“Januari 4–10. Joseph Smith—Historia ya 1: 1–26: ‘Niliona Nguzo ya Mwanga,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Januari 4–10. Joseph Smith—Historia ya 1: 1–26,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021
Januari 4–10
Joseph Smith—Historia ya 1:1-26
“Niliona nguzo ya mwanga”
Unaposoma maandiko, fikiria kuhusu watoto unaowafundisha. Roho Mtakatifu anaweza kukupa uvuvio, kupitia misukumo unayopokea, ili kujua nini cha kufokasia katika darasa.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waalike watoto wachache kushiriki kile wanachojua kuhusu Joseph Smith na sala yake katika Kijisitu Kitakatifu (kuonesha picha ya Ono la Kwanza kunaweza kusaidia). Waulize wanahisi vipi wanaposikia kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walimtembelea Joseph Smith. Ikiwa Joseph Smith angekuwa anatembelea darasa letu, ni nini tungemuuliza kuhusu uzoefu wake?
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Joseph Smith—Historia ya 1:3–20
Joseph Smith aliandaliwa kuwa nabii wa Mungu.
Kujifunza kuhusu ujana wa Joseph Smith kungeweza kuwasaidia watoto kujifananisha naye na kujitayarisha kujifunza kutoka kwenye uzoefu wake. Pengine unaweza kuwasaidia kuona jinsi uzoefu wa Joseph kama mvulana ulivyomuandaa kuwa nabii wa Mungu.
Shughuli za Yakini
-
Muombe mtoto kushikilia picha ya Joseph Smith (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 87) wakati ukishiriki baadhi ya kweli kuhusu Joseph zinazopatikana katika Joseph Smith—Historia ya 1:3–14 (ona pia “Sura ya 1: Joseph Smith na Familia Yake,” Hadithi za Mafundisho na Maagano, 6–8, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Wasaidie kufananisha maelezo kuhusu familia yake na maisha yake na yao wenyewe. Shiriki ushuhuda wako kwamba Joseph alichaguliwa na Mungu na kuandaliwa kuwa nabii (ona “Sauti za Urejesho: Familia ya Joseph Smith,” katika Njoo, Unifuate—Kwa Watu Binafsi na Familia). Ikiwa kuna umuhimu, wafundishe watoto kwamba nabii ni mtu ambaye anazungumza kwa niaba ya Mungu.
-
Mwalike mvulana katika kata yako kutembelea darasa lako, akijifanya kuwa Joseph Smith. Andaa maswali machache kwa ajili ya watoto kumuuliza ambayo yanajibiwa katika Joseph Smith—Historia ya 1:3–20 (unaweza kutaka kushiriki maswali haya pamoja na mvulana huyo kabla). Kisha mwalike mvulana kusoma baadhi ya maneno ya Joseph Smith mwenyewe kuhusu Ono la Kwanza (kwa mfano, Joseph Smith—Historia ya 1:25).
Joseph Smith—Historia ya 1:10–17
Baba wa Mbinguni husikia na kujibu sala zangu.
Uzoefu wa Joseph Smith unaweza kuwapa msukumo watoto kusali kwa imani kwamba Mungu atawasikia.
Shughuli za Yakini
-
Waambie watoto kuhusu maswali aliyokuwa nayo Joseph Smith (ona Joseph Smith—Historia ya 1:10. Tunaweza kufanya nini wakati tunapokuwa na maswali kuhusu Mungu? Waoneshe watoto nakala ya Biblia, na elezea kwamba wakati Joseph Smith aliposoma Biblia, alijifunza kwamba angeweza “kuomba dua kwa Mungu” (Yakobo 1:5; ona pia Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 89). Toa ushuhuda wako kwamba tunaweza kumuuliza Mungu maswali kupitia sala.
-
Simulia kuhusu uzoefu wakati ulipokuwa umekanganyikiwa, ukaomba msaada kwa Mungu, na kupokea jibu. Wasaidie watoto kufikiri juu ya nyakati wakati sala zao zilipojibiwa. Ungeweza pia kushiriki hadithi kutoka kwenye majarida ya Kanisa kuhusu sala ya mtoto ikijibiwa.
Joseph Smith — Historia ya 1:17–19
Joseph Smith aliwaona Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo.
Unaweza kuwasaidia watoto kujenga msingi kwa ajili ya ushuhuda imara wa Ono la Kwanza la Joseph Smith. Shiriki nao jinsi ulivyopata ushuhuda wako wa tukio hili muhimu.
Shughuli za Yakini
-
Onesha picha ya Ono la Kwanza kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, na shiriki kwa maneno yako mwenyewe kile kilichotokea wakati Joseph aliposali. Waalike watoto kuchora picha zao za hadithi.
