Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 49


Sehemu ya 49

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Sidney Rigdon, Parley P. Pratt, na Leman Copley huko Kirtland, Ohio, 7 Mei 1831. Leman Copley alikuwa ameikumbatia injili lakini bado ameshikilia baadhi ya mafundisho ya Shakers (United Society of Believers in Christ’s Second Appearing [Muungano wa Jumuiya ya Waumini wa Kuonekana kwa Kristo Mara ya Pili]), madhehebu ambayo alikuwepo awali. Baadhi ya imani za Shakers ilikuwa kwamba Ujio wa Pili wa Yesu Kristo tayari ulikwishatimia na kwamba alionekana katika umbile la mwanamke, Ann Lee; Wao hawakuona kama ubatizo wa maji ulikuwa ni kitu cha lazima. Walikataa ndoa na waliamini katika maisha ya useja. Baadhi ya Shakers pia walikataza ulaji wa nyama. Katika utangulizi wa ufunuo huu, historia ya Joseph Smith inaeleza, “Ili kuweza kupata ufahamu sahihi juu ya jambo hili, nilimwomba Bwana, na kupokea yafuatayo.” Ufunuo huu unakanusha baadhi ya imani ya kundi hili la Shakers. Ndugu waliotajwa mwanzoni mwa sehemu hii walichukua nakala ya ufunuo na kuwapelekea jumuiya ya Shakers (karibu na Cleveland, Ohio) na kuwasomea hadi mwisho wa ufunuo, lakini ufunuo ulikataliwa.

1–7, Siku na saa ya ujio wa Kristo zitabaki bila kujulikana hadi Yeye atakapokuja; 8–14, Watu lazima watubu, kuiamini injili, na kuzitii ibada ili kupata wokovu; 15–16, Ndoa imeagizwa na Mungu; 17–21, Ulaji wa nyama umeruhusiwa; 22–28, Sayuni itastawi na Walamani watachanua kama waridi kabla ya Ujio wa Pili.

1 Sikilizeni maneno yangu, watumishi wangu Sidney, na Parley, na Leman; kwani tazameni, amini ninawaambia, kwamba ninawapa ninyi amri ya kwenda kuhubiri injili yangu ambayo mmeipokea, kama vile mlivyoipokea, kuwahubiria waumini wa Shakers.

2 Tazama, ninawaambia, kwamba wanatamani kujua ukweli kwa kiasi fulani, lakini siyo wote, kwani hawako sahihi mbele zangu na lazima watubu.

3 Kwa hiyo, ninawatuma ninyi, watumishi wangu Sidney na Parley, kuwahubiria injili.

4 Na mtumishi wangu Leman atatawazwa kwa kazi hii, ili naye akahojiane na kujenga hoja pamoja nao, siyo kulingana na yale aliyopokea kutoka kwao, bali kulingana na yale atakayofundishwa na watumishi wangu; na kwa kufanya hivyo nitambariki yeye, vinginevyo hatastawi.

5 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana; maana Mimi ni Mungu, na nimemtuma Mwana wangu wa Pekee katika ulimwengu kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu, na nimeagiza kwamba yule ampokeaye ataokolewa, na yule asiyempokea atahukumiwa

6 Na wakamtenda Mwana wa Mtu kama walivyotaka; na amejitwalia uwezo wake mkono wa kuume wa utukufu wake, na sasa anatawala katika mbingu, na atatawala hadi atakaposhuka duniani kuwaweka maadui wote chini ya miguu yake, wakati ambao u karibu—

7 Mimi, Bwana Mungu, nimesema haya, walakini habari ya saa ile na siku ile hakuna mtu ajuaye, hata malaika walio mbinguni, wala hawatajua hadi atakapokuja.

8 Kwa hiyo, ningependa kwamba watu wote watubu, kwani wote wapo chini ya dhambi, isipokuwa wale ambao nimejisazia mwenyewe, watu watakatifu ambao ninyi hamuwajui.

9 Kwa hiyo, ninawaambia kwamba nimelileta kwenu agano langu lisilo na mwisho, hata lile ambalo lilikuwepo tangu mwanzo.

10 Na kwamba nilichokiahidi nimekitimiza, na mataifa ya dunia yataliinamia; na kama siyo kwa hiari yao wenyewe, watashushwa chini, kwani kile ambacho sasa kimejikweza chenyewe kitadhiliwa kiuwezo.

11 Kwa hiyo, ninawapa amri kwamba nendeni miongoni mwa watu hawa, na muwaambie, kama mtume wangu wa zamani, ambaye jina lake lilikuwa Petro:

12 Amini juu ya jina la Bwana Yesu, ambaye alikuwa hapa duniani, na atakuja, aliye mwanzo na mwisho;

13 Tubuni na mkabatizwe katika jina la Yesu Kristo, kulingana na amri takatifu, kwa ondoleo la dhambi;

14 Na yule afanyaye hivi atapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, kwa kuwekewa mikono na wazee wa kanisa.

15 Na tena, amini ninawaambia, kwamba yeyote akatazaye kuoa hakuamriwa na Mungu, kwani ndoa imeamriwa na Mungu kwa mwanadamu.

16 Kwa hiyo, ni sheria kwamba yampasa kuwa na mke mmoja, na wawili watakuwa mwili mmoja, na hii yote ili dunia iweze kujibu madhumuni ya kuumbwa kwake;

17 Na kwamba iweze kujazwa kwa kipimo cha mwanadamu, kulingana na uumbaji wake kabla ya ulimwengu kuumbwa.

18 Na yeyote akatazaye ili kuzuia nyama, kwamba mtu asiile, huyo hakuagizwa na Mungu;

19 Kwani, tazama, wanyama wa porini na ndege wa angani, na kile ambacho hutambaa ardhini, vimetawazwa kwa matumizi ya wanadamu kwa ajili ya chakula na mavazi, na kwamba aweze kuwa navyo vingi.

20 Lakini haikutolewa kwamba mwanadamu amiliki zaidi ya mwingine, kwa sababu hiyo ulimwengu umelala dhambini.

21 Na ole kwa mwanadamu ambaye humwaga damu au auharibuye mwili na wala havihitaji.

22 Na tena, amini ninawaambia, kwamba Mwana wa Mtu aja siyo katika umbile la mwanamke, wala la mwanadamu atembeaye juu ya nchi.

23 Kwa hiyo, msidanganyike, bali endeleeni kwa uthabiti, mkitazamia kutetemeka kwa mbingu, na kutingishika kwa ardhi na kuyumbishwa mbele na nyuma kama mtu mlevi, na kwa mabonde kuinuliwa, na kusawazishwa kwa milima, na mahali pa makorongo kutengenezwa—na haya yote wakati malaika atakapopiga parapanda yake.

24 Lakini kabla ya siku ile kuu ya Bwana itakuwa, Yakobo atastawi nyikani, na Walamani watachanua kama waridi.

25 Sayuni itashamiri juu ya vilima na kufurahia juu ya milima, na watajikusanya pamoja mahali nilipopachagua.

26 Tazama, ninawaambia, enendeni kama nilivyowaamuru; tubuni dhambi zenu zote; ombeni nanyi mtapokea; bisheni nanyi mtafunguliwa.

27 Tazama, nitakwenda mbele yenu na nitawafuata nyuma; na nitakuwa katikati yenu, na wala hamtaaibika.

28 Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, na naja haraka. Hivyo ndivyo. Amina.