“Januari 10–16. Mwanzo 3–4; Musa 4–5: Anguko la Adamu na Hawa’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano la Kale 2022 (2021)
“Januari 10–16. “Mwanzo 3–4; Musa 4–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2022
Januari 10–16
Mwanzo 3–4; Musa 4–5
Anguko la Adamu na Hawa
Fikiria kuhusu watoto unaowafundisha unaposoma Mwanzo 3–4 na Musa 4–5. Zingatia misukumo na hisia unazozipokea; zinaweza kusababisha mawazo mapya ya ufundishaji.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Onyesha picha ya Adamu na Hawa (ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia), na waombe watoto kusimama na kushiriki kile wanachokifahamu kuhusu hadithi hii.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Adamu na Hawa walifuata mpango wa Baba wa Mbinguni.
Wasaidie watoto kuelewa kile kilichotokea katika Bustani ya Edeni na jinsi ilivyosaidia kutimiza mpango wa wokovu wa Mungu. Baraka zipi tunazo kwa sababu ya uchaguzi ambao Adamu na Hawa waliufanya?
Shughuli Yamkini
-
Kufupisha hadithi ya Anguko la Adamu na Hawa, tumia “Adamu na Hawa” (katika Hadithi za agano la Kale). Wasaidie watoto kuelewa kwamba chaguo la Adamu na Hawa kula tunda lilikuwa sehemu ya mpango wa Baba wa Mbingu.
-
Mpe kila mtoto picha ambayo inawakilisha kitu kutoka kwenye hadithi ya Adamu na Hawa (kama vile mti, nyoka, bustani, au Yesu Kristo). Waombe wanyanyue picha zao juu kwa wakati unaofaa wakati unapoelezea hadithi na kusoma vifungu kutoka Musa 4. Ukurasa wa shughuli ya wiki hii pia unaweza kusaidia.
Ninaweza kuchagua mema.
Katika Musa 4:3, tunajifunza kwamba Shetani “alitafuta kuharibu uhuru wa kuchagua wa mwanadamu, ambao mimi, Bwana Mungu, nilikuwa nimempa.” Ni kwa jinsi gani utawasaidia watoto kuthamini uwezo wa kuchagua kati ya mema na mabaya?
Shughuli Yamkini
-
Ongea na watoto juu ya chaguzi kadhaa ulizozifanya leo, na uwasaidie kufikiria juu ya chaguzi walizozifanya. Wasomee kutoka Musa 4:3: “Uhuru wa kuchagua wa mwanadamu, ambao mimi, Bwana Mungu, nilikuwa nimempa.” Fafanua kuwa aya hii inatufundisha kuwa Mungu ametupa uwezo wa kufanya chaguzi. Toa shukrani yako kwamba una uwezo wa kuchagua haki, na ushuhudie kwamba watoto wanaweza pia kuchagua kufanya yaliyo sahihi.
-
Shiriki mifano michache rahisi ya mtoto kufanya chaguo sahihi au chaguo baya, na uwaombe watoto waonyeshe ikiwa chaguo ni sawa au sio sawa (wanaweza kusimama, kuonyesha ishara, au kuinua mikono yao). Toa ushuhuda wako kwamba Baba wa Mbinguni atatusaidia kuchagua haki, na waalike watoto kushiriki pia hisia zao.
-
Wasaidie watoto wafikirie chaguzi nzuri wanazoweza kufanya za kumfuata Yesu Kristo. Imbeni pamoja wimbo kuhusu kufanya maamuzi sahihi, kama vile ““Choose the Right Way”” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,160–61). Waambie watoto kuhusu wakati ambao ulifanya uchaguzi mzuri, na ongea juu ya jinsi ulivyohisi kwa sababu ya chaguo lako.
Ninaweza Kuomba kwa Baba wa Mbinguni.
Je, watoto unaowafundisha wanahitaji kujua nini kuhusu sala? Unapata nini katika mistari hii ambayo inaweza kuwasaidia?
Shughuli zYamkini
-
Soma Musa 5:4 kwa watoto. Wasaidie kuelewa kwamba wakati Adamu na Hawa walipoondoka kwenye Bustani ya Edeni, hawangeweza kuwa tena na Baba wa Mbinguni, lakini wangeweza kuomba kwake. Eleza kwamba tunaomba kwa Baba wa Mbinguni katika jina la Mwanawe, Yesu Kristo (ona Musa 5:8). Je, ni mambo gani tunaweza kusema kwa Baba wa Mbinguni katika sala zetu?
