na Maagano 121–123,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
Gereza la liberty

Gereza la Liberty, na Al Rounds

Oktoba 18–24

Mafundisho na Maagano 121–123

“Ee Mungu, Uko Wapi?”

Uzoefu wako wa kujifunza maandiko utakuwa wenye fahari kama lengo lako ni kufunua ukweli. Anza kwa sala, msikilize Roho, na andika misukumo yako.

Andika Misukumo Yako

Usawa wa chini wa gereza la wilaya la Liberty, Missouri, lilijulikana kama gereza la chini ya ardhi. Kuta zilikuwa nene, sakafu ya mawe ilikuwa ya baridi na chafu, chakula—kile kilichokuwepo—kilikuwa kimeoza, na mwanga pekee uliingia kutoka madirisha membamba mawili ya chuma karibu na dari. Gereza hili la chini ndimo Joseph Smith na wachache wa ndugu zake walitumia muda mwingi wa kifungo chao—miezi minne ya baridi ya mwaka 1838–39—wakisubiri kesi kwa ajili ya mashitaka ya uhaini dhidi ya jimbo la Missouri. Muda wote huu, Joseph alikuwa mara kwa mara akipokea habari kuhusu mateso ya Watakatifu. Amani na matumaini ya Magharibi ya Mbali yalikuwa yameisha miezi michache tu, na sasa Watakatifu walikuwa wasio na makazi mara nyingine tena, wamefukuzwa kwenda kweye nyika kutafuta mahali pengine kuanza upya—wakati huu Nabii wao akiwa gerezani.

Si ajabu Joseph Smith kupaza sauti, “Ee Mungu, Uko Wapi?” Majibu aliyopokea, “elimu kutoka mbinguni” ambayo ilikuja “ikitiririka chini” katika gereza lile lenye taabu, inaonesha kwamba ingawa siku zote inaweza isiwe sawa, Mungu kamwe hayupo mbali. Hakuna nguvu iwezayo “kuzuia mbingu,” Nabii alijifunza. “Mungu atakuwa na [Watakatifu Wake waaminifu] milele na milele.” (Mafundisho na Maagano 121:1, 33; 122:9.)

Ona Watakatifu, 1:323–96; “Ndani ya Kuta za Gereza la Liberty,” Ufunuo katika Muktadha, 256–63.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mafundisho na Maagano 121:1–10, 23-33122

Shida zinaweza “kuwa kwa ajili ya manufaa [yangu].”

Wakati sisi au wale tunaowapenda wako katikati ya mateso, ni kawaida kustaajabu kama Mungu anatujua. Unaposoma Mafundisho na Maagano 121:1–6, fikiri kuhusu wakati ambapo ulikuwa na maswali au hisia sawa sawa na za Joseph Smith. Unapata nini katika jibu la Bwana ambacho kingeweza kukusaidia wakati unapokuwa na maswali hayo au hisia? Kwa mfano, katika mistari ya 7–10, 26–33, ona baraka Anazoziahidi kwa wale ambao “wanavumila [mateso] vizuri.” Unaposoma sehemu ya 122, fikiria jinsi Bwana anavyotutaka kuona dhiki zako.

Ona pia Henry B. Eyring, “Where Is the Pavilion?Ensign au Liahona, Nov. 2012, 72–75.

Mafundisho na Maagano 121:34–46

Tunaweza kufikia “nguvu za mbingu.”

Katika kile kilichoonekana kama hali ya udhaifu katika Gereza la Liberty, Joseph alipewa ufunuo kuhusu nguvu—si ya kisiasa au nguvu ya jeshi ambayo ilimwagwa juu ya Watakatifu bali “nguvu za mbinguni.” Unaposoma Mafundisho na Maagano 121:34–46, unajifunza nini kuhusu nguvu za Mungu? Ni kwa jinsi gani iko tofauti na nguvu za kiulimwengu? Kwa mfano, angalia maneno Bwana anayotumia katika mistari ya 41–43 kueleza “nguvu au ushawishi.” Yanafundisha nini kuhusu jinsi Mungu anavyodumisha “nguvu na ushawishi” Wake? Pengine mistari hii ingeweza kukutia moyo kutafakari maisha yako na kile unachoweza kufanya kuwa ushawishi kwa ajili ya mazuri katika mahusiano yako na wengine.

Mafundisho na Maagano 122

Yesu Kristo amejishusha chini ya vitu vyote.

Joseph Smith alikuwa amefungwa bila haki kwa zaidi ya miezi minne wakati rafiki zake na familia walipofukuzwa kutoka katika nyumba zao. Kazi ambayo kwayo alijitolea maisha yake ilionekana kuwa katika anguko. Unajifunza nini kuhusu Yesu Kristo kutokana na maneno Yake kwa Joseph katika sehemu ya 122? Je, unajifunza nini kuhusu Joseph? Je, unajifunza nini kuhusu wewe mwenyewe?

Ona pia Alma 7:11–13; 36:3; Mafundisho na Maagano 88:6.

