2018
Sura ya 3: Mabamba ya Dhahabu
April 2018


Sura ya 3

Mabamba ya Dhahabu

Hii ni sura ya 3 ya juzuu mpya-nne za masimulizi ya historia ya Kanisa yenye kichwa cha habari Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo katika Siku za Mwisho. Kitabu hiki kitapatikana katika lugha 14 zilizochapishwa, katika sehemu ya Historia ya Kanisa ya Gospel Libary app, na mtandaoni kwenye Saints.lds.org. Sura kadhaa zinazofuata zitachapishwa katika matoleo yajayo mpaka juzuu ya 1 itakapotolewa baadaye mwaka huu. Sura hizo zitapatikana katika lugha 47 katika Gospel Libary app na kwenye Saints.lds.org. Sura ya 2 huelezea Ono la Kwanza la Joseph—akimwona Baba na Mwana katika majira ya kuchipua ya 1820.

hill cumorah line drawing
Moroni appearing

Aliniita kwa Jina, na Michael Malm

Miaka mitatu, na misimu mitatu ya mavuno ilipita. Joseph alitumia siku nyingi katika kufyeka ardhi, kugeuza udongo na kufanya kazi kama mwajiriwa wa muda shambani ili kupata fedha kwa ajili ya malipo ya kila mwaka ya mali za familia. Kazi ilifanya iwe vigumu kwake kuhudhuria shule mara kwa mara, na alitumia zaidi muda wake wa mapumziko pamoja na familia yake au wafanyakazi wengine.

Joseph na rafiki zake walikuwa wadogo na wachangamfu. Wakati mwingine walifanya makosa ya kipuuzi, na Joseph aligundua kuwa kusamehewa mara ya kwanza hakukumaanisha hangehitaji kamwe kutubu tena. Wala hata ono lake tukufu halikujibu maswali yote au kumaliza milele kutatizwa kwake.1 Kwa hivyo alijaribu kukaa karibu na Mungu. Alisoma Biblia yake, aliamini katika nguvu ya Yesu Kristo ya kumuokoa, na kutii amri ya Bwana ya kutojiunga na kanisa lolote.

Kama watu wengi katika eneo hilo, ikimjumuisha baba yake, Joseph aliamini kwamba Mungu angeweza kufunua ufahamu kupitia kwa vitu kama fimbo na mawe, kama alivyofanya kupitia kwa Musa, Haruni na wengine katika Biblia.2 Siku moja, wakati Joseph alikuwa akimsaidia jirani kuchimba kisima, alipata jiwe dogo lililofukiwa sana katika ardhi. Akijua kuwa watu wakati mwingine walitumia mawe maalum kwa ajili ya kutafuta vitu vilivyopotea au vitu vya thamani vilivyofichika, Joseph alijiuliza kama ndio alikuwa amepata jiwe la namna hiyo. Akiangalia kupitia kwa hilo jiwe, aliona vitu visivyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.3

Kipawa cha Joseph cha kutumia jiwe kiliwavutia wanafamila, ambao walikiona kama ishara ya upendeleo mtakatifu.4 Lakini ijapokuwa alikuwa na kipawa cha uonaji, Joseph bado hakuwa na hakika kama Mungu alikuwa anafurahishwa naye. Hakuhisi tena msamaha na amani ambayo alihisi baada ya ono lake la Baba na Mwana. Badala yake, mara kwa mara alihisi kujishutumu kutokana na udhaifu wake na kutokamilika kwake.5

Mnamo Septemba 21, 1823, akiwa na umri wa miaka kumi na saba Joseph alikaa macho kwenye chumba cha juu cha kulala alichotumia na kaka zake. Alichelewa kulala usiku ule, akisikiliza maongezi ya familia yake kuhusu makanisa tofauti tofauti na mafundisho waliofundisha. Sasa kila mmoja alikuwa amelala, na nyumba ilikuwa kimya.6

Katika kiza chumbani kwake, Joseph alianza kusali, akiomba kwa bidii kwamba Mungu angemsamehe dhambi zake. Alitamani kuwasiliana na mjumbe wa mbinguni ambaye angeweza kumhakikishia nafasi yake mbele za Bwana na kumpa uelewa wa injili ambao aliahidi katika kijisitu. Joseph alijua Mungu alijibu sala yake hapo awali, na alikuwa na ujasiri wa kutosha kwamba Angemjibu tena.

