Maandiko Matakatifu
Alma 43


Mlango wa 43

Alma na wanawe wanahubiri neno—Wazoramu na Wanefi wengine waasi wanakuwa Walamani—Walamani wanakabiliana na Wanefi katika vita—Moroni anawapa Wanefi silaha za kujilinda—Bwana anamwonyesha Alma mkakati wa Walamani—Wanefi wanalinda miji yao, uhuru, familia, na dini—Majeshi ya Moroni na Lehi yanawazingira Walamani. Karibia mwaka 74 K.K.

1 Na sasa ikawa kwamba wana wa Alma walikwenda miongoni mwa watu, kutangaza neno kwao. Na Alma, pia, mwenyewe, hangepumzika, na yeye pia alienda mbele.

2 Sasa hatutazungumza mengi kuhusu kuhubiri, kwao isipokuwa kwamba walihubiri neno, na ukweli, kulingana na roho ya unabii na ufunuo; na walihubiri kulingana na mpango mtakatifu wa Mungu ambao waliitiwa.

3 Na sasa narudia historia ya vita miongoni mwa Wanefi na Walamani, katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa waamuzi.

4 Kwani tazama, ikawa kwamba Wazoramu waligeuka na kuwa Walamani; kwa hivyo, katika mwanzo wa mwaka wa kumi na nane watu wa Wanefi waliona kwamba Walamani walikuwa wanataka kuwashambulia; kwa hivyo walijiandaa kwa vita; ndiyo, walikusanya pamoja majeshi yao katika nchi ya Yershoni.

5 Na ikawa kwamba Walamani walikuja kwa maelfu; na wakaja katika nchi ya Antionumu, ambayo ni nchi ya Wazoramu; ambamo mtu kwa jina la Zerahemna alikuwa kiongozi.

6 Na sasa, kwa vile Waamaleki walikuwa watu waovu na wauaji kuliko Walamani walivyokuwa, kwao wenyewe, kwa hivyo, Zerahemna aliteua makapteni wakuu juu ya Walamani, na wote walikuwa Waamaleki na Wazoramu.

7 Sasa alifanya hivi ili kuhifadhi chuki yao kwa Wanefi, ili awamiliki na kutimiza kusudi lake.

8 Kwani tazama, kusudi lake lilikuwa kuwavuruga Walamani wawe na hasira dhidi ya Wanefi; alifanya hivi ili apate uwezo mwingi juu yao, na pia kwamba ajipatie uwezo juu ya Wanefi kwa kuwaweka katika utumwa.

9 Na sasa kusudi la Wanefi lilikuwa kulinda nchi yao, na nyumba zao, na wake zao, na watoto wao, ili wawaokoe kutoka kwa mikono ya maadui wao; na pia kwamba wahifadhi haki zao na mapendeleo yao, ndiyo, na pia uhuru wao, kwamba wapate kumwabudu Mungu kulingana na kutaka kwao.

10 Kwani walijua kwamba ikiwa wangeshikwa mateka na Walamani, kwamba yeyote atakayemwabudu Mungu kwa roho na kwa ukweli, Mungu wa kweli na anayeishi Walamani wangemwangamiza.

11 Ndiyo, na walijua pia ile chuki mbaya iliyokuweko ya Walamani kwa ndugu zao, ambao walikuwa watu wa Anti-Nefi-Lehi, ambao waliitwa watu wa Amoni—na hawengechukua silaha, ndiyo, walikuwa wamefanya agano ambalo hawangevunja—kwa hivyo, kama wangeanguka kwenye mikono ya Walamani wangeangamizwa.