Picha
Yesu katika ardhi ya Gethsemane

Walakini si kama Nitakavyo Mimi, bali kama Utakavyo Wewe, na Walter Rane

Mafundisho na Maagano 123

“Acha kwa shangwe tufanye vitu vyote ambavyo vipo katika uwezo wetu.”

Mnamo machi 1839, inawezakuwa ilionekana kwamba hapakuwa na zaidi ambacho watakatifu wangeweza kufanya kubadili hali yao ya kuhuzunisha. Bali katika barua zake zilizoandikwa kutoka Gereza la Liberty, Joseph aliwaambia kile ambacho wangeweza kufanya: “[kukusanya] ufahamu wa kweli zote” na “kusimama imara, kwa uhakika mkubwa, kuona wokovu wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 123:1, 17). Unapofikiria udanganyifu na “ujanja wa binadamu” katika ulimwengu wa leo, fikiria kuhusu vitu gani “vilivyopo katika uwezo [wako]” vya kufanya (mistari ya 12, 17). Kwa nini ni muhimu kufanya vitu hivi “kwa furaha”? (mstari wa 17). Nani unaemjua ambaye “amezuiliwa kuupata ukweli” (mstari wa 12), na unawezaje kumsaidia mtu huyu kuupata?

Maelezo mengi ambayo Joseph aliomba katika barua hii yalipelekwa serikalini na kuchapishwa kama mfululizo wa sehemu ya 11 katika gazeti la Nauvoo, Times and Seasons (ona “Historia ya Mateso, ya Kanisa la Yesu Kristo, la Wataktifu wa Siku za Mwisho huko Missouri, Disemba 1839–Oktoba 1840,” [josephsmithpapers.org]).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 121:1–10.“Gereza la chini” la Liberty lilikuwa futi 14 kwa 14.5 tu (mita 4.2 kwa 4.4). Ni jinsi gani unaweza kuisaidia familia yako kufikiria ingekuwaje kufungwa kwenye nafasi ya ukubwa huo kwa miezi minne ya baridi? Unaweza kupata maelezo mengine kuhusu hali ya Gereza la Liberty katika “Sura ya 46: Joseph Smith ndani ya Gereza la Liberty” (Hadithi za Mafundisho na Maagano, 172–74). Ungeweza pia kusoma “Sauti za Urejesho: Gereza la Liberty” mwisho wa muhtasari huu au angalia video ya muda wa Joseph katika Gereza la Liberty katika video ya Joseph Smith: Prophet of the Restoration (ChurchofJesusChrist.org, kuanzia dakika ya 43:00). Ni jinsi gani taarifa hii inaathiri jinsi tunavyohisi kuhusu kanuni katika Mafundisho na Maagano 121:1–10?

Mafundisho na Maagano 121:34–36, 41–45.Pengine mfano ungesaidia familia yako kuelewa “nguvu za mbingu.” Kwa mfano, ungeweza kufananisha nguvu za Mungu na nguvu za umeme; ni nini kingeweza kuzuia chombo cha umeme kisipokee nguvu? Ni kwa vipi mfano huu, pomoja na mistari ya 34–36, 41–45, vinatufundisha kuhusu jinsi ya kuongeza nguvu zetu za kiroho? Pengine wanafamilia wangeshiriki hadithi kutoka katika maisha ya Mwokozi ambayo yanafafanua sifa hizi.

Mafundisho na Maagano 122:7–9.Pengine wanafamilia watafurahia kufanya ishara ndogo ndogo ambazo zinahusisha misemo kutoka kwenye mistari hii ambayo inawavutia. Ishara hizi zingeweza kuonyeshwa katika nyumba yenu. Kwa nini ni muhimu kujua kwamba “Mwana wa Mtu amejishusha chini” ya vitu vyote?

Mafundisho na Maagano 123:12.Ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia watu “kujua … wapi pa kupata” ukweli?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo Uliopendekezwa: “Where Can I Turn for Peace?Nyimbo za Kanisa, na. 129.

Picha
ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Gereza la Liberty

Wakati amefungwa katika Gereza la Liberty, Missouri, Joseph Smith alipokea barua kumtaarifu kuhusu hali ya hatari ya watakatifu wa siku za Mwisho waliokuwa wakifukuzwa kutoka jimboni kwa amri ya gavana. Barua yenye uchungu ilikuja kutoka kwa mke wake Emma. Maneno yake, na jibu la barua ya Joseph, inaonesha vyote mateso yao na imani yao wakati huu mgumu katika historia ya Kanisa.

Barua kutoka kwa Emma Smith kwenda kwa Joseph Smith, Machi 7, 1839

“Kipenzi Mume wangu

“Baada ya kupata fursa ya kutuma kupitia rafiki, ninafanya jaribio la kukuandikia, bali sitajaribu kuandika hisia zangu zote, kwani hali uliyopo, kuta, nondo, na komeo, mito inayounguruma, vijito vinavyotiririka, milima inayoinuka, mabonde yanayozama, na mbuga zinazosambaa ambazo zinatutenganisha, na udhalimu wa kikatili ambao kwanza ulikutupa gerezani na bado unakushikilia huko, pamoja na fikra nyingi zingine, zinaweka hisia zangu mbali kusikoelezeka.

