Mafundisho na Maagano 2021
Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9: “Hii ndiyo Roho ya Ufunuo”


“Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9: ‘Hii ni Roho ya Ufunuo,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Januari 25–31. Mafundisho na Maagano 6–9,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
mwandishi akiandika kwenye karatasi

Januari 25–31

Mafundisho na Maagano 6–9

“Hii ndiyo Roho ya Ufunuo”

Bwana anafunua kweli kwetu katika akili zetu na mioyo yetu (ona Mafundisho na Maagano 8:2–3). Unaposoma Mafundusho na Maagano 6–9, andika misukumo yoyote unayopokea.

Andika Misukumo Yako

Katika majira ya majani kupukutika ya mwaka 1828, mwalimu kijana aliyeitwa Oliver Cowdery alipata kazi Manchester, New York, na aliishi na familia ya Lucy na Joseph Smith, Mkubwa. Oliver alikuwa amesikia kuhusu kijana wao Joseph, ambaye kwa sasa alikuwa akiishi Harmony, Pennsylvania, na Oliver, ambaye alijifikiria ni mtafutaji wa ukweli, alitaka kujua zaidi. Akina Smith walielezea matembezi ya malaika, kumbukumbu ya kale, na karama ya kutafsiri kwa uwezo wa Mungu. Oliver alivutiwa sana. Je, ingeweza kuwa kweli? Lucy na Joseph Mkubwa walimpa ushauri ambao unatumika na yoyote anayetafuta ukweli: sali na umuulize Bwana.

Oliver alifanya hivyo, na Bwana alijibu, akizungumza amani na uthibitisho kwenye akili ya Oliver. Ufunuo, Oliver aligundua, unaweza kuwa binafsi—kitu ambacho angejifunza kwa undani zaidi katika miezi ambayo ingefuata. Ufunuo si tu kwa ajili ya manabii; ni kwa ajili ya kila mtu anayeutamani na kuutafuta. Oliver bado hakujua kila kitu, bali alijua vya kutosha kupiga hatua yake ya pili. Bwana alikuwa akifanya kitu fulani muhimu kupitia Joseph Smith, na Oliver alitaka kuwa sehemu ya hilo.

Kwa taarifa zaidi kuhusu historia ya Mafundisho na Maagano 6–9, ona Watakatifu, 1:58–64; “Siku za Harmony” (Video, ChurchofJesusChrist.org).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mafundisho na Maagano 6; 8–9

Baba wa Mbinguni huzungumza nami kupitia “Roho wa ukweli.”

Katika majira ya kuchipua ya mwaka 1829 Oliver Cowdery alisafiri kwenda Harmony na alijitolea kuwa mwandishi wa Joseph Smith alipokuwa akitafsiri Kitabu cha Mormoni. Oliver sasa alikuwa na mtazamo wa karibu wa mchakato wa ufunuo wa kutafsiri. Uzoefu huu ulimsisimua, na alijiuliza kama angeweza pia kubarikiwa na karama ya kutafsiri. Bwana alimruhusu ajaribu kutafsiri, lakini kupokea ufunuo lilikuwa jambo jipya kwa Oliver, na jaribio lake halikufanikiwa. Bado alikuwa na mengi ya kujifunza, na Mafundisho na Maagano 6, 8, na 9 inaonesha kwamba Bwana alikuwa tayari kumfundisha.

Unaposoma sehemu hizi, gundua kile Bwana alichofundisha kuhusu ufunuo binafsi. Ni kwa jinsi gani maneno Yake yanahusiana na uzoefu uliowahi kupata—au ambao ungependa kupata?

Kwa mfano, ni nini Mafundisho na Maagano 6:5–7; 8:1; 9:7–8 inapendekeza kuhusu kile Bwana anahitaji kutoka kwako kabla hajafunua mapenzi Yake?

Ni nini unajifunza kutoka katika Mafundisho na MaMaagano 6:14–17, 22–24; 8:2–3; 9:7–9 kuhusu njia tofauti ufunuo unavyoweza kuja?

Kuna kingine chochote unachojifunza kuhusu ufunuo kutoka sehemu hizi?

Kujifunza zaidi kuhusu ufunuo, ona Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Ensign au Liahona, Mei 2018, 93–96; Julie B Beck, “Na juu ya Mikono ya Watumishi wangu katika siku Hizo Nitaimimina Roho Yangu,” Ensign au Liahona, Mei 2010, 10–12. Kwa maelezo zaidi kuhusu “kipawa cha Haruni” kilichoelezwa katika sehemu ya 8, ona “Kipawa cha Oliver Cowdery,” Funuo katika muktadha,15–19.

Mafundisho na Maagano 6:18–21, 29–37

Mtegemee Kristo katika kila wazo.

