2022
Juni 1991: Ubatizo wa kwanza katika Jamhuri ya Kongo
Juni 2022


MWEZI HUU KATIKA HISTORIA YA KANISA

Juni 1991: Ubatizo wa kwanza katika Jamhuri ya Kongo

Mnamo miaka ya 1980, Watakatifu wa Siku za Mwisho waliokuwa wamebatizwa ughaibuni walianza kurejea Jamhuri ya Kongo. Mnamo 1991, wale waliokuwa Brazzaville walianza kukutana pamoja na, chini ya maelekezo ya rais wa misheni upande wa pili wa Mto Kongo huko Kinshasa, walianza kuanzisha Kanisa katika Jamhuri ya Kongo. Mnamo Januari 1991, Hyacinthe Massamba-Sita, aliyekuwa amejiunga na kanisa huko Ufaransa, aliitwa kama kiongozi wa kundi katika Brazzaville na alipewa mamlaka ya kufanya mikutano ya sakramenti na kuwatafuta waumini wengine. Wamisionari wa kwanza waliokuwa wakihudumu misheni ya Zaire Kinshasa waliwasili mnamo Aprili 1991 na kukutana na Hyacinthe na Veronique Massamba-Sita pamoja na familia yao.

Ubatizo wa kwanza katika Jamhuri ya Kongo ulifanyika mnamo Juni, 1991. Hyacinthe Massambe-Sita aliwabatiza na kuwathibitisha waumini 14 wa Kanisa wa mwanzo katika Jamhuri ya Kongo, ikiwa ni pamoja na mkewe, Veronique. Kanisa lilianzishwa rasmi na serikali ya Wakongo mnamo Oktoba, 1991. Wakati Wazee Russell M. Nelson na Richard G. Scott wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walipozuru mnamo 1992 ili kuiweka wakfu nchi kwa ajili ya injili kuhubiriwa, wilaya ya kwanza ilikuwa tayari imeanzishwa huko Brazzaville.

Miaka thelathini imepita tangu ubatizo wa kwanza ulipofanyika katika Jamhuri ya Kongo. Tangu wakati ule Kanisa limekua kujumuisha vigingi vinne na Misheni ya Jamhuri ya Kongo Brazzaville ambayo iliundwa mnamo 2014. Hekalu la Kinshasa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo liliwekwa wakfu mnamo Aprili 2019, ikileta hekalu karibu zaidi na waumini katika Jamhuri ya Kongo.