Maandiko Matakatifu
Alma 25


Mlango wa 25

Ujeuri wa Walamani unasambaa—Uzao wa makuhani wa Nuhu unaangamia vile nabii Abinadi alipobashiri—Walamani wengi wanageuka na kuungana na watu wa Anti-Nefi-Lehi—Wanaamini katika Kristo na kuhifadhi sheria ya Musa. Karibia mwaka 90–77 K.K.

1 Na tazama, sasa ikawa kwamba wale Walamani walikuwa na hasira sana kwa sababu walikuwa wamewaua ndugu zao; kwa hivyo waliapa kulipiza kisasi juu ya Wanefi; na hawakujaribu mara nyingine tena kuua watu wa Anti-Nefi-Lehi kwa wakati huo.

2 Lakini walichukua majeshi yao na wakaenda juu kwenye mipaka ya nchi ya Zarahemla, na kuwashambulia watu ambao walikuwa kwenye nchi ya Amoniha na kuwaangamiza.

3 Na baada ya hayo, walikuwa na vita vingi na Wanefi, ambako walikimbizwa na kuuawa.

4 Na miongoni mwa Walamani ambao waliuawa karibu wote walikuwa uzao wa Amuloni na ndugu zake, ambao walikuwa makuhani wa Nuhu, na waliuawa kwa mikono ya Wanefi;

5 Na waliosalia, wakikimbilia kwenye nyika ya mashariki, na wakijitwalia uwezo na mamlaka juu ya Walamani, walisababisha kwamba wengi wa Walamani waangamizwe kwa moto kwa sababu ya imani yao—

6 Kwa sababu wengi wao, baada ya kuumia kwa hasara nyingi na mateso mengi, walianza kuvurugwa na kukumbuka maneno ambayo Haruni na ndugu zake waliwahubiria nchini mwao; kwa hivyo, walianza kutoamini desturi za babu zao, na kuamini katika Bwana, na kwamba aliwapa Wanefi uwezo mwingi; na hivyo kulikuwa na wengi wao ambao waligeuka nyikani.

7 Na ikawa kwamba wale watawala ambao walikuwa baki la watoto wa Amuloni walisababisha kwamba wauawe, ndiyo, wale wote ambao waliamini katika vitu hivi.

8 Sasa haya mauaji yalisababisha kwamba wengi wa ndugu zao wachochewe na kukasirika; na kukaanza kuwa na ubishi nyikani; na Walamani wakaanza kufuata uzao wa Amuloni na ndugu zake na kuanza kuwaua; na wakakimbilia upande wa mashariki ya nyika.

9 Na tazama wanatafutwa hadi siku hii na Walamani. Hivyo maneno ya Abinadi yalitimizwa, ambayo alisema kuhusu uzao wa makuhani ambao walisababisha kwamba ateswe na kifo kwa moto.

10 Kwa sababu aliwaambia: Yale mtakayonifanyia yatakuwa mfano wa vitu vitakavyokuja.

11 Na sasa Abinadi alikuwa wa kwanza aliyeumia kifo kwa moto kwa sababu ya kuamini kwake katika Mungu; sasa hivi ndivyo alivyomaanisha, kwamba wengi wataumia kifo kwa moto, kulingana na vile alivyoumia.

12 Na akawaambia makuhani wa Nuhu kwamba uzao wao utasababisha wengi wauawe, kwa njia sawa vile alivyokuwa, na kwamba watatawanyika nje na kuuawa, hata vile kondoo huwa kama hawana mlinzi hukimbizwa na kuuawa na wanyama wa mwitu; na sasa tazama, maneno haya yalithibitishwa, kwani walikimbizwa na Walamani, na waliwindwa, na kuuawa.

13 Na ikawa kwamba Walamani walipoona kwamba hawangeweza kuwashinda Wanefi walirudi tena kwenye nchi yao; na wengi wao walienda kuishi kwenye nchi ya Ishmaeli na nchi ya Nefi, na wakaungana na watu wa Mungu, ambao walikuwa watu wa Anti-Nefi-Lehi.

14 Na pia walizika silaha zao za vita, vile ndugu zao walivyofanya, na wakaanza kuwa watu wenye haki; na wakatembea kwa njia za Bwana, na kuchunguza na kuweka amri zake na sheria zake.

15 Ndiyo, na walihifadhi sheria ya Musa; kwani ilikuwa ya manufaa kwamba wahifadhi sheria ya Musa bado, kwani yote ilikuwa haijatimizwa. Lakini ijapokuwa sheria ya Musa, walitazamia kuja kwa Kristo, wakifikiri kwamba sheria ya Musa ilikuwa mfano wa kuja kwake, na kuamini kwamba lazima wahifadhi kutenda mambo mengine hadi wakati ambao atafichuliwa kwao.

16 Sasa hawakufikiria kwamba wokovu ulikuja kwa sheria ya Musa; lakini sheria ya Musa ilitumika kwa kuweka nguvu imani yao kwa Kristo; na hivyo waliweka matumaini kupitia imani, kwa wokovu wa milele, wakitegemea roho ya unabii, ambayo ilizungumzia vitu vinavyokuja.

17 Na sasa tazama, Amoni, na Haruni, na Omneri, na Himni, na ndugu zao walifurahi sana, kwa ushindi ambao waliupata miongoni mwa Walamani, wakiona kwamba Bwana alikuwa amewakubalia kulingana na sala zao, na kwamba alikuwa amethibitisha neno lake kwao kwa jumla.