Wakati Joseph akisali, mwanga ulitokea pembezoni mwa kitanda chake na kuongezeka uangavu mpaka ukajaza chumba kizima cha juu. Joseph aliangalia juu na akamuona malaika amesimama angani. Malaika alivaa joho jeupe ambalo halijaunganishwa, ambalo lilifika mpaka kwenye vifundo vyake vya mikono na miguu. Mwanga uliangaza kutoka kwake, na uso wake ulingaa kama radi.

Mara ya kwanza Joseph aliogopa, lakini upesi amani ikamjaa. Malaika alimuita kwa jina na akajitambulisha kwake kama Moroni. Akamwambia Mungu amemsamehe Joseph dhambi zake na sasa ana kazi kwa ajili yake kufanya. Alitangaza kwamba jina la Joseph lingesemwa kwa mazuri na maovu kati ya watu wote.7

Moroni akazungumza kuhusu Mabamba ya Dhahabu yaliyozikwa katika kilima kilichokuwa karibu. Kwenye mabamba kulichorwa kumbukumbu ya watu wa kale ambao waliishi awali katika Amerika. Kumbukumbu ilizungumzia kuhusu chimbuko na kutoa maelezo ya kutembelewa kwao na Yesu Kristo na kufundisha utimilifu wa injili yake.8 Yakiwa yamezikwa pamoja na mabamba, Moroni alisema, yalikuwa ni mawe mawili ya mwonaji, ambayo Joseph baadaye aliyaita Urimu na Thumimu, au vitafsiri. Bwana aliandaa mawe haya ili kumsaidia Joseph kutafsiri kumbukumbu. Mawe maangavu yalifungwa pamoja na kuunganishwa kwenye dirii.9

Kwa muda uliobaki wa ugeni, Moroni alidondoa unabii toka kwenye vitabu vya biblia vya Isaya, Joeli, Malaki na Matendo ya Mitume. Bwana alikuwa anakuja hivi karibuni, alielezea, na familia ya binadamu isingeweza kutimiza lengo la uumbaji isipokuwa agano la Mungu la kale lifanywe upya kwanza.10 Moroni alisema kwamba Bwana amemchagua Joseph kufanya upya agano hilo, na hiyo ni tu kama angechagua kuwa mwaminifu katika amri za Mungu, angekuwa mmoja wa kufunua kumbukumbu iliyoko kwenye mabamba.11

Kabla ya kuondoka, malaika alimuamuru Joseph kuchunga mabamba na kutoyaonyesha kwa yeyote isipokuwa ameelekezwa, akimuonya kwamba ataangamizwa kama hatatii ushauri huu. Kisha mwanga ukajikusanya kumzunguka Moroni na akaelekea mbinguni.12

Wakati Joseph alipokuwa amelala akitafakari kuhusu ono, mwanga ukajaa tena chumbani na Moroni akatokea tena, akitoa ujumbe uleule kama awali. Kisha akaondoka, na akatokea kwa mara nyingine tena na kutoa ujumbe wake kwa mara ya tatu.

“Sasa, Joseph, kuwa makini,” alisema. “Wakati ukienda kuchukua mabamba, mawazo yako yatajazwa na kiza, na kila aina ya uovu utakuja kwa haraka mawazoni mwako kukuzuia wewe kutii amri za Mungu.” Akimuelekeza Joseph kwa mtu ambaye angemsaidia, Moroni alimuasa amwambie baba yake kuhusu ono lake.