-
Waalike watoto kupaka rangi ukurasa wa shughuli ya wiki hii na uutumie kusimulia hadithi ya Ono la Kwanza (ona pia “Sura ya 2: Ono la Kwanza la Joseph Smith,” Hadithi za Mafundisho na Maagano, 9–12, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org).
-
Soma Joseph Smith—Historia ya 1:17, na waoneshe watoto maneno ambayo Baba wa Mbinguni aliyasema kwa Joseph Smith.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Joseph Smith—Historia ya 1:10–13
Mungu anaweza kujibu maswali yangu kupitia maandiko.
Joseph Smith alipata msukumo kwenye kifungu cha maneno alichosoma katika Biblia, na hili lilipelekea Ono la Kwanza na Urejesho wa Kanisa la Kristo. Wasaidie watoto kuona jinsi kujifunza maandiko kunavyoweza kuwasaidia kupata majibu ya maswali yao ya kiroho.
Shughuli za Yakini
-
Waoneshe watoto vitabu tofauti (kama ensaiklopidia au kitabu cha upishi), na wasaidie kufikiria maswali ambayo vitabu hivi vingeweza kujibu. Kisha waoneshe nakala ya maandiko. Ni maswali gani vitabu hivi vinaweza kujibu? Ungeweza kutoa mfano wa swali ambalo linajibiwa katika maandiko. Someni pamoja Joseph Smith—Historia ya 1:10–11 kutafuta ni maswali yapi Joseph Smith alikuwa nayo na majibu yapi alipata katika maandiko.
-
Wasaidie watoto kutafuta maneno katika mstari wa 12 ambayo yanaelezea jinsi kusoma Yakobo 1:5 kulivyomuathiri Joseph Smith. Shiriki uzoefu ambao umekuwa nao kwenye maandiko—kwa mfano, wakati ulipopata jibu la mojawapo ya maswali yako kupitia kusoma maandiko. Imbeni pamoja “Search, Ponder, and Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,109).
Joseph Smith—Historia ya 1:10–19
Baba wa Mbinguni husikia na kujibu sala zangu.
Mungu alimfahamu Joseph Smith, na wakati Joseph aliposali, Mungu alimsikia. Wakati uzoefu wa watoto unaowafundisha unaweza kuwa tofauti na wa Joseph, unaweza kuwasaidia kuhisi kwamba Mungu anawafahamu na huwasikia wakati wanaposali.
Shughuli za Yakini
-
Mwalike mzazi wa mmoja wa watoto kusimama nje ya darasa na kujibu swali kutoka kwa mtoto kwa kutumia mbinu kama vile kutuma arafa, kupiga simu, kuandika ujumbe, au kutuma mjumbe. Ni zipi baadhi ya njia Baba wa Mbinguni huwasiliana nasi? (ona “Ufunuo,” Mwongozo kwenye maandiko, scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Kulingana na Joseph Smith—Historia ya 1:16–19, ni kwa jinsi gani Baba wa Mbinguni alijibu sala ya Joseph Smith? Ni kwa jinsi gani amejibu sala zetu?
-
Imbeni pamoja “A Child’s Prayer” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 12–13).
Joseph Smith—Historia ya 1:14–19, 25
Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walimtokea Joseph Smith.
Kila mmoja wa watoto unaowafundisha anahitaji ushuhuda wa uzoefu wa Joseph Smith katika Kijisitu Kitakatifu. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia kupata au kuimarisha ushuhuda wao?
Shughuli za Yakini
-
Kufanyia marejeo tukio la Ono la Kwanza, andika ufupisho wa kila mstari kutoka Joseph Smith—Historia ya 1:14–19 kwenye vipande tofauti vya karatasi. Weka karatasi ndani ya kopo, na waalike watoto kuvichagua kimoja baada ya kingine na kuviweka ubaoni katika mpangilio sahihi.
-
Waalike watoto kufumba macho yao na kufikiria vile ambavyo ingekuwa kuwa Joseph pale unaposoma sehemu zilizochaguliwa za Joseph Smith—Historia ya 1:14–17. Waombe washiriki mawazo yao na hisia zao kuhusu uzoefu wa Joseph.
-
Onesha video “Ask of God: Joseph Smith’s First Vision” (ChurchofJesusChrist.org), na waombe watoto washiriki jambo wanalojifunza kuhusu ono la Joseph la Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
-
Someni pamoja ushuhuda wa Joseph katika Joseph Smith—Historia ya 1:25. Waombe watoto watafute maneno na virai ambavyo vinaonyesha imani ya Joseph. Ni kwa jinsi gani tunaweza kubaki waaminifu wakati watu wengine wanapotupinga?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kushiriki hadithi ya Ono la Kwanza la Joseph Smith na mtu mwingine—ikiwezekana, na mtu ambaye hajawahi kuisikia kabla. Wangeweza kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kuwasaidia kusimulia hadithi.