Agano Jipya 2023
Desemba 18–24. Krisimasi: “Habari Njema ya Shangwe Kuu”


“Desemba 18–24. Krisimasi ‘Habari Njema ya Shangwe Kuu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2021)

“Desemba 18–24. Krisimasi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023

Mtoto mchanga

Mwanakondoo, na Jenedy Paige

Desemba 18–24

Krisimasi

“Habari Njema ya Shangwe Kuu”

Somo hili ni nafasi ya kuwasaidia watoto unaowafundisha kusherehekea kuzaliwa, maisha, na misheni ya Mwokozi wakati wa Krismasi. Weka wazo hili katika akili unapojiandaa kufundisha.

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Onyesha picha katika muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, na waalike watoto kushiriki kile wanachojua kuhusu kuzaliwa kwa Mwokozi.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

Mathayo 2:1–12; Luka 2:1–14

Yesu Kristo alikuja duniani kama mtoto.

Watoto wanapenda hadithi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Ni ukweli gani wa kimafundisho unaouona katika hadithi hii ambao unaona watoto wanapaswa kuuelewa?

Shughuli Yamkini

  • Wasomee watoto Luka 2:1–44, au uelezee matukio katika mistari hii kwa kurejelea kwenye “Sura ya 5: Yesu Kristo Amezaliwa” (katika Hadithi za Agano Jipya, 13–15, au video zinazofanana nazo katika ChurchofJesusChrist.org. Waalike watoto kuchora picha za matukio haya na wao wenyewe wazitumie picha hizi kueleza hadithi hizo. Kwa nini tuna furaha kwamba Yesu Kristo alizaliwa?

  • Waombe watoto kukueleza hadithi ya Mamajusi wakifuata nyota kumtafuta Yesu. Kama wanahitaji kukumbushwa juu ya hadithi, ona Mathayo 2:1–12 au “Sura ya 7: MamajusiHadithi za Agano Jipya, 18, au video inayofanana katika ChurchofJesusChrist.org. Ficha picha ya Yesu chumbani. Chora au kata kutoka kwenye karatasi nyota na uishike hewani. Waalike watoto kujifanya kuwa mamajusi wakibeba zawadi, na waongoze kuzunguka chumba kumtafuta Yesu. Wasaidie watoto wafikirie juu ya zawadi ambazo tunaweza kumpatia Yesu.

  • Imbeni nyimbo za dini za Krismasi au nyimbo nyingine pamoja na watoto (ona Nyimbo za Dini, na. 201–14; Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–54). Waombe waelezee kitu fulani ambacho kila wimbo unafundisha ambacho wanakiona ni muhimu kujua.

Yesu akipiga magoti katika Bustani ya Gethsemane

Gethsemane, na J. Kirk Richards

Yohana 3:16

Yesu Kristo alifanya iwezekane kwangu mimi kuishi pamoja na Baba wa Mbinguni tena siku moja.

Je, watoto unaowafundisha wanaelewa kwa nini Yesu Kristo alikuja duniani? Chukua muda kutafakari kile Mwokozi amekifanya kwako wewe binafsi na jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto kuelewa kile alichofanya kwa ajili yao.

Shughuli Yamkini

  • Leta zawadi iliyofungwa au boksi darasani na picha ya Yesu Kristo ikiwa ndani yake. Weka kibandiko kwenye zawadi na “Yohana 3:16” kimeandikwa juu yake, na waeleze watoto kwamba hili ni dokezo kuhusu zawadi hiyo ni nini. Soma Yohana 3:16 pamoja na watoto, na waalike kukisia zawadi hiyo ni kitu gani na ifungue. Je, ni kwa nini Mungu alimtuma Mwanaye kwetu?

