Mlango wa 17
Yesu anawaelekeza watu kutafakari maneno Yake na kuombea ufahamu—Anaponya wagonjwa wao—Anawaombea watu, akitumia lugha ambayo haiwezi kuandikwa—Malaika wanawahudumia na moto unawazingira watoto wao wadogo. Karibia mwaka 34 B.K.
1 Tazama, sasa ikawa kwamba baada ya Yesu kuzungumza maneno haya alitazama tena kwa umati, na akasema kwao: Tazama, muda wangu umewadia.
2 Ninahisi kwamba ninyi ni wadhaifu, kwamba hamwezi kufahamu maneno yangu yote ambayo nimeamrishwa na Baba kuwazungumzia wakati huu.
3 Kwa hivyo, nendeni nyumbani kwenu, na mfikirie vitu ambavyo nimesema, na mwulize kutoka kwa Baba, katika jina langu, ili muweze kufahamu, na kutayarisha akili zenu kwa kesho, na nitakuja kwenu tena.
4 Lakini sasa ninaenda kwa Baba, na pia kujidhihirisha kwa makabila yaliyopotea ya Israeli, kwani hawajapotea kwa Baba, kwani anajua mahali ambapo aliwapeleka.
5 Na ikawa kwamba baada ya Yesu kusema hivyo, alielekeza macho yake tena kwa umati, na akaona kuwa wanalia, na walikuwa wanamwangalia kwa uthabiti kama wanaotaka kumwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi.
6 Na akawaambia: Tazama, matumbo yangu yamejawa na huruma juu yenu.
7 Mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu? Waleteni hapa. Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au wa kupooza, au vilema, au ukoma, au walionyauka au ni viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu; matumbo yangu yamejaa na huruma.
8 Kwani ninaona kwamba mnataka kwamba niwaonyeshe kile ambacho nilifanya kwa ndugu zenu wa Yerusalemu, kwani naona kwamba imani yenu ni ya kutosha kwamba ningewaponya.
9 Na ikawa kwamba wakati alipokuwa amesema hivyo, umati wote, kwa lengo moja, ulisonga mbele na wagonjwa wao na waliosumbuka wao, na vilema wao, na vipofu wao, na bubu wao, na wote waliosumbuka kwa jinsi yoyote; na akawaponya kila mmoja vile waliletwa kwake.
10 Na wote, ambao walikuwa wameponywa, na wale ambao walikuwa wazima, waliinama chini miguuni mwake, na kumwabudu; na kadiri wengi walivyoweza walikuja kutoka miongoni mwa umati walibusu miguu yake, mpaka kwamba waliosha miguu yake na machozi yao.
11 Na ikawa kwamba aliamuru kwamba watoto wao wachanga waletwe.
12 Kwa hivyo walileta watoto wao wachanga na kuwapanga chini juu ya ardhi kumzunguka, na Yesu alisimama katikati; na umati ulitoa nafasi mpaka wote walipoletwa kwake.
13 Na ikawa kwamba baada ya wote kuletwa, na Yesu kusimama katikati, aliamuru umati kwamba wapige magoti chini.
14 Na ikawa kwamba baada ya hao kupiga magoti chini, Yesu alisononeka moyoni mwake, na kusema: Baba, ninasumbuliwa kwa sababu ya uovu wa nyumba ya Israeli.
15 Na baada ya kusema maneno haya, yeye mwenyewe pia alipiga magoti ardhini; na tazama aliomba kwa Baba, na vitu ambavyo aliomba haviwezi kuandikwa, na umati uliomsikiliza ulishuhudia.
16 Na kwa maneno haya walishuhudia: Jicho halijaona, wala sikio kusikia, hapo mbeleni, vitu vikubwa na vya ajabu vile tuliona na kusikia Yesu akisema kwa Baba;
17 Na hakuna ulimi unaoweza kusema, wala haiwezi kuandikwa na mtu yeyote, wala mioyo ya watu haiwezi kufikiria vitu vikubwa na vya ajabu kama tulivyoona na kusikia Yesu akisema; na hakuna yeyote ambaye anaweza kuona shangwe iliyojaza nafsi zetu wakati tulipomsikia akituombea kwa Baba.
18 Na ikawa kwamba baada ya Yesu kumaliza kuomba kwa Baba, aliinuka; lakini umati ulikuwa na shangwe iliyokuwa kubwa sana kwamba walishindwa.
19 Na ikawa kwamba Yesu aliwazungumzia, na kuwaambia wasimame.
20 Na waliinuka kutoka ardhini, na akawaambia: Heri kwenu kwa sababu ya imani yenu. Na sasa tazama, shangwe yangu imetimia.
21 Na baada ya kusema maneno haya, alilia, na umati ulishuhudia hii, na akachukua watoto wao wachanga, mmoja mmoja, na kuwabariki, na kuomba kwa Baba juu yao.
22 Na baada ya kufanya hivi alilia tena;
23 Na alizungumza kwa umati, na kuwaambia: Tazama wachanga wenu.
24 Na walipotazama kuona walielekeza macho yao mbinguni, na wakaona mbingu zikifunguka, na wakaona malaika wakiteremka kutoka mbinguni kama wakiwa katikati ya moto; na walikuja chini na kuzunguka wale wachanga, na walizungukwa na moto; na malaika waliwahudumia.
25 Na umati uliona na kusikia na wanashuhudia; na wanajua kwamba maandishi yao ni ya kweli kwani wote waliona na kusikia, kila mtu binafsi; na idadi yao ilikuwa karibu watu elfu mbili na mia tano; na walikuwa wanaume, wanawake, na watoto.