“Mazungumzo na Eilish kuhusu Roho Mtakatifu,” Rafiki, Jan. 2024, 40–41.
Mazungumzo na Eilish kuhusu Roho Mtakatifu
Eilish ni msichana wa miaka 12 kutoka Mkoa wa Mashariki ya Singapore. Tulimuuliza kuhusu jinsi Roho Mtakatifu anavyomsaidia.
Tuambie kuhusu wewe mwenyewe.
Ninapenda hasa kusoma na kucheza mpira wa wavu na somo langu pendwa shuleni ni hisabati. Chakula changu pendwa ni lazanya na rangi yangu pendwa ni nyekundu. Nitakapokua mkubwa, natumaini kuwa mwanasheria na kufanya kazi mahakamani.
Je, kwako wewe Roho Mtakatifu unamhisije?
Kwangu mimi, Roho Mtakatifu ni kama kuwa na rafiki wa karibu. Nahisi kama vile ni mtu ninayeweza kumtegemea pale ninapotii amri na maagano yangu na Baba wa Mbinguni. Ninamfikiria kama mwongozo na mwenzi wangu. Anaweza kunisaidia nifanye chaguzi nzuri.
Ni ushauri upi ungempa mtu ambaye hana hakika kama amemhisi Roho Mtakatifu?
Nyakati zingine mimi pia huwa sina hakika kuhusu ikiwa ninamhisi Roho Mtakatifu. Lakini ikiwa utalifikiria jambo hilo kwa undani, kusoma maandiko na kusali na ukahisi vizuri kulihusu, huyo ni Roho Mtakatifu. Wakati mwingine kumsikia Roho Mtakatifu si tu hisia. Inaweza pia kuwa wazo au dhana. Ikiwa bado unahisi kukanganyikiwa, unaweza mara zote kusali na kumwomba Bwana usaidizi tena.
Ni lini umemhisi Roho Mtakatifu?
Mwaka uliopita, nilicheza kwenye mashindano ya mpira wa wavu. Kama vile wengi wa wanatimu wenzangu, nilikuwa na hofu. Nilipoanza kucheza, timu yetu ilikuwa tayari imeshapoteza michezo miwili. Tulikata tamaa. Kisha watu waliokuwa wakitazama mchezo walisema maneno yasiyo ya ukarimu na tulihisi vibaya zaidi. Tulipoteza mchezo.
Mama yangu aliponiuliza jinsi mchezo ulivyokuwa, nilianza kulia. Nilikuwa nimevunjika moyo. Nilikwenda chumbani kwangu, ambapo palikuwa pazuri na patulivu na nilisali. Baada ya kusali, nilihisi utulivu na amani zaidi moyoni mwangu. Nilijua Roho Mtakatifu alikuwa amenifariji na kwamba daima angenisaidia. Kwa mashindano mengine yanayokuja mwaka huu, ninajua Roho atakuwa pamoja nami wakati ninapocheza.
Ni kwa namna ipi nyingine Roho Mtakatifu amekusaidia?
Roho Mtakatifu pia alinisaidia nilipohama kutoka darasa la Msingi kwenda darasa la Wasichana. Nilikuwa na shauku kuhusu kuhamia darasa la Wasichana. Lakini wakati huo huo pia nilihisi hofu. Nilikuwa pia kidogo na huzuni kuondoka darasa la Msingi.
Kabla ya darasa langu la kwanza, nilisali na kumwomba Baba wa Mbinguni anisaidie nifurahie darasa la Wasichana. Nilihisi amani moyoni mwangu wakati nilipoingia kwenye darasa langu jipya. Nilikuwa tayari kujifunza. Ilinisaidia nikumbuke kwamba Roho Mtakatifu daima atakuwepo kwa ajili yangu!