  • Wasaidie watoto kumalizia sentensi hii: “Yesu Kristo alikuja duniani ili .” Kisha onyesha picha zinazohusiana na dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi, kifo, na Ufufuko (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 56–59), na kwa kifupi simulia kuhusu matukio haya. Mngeweza pia kuimba wimbo kuhusu kwa nini Yesu alikuja duniani, kama vile “He Sent His Son” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–35). Toa ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo na kile alichofanya kwa ajili yako.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

Mathayo 1:18–25; 2:1–12; Luka 1:26–38; 2:1–20

Yesu Kristo alikuja duniani kama mtoto.

Utawezaje kuwasaidia watoto kufokasi juu ya Yesu Kristo wakati wa Krismasi?

Shughuli Yamkini

  • Muombe mmoja wa watoto kusoma kuhusu matukio yanayohusiana na kuzaliwa kwa Mwokozi katika Mathayo 1:18–25; 2:1–12; Luka 1:26–38; 2:1–20. Waombe watoto wengine kuchukua zamu kuchora picha ubaoni za kile maandiko yanachoelezea. Je, hadithi hizi zinatufundisha nini kuhusu Yesu Kristo?

  • Waalike watoto waandike kwenye vipande kadhaa vya karatasi vitu ambavyo wangeweza kufanya ili kuwasaidia kuzingatia kwa Mwokozi wakati wa msimu wa Krismasi. (Wangeweza kupata mawazo kutoka kwenye video ya “Good Tidings of Great Joy: The Birth of Jesus Christ” katika ChurchofJesusChrist.org.) Waalike kushiriki kile walichoandika. Wahimize watoto kupeleka vipande hivyo vya karatasi nyumbani na kufanya pamoja na familia zao mapendekezo waliyoandika kwenye vipande hivyo.

  • Imbeni nyimbo za Krismasi zinazomhusu Mwokozi (ona Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–54; Nyimbo, na. 201–14), na waalike watoto kushiriki na wengine mstari wanaoupenda au kirai kutoka kwenye nyimbo hizo.

Yohana 3:16

Yesu Kristo alifanya iwezekane kwangu mimi kuishi pamoja na Baba wa Mbinguni tena siku moja.

Unawezaje kuwasaidia watoto kupitia upya kile walichojifunza mwaka huu na kuelewa kwa nini wanamhitaji Yesu Kristo katika maisha yao?

Shughuli Yamkini

  • Weka lebo kwenye kipande kimoja cha karatasi Yesu Kristo ni nani? Na kingine Kwa nini alikuja duniani? Na vibandike kwenye kuta tofauti za darasa. Mwalike kila mtoto kusoma mojawapo ya maandiko yafuatayo: Mathayo 16:15–16; Yohana 3:16; 1 Nefi 10:4; Mosia 3: 8; Alma 7:10–13; 3 Nefi 27:14–15. Waambie watoto watafute majibu ya maswali katika maandiko wanayosoma, kwa maswali mawili yaliyoko kwenye kuta. Waalike kuandika majibu yao na wayabandike kwenye ukuta karibu na swali sahihi. Je, tunawezaje kuonyesha shukrani zetu kwa kile ambacho Yesu Kristo amefanya kwa ajili yetu?

  • Waalike watoto kuorodhesha ubaoni majina yote au vyeo vya Yesu ambavyo wanaweza kuvifikiria (ona Kamusi ya Biblia, “Kristo, majina ya”). Je, majina haya yanatufundisha nini kuhusu Yesu Kristo na misheni Yake? Kwa nini tunamhitaji Yesu Kristo katika maisha yetu? Ili kusaidia kujibu swali hili, onyesha video ya “Why We Need a Savior—A Christmas Message about Our Savior Jesus Christ” (ChurchofJesusChrist.org).

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Himiza watoto kutafuta angalau njia moja ya kumhudumia mtu fulani mwingine au kuja karibu zaidi kwa Kristo Krismasi hii.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Waalike watoto kuelezea kitu wanachojifunza. Watoto wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa wa mema katika familia zao. Wahimize watoto unaowafundisha kushiriki na familia zao kitu walichojifunza katika Msingi. (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi30.)