Mafundisho na Maagano 2021
Novemba 22–28. Mafundisho na Maagano 135–136: “Yeye ‘Ametia Muhuri Huduma Yake na Kazi Yake kwa Damu Yake Mwenyewe’”


“Novemba 22–28. Mafundisho na Maagano 135–136: ‘Yeye “Ametia Muhuri Huduma Yake na Kazi Yake kwa Damu Yake Mwenyewe,”’” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Shule ya Jumapili: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Novemba 22–28. Mafundisho na Maagano 135–136,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2021

mwonekano wa nje wa Gereza la Carthage

Gereza la Carthage.

Novemba 22–28

Mafundisho na Maagano 135–136

Yeye “Ametia Muhuri Huduma Yake na Kazi Yake kwa Damu Yake Mwenyewe”

Unaposoma sehemu ya 135–36, Roho Mtakatifu anaweza kukupatia maarifa ambayo yanaweza kuwa muhimu kwa washiriki wa darasa lako. Mawazo katika muhtasari huu pia yanaweza kuchochea mawazo unayoweza kutumia unapofundisha.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki na wengine

Alika Kushiriki

Hii hapa ni njia moja ya kuwaalika washiriki wa darasa kutoa mawazo yao kuhusu sehemu ya 135–36. Waalike ili wafikirie kwamba wanaweza kuzungumza na mshiriki wa Kanisa wa mwaka 1844, mtu ambaye amefadhaishwa na kifo cha Joseph Smith na aliyekuwa na hofu kuhusu kile ambacho kifo hicho kingemaanisha kwa Kanisa. Je, tungeweza kushiriki naye nini kutoka kwenye sehemu hizi ambacho kingeweza kumsaidia mtu huyu?

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho

Mafundisho na Maagano 135; 136:37–39

Joseph na Hyrum Smith walitia muhuri ushuhuda wao kwa damu yao.

  • Je, ni kwa namna gani dhabihu za Joseph na Hyrum Smith “zilitia muhuri” shuhuda zao? Pengine washiriki wa darasa wanaweza kufikiria swali hili wanapopitia Mafundisho na Maagano 135; 136:37–39. Wanaweza kisha kuelezea utambuzi wowote wanaopokea. Pia wanaweza kuelezea hisia zao kuhusu utayari wa Joseph na Hyrun kutoa maisha yao kwa ajili ya ukweli. Wakati yawezekana tusiombwe kufa kwa ajili ya ukweli, je, maisha yetu yanawezaje kuwa kama “kutia muhuri” kwa ajili ya shuhuda zetu?

Mafundisho na Maagano135:3

Joseph Smith amefanya mengi kwa ajili ya wokovu wetu zaidi ya yeyote mwingine isipokuwa Yesu Kristo.

  • Je, unawezaje kuwasaidia washiriki wa darasa kufahamu kile ambacho Joseph Smith amefanya kwa ajili ya wokovu wao? Unaweza kuandika ubaoni Kwa sababu ya kile ambacho Bwana amefunua kupitia Joseph Smith, Mimi … na kisha waalike washiriki wa darasa kufikiria njia za kukamilisha sentensi hii. Wanaweza kuanza kwa kupekua Mafundisho na Maagano 135:3 kwa vitu ambavyo Joseph Smith alifanya ili kutusaidia sisi kupata wokovu. Zingatia kuwaalika washirki wa darasa kuelezea hisia zao kuhusu Joseph Smith na kile ambacho Bwana amekifunua kupitia kwake.

  • Njia nyingine ya kuwasaidia washiriki wa darasa kufikiria kuhusu wito wa Joseph Smith ni kuwaalika waandike wasifu mfupi wa marehemu Joseph Smith. Unaweza kutaka kujadili matukio au mafanikio muhimu kutokana na maisha yake ambayo wanaweza kujumuisha. Wanapata nini katika Mafundisho na Maagano 135 ambacho wanaweza kutaja? Ni nini wanaweza kusema katika wasifu wao wa marehemu ili kuwasaidia wengine kuimarisha imani yao katika huduma ya kiungu ya Joseph Smith?

  • Kweli nyingi kuhusu Yesu Kristo na Upatanisho wake zimefunuliwa kupitia kwa Joseph Smith—kweli ambazo zimechangia kwenye wokovu wa wanaume na wanawake wote. Ili kuwasaidia washirki wa darasa kutambua michango hii, unaweza kuonesha picha ya Yesu Kristo na waombe washiriki wachache wa darasa kushiriki mstari wanaoupenda zaidi kuhusu Yesu Kristo kutoka katika maandiko ambayo yamefunuliwa kupitia Joseph Smith: Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu. Maandiko haya yanatusaidiaje kufahamu na kusonga karibu na Mwokozi? Kweli zilizopo kwenye mistari hii zinachangia vipi katika wokovu wetu?

Mafundisho na Maagano 136

Tunaweza kutimiza mapenzi ya Bwana tukifuata ushauri wake.

  • Muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate— Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia unapendekeza kwamba washiriki wa darasa watafute ushauri katika Mafundisho na Maagano 136 ambao ungewasaidia kugeuza jaribu kuwa uzoefu wa kiroho. Unaweza kuwaomba washiriki wa darasa kueleza ushauri wowote wanaopata. Ungeweza pia kuwaomba kupekua sehemu hii wakitafuta ushauri ambao unaweza kutusaidia kufanikisha mapenzi ya Bwana katika siku yetu, kama vile ulivyowasaidia Watakatifu katika “misafara ya kwenda Magharibi” (mstari wa 1).

    Winter Quarters

    Winter Quarters, na Greg Olsen

  • Inaweza kuwa burudani kwa darasa lako kutengeneza bango kama yale yanayopatikana katika magazeti ya Kanisa kuhusu moja ya mistari inayopatikana katika sehemu ya 136. Wakifanya kazi wawili wawili au kibinafsi, washiriki wa darasa wanaweza kuanza kwa kupekua hiyo mistari kwa ajili ya ukweli ambao unawavutia sana. Kisha wanaweza kuunda bango rahisi linaloonesha jinsi ukweli huu, uliofundishwa mwaka 1847, bado unaweza kutusaidia leo.

ikoni ya nyenzo za ziada

Nyenzo za Ziada

Muziki Unaohusiana

Kuimba nyimbo zifuatazo za kanisa au kutazama video kunaweza kumwalika Roho Mtakatifu au kuvuvia majadiliano kuhusu kazi ya Nabii Joseph Smith na dhabihu za Watakatifu walioendelea baada yake.

“A Poor Wayfaring Man of Grief” (Nyimbo za Kanisa, na. 29). Akiwa katika Gereza la Carthage, Joseph Smith alimwomba John Taylor aimbe wimbo huu.

“Praise to the Man” (Nyimbo za Kanisa, na. 27; video, www.thetabernaclechoir.org/videos/praise-to-the-man-mormon-tabernacle-choir). Maneno ya wimbo huu wa Kanisa yaliandikwa kama heshima kwa Joseph Smith.

Come, Come, Ye Saints” (Nyimbo za Kanisa, na. 30; video, www.thetabernaclechoir.org/videos/come-come-ye-saints-mormon-tabernacle-choir).

Faith in Every Footstep” (video, www.thetabernaclechoir.org/videos/faith-in-every-footstep).

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Shuhudia juu ya mafundisho ya kweli. Unaweza kutoa ushuhuda wako kuhusu ukweli wa mafundisho katika kipindi kizima, si tu mwishoni mwa kipindi. Unapofanya hivyo, Roho atathibitisha ukweli wa mafundisho katika mioyo ya wale unaowafundisha. (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 21.)