“Kama isingekuwa kufahamu kutokuwa na hatia, na mwingiliano wa rehema takatifu, nina uhakika kabisa kamwe nisingekuwa na uwezo kuweza kuvumilia vitendo vya mateso ambayo nimevipitia … ; lakini bado ninaishi na bado niko tayari kuteseka zaidi kama ni mapenzi ya huruma ya Mbinguni ambayo ninapaswa kuteseka kwa ajili yako.

“Sote tuko salama wakati huu, isipokuwa Fredrick ambaye anaumwa sana.

Alexander mdogo ambaye sasa yupo mikononi mwangu ni mmoja wa wadogo wanaopendeza uliowahi kuwaona katika maisha yako. Ana nguvu sana kwamba kwa msaada wa kiti atakimbia kuzunguka chumba kizima. …

“Hakuna yeyote bali Mungu anayejua fikra za akili yangu na hisia za moyo wangu nilipoiacha nyumba na mji wetu, na karibia vitu vyote ambavyo tulikuwa navyo isipokuwa Watoto wetu wadogo, na kuanza safari yangu kutoka Jimbo la Missouri, nikikuacha umefungiwa katika gereza lile la upweke. Bali kumbukumbu ni zaidi kuliko asili ya mwanadamu anayostahili kubeba. …

“… Ninatumaini siku nzuri zaidi bado zinakuja kwetu. … [Mimi] siku zote ni wako akupendaye.

“Emma Smith”1

Barua kutoka kwa Joseph Smith kwenda kwa Emma Smith, Aprili 4, 1839

“Mke—kipenzi—na nikupendaye.

“Usiku wa Alhamisi niliketi chini wakati jua likizama, tulipokuwa tunachungulia kupitia viunzi vya nondo vya gereza hili la upweke, kukuandikia, ili niweze kukujulisha hali yangu. Ni kwamba ninaamini sasa karibia miezi mitano na siku sita2 tangu nimekuwa chini ya mkunjo wa uso wa mlinzi usiku na mchana, na ndani ya kuta, viunzi vya nondo, na misuguano ya milango ya chuma ya Gereza ya upweke, giza, na chafu. Kwa hisia kubwa zinazojulikana kwa Mungu tu naandika barua hii. Tafakari za akili katika hali kama hizi zinaishinda kalamu, au ulimi, au Malaika, kuelezea, au kuchora, kwa mwanadamu ambaye kamwe hajapata uzoefu wa kile tunachopata sisi. … Tunaegemea kwenye mkono wa Yehova, na hakuna mwingine, kwa ajili ya wokovu wetu, na kama hafanyi, haitafanyika, unaweza kuwa na uhakika, kwani kuna kiu kubwa kwa ajili ya damu yetu katika jimbo hili; sio kwa sababu tuna hatia ya kitu chochote. … Mpenzi wangu Emma ninakufikiria wewe na watoto mara kwa mara. … Ninataka kumwona Frederick mdogo, Joseph, Julia, Alexander, Joana, na meja mzee [mbwa wa familia]. … Ningependa kutembea peku kutoka hapa kuja kwako, na kichwa wazi, na nusu uchi, kukuona na kufikiri ni furaha kubwa, na kamwe kutoona ni kazi. … Navumilia kwa ushupavu mateso yangu yote, na ndivyo ilivyo kwa wale ambao wapo nami; bado hakuna hata mmoja wetu aliyeasi. Ninakutaka wewe [kuto]ruhusu [watoto wetu] kunisahau mimi. Waambie Baba anawapenda kwa upendo mkamilifu, na anafanya yote awezayo kuwatoroka majambazi na kuja kwao. … Waambie Baba anasema hawana budi kuwa watoto wazuri, na kumjali mama yao. …

“ Wako,

“Joseph Smith Mdogo.”3

Muhtasari

  1. Letter from Emma Smith, 7 March 1839,” Letterbook 2, 37, josephsmithpapers.org; tahajia, alama za uandishi, na sarufi vimeboreshwa.

  2. Joseph na wenzake walikamatwa oktoba 31, 1838, na kuwekwa chini ya ulinzi mkali mchana na usiku. Baada ya shtaka la mwanzo huko Richmond, Missouri, walipelekwa kwenye Gereza la Liberty mnamo Desemba 1.

  3. Letter to Emma Smith, 4 April 1839,” 1–3, josephsmithpapers.org; tahajia, alama za uandishi na sarufi vimeboreshwa.

Picha
Joseph Smith katika Jela ya Liberty

Wakati Joseph Smith alipokuwa anateseka kwenye Gereza la Liberty, Bwana alimfariji na alimfunulia kweli kuu.

Chapisha