Mafundisho na Maagano 2021
Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9: “Huyu Ni Roho wa Ufunuo”


“Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9: ‘Huyu Ni Roho wa Ufunuo,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2021

Picha
mwandishi akiandika kwenye karatasi

Januari 25–31

Mafundisho na Maagano 6–9

“Huyu Ni Roho wa Ufunuo”

Anza kujitayarisha kufundisha kwa kusoma Mafundisho na Maagano 6–9. Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia na muhtasari huu unaweza kuchochea mawazo kuhusu jinsi ya kufundisha watoto katika darasa lako.

Andika Misukumo Yako

Picha
ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Je, watoto wanafahamu hadithi ya Oliver Cowdery kuhusu kupokea jibu la sala? (ona Saints, 1:58–60). Pengine wao pia waliwahi kuwa na uzoefu wa sala ambao wangeweza kuushiriki.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Mafundisho na Maagano 6:5; 8:2; 9:7–9

Baba wa Mbinguni anaweza kuzungumza nasi kupitia Roho Mtakatifu.

Wasaidie watoto kuelewa kwamba wanaye Baba mwenye upendo huko Mbinguni anayesikiliza sala zao na kuzijibu kupitia Roho Wake.

Shughuli Yamkini

  • Tumia “Sura ya 5: Joseph Smith na Oliver Cowdery” (Hadithi za Mafundisho na Maagano, 22–25, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org) kuwasimulia watoto kuhusu Oliver Cowdery na kile alichojifunza kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni anavyozungumza nasi. Waombe watoto wakuambie sehemu za hadithi wanazozipenda, na waache wafanye zamu kukusimulia kuhusu Oliver Cowdery.

  • Waambie watoto kwamba Oliver Cowdery alijaribu kutafsiri Kitabu cha Mormoni lakini hakuweza, hivyo Joseph alimuuliza Bwana ni kwa nini. Wasomee watoto jibu la Bwana: “unalazimika kulichunguza katika akili yako; ndipo uniulize kama ni sahihi” (Mafundisho na Maagano 9:8). Waalike wajifanye kama wanasoma na kusali. Wasaidie watoto kuelewa kwamba hivi pia ndivyo tunavyoweza kupokea majibu kutoka kwa Bwana—kwa kusoma na kuomba msaada Wake.

    Picha
    Oliver Cowdery

    Oliver Cowdery, na Lewis A. Ramsey

  • Waalike watoto kugusa vichwa vyao na vifua vyao pale unaposoma maneno “akili” na “moyo” katika Mafundisho na Maagano 8:2. Wasaidie kuelewa kwamba Baba wa Mbinguni huzungumza nasi kupitia Roho Mtakatifu, ambaye hutupatia mawazo na hisia. Imbeni pamoja wimbo kuhusu Roho Mtakatifu, kama vile “The Holy Ghost” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 105). Ni nini wimbo unafundisha kuhusu jinsi Roho anavyozungumza nasi? Shiriki uzoefu wakati ulipomhisi Roho Mtakatifu katika akili na moyo wako.

Mafundisho na Maagano 6:33–36

Kwa msaada wa Mwokozi, sipaswi kuogopa.

Joseph Smith na Oliver Cowdery walikuwa na sababu nyingi za kuogopa—mateso na umasikini vilikuwa baadhi tu ya changamoto zilizowakabili. Ujumbe wa Bwana kwa Joseph na Oliver unaweza pia kuwatia moyo watoto wakati wanapohisi kuogopa.

Shughuli Yamkini

  • Waombe watoto warudie kirai “msiogope, enyi kundi dogo” (Mafundisho na Maagano 6:34) mara kadhaa. Elezea kwamba kundi ni mkusanyiko wa wanyama, kama kondoo. Onesha picha ya Mwokozi kama mchungaji (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 64) na shuhudia kwamba Yeye anatulinda kama mchungaji anavyowalinda kondoo Wake. Kwa sababu anatupenda, hatuhitaji kuogopa.

  • Waruhusu watoto wajifanye kuwa kundi la kondoo wenye hofu. Ni nini wakati mwingine kondoo wanaweza kuogopa? Muache mtoto mmoja ajifanye kuwa mchungaji akiwaweka kondoo salama. Je, ni nini wakati mwingine tunakuwa na hofu nacho? Toa ushuhuda wako kwamba Yesu Kristo ni kama mchungaji wetu na kwamba Yeye anaweza kutuliza hofu zetu. Imbeni pamoja wimbo kuhusu Mwokozi, kama vile “Little Lambs So White and Fair” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 58).

  • Soma Mafundisho na Maagano 6:36 kwa watoto, na waalike warudie kirai “msitie shaka, msiogope.” Wasaidie watoto kufikiria njia ambazo wanaweza “kumtegemea,” au kumkumbuka Mwokozi katika wiki inayokuja (ona pia ukurasa wa shughuli ya wiki hii).

