“Sherehe ya Kupendeza ya Papa,” Rafiki, Jan. 2024, 18–19.
Sherehe ya Kupendeza ya Papa
Vipi ikiwa mvua haitakata?
Hadithi hii ilitokea huko Samoa.
Mawingu meusi, mazito yalining’inia angani. Alex aliyakazia macho.
BOOM!
Radi zaidi zilinguruma. Matone makubwa, mazito ya mvua yalipiga kila mahala.
Alex alitikisa kichwa chake. Hii haikuwa nzuri. Si nzuri hata kidogo. Nyakati zingine, katika Samoa, mvua ingeweza kunyesha kwa siku kadhaa bila kukata. Lakini alitaka kumbukizi ya kuzaliwa ya babu yake iwe ya kupendeza.
Alex alikwenda chumbani kwake na kupiga magoti kando ya kitanda chake.
“Baba Mpendwa wa Mbinguni,” alisema: “Tafadhali sababisha mvua ikate kwa wakati kwa ajili ya sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa babu kesho. Tayari tumekwisha toa mialiko. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.”
Wakati Alex aliposimama, aliwaona Mama na Baba wamesimama mlangoni kwake. Walikuwa wakitabasamu.
“Nadhani hutojali kwamba tumesikia sala yako,” Mama alisema.
Alex alitabasamu. “Hiyo ni SAWA. Ninataka tu kesho iwe maalumu kwa ajili ya Papa. Haitakuwa kama ilivyozoeleka ikiwa tunahitaji kubaki ndani. Hatutakuwa na nafasi ya kudansi!”
Baba aliminya mabega ya Alex. “Bila kujali hali ya hewa ikoje, Papa atajua jinsi gani unavyompenda.”
Asubuhi iliyofuata, Mama na Baba walimwomba Alex atoe sala ya familia. Mvua ilikuwa bado inanyesha kwa wingi. Na bado haikuonekana kama ingekata.
“Tafadhali ibariki mvua ikate kwa wakati kwa ajili ya sherehe,” alisema. “Na tafadhali tubariki sote ili tuwe na wakati mzuri. Hususani Papa!”
Alex alitazama angani asubuhi yote. Kwa muda mrefu, hakuna kilichobadilika. Lakini kisha jambo la kustaajabisha lilitokea.
“Tazama!” Alex alipaza sauti. “Sehemu ya anga la bluu!” Familia yake ilikimbia nje kwenye ua. Mawingu yalikuwa yakianza kutoweka.
Ndani ya masaa machache, mawingu yote yalikuwa yametoweka! Hata matone ardhini yalikuwa yamekauka. Alex aliharakisha kupamba ua. Papa na wageni wengine watafika hapa punde.
Wakati Papa alipofika, alishangazwa. Aliangalia taa, mapambo yenye rangi za kupendeza na wageni wote. “Kila kitu kilionekana cha kupendeza,” alisema. “Asanteni sana!”
Sherehe ilikuwa ya kuburudisha kama vile Alex alivyotumaini. Walidansi nyimbo pendwa za Papa. Chakula kilikuwa kitamu—hasa mkate mtamu wa nazi. Alex hata aliimba na Papa.
Kipengele kizuri, hata hivyo, kilikuwa wakati ulipofika muda wa Siva Taualuga. Dansi hii kwa kawaida ilichezwa na mtu muhimu zaidi katika siku hiyo. Na, hakika, mtu huyo alikuwa Papa!
Papa alinyanyuka kucheza, lakini kisha akamtazama Alex. “Njoo uungane nami, Alex!” Papa aliita. Alex aliruka juu na kudansi pembeni ya Papa. Punde wengine wote walikuwa wakidansi pia.
Papa aliinama kumkumbatia Alex. “Umenifanya nijihisi mtu maalumu sana leo,” Papa alisema. “Hii ilikuwa sherehe ya kupendeza sana ya kumbukizi ya kuzaliwa.”
Baada ya sherehe kwisha, Alex alitazama juu angani. Mawingu meusi mazito yalikuwa yamerejea. Mvua ilianza kuwanyeshea tena. Lakini wakati huu, Alex hakujali. Alijua kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa amesaidia hali ya hewa ibaki kuwa rafiki muda mrefu vya kutosha kwa ajili ya sherehe ya Papa.
“Nakushukuru kwa hali ya hewa rafiki,” Alex alisali. “Na asante kwa Papa mzuri kama huyu.”