12 Na Wanefi hawangekubali kwamba waangamizwe; kwa hivyo waliwakabidhi nchi kwa ajili ya urithi wao.

13 Na watu wa Amoni walitoa sehemu kubwa ya mali yao kwa Wanefi kusaidia majeshi yao; na hivyo Wanefi walilazimishwa, kusimama, pekee yao, dhidi ya Walamani, ambao walikuwa muungano wa Lamani na Lemueli, na wana wa Ishmaeli, na wale wote ambao hawakukubaliana na Wanefi, ambao walikuwa ni Waamaleki na Wazoramu, na uzao wa makuhani wa Nuhu.

14 Sasa vile vizazi vilikuwa vingi, karibu vile na vya Wanefi walivyokuwa; na hivyo Wanefi walilazimishwa kupigana na ndugu zao, hata kwa kumwaga damu.

15 Na ikawa wakati majeshi ya Walamani yalipokuwa yamejikusanya pamoja katika nchi ya Antionumu, tazama, majeshi ya Wanefi yalikuwa yamejiandaa kukabiliana nao katika nchi ya Yershoni.

16 Sasa, kiongozi wa Wanefi, au mtu ambaye alichaguliwa kuwa kapteni mkuu juu ya Wanefi—sasa kapteni mkuu alichukua jukumu la kuamrisha majeshi yote ya Wanefi—na jina lake lilikuwa Moroni;

17 Na Moroni alijitwalia amri yote, na utawala wa vita vyao. Na alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano tu alipochaguliwa kuwa kapteni mkuu juu ya majeshi ya Wanefi.

18 Na ikawa kwamba alikabiliana na Walamani kwenye mipaka ya Yershoni, na watu wake walijihami na panga, na vitara, na kila aina ya silaha za vita.

19 Na wakati majeshi ya Walamani yalipoona kwamba watu wa Nefi, au kwamba Moroni, ameandaa watu wake kwa dirii na ngao za vita, ndiyo, na pia ngao za kujikinga vichwa, na pia kuwa walikuwa wamevaa mavazi mazito—

20 Sasa jeshi la Zerahemna halikuwa limejitayarisha kwa kitu cha aina hii; walikuwa tu na panga zao na vitara vyao, pinde zao na mishale yao, mawe yao na kombeo zao; na walikuwa uchi, isipokuwa tu ngozi iliyofunika viuno vyao; ndiyo, wote walikuwa uchi, isipokuwa Wazoramu na Waamaleki;

21 Lakini hawakuwa wamejihami dirii, wala ngao—kwa hivyo, waliogopa sana majeshi ya Wanefi kwa sababu ya silaha zao, ingawaje idadi yao ilikuwa kubwa mno kuliko ya Wanefi.

22 Tazama, sasa ikawa kwamba hawakuthubutu kuwashambulia Wanefi kwenye mipaka ya Yershoni; kwa hivyo waliondoka nje ya nchi ya Antionumu hadi kwenye nyika, na kusafiri wakizingira nyika, mbali na chimbuko la mto Sidoni, ili waingie katika nchi ya Manti na kuimiliki nchi; kwani hawakutarajia kwamba majeshi ya Moroni yangejua kule walikokwenda.

23 Lakini ikawa kuwa, walipoondoka kuelekea nyikani Moroni alituma wapelelezi nyikani kuchunguza kambi yao; na Moroni, pia, akiwa anaelewa unabii wa Alma, akatuma watu kwake, akitamani kwamba amwulize Bwana wapi majeshi ya Wanefi yangeenda kujikinga dhidi ya Walamani.

24 Na ikawa kwamba neno la Bwana lilimjia Alma, na Alma akawajulisha wajumbe wa Moroni, kwamba majeshi ya Walamani yalikuwa yameenda taratibu yakizunguka nyikani, ili yaingie kwenye nchi ya Manti, ili yaanzishe vita mahali ambapo watu walipungukiwa na nguvu. Na wale wajumbe walienda na kufikisha ujumbe kwa Moroni.

25 Sasa Moroni, akiacha sehemu ya jeshi lake katika nchi ya Yershoni, isiwe kwa vyovyote kwamba sehemu ya Walamani ije katika nchi hiyo na kumiliki mji, alichukua jeshi lililosalia na akaenda kwenye nchi ya Manti.