-
Waombe watoto wakuonyeshe kile ambacho wanafanya wanaposali. Pia unaweza kuonyesha picha ya mtu akiwa anasali (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 111–12) kuwafundisha watoto kwamba tunainamisha vichwa vyetu, kukunja mikono yetu, na kufumba macho yetu hutusaidia kuwa wanyenyekevu tunaposali.
-
Shiriki uzoefu wa kibinafsi kuhusu sala au ushuhuda wako wa sala. Imba na watoto wimbo kuhusu sala, kama vile “A Child’s Prayer” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 12–13).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Anguko la Adamu na Hawa lilikuwa sehemu ya mpango wa Mungu.
Kama Adamu na Hawa wangekaa katika Bustani ya Edeni, wasingekuwa na watoto na wasingesonga mbele kuwa kama Baba wa Mbinguni. Tunashukuru kwa chaguo lao la kula tunda kwa sababu uchaguzi huu ulituwezesha maisha yetu hapa duniani na fursa yetu ya uzima wa milele.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kufanya kazi pamoja kuelezea hadithi ya Anguko la Adamu na Hawa kwa maneno yao wenyewe. Shiriki mistari kutoka Mwanzo 3 kuwasaidia.
-
Wasaidie watoto kutafuta katika Musa 4:22–25, 29; 5:10–11 matokeo ya Adamu na Hawa kula tunda (ona pia 2 Nefi 2:19–25). Kwa nini uchaguzi wao ni baraka kwetu? Mwokozi alitusaidiaje kushinda dhambi na kifo?
Nina nguvu ya kuchagua.
Je, watoto unaowafundisha wanatambua ni zawadi ya thamani gani ya kuweza kuchagua kati ya zuri na baya? Hadithi ya Adamu na Hawa inawezaje kuwasaidia kuthamini zawadi hii?
Shughuli Yamkini
-
Fikiria somo rahisi la vitendo kama lifuatalo kuonyesha umuhimu wa chaguzi zetu: Waalike watoto kupaka rangi ukurasa wa shughuli za wiki hii, lakini wape rangi moja tu ya kutumia. Kwa nini itakuwa bora kuwa na chaguzi katika hali hii? Someni pamoja Musa 4:1–4 ili kuzungumzia juu ya kwa nini chaguzi ni za muhimu katika mpango wa Mungu.
-
Waalike watoto washiriki uzoefu wa kibinafsi wakati ilipobidi wao kuchagua kati ya zuri na baya. Acha wajadili athari yamkini za kila chaguo.
Kwa sababu ya Yesu Kristo, ninaweza kutubu na Kuishi tena na Mungu.
Baba wa Mbingu alimtuma Yesu Kristo kutuokoa kutoka kwenye matokeo ya Anguko. Kupitia dhabihu Yake ya upatanisho, Yesu aliwezesha iwezekane kwetu sisi kufufuliwa baada ya kufa na kusamehewa dhambi zetu tunapotubu.
Shughuli Yamkini
-
Andika vichwa vya habari viwili kwenye ubao: Kwa sababu ya Adamu na Hawa na Kwa sababu ya Yesu Kristo. Wasaidie watoto kutambua matokeo ya kuanguka mnaposoma pamoja Musa 4:25; 6:48; Warumi 5:12; 2 Nefi 2:22–23. Acha waandike wanachojifunza chini ya kichwa cha habari cha kwanza. Kisha wasaidie kutambua ni jinsi gani Yesu Kristo alishinda dhambi na kifo Moses 5:8–11, 14–15; 6:59; Alma 11:42. Acha waandike wanachojifunza chini ya kichwa cha habari cha pili. Kwa nini tunamshukuru Yesu Kristo?
-
Onyesha video inayohusu Upatanisho wa Mwokozi, kama vile “Because of Him” (ChurchofJesusChrist.org). Waalike watoto kushiriki jinsi wanavyohisi kuhusu Yesu Kristo.
-
Siku chache kabla, waombe watoto kadhaa kuchagua andiko au wimbo juu ya Upatanisho wa Mwokozi kwa ajili ya kushiriki darasani. Wahimize wazungumzie juu ya kwanini wanapenda andiko au wimbo huo. Imba wimbo mmoja au zaidi kwa pamoja.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kushiriki ukurasa wa shughuli wa wiki hii na familia zao na kuzungumzia juu ya baraka tulizo nazo kwa sababu ya Anguko la Adamu na Hawa.