“Ataamini kila neno usemalo,” malaika alimwahidi.13

Asubuhi yake, Joseph hakusema chochote kuhusu Moroni, ijapokuwa alijua kwamba baba yake pia aliamini katika maono na malaika. Badala yake, walitumia asubuhi pamoja na Alvin katika kuvuna kwenye shamba karibu yao.

Kazi ilikuwa ngumu. Joseph alijaribu kwenda sambamba na kaka yake walipokuwa wakipeleka mundu zao mbele na nyuma kukata nafaka zilizokuwa ndefu. Lakini ugeni wa Moroni ulimweka macho wazi usiku kucha, na mawazo yake yalikuwa yakirudi kwenye kumbukumbu za kale na kilima ambapo zilikuwa zimezikwa.

Punde aliacha kufanya kazi, na Alvin alitambua hilo. “Lazima tuendelee kufanya kazi” alipaza sauti kwa Joseph, “au la sivyo hatutamaliza shughuli yetu.”14

Joseph alijaribu kufanya kazi kwa nguvu zaidi na kwa haraka, lakini kwa vyovyote alivyofanya, hakuweza kwenda sambamba na Alvin. Baada ya muda, Joseph Mkubwa alitambua kwamba Joseph amekuwa dhaifu na ameacha tena kufanya kazi. “Nenda nyumbani,” alisema, akiamini mwanawe alikuwa mgonjwa.

Joseph alimtii baba yake akitatanika kuelekea nyumbani. Lakini alipokuwa akijaribu kuvuka ua, alianguka chini, mwenye uchovu.

Wakati akiwa amelala pale, akikusanya nguvu, alimuona Moroni amesimama tena angani juu yake, akizungukwa na mwanga. “Kwa nini hukumwambia baba yako nilichokuambia?” aliuliza.

Joseph alisema alikuwa akiogopa baba yake hangemwamini.

“Atakuamini” Moroni alimuhakikishia, kisha akarudia ujumbe wake wa usiku uliopita.15

Joseph Mkubwa alilia wakati mwanawe alipomwambia kuhusu malaika na ujumbe wake. “Lilikuwa ni ono kutoka kwa Mungu,” alisema. “lishughulikie.”16

Hill Cumorah

Picha toka angani ya Kilima Kumora na maeneo yanayouzunguka na Craig Dimond

Joseph mara moja alijiandaa kwa ajili ya kwenda kilimani. Wakati wa usiku, Moroni alimuonyesha ono la wapi mabamba yalikuwa yamefichwa, hivyo alijua wapi pa kwenda. Kilima, kimoja kati ya vikubwa katika lile eneo, kilikuwa kiasi cha umbali wa maili tatu kutoka nyumbani kwake. Mabamba yalizikwa chini ya mwamba mkubwa, wa mviringo katika upande wa magharibi wa kilima, ambao si mbali sana na kilele chake.

Joseph alifikiria kuhusu mabamba akiwa anatembea. Ijapokuwa alijua yalikuwa matakatifu, ilikuwa vigumu kwake kujizuia kujiuliza thamani yake ilikuwa kiasi gani. Alikuwa amesikia hadithi kuhusu vitu vya thamani vilivyolindwa na roho walinzi, lakini Moroni na mabamba aliyoelezea ilikuwa ni tofauti. Moroni alikuwa mjumbe kutoka mbinguni aliyeteuliwa na Mungu kukabidhi salama kumbukumbu kwa mwonaji Wake mteule. Na mabamba yalikuwa na thamani si kwa sababu yalikuwa ya dhahabu, lakini kwa sababu yalishuhudia kuhusu Yesu Kristo.

