2022
Imani katika Mungu Baba na katika Yesu Kristo Mwokozi na Mkombozi wetu
Juni 2022


SAUTI ZA WAUMINI

Imani katika Mungu Baba na katika Yesu Kristo Mwokozi na Mkombozi wetu

Kupitia imani katika Yesu Kristo tunaweza kuhamisha milima katika maisha yetu.

Wakati wa Mkutano Mkuu wa Aprili 2021, nabii wetu mpendwa, Russell M. Nelson, alitufundisha kwamba daima tuwe na imani katika Yesu Kristo; na kwamba kupitia imani katika Yesu Kristo tunaweza kuhamisha milima ya maisha yetu.1

Ujumbe huu ulinigusa, na nilikumbuka majadiliano tuliyokuwa nayo na baadhi ya viongozi wa kanisa kwenye Mkutano wa Wilaya ya Yaoundé mapema mwaka huu. Wakati wa majadiliano, kila kiongozi alishiriki ushuhuda wake. Kama matokeo ya mimi na mke wangu kushiriki shuhuda zetu, tulielewa kwamba ilikuwa ni kupitia imani kwamba tulishinda changamoto nyingi.

Moja ya milima tuliyopaswa kuipanda ilikuwa ni wakati tulipokuwa tunafanya maandalizi pamoja na familia ya mke wangu kwa ajili ya ndoa yetu. Familia yake, ambayo ni Wakatoliki, waliweka sharti kwamba kama nilitaka kumuoa binti yao, tulipaswa kuoana kwa njia ya kidini katika Kanisa Katoliki. Tulikuwa hatujui kabisa nini cha kufanya.

Mimi na mke wangu tuliambiana kwamba ndoa ya hekaluni ni amri ya Mungu. Tunayo imani Kwake na kwa Mwanaye Yesu Kristo; tutasali na kufunga, na kisha chochote kile Baba yetu wa Mbinguni atakachokifunua kwetu tutakifanya, hata kama ni kuoana katika Kanisa Katoliki. Tuliamua kukutana na familia ya mke wangu ili kuwaomba kama tungeweza kuomba pamoja. Kama Baba yetu wa Mbinguni atafunua kwetu kwamba tunapaswa kufunga ndoa katika Kanisa Katoliki, hakika tutafanya hivyo. Lakini kama Mungu akifunua kwetu kwamba tunapaswa kufunga ndoa hekaluni, basi tungewaalika familia ya mke wangu kukubali jibu hilo. Lengo: kukubali mapenzi ya Mungu.

Baada ya kusali na kufunga, Baba yetu wa Mbinguni alitufunulia kwamba tulipaswa kufunga ndoa hekaluni. Kwa mshangao wetu mkuu, wakwe zangu hawakutukatalia tena.

Sisi ni wanandoa sasa kwa miaka 3 na tunapanga kwenda hekaluni mwezi ujao.

Miezi michache iliyopita mama mkwe wangu alimwambia mke wangu kwamba alihisi “tuliwaroga” wakati wa kuomba. Hawakuelewa nini kilitokea! Mke wangu kwa upendo alielezea kwamba alikuwa ni Roho wa Mungu ambaye aligusa moyo wa mama yake.

Tunapomtumaini Mungu, hatutakatishwa tamaa. Kama nabii, Russell M. Nelson alivyosema, “Bwana haitaji imani iliyo kamili ili tuweze kupokea nguvu Yake iliyo kamili. Lakini Anatutaka sisi tuamini”.2

Muhtasari

  1. Ona Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima”, Mkutano Mkuu wa Aprili 2021.

  2. Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima”, Mkutano Mkuu wa Aprili 2021.

Chapisha