Rafiki
Maandiko ya Sami
Januari 2024


“Maandiko ya Sami,” Rafiki, Jan. 2024, 10–11.

Maandiko ya Sami

Sami pia alitaka kusoma.

Hadithi hii ilitokea huko Bolivia.

alt text

Papi alipiga makofi mwishoni mwa jioni ya familia nyumbani. “Nina wazo kwa ajili ya lengo la familia,” alisema. “Tusome Kitabu cha Mormoni pamoja kila siku.”

Kaka wakubwa wa Sami, Andrés na Juan, walilikubali wazo kwa kuitikia kwa kichwa na tabasamu pana.

“SAWA!” alisema Andrés.

Sami alikuwa na shauku pia. Lakini punde alikumbuka jambo. Aliinua mkono wake. “Sijui kusoma. Nitawezaje Kusaidia?”

Juan alipandisha na kushusha mabega. “Unaweza tu kusikiliza.”

Kaka zake Sami tayari walijua kusoma. Lakini Sami alikuwa na miaka mitano tu. Alikuwa bado hajajifunza kusoma.

“Lakini ninataka kusaidia pia!” Sami alisema kwa kukunja paji la uso.

Mama alimkumbatia Sami. “Na utasaidia,” alisema. “Daima kuna njia ya kufanya kile ambacho Mungu ametuamuru.”

Usiku uliofuata, familia ya Sami ilikusanyika kusoma Kitabu cha Mormoni. Wote walikuja na maandiko yao, isipokuwa Sami. Mama alimpa kitabu cha picha cha hadithi za Kitabu cha Mormoni.

“Bado huwezi kusoma maneno. Lakini unaweza kusoma picha,” alisema kwa tabasamu.

Sami alisogeza kitabu karibu. Sasa angeweza pia kusoma pamoja na familia yake!

Wote walipokezana zamu ya kusoma. Sami alitazama picha ambazo zilionesha hadithi. Ilipofika zamu yake, aliwaambia wengine kile alichokiona kwenye picha. Alisimulia maelezo mengi kadiri alivyoweza.

alt text

Kadiri siku zilivyoenda, Sami alitaka zaidi na zaidi kusoma. Mama alimfundisha sauti inayotengenezwa na kila herufi. Kisha akamwonesha jinsi ya kutoa sauti za maneno. Miezi kadhaa baadaye, Sami hakuhitaji sana kitabu cha picha. Badala yake, alisoma neno la mwisho la kila mstari ambao familia yake iliusoma. Mama alisoma neno kwanza, na Sami alilirudia.

Mwanzoni, walisoma taratibu. Kufikia mwisho wa kila mlango kulichukua muda mrefu. Andrés and Juan waligumia wakati ilipofika zamu ya Sami. Lakini bado walisoma kama familia.

Kidogo kidogo, Sami alisoma mengi zaidi. Alisoma neno moja kwenye mstari, kisha maneno mawili, kisha matatu. Kisha alianza kusoma mstari wote!

Karibu na mwisho wa lengo lao, Sami aliweza kusoma mistari michache peke yake. Usomaji wake ulikuwa umeboreka. Upendo wake kwa Kitabu cha Mormoni ulikuwa umeongezeka pia.

Hatimaye, familia ya Sami ilimaliza Kitabu cha Mormoni. Ilikuwa imechukua miaka miwili! Sasa Sami alikuwa na miaka saba na alikuwa amejifunza kusoma viruzi sana.

“Hongera!” Papi alisema. “Tumefanikisha!”

Sami alishangilia pamoja na familia yake. Alikuwa amewasaidia wamalize Kitabu cha Mormoni!

Juan alimpa Sami kumbatio kubwa. “Lipi litakuwa lengo lako kwa miaka miwili ijayo?”

Sami alitabasamu. Alisimama wima na kusema, “Nitasoma tena Kitabu cha Mormoni!”

PDF ya hadithi

Vielelezo na Melissa Manwill Kashiwagi