Hata hivyo, Joseph bado hakuweza kujizuia kutafakari kwamba sasa alijua hususani wapi pa kupata vitu vya thamani vya kutosha kuikomboa familia yake kutoka umasikini.17

Akifika kwenye kilima, Joseph aliipata ile sehemu aliyoiona kwenye ono na akaanza kuchimba kwa chini kwenye kitako cha mwamba mpaka kona zake zilipoonekana sawia. Kisha akachukua tawi kubwa la mti na kulitumia kama mtaimbo kunyanyua jiwe na kulisukuma pembeni.18

Chini ya jabali kilikuwa ni kisanduku, kuta zake na kitako chake vikitengenezwa kwa jiwe. Akiangalia kwa ndani, Joseph aliona Mabamba ya Dhahabu, mawe ya mwonaji, na dirii.19 Mabamba yalikuwa yamejaa michoro ya kale na kufungwa pamoja kwa upande mmoja na vizingo tatu. Kila bamba ilikuwa takribani nchi sita kwa upana, inchi nane kwa urefu na nyembamba. Sehemu ya bamba pia ilionekana kufungwa kwamba yeyote asiweze kuisoma.20

Akishangazwa, Joseph alijiuliza tena ni kiasi gani mabamba yangegharimu. Alijaribu kuyashika—na kisha alipata hisia ya mtikisiko Akarudisha mkono wake lakini akijaribu kuyashika mabamba kwa mara ya pili zaidi alipata mtikisiko kila wakati.

“Kwa nini siwezi kukipata kitabu hiki?” alipaza sauti.

“Kwa sababu hujatii amri za Bwana,” sauti ilisema kwa karibu.21

Joseph aligeuka na akamuona Moroni. Mara moja ujumbe wa usiku uliopita ulijaza mawazo yake, na akaelewa kwamba alikuwa amesahau dhumuni la kweli la kumbukumbu ile. Akaanza kusali, na mawazo yake na nafsi yake ikajazwa na Roho Mtakatifu.

“Tazama” Moroni akaamuru. Ono jingine likafunuliwa mbele ya Joseph, na akamuona Shetani akiwa amezungukwa na jeshi lake lisilo na idadi. “Vyote hivi vinaonyeshwa, mazuri na maovu, utakatifu na visivyo safi, utukufu wa Mungu na nguvu za giza,” malaika alisema, “Kwamba upate kujua nguvu mbili baada ya hapa na kamwe usiathiriwe au kushindwa na yule muovu.”

Alimulelekeza Joseph kujitakasa moyo wake na kuimarisha mawazo yake kupokea ile kumbukumbu. “Ikiwa kama vitu hivi vitakatifu vinapatikana ni lazima iwe kupitia sala na uaminifu katika kutii amri za Bwana,” Moroni alifafanua. “Havikutunzwa hapa kwa madhumuni ya kukusanya faida na utajiri kwa ajili ya utukufu wa dunia hii. Vilifungwa kwa sala ya imani.”22

Joseph aliuliza ni lini angeweza kuwa na mabamba.

“Siku ya tarehe ishirini na mbili ya Septemba ijayo,” Moroni alisema, kama utakuja na mtu sahihi pamoja nawe.”

“Yupi ni mtu sahihi?” Joseph aliuliza.

“Kaka yako mkubwa.”23

Tangu alipokuwa mdogo, Joseph alijua kuwa angeweza kumtegemea kaka yake mkubwa. Alvin sasa alikuwa na miaka ishirini na tano na angeweza kupata shamba lake mwenyewe kama angetaka. Lakini aliamua kubaki katika shamba la familia kuwasaidia wazazi wake kukaa vyema na kuilinda ardhi yao wanapoelekea uzeeni. Alikuwa mwenye msimamo na mwenye bidii katika kazi, na Joseph alipendezwa naye sana.24

Labda Moroni alihisi Joseph alihitaji nguvu na hekima ya kaka yake ili kuwa aina ya mtu Bwana angemwamini na mabamba.

Akirudi nyumbani jioni ile, Joseph alikuwa amechoka. Lakini familia yake punde ikamzonga kumzunguka alipokuwa akiingia kupitia mlango, wakiwa na shauku kujua nini alikipata katika kilima. Joseph akaanza kuwaambia kuhusu mabamba, lakini Alvin aliingilia wakati alipogundua ni jinsi gani Joseph alionekana mchovu.