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Mafundisho na Maagano 6:5, 15–16, 22–23; 8:2; 9:7–9

Roho Mtakatifu huzungumza kwenye akili na moyo wangu.

Watoto unaowafundisha wanaweza kuwa wamepokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Je, wanaelewa jinsi ya kutambua ufunuo binafsi kutoka kwa Roho?

Shughuli Yamkini

  • Chora kichwa na moyo ubaoni. Wasaidie watoto kusoma mistari ifuatayo na kutambua ipi inaelezea Roho Mtakatifu akizungumza kwenye akili zetu, mioyo yetu, au vyote: Mafundisho na Maagano 6:15, 23; 8:2; 9:89:9. Waambie watoto, kutoka kwenye uzoefu wako, jinsi ilivyo wakati Roho Mtakatifu anapozungumza kwenye akili na moyo wako.

  • Someni pamoja Mafundisho na Maagano 6:5, na waalike watoto kushiriki uzoefu waliowahi kuwa nao wa kusali na kupokea majibu. Wasaidie kufikiria mifano ya mtu katika maandiko ambaye alisali na kupokea jibu la swali (ona 1 Nefi 2:16; Enoshi 1:1–6; Etheri 2:18–3:6).

  • Andika ubaoni Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu huzungumza nasi? Waalike watoto kupekua Mafundisho na Maagano 6:15–16, 22–23; 8:2; 9:7–9 kwa ajili ya majibu ya swali. Shiriki uzoefu ambapo wewe ulimhisi Roho Mtakatifu akizungumza nawe.

Mafundisho na Maagano 6:33–37

“Msiogope kufanya mema.”

Watoto unaowafundisha wanaweza wakati mwingine kuhisi woga kusimamia ukweli. Mafundisho na Maagano 6:33–37 inaweza kuwatia moyo kuwa majasiri, hata katika hali ngumu.

Shughuli Yamkini

  • Someni pamoja Mafundisho na Maagano 6:33, na jadilini kwa nini mtu anaweza kuogopa kufanya mema (ona pia mistari ya 28–29). Wasaidie watoto kutafuta maneno au virai katika mistari ya 33–37 ambavyo vinawapa ujasiri wa kufanya mema.

  • Wasaidie watoto kutengeneza michoro wanayoweza kubandika nyumbani ili kuwakumbusha “kumtegemea [Yesu Kristo] katika kila wazo” (mstari wa 36). Pale wanapotengeneza michoro yao, jadilini kile kumtegemea Mwokozi humaanisha na kwa jinsi gani kunaweza kuwaweka salama.

  • Imbeni pamoja wimbo kuhusu ujasiri, kama vile “Dare to Do Right” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 158) au “Let Us All Press On” (Nyimbo za Kanisa, na. 243). Waombe watoto watafute katika wimbo baadhi ya sababu za kwa nini “hatupaswi kuogopa” (mstari wa 36).

Mafundisho na Maagano 8:10

Ninaweza kuomba kwa imani.

Kote katika maandiko, Bwana anatukumbusha kuwa na imani Kwake. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto unaowafundisha kuwa na imani kubwa katika Yesu Kristo?

Shughuli Yamkini

  • Andika ubaoni Pasipo huwezi kufanya lolote; hivyo basi omba kwa . Waalike watoto kujaribu kufikiria neno ambalo linafaa katika sehemu zote mbili zilizo wazi. Kisha someni pamoja Mafundisho na Maagano 8:10 ili kupata jibu. Je, ni baadhi ya mambo gani ambayo tunaweza kufanya ikiwa tutakuwa na imani?

  • Baada ya kusoma kwa pamoja Mafundisho na Maagano 8:10, wasaidie watoto wafikirie mambo ambayo wangeweza kumuomba Bwana awasaidie kwayo. Waalike wachore picha ambayo inawakilisha kitu wanachopaswa kukiombea. Pale wanapolionesha darasa picha zao, waruhusu watoto wengine wabashiri kile picha inachowakilisha.

Picha
ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Wasaidie watoto kuchagua kirai kifupi kutoka Mafundisho na Maagano 6–9 ambacho wangependa kushiriki na mtu fulani nyumbani, kama vile “msiogope kufanya mema” (6:33), “msitie shaka, msiogope” (6:36), au “pasipo imani huwezi kufanya lolote” (8:10).

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Tumia hadithi. Hadithi huwasaidia watoto kuelewa kanuni za injili kwa sababu zinaonesha kwa mifano jinsi wengine wanavyoishi kanuni hizo. Unapofundisha, tafuta njia za kujumuisha hadithi—kutoka kwenye maandiko, kutoka kwenye historia ya Kanisa, au kutoka kwenye maisha yako mwenyewe—ambayo inaelezea kwa mfano kanuni katika maandiko.

Chapisha