2022
Anzisha Sayuni Kati Yetu
Juni 2022


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Anzisha Sayuni Kati Yetu

Tunapowasaidia wengine wahisi kwamba wao ni sehemu ya, wanapoamini katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, wanaweza—na wataweza—kuwa waongofu kwa Bwana na kuwa wamoja kwenye Kanisa Lake la urejesho.

Nabii Moroni alifundisha kuhusu wale wanaokuja kwa Kristo kupitia ibada ya ubatizo na kufanya agano la kujichukulia juu yao jina la Yesu Kristo, “na daima kumkumbuka, na kushika amri zake ambazo amewapa”1.

“Na baada ya hao kupokewa kwenye ubatizo, na kupokelewa na kusafishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa na neno zuri la Mungu, kuwaweka kwa njia nzuri, kuwaweka waangalifu siku zote kwenye sala, wakitegemea tu katika nguvu ya wokovu wa Kristo, ambaye alikuwa mwanzilishi na mtimizaji wa imani yao”2.

Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Wakati wowote tunapofanya jambo lolote ambalo humsaidia yeyote kwenye upande wowote wa pazia kufanya na kutunza maagano yao na Mungu, tunasaidia kuikusanya Israeli”3. Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008) alitukumbusha kwamba “Kila mwongofu ni wa thamani.Kila mwongofu ni mwana au binti wa Mungu.Kila mwongofu ni jukumu kubwa na lenye uzito”4. Ni jambo la muhimu kwamba tuwape uangalizi wale ambao wamekuwa sehemu yetu wakati tunaposhiriki katika kazi hii kuu ya siku za mwisho.

Jukumu letu ni kufuata mfano wenye mwongozo wa kiungu wa Mwokozi Wetu na Mkombozi Wetu Yesu Kristo, wakati akikaribia mwisho wa huduma Yake duniani, alisema kwa Baba, “Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.

Anaendelea kusema “Mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea”5.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, ni sisi tunaoweza kuelewa vyema hali ya wale wanaofanya uamuzi wa kumwacha Mungu ashinde katika maisha yao. Hii ni sehemu ya agano tunalofanya na Baba yetu wa Mbinguni—mahususi, kwamba tutawaimarisha kaka na dada zetu katika mazungumzo yetu yote, katika sala zetu zote, katika kushawishi kwetu kote, na katika matendo yetu yote6.

Mnamo 1999, mwanamke aliyebatizwa karibuni katika Kanisa aliandika yafuatayo kwa Rais Gordon B. Hinckley, akisema: “‘Safari yangu ndani ya Kanisa ilikuwa ya pekee na yenye changamoto sana. Mwaka huu uliopita umekuwa mwaka mgumu ambao sijawahi kuuishi katika maisha yangu. Umekuwa pia wenye manufaa sana. Kama muumini mpya, ninaendelea kupata changamoto kila siku,’ . . .

‘Waumini wa Kanisa hawaelewi jinsi ilivyo kuwa muumini mpya wa Kansia. Kwa hivyo, ni vigumu kwao kuelewa jinsi ya kutusaidia.’ . . .

Anaendelea kusema, ‘pale sisi wachunguzi tunapokuwa waumini wa Kanisa, tunashangazwa kugundua kwamba tumeingia kwenye ulimwengu wa kigeni kabisa, ulimwengu wenye kaida zake, utamaduni na lugha yake. Tunagundua kwamba hakuna hata mtu mmoja au sehemu moja ya rejeleo ambayo tunaweza kuigeukia kwa ajili ya mwongozo katika safari yetu kwenye ulimwengu huu mpya. Mwanzoni safari inafurahisha, makosa yetu hata yanafurahisha, kisha hali inakuwa ya kukatisha tamaa na hatimaye, kukata tamaa kunageuka hasira. Na ni kwenye hatua hizi za kukata tamaa na hasira ndipo tunaondoka. Tunarudi kwenye ulimwengu tulikotoka, ambapo tulijua sisi ni akina nani, ambapo tuliweza kushiriki na ambapo tuliweza kuzungumza lugha.’”7

Ili kutusaidia kuwaimarisha waongofu wapya, Bwana amefunua kupitia Nabii wetu aliye hai, Rais Nelson, mbinu mpya, takatifu zaidi ya kuwatunza na kuwasaidia wengine. Inaitwa “Kuhudumu”, hii ni pale tunapowalinda watu wetu, na kuwalisha vitu vinavyohusu utakatifu8. Sala yangu, akina kaka na dada zangu wapendwa ni kwamba sote tuweke msimamo wa kujaliana sisi kwa sisi—na hasa waongofu wapya Kanisani.

Tunaweza kufanya hilo kwa kuzungumza, kusikiliza, kuelekeza, kujibu maswali yao, kutabasamu na kuwalisha. Haya yanaweza kuwa matendo rahisi, lakini yatakuwa na athari kubwa kwa wengine. Tunapaswa kuwasaidia wengine, ili wasihisi wapweke katika juhudi zao za kubaki na kuendelea kwenye njia ya agano, huku bado tukiwa na hisia za kuwa sehemu ya, katika familia ya Kristo9.

Ninawaalika muwafikie kwa urafiki na upendo wale wanaokuja Kanisani kama waongofu wapya. Hatuwezi kuwaacha wasimame peke yao. Wanahitaji usaidizi ili kuzoea taratibu na utamaduni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Acha tuwafundishe jinsi ya kusali, jinsi ya kusoma maandiko, jinsi ya kushuhudia, jinsi ya kulipa zaka na matoleo ya mfungo—acha tuwaalike kwenye madarasa ya seminari na kozi za Chuo cha Dini, acha tuwasaidie wafahamu jinsi ya kufanya Jioni ya Nyumbani, jinsi ya kushiriki kwenye kazi ya hekalu na Historia ya Familia, jinsi ya kutuma au kupeleka jina hekaluni kwa ajili ya ibada kwa niaba ya wafu. Acha tuwapeleke wakazuru hekaluni pamoja nasi punde tu wanapokuwa wamebatizwa.

Ninawaahidi kwamba ikiwa tutafanya mambo haya, Sayuni itajengwa hapa kati yetu. Tunapowasaidia wengine wahisi kwamba wao ni sehemu ya, wanapoamini katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, wanaweza—na wataweza—kuwa waongofu kwa Bwana na kuwa wamoja kwenye Kanisa Lake la urejesho.

Thierry K. Mutombo aliidhinishwa kama Sabini Mkuu mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2020. Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda, wao ni wazazi wa watoto sita.

Muhtasari

  1. Moroni 4:3.

  2. Moroni 6:4.

  3. Russell M. Nelson, “Acha Mungu Ashinde”, Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020.

  4. Teachings of Presidents of the Church: Gordon B. Hinckley, [2016], 298; “Converts and Young Men,” April 1997 General Conference.

  5. Yohana 17:8, 12.

  6. Ona Mafundisho na Maagano 108:7.

  7. Teachings of Presidents of the Church: Gordon B. Hinckley, 300-301; “Find the Lambs, Feed the Sheep,” Ensign, May 1999.

  8. Ona Mosia 23:18.

  9. Ona Waefeso 2:19.

Chapisha