“Twende kulala,” alisema, “na tutaamka mapema asubuhi na kwenda kazini.” Wangekuwa na muda mwingi kesho kusikia sehemu iliyobaki ya hadithi ya Joseph. “Kama mama atatupatia chakula cha jioni mapema,” alisema, “tutakuwa na jioni nzuri ndefu na kukaa chini na kukusikiliza ukiongea.”25

Jioni iliyofuata, Joseph alishiriki kile kilichotokea katika kilima, na Alvin alimuamini. Kama mtoto wa kiume mkubwa kwenye familia, Alvin kila mara alihisi uwajibikaji katika hali njema ya kimwili ya wazazi wake wazee. Yeye pamoja na kaka zake walikuwa hata wameanza kujenga nyumba kubwa kwa ajili ya familia kwamba wangeweza kustarehe zaidi.

Sasa ilionekana Joseph alikuwa akiangalia ustawi wao wa kiroho. Usiku baada usiku aliivutia familia kwa mazungumzo ya Mabamba ya Dhahabu na wale walioyaandika. Familia ilikuwa na ukaribu pamoja, na nyumba yao ilikuwa ya amani na furaha. Kila mmoja alihisi kuwa kitu fulani kizuri ki karibu kutokea.26

Kisha asubuhi moja ya majira ya kupukutika kwa majani, chini ya miezi miwili tangu ugeni wa Moroni, Alvin alirudi nyumbani akiwa na maumivu makali katika tumbo lake. Akijikunja kwa maumivu makali, alimuomba baba yake aite msaada. Hatimaye daktari alipofika, alimpa Alvin kipimo kikubwa cha dawa kama chaki, lakini ilifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Alvin alilala kitandani kwa siku nyingi, akiteseka kwa maumivu. Akijua kwamba kuna uwezekano angekufa, alimuita Joseph. “Fanya kila lililo ndani ya uwezo wako kuzipata kumbukumbu,” Alvin alisema. “Kuwa mwaminifu katika kupokea maelekezo na kushika kila amri ambazo unapewa.”27

Alifariki muda mfupi baadaye, na huzuni ikatawala katika nyumba. Katika mazishi, mhubiri alisema Alvin amekwenda jahanamu, akitumia kifo chake kuwaonya wengine kuhusu ambacho kingetokea isipokuwa Mungu aingilie kati na kuwaokoa. Joseph Mkubwa Alichukizwa. Mwanawe alikuwa kijana mzuri, na hakuamini kwamba Mungu angemtakia adhabu ya milele.28

Kwa kifo cha Alvin, maongezi juu ya mabamba yaliisha. Alikuwa ni msaidizi dhabiti katika wito mtakatifu wa Joseph kwamba kuyataja kwa aina yoyote ile kulirudisha kifo chake mawazoni. Familia haikuweza kuvumilia.

Joseph alimkosa Alvin kwa kiasi kikubwa sana na alichukulia kifo chake hasa kwa uchungu. Alikuwa akitumaini kumtegemea kaka yake mkubwa katika kumsaidia kupata kumbukumbu. Sasa alihisi kuachwa peke yake.29

statue of Moroni

Sanamu ya Moroni imesimama juu ya Kilima Kumora kuadhimisha mahali ambapo Joseph Smith aliyaona mabamba ya Kitabu cha Mormoni mnamo Septemba 1823, na kuyapokea miaka minne baadaye.

Wakati siku ya kurudi kwenye kilima ilipofika, Joseph alikwenda peke yake. Bila kuwa na Alvin, hakuwa na uhakika kama Bwana angemwamini kumpa mabamba. Lakini alifikiri angeweza kushika kila amri Bwana alikuwa amempa, kama kaka yake Alvin alivyomshauri. Maelekezo ya Moroni ya kuchukua mabamba yalikuwa wazi. “Lazima uyachukue mikononi mwako na kwenda moja kwa moja nyumbani kwenu bila kuchelewa,” malaika alisema “na uyafungue.”30

Katika kilima, Joseph aliinua mwamba, akafikia kwenye kisanduku cha jiwe, na akayatoa yale mabamba. Wazo likamjia kichwani: vitu vingine katika kisanduku vilikuwa vya thamani na vinahitajika kufichwa kabla hajaenda nyumbani. Akayaweka mabamba chini na kurudi kufunika kisanduku. Lakini aliporudia mabamba, hakuyakuta. Akiwa mwenye wasiwasi, alipiga magoti na kuomba kujua pale yalipo.

