“Januari 11–17. Mafundisho na Maagano 2; Joseph Smith—Historia ya 1:27–65: ‘Mioyo ya Watoto Itawageukia Baba Zao,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Januari 11–17. Mafundisho na Maagano 2; Joseph Smith—Historia ya 1:27–65,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021
Januari 11–17
Mafundisho na Maagano 2; Joseph Smith—Historia ya 1:27–65
“Mioyo ya Watoto Itawageukia Baba Zao”
Roho Mtakatifu anaweza kukufundisha kila wakati unaposoma maandiko—hata maandiko uliyoyasoma mara nyingi kabla. Kwa hiyo kuwa tayari kwa umaizi na msukumo mpya.
Andika Misukumo Yako
Imekuwa miaka mitatu tangu Mungu Baba na Mwanaye, Yesu Kristo, walipomtokea Joseph Smith katika kijisitu, lakini Joseph hakuwa amepokea ufunuo wowote wa ziada tangu hapo. Alianza kuwa na shaka kuhusu msimamo wake mbele ya Bwana. Kama sisi sote, alikuwa amefanya makosa, na alihisi kushutumiwa kwayo. Bado hata hivyo Mungu alikuwa na kazi kwa ajili yake kufanya. Na kazi Joseph aliyoitwa kuifanya imeunganishwa na kile Mungu anataka kutoka kwetu. Joseph angeleta Kitabu cha Mormoni; sisi tumetakiwa kukifanyia nini? Joseph angepokea funguo za ukuhani kuigeuza mioyo ya watoto kuwaelekea baba zao; ni kwa jinsi gani tunaigeuza mioyo yetu kwa mababu zetu? Joseph aliambiwa juu ya unabii ambao ungetimizwa punde; sehemu yetu ni ipi katika kusaidia kuutimiza? Tunaposhiriki katika kazi ya Mungu, tunaweza kutegemea kukabiliana na upinzani na hata mateso, kama vile Nabii alivyofanya. Lakini tunaweza pia kuwa na imani kwamba Bwana atatufanya vyombo katika mikono Yake, kama vile Alivyofanya kwa Joseph.
ona pia Saints, 1:20–48.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Joseph Smith—Historia ya 1:27–33
Mungu ana kazi ya kufanywa nami.
Unaposoma Joseph Smith—Historia ya 1:27–33, fikiria kwamba Mungu ana kazi ya kufanywa nawe, kama alivyofanya kwa Joseph Smith. Tafakari mwaliko huu kutoka kwa Rais Russell M. Nelson: “Muulize Baba yako wa Mbinguni, katika jina la Yesu Kristo, jinsi Anavyohisi kuhusu wewe na wito wako hapa duniani. Kama utauliza kwa dhamira ya kweli, baada ya muda Roho atanong’ona ukweli unaobadili maisha kwako. … Ninakuahidi kwamba unapoanza kupata hata mtazamo mmoja wa jinsi Baba yako wa Mbinguni anavyokuona na nini anachotegemea kwako kufanya kwa ajili Yake, maisha yako kamwe hayatakuwa yale yale!” (“Becoming True Millennials” [ibada ya vijana wakubwa ya ulimwenguni kote, Jan. 10, 2016], broadcasts.ChurchofJesusChrist.org).
Unaweza wakati mwingine ukahisi jinsi Joseph alivyohisi katika mistari 28–29. Unaweza kujifunza nini kutokana na mfano wa Joseph kuhusu nini cha kufanya wakati matendo yako hayaendani na kazi ambayo Mungu alikuita uifanye?
Joseph Smith—Historia ya 1:34–65
Kitabu cha Mormoni kina “utimilifu wa Injili isiyo na mwisho.”
Unaposoma Joseph Smith—Historia ya 1:34–65, fikiria ni maelezo gani katika mistari hii yanaweza kujitokeza kwako ikiwa hujawahi kusikia juu ya Kitabu cha Mormoni. Kama muumini, kwa nini maelezo haya ni muhimu kwenye ushuhuda wako wa Kitabu cha Mormoni?
Fikiria jinsi Kitabu cha Mormoni kinavyotimiza unabii katika Isaya 29:4, 11–18.
