UJUMBE WA KIONGOZI WA ENEO HUSIKA
Kuwaimarisha Waongofu Wapya
Bwana anatuhitaji tuwafikie waumini wapya wa Kanisa waliobatizwa.
Baba yetu wa Mbinguni ni pendo; Yeye anawapenda watoto Wake wote kwa upendo usio na masharti. Anataka kila nafsi ipewe thamani na kutunzwa kwa usawa ili kwamba hata mmoja asipotee.1
Waongofu wapya wanahitaji upendo, wanahitaji mtu wa kuwajali. Wanahitaji mtu anayeweza kuwasaidia waelewe mafundisho ya injili.
Wanaweza kufananishwa na mbegu iliyopandwa. Ni muhimu kwamba udongo uwe umeandaliwa vyema na kwamba mbolea imeongezwa kurutubisha udongo kabla ya mbegu kupandwa. Baada ya udongo kuandaliwa na kuongezewa mbolea, mbegu inapandwa na matunzo yanatolewa kuhakikisha kwamba mbegu inakua vyema kwa kumwagiliwa kila siku. Pia tunahakikisha kwamba magugu mabaya hayakui kwenye udongo kuzuia mbegu isikue vyema.
Waongofu wapya pia wanahitaji ukarimu wetu na kujali kwetu. Wanahitaji kulishwa injili baada ya ubatizo wao ili kuwaimarisha ili wasishindwe wakati wanapokabiliwa na mambo au watu ambao wanaweza kutikisa imani yao.
Ukweli rahisi wa kutambua sura mpya katika mkusanyiko ni muhimu sana na kuonesha kuvutiwa kwa mtu yule ni muhimu zaidi na inaonesha kwamba sisi tumeongoka kikweli kweli na tu wanyenyekevu. Matendo haya rahisi yanayoonekana madogo kwenye macho yetu yanaweza kuwa na matokeo muhimu na yanaweza kukumbukwa na waongofu wapya kati yetu.
Ninamkumbuka dada ambaye alibatizwa katika kata ya Kasavubu ambapo nilikuwa muumini takriban miaka ishirini iliyopita. Siku moja, wakati nikihudhuria moja ya shughuli za akina dada, nilishangazwa kumsikia akitoa ushuhuda wake akisema kwamba alikuwa na shukrani kwangu (Dada Tarr) kwamba alikuwa imara kanisani kwa sababu ya makaribisho yangu ya upendo na kumzingatia.
Kwa kuwa sikukumbuka kile hasa ambacho nilikuwa nimefanya, nilianza kutafakari juu ya ushuhuda huu wa kugusa moyo. Hitimisho langu ni kwamba hatupaswi kungoja mpaka tufanye mambo makubwa kwa ajili ya watu wapya tunaokutana nao kati yetu. Tunaweza kufanya mambo rahisi, ya kirafiki.
Acha tuwe wawazi kwenye misukumo ya upole ya Roho Mtakatifu ambayo itatupatia msukumo wa kutenda katika njia rahisi. Hiyo wakati mwingine yaweza kuwa tabasamu, makaribisho au kuwazingatia wengine.
Acha tuweke juhudi kwenye kuwa hasa wenye kuzaliwa upya, kwamba roho wa Mungu aweze kukaa ndani yetu katika njia ambayo itasababisha badiliko kuu ndani ya mioyo yetu kwamba hatutamani tena kutenda maovu bali kuyatafuta mambo yanayohusiana na Mungu.
Badiliko hili la moyo litatusaidia kuwa watu wanyenyekevu zaidi, wenye upendo zaidi, na marafiki zaidi. Tutakuwa radhi kwa haraka kuwakaribisha waumini wapya kanisani.
Waumini wapya wanahitaji watu sahihi wa kuwapa usaidizi wanaohitaji. Walithibitishwa kuwa waumini wa Kanisa kwa kuwekewa mikono na kupokea Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu kisha anaweza kuleta na kuthibitisha mafundisho ya injili ndani ya mioyo yao katika njia ambayo wanaweza kubaki waaminifu.
Kama mwongofu mpya, ninachagua kusimama imara, kutubu na kubaki kwenye njia ya agano. Haya ni maandiko mawili kati ya mengi ambayo yamenisaidia kuelewa mapenzi ya Mungu kwangu: Mosia 4:9–15, Zaburi 104:33–34.
Dada Kabongo Angelique Tarr alizaliwa Mwene-Ditu, Kasai-Oriental, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Yeye na mumewe ni wazazi wa watoto watano na aliitwa kama Mshauri wa Taasisi wa Eneo mnamo Julai 2021.