Moroni alitokea tena na kumwambia Joseph kwamba ameshindwa kufuata maelekezo kwa mara nyingine. Si tu kwamba aliweka mabamba chini kabla ya kuyahifadhi salama, aliyaacha mbali na upeo wake wa kuyaona. Japo kwa utayari aliokuwa nao mwonaji mdogo kufanya kazi ya Bwana, hakuwa tayari na uwezo wa kulinda kumbukumbu ile ya kale.

Joseph alisikitishwa nafsini mwake, lakini Moroni alimuaelekeza kurudi kwa ajili ya mabamba mwaka uliofuata. Pia alimfundisha zaidi kuhusu mpango wa Bwana kwa ajili ya ufalme wa Mungu na kazi kuu kuanza kukua.

Hata hivyo, baada ya malaika kuondoka, Joseph alishuka taratibu kilimani, akihofia kile familia yake ingefikiria akirudi nyumbani mikono mitupu.31 Alipoingia ndani ya nyumba, walikuwa wakimsubiri Baba yake alimuuliza mara moja kama alikuwa na mabamba.

“Hapana,” alisema. “Sikuweza kuyapata.”

“Uliyaona?”

“Niliyaona lakini sikuweza kuyachukua.”

“Ningeweza kuyachukua,” Joseph Mkubwa Alisema, “kama ningekuwa kwenye nafasi yako.”

“Hujui ukisemacho,” Joseph alisema. “Sikuweza kuyachukua, kwani malaika wa Bwana hakuniruhusu.”32

Muhtasari

  1. Historia ya Joseph Smith,1838–56, Toleo A-1, 4–5, katika JSP, H1:220 (draft 2); Joseph Smith History, circa Summer 1832, 1, katika JSP, H1:11.

  2. “Joseph Smith kama Mfunuzi na Mtafsiri,” katika JSP, MRB:xxi; Turley, Jensen, and Ashurst-McGee, “Joseph Mwonaji,” 49–50; ona pia Mosia 8:17; Alma 37:6–7, 41; and Mafundisho na Maagano 10:1, 4 (Revelation, Spring 1829, at josephsmithpapers.org).

  3. Bushman, Rough Stone Rolling, 48–49; Bushman, “Joseph Smith kama Mtafsiri,” 242. Mada: Mawe ya Mwonaji

  4. Lucy Mack Smith, History, 1845, 95; Ona pia Alma 37:23.

  5. Joseph Smith Historia, circa Summer 1832, 4, katika JSP, H1:13–14; Joseph Smith—Historia 1:28–29; Joseph Smith Historia, 1838–56, volume A-1, 5, in JSP, H1:218–20 (draft 2).

  6. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [10].

  7. Joseph Smith Historia, circa Summer 1832, 4, katika JSP, H1:13–14; Joseph Smith—History 1:29–33; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 5, in JSP, H1:218–22 (draft 2); Pratt, Interesting Account, 6, in JSP, H1:524; Hyde, Ein Ruf aus der Wüste, 17–20. Mada: Malaika Moroni

  8. Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, katika JSP, J1:88.

  9. Joseph Smith—Historia 1:35; Joseph Smith Historia, 1838–56, volume A-1, 5, in JSP, H1:222 (draft 2); Joseph Smith Historia, circa Summer 1832, 4, katika JSP, H1:14; Oliver Cowdery, “Letter IV,” LDS Messenger and Advocate, Feb. 1835, 1:65–67; Turley, Jensen, and Ashurst-McGee, “Joseph Mwonaji,” 49–54; “Mormonism—No. II,” Tiffany’s Monthly, Julai 1859, 164. Mada: Mawe ya Mwonaji

  10. Joseph Smith—Historia 1:36–41; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 5–6, in JSP, H1:222–26 (draft 2); Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, in JSP, J1:88–89.