Joseph Smith—Historia ya 1:36–41
Urejesho wa injili ulitimiza unabii wa kale.
Moroni alinukuu kwa Joseph baadhi ya unabii wa Agano la Kale na Agano Jipya, kama vile Isaya 11; Matendo ya Mitume 3:22–23; na Yoeli 2:28–32. Kwa nini unabii huu umekuwa muhimu kwa Joseph kuujua? Kwa nini ni muhimu kwako kuujua?
Eliya alirejesha nini?
Rais Henry B. Eyring alisema: “Ni muhimu kujua kwa nini Bwana aliahidi kumtuma Eliya. Eliya alikuwa nabii mkuu mwenye uwezo mkuu aliopewa na Mungu. Alikuwa na nguvu kubwa mno itolewayo na Mungu kwa watoto Wake: alishikilia nguvu ya kuunganisha, uwezo wa kufunga duniani na kukifanya kifungwe mbinguni” (“Hearts Bound Together,” Ensign au Liahona, Mei 2005, 78).
Ona pia Mafundisho na Maagano 110:13–16; David A. Bednar, “Acha Nyumba Hii Ijengwe Katika Jina Langu,” Ensign au Liahona, Mei 2020, 84–87.
Eliya alikuja kugeuza moyo wangu uwageukie mababu zangu.
Ni nini maneno kama “panda,” “mioyo,” na “geuza” katika sehemu hii yanakufundisha kuhusu wito wa Eliya na baraka za funguo za ukuhani alizozirejesha? Ni kwa jinsi gani umehisi moyo wako ukiwageukia mababu zako? Fikiria jinsi unavyoweza kupata uzoefu kama huu mara kwa mara. Labda ungeweza kumuomba jamaa kushiriki hadithi pamoja nawe kuhusu mmojawapo wa mababu zenu—vyema zaidi, mngeirekodi. Huenda mngeweza kumtambua babu aliyefariki ambaye kamwe hakupokea ibada za injili na kisha kufanya kazi hiyo hekaluni.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
Joseph Smith—Historia ya 1:28–29.Joseph Smith alihisi vipi kuhusu makosa yake? Alifanya nini katika kujibu hisia hizo? Tunajifunza nini kutoka kwake kuhusu nini cha kufanya wakati tunapofanya makosa?
-
Joseph Smith—Historia ya 1:33–54.Ungeweza kumwomba mwanafamilia kusoma kwa sauti sehemu au ujumbe wote wa Moroni kutoka Joseph Smith—Historia ya 1:33–42 mara nne (kwa sababu Mormoni alirudia ujumbe huu mara nne). Kati ya kila kipengele kinachosomwa, waombe wanafamilia wengine kushiriki kile wanachokumbuka kutoka kwenye ujumbe huu, bila kuangalia maandiko. Kwa nini Bwana aliweza kurudia jumbe muhimu mara kadhaa? Ni kwa njia zipi zingine Bwana anatufundisha kupitia kurudiarudia?
-
Mafundisho na Maagano 2:2.Kuwasaidia watoto wako kuelewa “ahadi zilizofanywa kwa baba,” mngeweza kusoma Ibrahimu 2:9–11 pamoja au kuangalia video “Special Witnesses of Christ—Rais Russell M.Nelson” (ChurchofJesusChrist.org). Zitambue ahadi Mungu alizofanya kama sehemu ya agano lake kwa Ibrahimu. Ni kwa jinsi gani “tunapanda” ahadi hizi katika mioyo yetu?
-
Mafundisho na Maagano 2:2–3.Kuwasaidia wanafamilia kuigeuza mioyo yao kwa baba zao (au mababu), ungeweza kuwaalika kujifunza kuhusu babu na kushiriki kile wanachojifunza pamoja na familia nzima. Kwa nini Bwana anatutaka sisi kujifunza kuhusu wanafamilia wetu na kufanya ibada za hekaluni kwa ajili yao? Tunabarikiwa vipi wakati tunaposhiriki katika historia ya familia na kazi ya hekalu? (Ona Dale G. Renlund, “Historia ya Familia na Kazi ya Hekalu: Kuunganisha na Kuponya, “ Ensign au Liahona, Mei 2018, 46–49).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “Family History—I Am Doing It,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 94.