Japokuwa Joseph tayari alipata uzoefu wa “hali ngumu” wakati akifanya kazi ya Bwana (Mafundisho na Maagano 6:18), yeye na Oliver yaelekea hawakujua jinsi gani hali hizo zingekuwa ngumu baada ya miaka kadhaa iliyofuata. Lakini Bwana alijua, na anajua majaribu gani yapo katika siku zako za baadaye pia. Ushauri Wake kwa Joseph na Oliver katika Mafundisho na Maagano 6:18 –21, 29–37 unaweza pia kukusaidia. Ni kwa jinsi gani Joseph na Oliver waliweza kuhisi baada ya kusikia maneno haya? Unapata nini katika mistari hii ambacho kinakusaidia kumwamini Bwana? Unawezaje kumtegemea Kristo zaidi katika maisha yako?

Picha
Oliver Cowdery

Oliver Cowdery, na Lewis A. Ramsey

Mafundisho na Maagano 6–7; 9:3, 7–14

“Kwani ukiomba kile utakachotaka, utapewa.”

Tambua ni mara ngapi maneno kama “taka” au “matakwa” yanatokea katika sehemu ya 6 na7. Unajifunza nini kutoka sehemu hizi kuhusu umuhimu Mungu anaouweka katika matamanio yako? Jiulize mwenyewe swali la Bwana katika Mafundisho na Maagano 7:1: “Wataka nini wewe?”

Mojawapo ya matamanio ya haki ya Oliver Cowdery—kutafsiri kama Joseph Smith alivyotafsiri—halikutimizwa. Unaposoma Mafundisho na Maagano 9:3, 7–14, ni misukumo gani unayopokea ambayo ingeweza kukusaidia wakati matamanio yako ya haki hayatimizwi?

Ona pia Mafundisho na Maagano 11:8; Dallin H. Oaks, “Tamani,” Ensign au Liahona, Mei 2011, 42–45.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Mafundisho na Maagano 6:7, 13.Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuisaidia familia yako kuelewa kwamba “utajiri” wa kweli unapatikana katika uzima wa milele? (mstari wa 7. Ungeweza kuwaalika wanafamilia kutengeneza pesa bandia na kuandika au kuchora juu yake baadhi ya baraka nyingi familia yako imezipata kwa sababu ya injili ya urejesho.

Mafundisho na Maagano 6:15, 22–23; 8:2–3; 9:7–8.Kusoma mistari hii kuhusu jinsi Mungu anavyozungumza na watoto Wake inaweza kuwa nafasi ya kupendeza kushiriki na familia yako jinsi Alivyozungumza nanyi.

Mafundisho na Maagano 6:33–37.Wanafamilia wangeweza kushiriki jinsi wanavyoweza “kufanya mema,” hata wakati wanapohisi woga. Ingeweza pia kusaidia kuangalia wote au baadhi ya ujumbe wa Mzee Ronald A. Rasband “Msiogope” (Ensign au Liahona, Nov. 2018, 18–21). Je, inamaanisha nini “kumtegemea [Kristo] katika kila wazo”? (mstari wa 36). Ni ipi baadhi ya mifano mingine ya watu waliomgeukia Bwana ili kushinda shaka na woga? (Ona, kwa mfano, Etheri 4; Alma 26:23–31).

Mafundisho na Maagano 8:10.Hii yaweza kuwa nafasi nzuri kushiriki jinsi imani katika Yesu Kristo ilivyokuimarisha wewe na familia yako. Kwa nini ni muhimu kwamba sisi “tuombe kwa imani”? Umeona baraka zipi kutokana na kutafuta majibu au msaada kwa imani?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Dare to Do Right,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 158.

Picha
ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Tafsiri ya Kitabu cha Mormoni

Mnamo Aprili 1829, mwezi ambao sehemu ya 6–9 ya Mafundisho na Maagano ilipopokelewa, kazi kubwa ya Joseph Smith ilikuwa kutafsiri Kitabu cha Mormoni. Wakati alipoombwa baadaye kutoa maelezo ya jinsi rekodi hii ilivyotafsiriwa, Joseph alisema “kwamba haikukusudiwa kuueleza ulimwengu ukamilifu wote.”1 Mara kwa mara alisema kikawaida kwamba kilitafsiriwa “kwa karama, na uwezo wa Mungu.”2

Hatujui maelezo mengi kuhusu mchakato wa kimiujiza wa kutafsiri, lakini tunajua ya kwamba Joseph Smith alikuwa mwonaji, akipata usaidizi kutokana na vyombo ambavyo Mungu alikuwa amevitayarisha: mawe mawili angavu yaliyoitwa Urimu na Thumimu na jiwe lingine lililoitwa jiwe la mwonaji.3

Maelezo yafuatayo, kutoka kwa mashahidi walioshuhudia mchakato wa kutafsiri, wanaunga mkono ushahidi wa Joseph.

