Maandiko Matakatifu
2 Nefi 24


Mlango wa 24

Israeli itakusanywa na kufurahia pumziko la Milenia—Lusiferi alifukuzwa kutoka mbinguni kwa sababu ya maasi—Israeli itashinda Babilonia (ulimwengu)—Linganisha Isaya 14. Karibia mwaka 559–545 K.K.

1 Kwani Bwana atamrehemu Yakobo, na hata hivyo atachagua Israeli, na kuwaweka katika nchi yao wenyewe; na wageni wataunganishwa na wao, na kuungana na nyumba ya Yakobo.

2 Na watu watawachukua na kuwaleta mahali pao; ndiyo, kutoka mbali hadi miisho ya dunia; nao watarejea katika nchi zao za ahadi. Na nyumba ya Israeli itawamiliki, na nchi ya Bwana itakuwa kwa ajili ya watumishi na wajakazi; na watawachukua wafungwa wale waliowafunga; na watatawala juu ya watesi wao.

3 Na itakuwa kwamba katika siku ile kwamba Bwana atakupatia pumziko, kutoka kwa huzuni yako, na kutoka woga wako, na kutoka ufungwa mgumu ambao ulifanywa kutumika.

4 Na itakuwa kwamba katika siku ile, kwamba utarudia methali hii dhidi ya mfalme wa Babilonia, na kusema: Jinsi gani mwenye kudhulumu amekoma, na mji wa dhahabu kukoma!

5 Bwana amelivunja gongo la waovu, dalili za enzi za watawala.

6 Yeye aliyewapiga watu katika ghadhabu kwa mapigo yasiyokoma, yeye ambaye alitawala mataifa kwa hasira, ana adhibiwa, na hakuna yeyote atakayezuia.

7 Ulimwengu wote unapumzika, na umekuwa kimya; wanaanza kuimba.

8 Ndiyo, misunobari inakusherekea, na pia mierezi ya Lebanoni, ikisema: Tangu wewe ulazwe chini hakuna yeyote amekuja dhidi yetu.

9 Jehanamu imetaharuki kukulaki utakapokuja; inawaamsha wafu kwa sababu yako, hata walio wakuu wote wa dunia; imewainua kutoka viti vyao vya enzi wafalme wote wa mataifa.

10 Wote watanena na kukwambia: Je, nawe pia umekuwa mnyonge kama sisi? Je, nawe umekuwa kama sisi?

11 Fahari yako imeshushwa chini kaburini; na kelele ya mazeze yako haisikiki; funza ametandazwa chini yako, na funza wamekufunika.

12 Jinsi gani umeanguka kutoka mbinguni, Ee Lusiferi, mwana wa asubuhi! Je, umekatwa chini, ambaye alidhoofisha mataifa!

13 Kwani umesema moyoni mwako: Mimi nitapanda mbinguni, nitainua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu; nitaketi pia juu ya mlima wa mkutano, katika pande za kaskazini;

14 Nitapanda kupita vimo vya mawingu; nitakuwa kama yeye Aliye Juu Sana.

15 Bado wewe utashushwa chini jehanamu, hadi pande za shimo.

16 Wale watakaokuona watakukazia macho kwa makini, na kukufikiria, na watasema: Je huyu ni yule mtu aliyetetemesha dunia, aliyetingisha falme?

17 Na kufanya ulimwengu kama nyika, na kuangamiza miji iliyomo ndani yake, na hakufungua nyumba za wafungwa wake?

18 Wafalme wote wa mataifa, ndiyo, wote, wamezikwa kwa utukufu, kila mmoja wao katika nyumba yake mwenyewe.

19 Lakini wewe umetupwa mbali na kaburi lako kama tawi linalochukiza, na baki la wanaouawa, wanaodungwa kwa upanga, ambao wanashuka chini hadi kwenye mawe ya shimo; kama mzoga uliokanyagwa chini miguuni.

20 Wewe hutaunganishwa na wao katika mazishi, kwa sababu umeangamiza nchi yako na kuwaua watu wako; uzao wa waovu hautaheshimiwa kamwe.

21 Tayarisheni machinjo kwa watoto wao kwa sababu ya maovu ya baba zao, ili wasije wakainuka, wala kumiliki nchi, wala kujaza uso wa dunia na miji.

22 Kwani nitainuka dhidi yao, asema Bwana wa Majeshi, na kutenga kutoka Babilonia jina, na baki, na mwana, na mpwa, asema Bwana.

23 Pia nitaifanya makao ya ngojamaliko, na maziwa ya maji; na nitaifagia kwa ufagio wa maangamizo, asema Bwana wa Majeshi.

24 Bwana wa Majeshi ameapa, akisema: Kwa kweli vile nimefikiria, hivyo yatatimia; na yale niliyoamua, ndiyo yatabaki imara—

25 Kwamba nitamleta Mwashuri nchini mwangu, na kwenye milima yangu nitamkanyaga chini ya miguu; kisha nira yake itawaondokea, na mzigo wake kuondoka kutoka mabega yao.

26 Hili ndilo kusudi lililonuiwa duniani kote; na huu ndiyo mkono ambao umenyooshwa kwa mataifa yote.

27 Kwani Bwana wa Majeshi amenuia, na nani atakayelibatilisha? Na mkono wake umenyooshwa, na nani atakayeurudisha nyuma?

28 Katika ule mwaka ambao mfalme Ahazi alikufa kulikuwa na mzigo huu.

29 Usifurahi ewe, Ufilisti wote, kwa sababu fimbo ya aliyekupiga imevunjika; kwani kutoka mzizi wa nyoka atatoka fira, na uzao wake utakuwa nyoka wa moto arukaye.

30 Na mzaliwa wa kwanza wa maskini watakula, na walio na shida watalala kwa usalama; na nitaua mzizi wako kwa njaa, na yeye ataua baki lako.

31 Pigeni yowe, Ee lango; lia, Ee mji, wewe, Ufilisti wote, umeyeyuka; kwani kutoka kaskazini kutakuja moshi, na hakuna yeyote atakayekuwa pekee mahali alipopangiwa.

32 Nini hapo kitakacho wajibu wajumbe wa mataifa? Kwamba Bwana ameimarisha Sayuni, na walio maskini wa watu wake wataitumaini.