26 Na alisababisha kwamba watu wote katika sehemu hiyo wajikusanye wenyewe pamoja kukabiliana dhidi ya Walamani, kulinda ardhi yao na nchi yao, haki zao na uhuru wao; kwa hivyo walijiandaa dhidi ya ule wakati ambao Walamani wangekuja.

27 Na ikawa kwamba Moroni alisababisha kwamba jeshi lake lijifiche kwenye bonde ambalo lilikuwa karibu na ufuko wa mto Sidoni, ambao ulikuwa magharibi mwa mto Sidoni katika nyika.

28 Na Moroni aliweka wapelelezi kila mahali, ili aweze kujua wakati kambi ya Walamani itapokuja.

29 Na sasa, kwa vile Moroni alijua nia ya Walamani, kwamba ilikuwa nia yao kuangamiza ndugu zao, au kuwaweka chini yao na kuwafanya watumwa ili waanzishe utawala wao nchini kote;

30 Na pia akijua kwamba ilikuwa nia ya pekee ya Wanefi kuhifadhi nchi yao, na uhuru wao, na kanisa lao, kwa hivyo hakufikiri ni dhambi kuwalinda kwa werevu; kwa hivyo, aligundua kupitia kwa wapelelezi wake njia ambayo Walamani watafuata.

31 Kwa hivyo, aligawanya jeshi lake na kuleta sehemu moja kwenye bonde, na akawaficha mashariki, na kusini mwa mlima Ripla;

32 Na waliosalia aliwaficha kwenye bonde la magharibi, magharibi mwa mto Sidoni, na hivyo chini hadi kwenye mipaka ya nchi ya Manti.

33 Na hivyo akiwa ameweka jeshi lake kulingana na mipango yake, alikuwa tayari kukabiliana nao.

34 Na ikawa kwamba Walamani walikuja juu kaskazini mwa mlima, ambapo sehemu ya jeshi la Moroni ilijificha.

35 Na vile Walamani walikuwa wamepita mlima Ripla, na wakaja ndani ya bonde, na wakaanza kuvuka mto Sidoni, jeshi ambalo lilikuwa limefichwa kusini mwa mlima, ambalo liliongozwa na mtu ambaye jina lake lilikuwa Lehi, na akaongoza jeshi lake mbele na kuzingira Walamani mashariki nyuma yao.

36 Na ikawa kwamba Walamani, wakati walipoona Wanefi wakiwajia kutoka nyuma yao, waligeuka na kuanza kukabiliana na jeshi la Lehi.

37 Na kazi ya mauaji ilianza pande zote mbili, lakini ilikuwa ya kutisha zaidi kwa upande wa Walamani, kwani uchi wao ulijidhihirisha kwa mapigo makubwa ya Wanefi kwa panga zao na vitara vyao, ambavyo vilileta vifo karibu kwa kila pigo.

38 Wakati kwa upande mwingine, kulikuwa na mtu mmoja hapa na pale akiuawa miongoni mwa Wanefi, kwa panga zao na kwa kupoteza damu, hawa wakiwa wemejikinga sehemu muhimu za mwili, au sehemu muhimu za mwili zikikingwa kutoka na mapigo ya Walamani, kwa dirii zao, na ngao zao za mikono, na vyapeo vyao; na hivyo Wanefi waliendelea na kazi ya mauaji miongoni mwa Walamani.

39 Na ikawa kwamba Walamani waliogopa, kwa sababu ya uharibifu mkuu miongoni mwao, hata mpaka wakaanza kutoroka kuelekea mto Sidoni.

40 Na walifuatwa na Lehi na watu wake; na walikimbizwa na Lehi hadi kwenye maji ya Sidoni, na wakavuka maji ya Sidoni. Na Lehi aliweka majeshi yake kwenye ukingo wa mto Sidoni kwamba wasivuke.