  11. Oliver Cowdery, “Letter IV,” LDS Messenger and Advocate, Feb. 1835, 1:78–79; Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [11].

  12. Joseph Smith—Historia 1:42–43; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 6, katika JSP, H1:226 (draft 2).

  13. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [10]–[11]; Oliver Cowdery, “Letter IV,” LDS Messenger and Advocate, Feb. 1835, 1:79–80; Oliver Cowdery, “Letter VII,” LDS Messenger and Advocate, July 1835, 1:156–57; Joseph Smith—Historia 1:44–46; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 6–7, in JSP, H1:230–32 (draft 2); Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, katika JSP, J1:88–89.

  14. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [11]; ona pia Smith, William Smith on Mormonism, 9.

  15. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [11]; Smith, Biographical Sketches, 82; Joseph Smith—Historia 1:48–49; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 7, katika JSP, H1:230–32 (draft 2); Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, katika JSP, J1:89.

  16. Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, katika JSP, J1:89.

  17. Oliver Cowdery, “Letter VIII,” LDS Messenger and Advocate, Oct. 1835, 2:195–97. Topic: Treasure Seeking

  18. Oliver Cowdery, “Letter VIII,” LDS Messenger and Advocate, Oct. 1835, 2:195–97; Joseph Smith—Historia 1:51–52; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 6–7, in JSP, H1:230–32 (draft 2); see also Packer, “A Study of the Hill Cumorah,” 7–10.

  19. Joseph Smith—Historia 1:52; Joseph Smith Historia, 1838–56, volume A-1, 7, katika JSP, H1:232 (draft 2). Topic: Bamba za Dhahabu

  20. Joseph Smith, “Historia ya Kanisa,” Times and Seasons, Mar. 1, 1842, 3:707, in JSP, H1:495.

  21. Oliver Cowdery, “Letter VIII,” LDS Messenger and Advocate, Oct. 1835, 2:197–98; see also Pratt, Interesting Account, 10, in JSP, H1:527–29.

  22. Oliver Cowdery, “Letter VIII,” LDS Messenger and Advocate, Oct. 1835, 2:198–99.

  23. Knight, Reminiscences, 1; Joseph Smith, shajara, Nov. 9–11, 1835, in JSP, J1:89; Joseph Smith—Historia 1:53–54; Joseph Smith Historia, 1838–56, toleo A-1, 7, katika JSP, H1:232–34 (draft 2); see also Jessee, “Joseph Knight’s Recollection of Early Mormon History,” 31.

  24. Joseph Smith, Journal, Aug. 23, 1842, in JSP, J1:116–17.

  25. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 3, [12]; book 4, [3]; Smith, Biographical Sketches, 83.

  26. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [1]–[3]; Smith, Biographical Sketches, 86–87; see also Lucy Mack Smith, History, 1845, 89; and Bushman, Refinement of America, 425–27. Topic: Joseph Sr. and Lucy Mack Smith Family

  27. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [3]–[5].

  28. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [6]–[8]; “Wm. B. Smith’s Last Statement,” Zion’s Ensign, Jan. 13, 1894, 6.

  29. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [7]; Joseph Smith, shajara, Aug. 23, 1842, in JSP, J2:116–17.

  30. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [2]–[3].

  31. Lucy Mack Smith, History, 1844–45, book 4, [2]–[3]; Smith, Biographical Sketches, 85–86; Knight, Reminiscences, 1; Joseph Smith—Historia 1:54; Lucy Mack Smith, History, 1845, 88; ona pia Jessee, “Joseph Knight’s Recollection of Early Mormon History,” 31.

  32. Smith, Biographical Sketches, 86.