Picha
Sanduku la mbao la Hyurm Smith ambalo lilibeba mabamba ya dhahabu

Inaaminiwa kwamba sanduku hili, ambalo lilikuwa la Hyrum Smith, lilitumika kwa muda kuficha mabamba ya dhahabu.

Emma Smith

Picha
Emma Smith

“Wakati mume wangu alipokuwa anatafsiri Kitabu cha Mormoni, niliandika sehemu yake, alipokuwa anatoa imla ya kila sentensi, neno kwa neno, na alipofika kwenye majina halisi hakuweza kuyatamka, au maneno marefu, aliyasoma neno kwa neno, na wakati nilipokuwa nayaandika, kama nilifanya makosa katika tahajia, angenisimamisha na kusahihisha tahajia yangu ingawa ilikuwa haiwezekani kwa yeye kuona jinsi nilivyokuwa nayaandika wakati ule. Hata neno Sera hakuweza kulitamka mara ya kwanza, lakini ilibidi atoe tahajia yake, na nililitamka kwa ajili yake. “4

“Mabamba mara kwa mara yaliwekwa kwenye meza bila jaribio lolote la kuyaficha, yalifungwa kwenye kitambaa kidogo cha kitani cha meza, ambacho nilimpa kuyafungia. Mara moja nilihisi mabamba, wakati yalipowekwa mezani, nikifuatisha mipaka yake na maumbo yake. Yakionekana kuwa ya kupindika kiurahisi kama karatasi nene, na yaliweza kuchakacha kwa sauti ya metali wakati ncha zake ziliposogezwa na kidole gumba, kama wakati mwingine unaposogeza ncha za kitabu. …

“Imani Yangu ni kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha uhalisia mtakatifu—sina wasiwasi hata kidogo wa hilo. Nimeridhika kwamba hakuna mtu angeweza kutolea imla uandikaji wa miswada isipokuwa alikuwa ametiwa msukumo; kwani, wakati nikikaimu kama mwandishi wake, [Joseph] alitoa imla kwangu saa baada ya saa; na wakati wa kurejea baada ya chakula, au baada ya shughuli, mara moja angeanzia pale alipoachia, bila kuangalia muswada au kutaka sehemu yake kusomwa kwake. Hili lilikuwa jambo la kawaida kwake kufanya. Isingeeleweka kweli kwamba mtu msomi angeweza kufanya hivi; na, kwa yule ambaye ni mjinga hasa na asiye na elimu kama alivyokuwa, ilikuwa haiwezekani kabisa.”5

Picha
Emma Smith akisaidia kwenye kutafsiri

Kielelezo cha Emma na Joseph Smith na Michael T. Malm

Oliver Cowdery

Picha
Oliver Cowdery

“Niliandika kwa kalamu yangu mwenyewe Kitabu cha Mormoni chote (isipokuwa kurasa chache) kama yalivyotoka kutoka kwenye mdomo wa nabii, alipokuwa anakitafsiri kwa karama na uwezo wa Mungu, kwa njia ya Urimu na Thumimu, au, kama vinavyoitwa na kitabu, vikalimani vitakatifu. Niliona kwa macho yangu, na kushika kwa mikono yangu, mabamba ya dhahabu ambayo kwayo kilitafsiriwa. Pia niliona vikalimani.”6

Muhtasari

  1. Minutes, 25–26 Oktoba 1831,” Minute Book 2, 13, josephsmithpapers.org.

  2. Katika “Historia ya Kanisa,” Times and Seasons, mar. 1 1842, 707; ona pia Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007),441.

  3. Kwa maelezo zaidi, ona “Tafsiri ya Kitabu cha Mormoni,” Mada za injili, topics.ChurchofJesusChrist.org; Richard E. Turley Jr., Robin S. Jensen, na Mark Ashurst-McGee, “Joseph Mwonaji,” Ensign, Okt. 2015, 48–55.

  4. Katika Edmund C, Briggs, “A Visit to Nauvoo in 1856 “ Journal of History, vol.9, no. 4 (Okt.1916), 454; iliyonukuliwa katika Russell M. Nelson, “A Treasured Testiment,” Ensign, Jul.1993, 62.

  5. Katika “Last Testimony of Sister Emma,” Saints’ Herald, Okt. 1, 1879, 290; Tahajia zimebadilishwa.

  6. Katika shajara la Reuben Miller, Okt. 21, 1848, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake; tahajia za neno, matamshi, na herufi kubwa vimebadilishwa.

Picha
Joseph Smith na Oliver Cowdery wakitafsiri mabamba ya dhahabu

Joseph Smith na Oliver Cowdery walijifunza mengi kupitia mchakato wa kutafsiri mabamba ya dhahabu.

Chapisha