41 Na ikawa kwamba Moroni na jeshi lake walikabiliana na Walamani kwenye bonde, kwa upande mwingine wa mto Sidoni, na wakaanza kuwaangukia na kuwauwa.

42 Na Walamani wakakimbia kutoka kwao, kuelekea nchi ya Manti; na wakakutana tena na majeshi ya Moroni.

43 Sasa kwa hali hii Walamani walipigana sana; ndiyo, hakujakuwa na wakati Walamani wamejulikana kwa kupigana kwa nguvu kama hii na ujasiri, la, sio hata kutoka mwanzoni.

44 Na walitiwa moyo na Wazoramu na Waamaleki, ambao walikuwa makapteni wao wakuu na viongozi, na Zerahemna, ambaye alikuwa kapteni wao mkuu, au kiongozi wao mkuu na amri jeshi; ndiyo, walipigana kama majoka yenye, na wengi wa Wanefi waliuawa kwa mikono yao, ndiyo, kwani walipasua kwa vipande viwili vyapeo vyao, na wakatoboa dirii zao nyingi, na wakakata mikono yao; na hivyo Walamani walikata kwa hasira yao nyingi.

45 Walakini, Wanefi waliongozwa na sababu njema, kwani hawakuwa wanapigania utawala wala uwezo lakini walipigania maskani yao na uhuru wao, wake zao na watoto wao, na vyote vyao, ndiyo, kwa kanuni zao za kuabudu na kanisa lao.

46 Na walifanya hayo ambayo walifikiri ni jukumu ambalo waliwiwa Mungu wao; kwani Bwana alikuwa amewaambia, na pia kwa babu zao, kwamba: Kwa kuwa hamna hatia kwa kosa la kwanza, wala la pili, hamtakubali wenyewe kuuawa kwa mikono ya maadui wenu.

47 Na tena Bwana, amesema kwamba: Mtalinda jamaa zenu hata kwa umwagaji wa damu. Kwa hivyo kwa sababu hii Wanefi walikuwa wakipigana na Walamani, kujilinda wenyewe, na jamaa zao, na nchi yao, na haki zao, na dini yao.

48 Na ikawa kwamba watu wa Moroni walipoona ukali na hasira ya Walamani, walikuwa karibu kurudi nyuma na kutoroka kutoka kwao. Na Moroni akiona kusudi lao, alituma ujumbe mbele na akavuta mioyo yao kwa mawazo haya—ndiyo, mawazo ya nchi yao, uhuru wao, ndiyo, uhuru wao kutoka utumwani.

49 Na ikawa kwamba waliwashambulia Walamani, na wakapaza sauti pamoja kwa Bwana Mungu wao, kwa ungwana wao na uhuru wao kutoka utumwani.

50 Na wakaanza kusimama dhidi ya Walamani kwa nguvu; na kwenye ile saa yenyewe kwamba walimlilia Bwana kwa uhuru wao, Walamani walianza kukimbia kutoka kwao; na wakakimbia hata kwenye maji ya Sidoni.

51 Sasa Walamani walikuwa wengi zaidi, ndiyo, zaidi ya mara mbili kuliko idadi ya Wanefi; walakini, walikimbizwa sana kwamba wakajikusanya kwa kundi moja katika bonde, kando ya mto Sidoni.

52 Kwa hivyo majeshi ya Moroni yaliwazingira, ndiyo, hata pande zote mbili za mto, kwani tazama, kwa upande wa mashariki kulikuwa na watu wa Lehi.

53 Kwa hivyo wakati Zerahemna alipoona watu wa Lehi upande wa mashariki wa mto Sidoni, na majeshi ya Moroni upande wa magharibi wa mto Sidoni, kwamba walikuwa wamezingirwa na Wanefi, walishikwa na woga.

54 Sasa Moroni, alipoona woga wao, aliamuru watu wake waache kumwaga damu yao.